Sura Ya 20: Vikwazo Vya Kiuchumi

Njia ya rahisi na ifaayo kabisa ya kuwaangusha walio wachache kwenye jamii ni kufanya kampeni hasi, ile iliyomo kwenye msingi wa umoja na mapatano.

Kampeni chanya hulazimu vyanzo mbali mbali, kwa kuwa huwa muhimu kwamba lile kundi linalopigana linapaswa litumie silaha za kisasa na linapaswa pia lifikie lengo lake kwa kutoa mihanga ya kimwili na kiuchumi na kwa kushinda mamia ya vizuizi. Ni dhahiri kwamba aina hii ya kampeni inaandamana na maumivu na taabu nyingi. Watawala wenye hekima huitumia kampeni hii baada ya kufanya matayarisho na maandalizi ya hitajikayo na hawautumii mpango huu ila pale ikosekanapo njia nyingine na kubakiwa na njia ya vita tu.

Hata hivyo, kampeni hasi haiyahitaji yote hayo. Inakihitaji kipengele kimoja tu nacho ni umoja na mapatano ya walio wengi. Hii ina maana ya kwamba, kikundi cha watu ambao lengo lao ni kuliangusha kundi la walio wachache, huungana kwa uaminifu na kufanya mkataba na kuapa kwamba watakata uhusiano na lile kundi pinzani la wachache, wasiruhusu kufanya biashara nao, kukatisha uhusiano wa ndoa nao, hawatawaruhusu kushiriki kwenye mambo ya pamoja na hawatashirikiana nao kwenye mambo ya mtu na mtu. Katika hali hiyo, dunia pamoja na upana wake wote huu, huwa kama jela ndogo na nyembamba kwao wale wa kundi dogo, na kila wakati; shinikizo lake hulihofisha kundi hili juu ya maangamizo.

Wakati mwingine kundi hili pinzani la walio wachache kufikia hapa hujisalimisha na kutii uamuzi wa walio wengi. Hata hivyo, kundi la walio wachache la aina hiyo, halina budi kuwa la watu wale ambao upinzani wao hausukumwi na lengo la kiroho. Kwa mfano, wanaweza kuwa wamefanya kampeni ili wajipatie utajiri, vyeo muhimu na nafasi za kiserikali.
Watu kama hawa pale wanapoihisi hatari, na wakawa wanakabiliwa na matatizo ya vizuizi, wao kutokana na kutokuwa kwao na msukumo wa kiroho, na sababu zao zikawa ni za kidunia tu, hupendelea faida kuu iwezayo kupatikana kuliko zile furaha za muda mfupi na kuyakubali matakwa ya walio wengi.

Hata hivyo, wale watu ambao upinzani wao unatokana na imani hawa- hofishwi na magumu ya aina hiyo. Shinikizo la vizuizi huiimarisha imani yao na huyakubali mapigo na mashambulio ya adui kwa ngao ya subira na ustahimilivu.

Kurasa za historia ya mwanaadamu zinashuhudia ukweli uliopo ya kwam- ba kipengele chenye nguvu zaidi kwa ajili ya uthabiti na uimara wa wachache dhidi ya malengo ya walio wengi ni nguvu yao ya imani, na wakati mwingine hulitoa mhanga tone la mwisho la damu yao katika kulifikia lengo lao. Na yako mamia ya ushahidi wa kuthibitisha usahihi wa maneno haya.

Azimio La Waquraishi

Machifu wa Waquraishi walipatwa na wasiwasi mno kutokana na kukua kushangazako kwa Uislamu, nao walikuwa na shauku ya kupata njia fulani ya kujitoa kwenye hali hii. Kusilimu kwa watu wengi kama vile Bwana Hamza na mwelekeo wa wenye uoni wa dhahiri wa Quraishi kwenye Uislamu, pamoja na uhuru walioufaidi wale Waislamu walioko kule Ethiopia nako kuliongeza mashaka na mshangao wa watawala wa zama zile. Vile vile walisikitishwa mno na kushindwa kwa mipango yao, na hivyo basi wakaufikiria mpango mwingine. Walifikiria kizuizi cha uchumi juu ya Waislamu ili waweze kuzuia kupenya na kuenea kwa Uislamu, na kumzuia yule mwasisi na wafuasi wa dini ya Allah wasiyatekeleze mambo yao.

Hivyo basi, machifu wa utawala walibandika kwenye Al-Ka’ba hati ya mapatano iliyoandikwa na Mansur bin Akramah na kuidhinishwa na halmashauri kuu ya Waquraishi na wakaapa ya kwamba jamii ya Waquraishi watatekeleza hadi kifo chao mambo yafuatayo:

1. Kila aina ya biashara na kazi na wasaidizi wa Muhamad itapigwa marufuku.
2. Kushirikiana nao kwa njia yoyote ile kumepigwa marufuku kabisa.
3. Hakuna mtu yeyote aruhusiwaye kufanya mapatano ya ndoa na Waislamu.
4. Wapinzani wa Muhammad ni lazima wasaidiwe kwa hali yoyote ile.

Maandiko ya mkataba huo wenye mambo tuliyoyataja hapo juu yalitiwa saini na Waquraishi wote walio maarufu na ulitwaliwa na kuanza kutekelezwa kikamilifu dhidi yao. Bwana Abu Twalib, mfuasi mashuhuri wa Mtume (s.a.w.w.) aliwaalika ndugu zake (dhuria wa Hashim na Abdul- Muttalib) na kuwawajibisha kumsaidia Mtume (s.a.w.w.). Vile vile aliamua kwamba familia hizo zote zitoke mjini Makkah na ziende zikaishi kwenye bonde lijulikanalo kwa jina la ‘Bonde la Abu Twalib’ lililoko baina ya milima ya Makkah, wajenge hapo nyumba ndogondogo na mahema, na wawe mbali na mazingira ya wenye kuabudu masanamu. Ili kujikinga na mashambulizi ya ghafla, yawezayo kufanywa na Waquraishi, pia alipanga kujenga minara ya doria (ziginari) hapo na kuweka doria watakaomtaarifu matukio mapya yoyote yale.1

Kizuizi hiki kilidumu kwa muda wa miaka mitatu na shinikizo na taabu walizozipata zilichukua ukubwa usio na kifani. Vilio vyenye kuzipasua nyoyo vya watoto wa Bani Hashim viliyafikia masikio ya watu wa Makkah wenye nyoyo za mawe, lakini havikuwa na athari zozote masikioni humo. Vijana na watu wazima walikula tende moja tu kwa kila mtu na nyakati zingine waliigawa tende nusu kwa nusu. Katika kipindi chote hiki cha miaka mitatu, watu wa ukoo wa Bani Hisham walitoka nje ya bonde lile wakati ule tu wa ile miezi mitakatifu tu (ambayo vita imeharimishwa) wakati amani ilipotawala kila mahali kwenye Penisula ya Uarabuni. Katika vipindi hivi, walinunua vitu vidogo vidogo na kisha wakarudi kule bondeni.
Kiongozi wao mashuhuri, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) nae aliweza kuilighania dini yake kwenye miezi hii tu. Hata hivyo, washauri na mawakala wa Waquraishi walilitekeleza lile shinikizo la kiuchumi hata kwenye miezi hii, kwa sababu, kwa kawaida wao walikuja madukani na kwenye maghala na pale Waislam walipotaka kununua kitu, wao walilipa bei kubwa kubwa kwa kitu kile na wakakin- unua wao ili kuwafanya Waislamu wasiweze kukipata. Abu Lahab alikuwa hasa ndiye mshughulikaji sana katika hili. Aliwaambia watu kwenye mitaa ya maduka kwa sauti kubwa kwamba: “Enyi watu! Pandisheni bei za vitu na muwakoseshe wafuasi wa Muhammad uwezo wao wa kununua.” Hivyo basi, ili kuhakikisha ya kwamba kunadhibitiwa bei kwenye kiwango cha juu, yeye mwenyewe alivinunua vitu kwa bei ya juu. Kwa sababu hii, kiwango cha bei kilisalia kuwa cha juu wakati mwingi.

Hali Ya Kuhuzunisha Ya Bani Hashim

Shinikizo la njaa lilikuwa limefikia hatua ambayo Sa’ad bin Waqqas anase- ma: “Usiku mmoja nilikuwa nikitoka mle bondeni katika hali ambayo kwamba nilikuwa karibuni kuzimaliza nguvu zangu zote. Mara nikaiona ngozi ya ngamia iliyokauka. Nikaiokota, nikaiosha, nikaichoma na kuifunda. Baada ya hapo niliikanda na maji na nikaitumia kwa muda wa siku tatu.”

Wapelelezi wa Waquraishi waliendelea kuzilinda njia zote ziingiazo mle bondeni ili kuhakikisha kwamba mtu yeyote asiwaletee mahitaji yoyote Bani Hashimu. Hata hivyo, ingawa walizitawala hivyo njia zile, Hakim bin Hizaam mpwawe Bibi Khadijah, Abul Aas bin Rabi,i na Hisham bin Umar, kila mara walikuwa wakiwasheheni ngamia kwa ngano na tende kwenye nyakati za usiku na kuwaleta karibu na bonde lile. Kisha walizifunga hata- mu zao shingoni mwao na kuwaachia. Wakati mwingine kuutoa msaada huu nako kuliwaletea matatizo.

Siku moja Abu Jahl aliona kwamba Hakim alikuwa amemsheheni ngamia kwa chakula na kumwongozea kwenye bonde lile. Alichukizwa mno na Hakim na akamwambia: “Nadhani nikupeleke kwa Waquraishi na kukufedhehesha.” Ugomvi wao ule uliendelea. Abul Bakhtari aliyekuwa mmoja wa maadui wa Uislam hakukikubali kitendo kile cha Abu Jahl na akasema: “Anampelekea chakula shangazi yake (Khadija). Huna haki ya kumzuia asifanye hivyo.” Hakutosheka na sentensi hii tu, bali vile vile alimshambulia Abu Jahl.

Ukali wa kitendo cha Waquraishi katika kuyatekeleza mapatano yao haukuipunguza subira na umadhubuti wa Waislamu. Hatimaye, makelele ya vichanga na watoto yenye kuhuzunisha na hali ya kisikitisha ya Waislamu viliamsha hisia za baadhi ya watu. Walijutia mno kutia saini kwao mkataba ule na wakaanza kuzifikiria njia za kulimaliza tatizo lile.

Siku moja Hisham bin Umar alikwenda kuonana na Zuhayr bin Abi Umayyah aliyekuwa mwana wa bint yake Abdul-Muttalib na kumwambia: “Je, ni sahihi kwamba wewe uwe unakula chakula na kuvaa nguo nzuri ambapo ndugu zako wanabakia na njaa na uchi? Ninaapa kwa jina la Allah! Kama ungechukua uamuzi wa aina hiyo, juu ya nduguze Abu Jahl na ukamtaka autekeleze uamuzi huo, katu asingekubali kufanya hivyo.” Zuhayr akasema: “Mimi peke yangu siwezi kuubadili uamuzi wa Waquraishi, lakini kama mtu mwingine akiniunga mkono nitaupasua mkataba ule.” Hisham akasema: “Mimi niko pamoja nawe.” Zuhayr akasema: “Mtafute mtu wa tatu pia.” Hisham akaamka na kutoka nje kumtafuta Mut’am bin Adi.

Alikutana nae na akamwambia: “Sidhanii ya kwamba ungalipenda kwamba yale makundi mawili (yaani Bani Hashim na Bani Muttalib) ya kizazi cha Abd Munaf, familia ambayo wewe nawe unayo heshima ya kuwa ndiyo familia zako, yafe.” Akajibu akisema: “Nifanye nini? Mtu mmoja hawezi kufanya lolote kwenye jambo hili.” Hisham akajibu: “Watu wawili nao wako pamoja nawe, nao ni mimi na Zuhayr.” Mut’am akasema; “Ni muhimu kwamba watu wengine nao washirikiane nasi.”

Kisha Hisham akalieleza jambo hili kwa Abul Bakhtari, na Zam’a pia, na kuwaomba washirikiane nao. Matokeo yake ni kwamba wote walikubaliana wakutane msikitini siku iliyofuata, asubuhi na mapema.

Mkutano wa Waquraishi hawa ulifanyika na Zuhayr na wasiri wake wal- ishiriki. Zuhayr akasema: “Inafaa tu kwamba leo Waquraishi washike usukani wa kuliondoa hili doa lenye kuaibisha. Ni muhimu kwamba huu mkataba wa kikatili ni lazima upasuliwe leo hii, kwa kuwa hali yenye kuhuzunisha ya watoto wa Hashim imefanya kila mtu akose raha.”

Abu Jahl aliyaingilia mazungumzo yale na akasema: “Mpango huu hautekelezeki hata kidogo na yale mapatano ya Waquraishi ni lazima yaheshimiwe.” Kutoka ule upande wa pili, aliamka Zum’a na kumwunga mkopno Zuhayr, akasema: “Ni lazima yapasuliwe, nasi hatukuyapendelea tangu mwanzoni.” Kutoka kwenye pembe nyingine, waliokuwa na shauku ya kwamba yale mapatano yakome, waliamka na kumwunga mkono Zuhayr. Abu Jahl akatambua ya kwamba jambo lile limefika kwenye hatua iliyo ngumu na kwamba ulifanyika ushauriano wa kabla, na kwamba watu wale walikuwa tayari walishachukua maamuzi yeye(Abu Jahl) akiwa hayupo.

Hivyo hakuushikilia msimamo wake na akakaa kimya. Mut’am aliitumia fursa ile na akaenda pale ilipokuwapo ile karatasi ya mapatano ili akaipasue. Hata hivyo, aliona ya kwamba karatasi lote limeliwa na mchwa, na ni yale maneno: “Kwa jina la Allah” (ambayo kwayo wale Waquraishi waliyaanza maandiko yao) ndiyo tu yaliyobakia.2

Baada ya kuyaona mabadiliko yale, Bwana Abu Twalib alimsimulia mpwa wake Muhammad jambo lile na matokeo yakawa kwamba wale waliokim- bilia kwenye bonde lile wakarejea majumbani mwao.3

  • 1. Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 350; na Tarikh-i Tabari, Juzuu 2, uk. 78.
  • 2. Siirah-i Ibn Hishamu, Juzuu 1, uk. 375; na Tarikh-i Tabari, Juzuu 2, uk. 79.
  • 3. Kauli yenye nguvu kwetu ni kuwa ni yeye mwenyewe Mtume ndiye aliyempa Abu Talib habari za kuliwa karatasi ile, naye akaenda moja kwa moja kwa Waquraishi kuwapa habari hiyo - Mhariri.