Sura Ya 25: Tukio La Kuhajiri (Kuhama)

Serikali ya watu wa Makkah ilifanana na serikali ya kikatiba. Darun-Nadwah yao ilikuwa kama baraza la ushauri ambamo viongozi wa makabila hukutana kwenye wakati wa hatari na wakabadilishana mawazo kwenye mambo magumu na kuchukua uamuzi wa pamoja.

Katika mwaka wa kumi na tatu wa utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) watu wa Makkah walikabiliwa na hatari kuu kutoka kwa Waislamu. Ilitishia uhai na uhuru wao. Kile kituo kikuu kilichoundwa na Waislamu mjini Yathrib na lile jukumu walilolibeba watu wa Yathrib kwa ulinzi wa Mtume (s.a.w.w.) vilikuwa dalili za dhahiri za tishio hili.

Katika mwezi wa Rabiul Awwal wa mwaka wa kumi na tatu wa Utume wa Mtume (s.a.w.w.), wakati kuhajiri kwa Mtume (s.a.w.w.) kulipofanyika, hakuna Mwislamu yeyote aliyesalia mjini Makkah isipokuwa Mtukufu Mtume, Ali na Abu Bakr na Waislamu wengine wachache waliokuwa wamezuiwa na Waquraishi au wale waliokuwa wazee au wagonjwa. Hata hivyo, ulikuwako uwezekano wa kila namna kwa watu hawa nao kutoka mjini Makkah na kwenda Yathrib. Wakati ule ule, kwa ghafla, Waquraishi waliuchukua uamuzi wa utata na wa hatari.

Ulifanyika mkutano wa ushauriano wa machifu kwenye Darun-Nadwah. Mtu mmoja kutoka miongoni mwao alizungumza tangu mwanzoni juu ya kukusanyika kwa majeshi ya Muhammad mjini Yathrib na yale mapatano yaliyofanywa na Bani Aws na Bani Khazraji. Baada ya hapo mtu yule aliongezea kusema: ‘Sisi watu wa Haraam, tulikuwa tukiheshimiwa na makabila yote.

Hata hivyo, Muhammad alipanda mbegu ya ugomvi na hivyo inatuletea hatari kubwa. Sasa tuishapoteza uvumilivu wetu wote. Njia pekee ya usalama wetu ni ule wa kwamba ateuliwe shujaa mmoja kutoka miongoni mwetu, na kwa siri, aumalizie mbali uhai wake. Na kama Bani Hashim wataamka kugombana nasi, tunaweza kuwalipa dia.”

Mzee mmoja asiyetambulika na aliyejitambulisha kuwa ni ‘Mnajdi’ alilikataa wazo hili na kusema: “Mpango huu hauwezi kutekelezeka hata kidogo, kwa sababu Bani Hashim hawatausaza uhai wa huyo mwuwaji wa Muhammad na kulipa dia hakutawaridhisha. Hivyo basi, yeyote ajitoleaye kuutekeleza mpango huu hana budi kwanza aanze kujitenga na maisha yake mwenyewe, na mtu wa aina hiyo hapatikani miongoni mwenu.”

Mmoja wa machifu aliyeitwa Abul Bakhtari akasema: “Jambo lililo bora ni kumfunga Muhammad na kumpa chakula na maji kwa kupitia kwenye tundu na hivyo tutaweza kuzuia kuenea kwa dini yake”. Yule mzee wa Najdi akazungumza tena: “Mpango huu nao si tofauti sana na ule wa kwanza, kwa kuwa kwa tukio hilo Bani Hisham watapigana vita dhidi yenu ili kumfungulia. Na hata wao wenyewe wasifaulu kulifikia lengo hili, wataomba msaada wa makabila mengine kwenye wakati wa Hajj na watamfungulia kwa msaada wao.”

Mtu wa tatu alitoa ushauri mwingine na akasema: “Ingalifaa kama tungal- imfanya Muhammad amrekebu ngamia mkaidi na kuifunga miguu yake yote miwili na kumfanya ngamia yule akimbie ili amgongegonge kwenye vilima na mawe na hivyo kuupondaponda mwli wake. Na kama kwa bahati uhai wake utabakia, na akashukia kwenye ardhi ya kabila jingine na akata- ka kuibalighisha dini yake miongoni mwao wenyewe, wale wenye kuyaabudu masanamu kwa shauku kuu, watalimaliza mbali jambo hili kuhusiana naye na watatuokoa sisi na wao wenyewe kutokana na fitna yake.”

Yule mzee wa Najdi aliukataa mpango huu tena na akasema: “Mnaitambua njia ya uzungumzaji wa Muhammad. Kwa maneno yake yenye kuvutia na kushinda kwa uzuri wake. Kwa hotuba zake tamu na ufasaha wa lugha, atayafanya makabila mengine yamuunge mkono na kisha atakurukieni.”

Utulivu kamili uliutawala mkutano mzima. Mara, kwa ghafla Abu Jahl, na kwa mujibu wa wasimulizi wengine, yule mzee wa Najdi mwenyewe, alilitoa wazo lake na akasema: “Njia pekee yenye kufaa na iliyo rahisi ni kwamba wateuliwe watu kutoka miongoni mwa familia zote na kwa pamo- ja waishambulie nyumba yake wakati wa usiku na kumkata vipande vipande, ili kwamba familia zote ziweze kuhusika na mauaji yake.

Ni dhahiri kwamba, katika hali hiyo, Bani Hashim hawataweza kulipiza kisasi dhidi ya familia zote.” Wazo hili lilikubaliwa na watu wote kwa pamoja na wale wauaji wakachaguliwa. Hivyo ikaamuliwa kwamba utakapoingia usiku wale watu waitekeleze kazi yao hiyo.1

Msaada Wa Kimungu

Hawa watu wenye vichwa vilivyoshanganyikiwa walikuwa wakifikiria ya kwamba, kama yalivyo mambo mengine ya kidunia, kazi ya Utume nayo ingaliweza kuteketezwa kwa mipango kama hii. Hawakuweza kutambua ya kwamba kama walivyokuwa mitume wengine, Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w.) alikuwa naye amejaaliwa kwa msaada wa kimungu, na ule mkono uliouhami huu mwenge uangazao kutokana na vimbunga vya ajali kwa miaka kumi na tatu, vile vile ungeweza kuvuruga mpango huu wa sasa wa maadui zake.

Kwa mujibu wa wafasiri wa Qur’anii Tukufu, Malaika Mkuu Jibrail alikuja na kumtaarifu Mtume (s.a.w.w.) juu ya ile makri ya uovu wa washirikina. Qur’anii inalizungumzia tukio hili kwa maneno haya: “Na walipokupangia mpango waliokufuru wakufunge, au wakuuwe au wakutoe. Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango.” (Sura al-Anfal, 8:30).

Mtume (s.a.w.w.) aliamrishwa na Allah kwenda Yathrib. Hata hivyo, haikuwa jambo rahisi kuiepuka mikono ya ukatili ya waabudu masanamu, hasa pale walipokuwa wakimpeleleza, na umbali baina ya Makka na Yathrib nao ulikuwa mrefu. Kama asingelitoka mjini Makka baada ya kupanga vizuri ingeliwezekana kwamba watu wa Makka wangelimkamata na kumtia kizuizini na kumuuwa kabla ya kuwafikia marafiki zake.

Wanahistoria na waandishi wa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.) wametoa maelezo tofauti tofauti juu ya kuhajiri kwa Mtume (s.a.w.w.) na tofauti zilizopo baina ya maelezo ya tukio hili hazina kifani. Mwandishi wa Siiratul-Halabi amefaulu kwa kiasi fulani katika kuyafanya hayo maelezo tofauti tofauti yaafikiane, lakini ameshindwa kuondoa tofauti katika baadhi ya sehemu.

Jambo lipasalo kuzingatiwa ni kwamba wengi wa wanachuoni wa hadith wa Kissuni na Kishia wamekuweka kuhajiri kwa Mtume (s.a.w.w.) katika njia ambayo mtu anaamua kwamba lilikuwa ni jaribio la kimiujiza ya kujiokoa na maadui, ambapo ukichunguza tukio hili kwa makini, itakufunukia ya kwamba kutoroka kwa Mtukufu Mtume kulikuwa ni matokeo ya uoni wa mbali wake, wa mpango wa kiuangalifu na hatua za tahadhari alizozichukua; na Allah Alipenda kumpa usalama kwa njia za kawaida na wala si kwa matendo ya kimuujiza.

Jambo lenye kutoa ushahidi juu ya maoni haya ni kwamba Mtume (s.a.w.w.) alitumia sababu za kawaida na njia za kiakili (kama vile kumfanya Sayyidna Ali (a.s.) alale kitandani mwake na yeye mwenyewe kujificha pangoni n.k na hivyo akajihakikishia usalama).

Malaika Mkuu Amwarifu Mtume (S.A.W.W).

Malaika Mkuu Jibriil alimwarifu Mtume (s.a.w.w.) kuhusu ule mpango mwovu wa makafiri na kumtaka ahajiri. Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha Sayyidna Ali (a.s.) alale kitandani mwake, na kupita kwenye majaribu ya hatari kwa ajili ya usalama wa Uislamu, ili kwamba makafiri wasidhanie ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) ameondoka, bali wasalie kwenye dhana ya kwamba alikuwa bado yumo mle nyumbani. Hivyo Sayyidna Ali (a.s.) alibakia mwenye kutosheka na kusalia mle nyumbani, ili kwamba yeye Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe aweze kupita kwenye mitaa ya mji wa Makka na kwenye viunga vyake kwa uhuru kabisa.

Faida iliyomo kwenye mpango huu ni kwamba maadui waliendelea kuilinda tu nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) na yeye mwenyewe kupata muda wa kufika sehemu ya usalama.

Sasa yatupasa tuone kwamba ni nani yule ajitoleaye kulala kitandani mwa Mtume (s.a.w.w.) na kuyatoa mhanga maisha yake? Bila shaka utasema: “Ni yule aliyemwamini kwanza na kumzunguka tangu siku ya kuteuliwa kwake kuishika kazi ya Utume, kama vile nondo wazungukavyo mshumaa.” Yeye ndiye apasikaye kufanya kafara kwenye njia hii na mtu yule mwenye kujitoa mhanga mwenyewe hasa ni Sayyidna Ali (a.s.). Hivyo, Mtume (s.a.w.w.) alimgeukia Sayyidna Ali (a.s.) na kumwambia: “Lala kitandani mwangu usiku huu na ujifunike lile shuka la kijani ninalotumia wakati wa kulala, kwa vile maadui wamefanya shauri la kuniua na hivyo basi, ni muhimu kwamba nihamieYathrib.”

Sayyidna Ali (a.s.) alilala kitandani mwa Mtume (s.a.w.w.) mapema usiku ule. Baada ya kupita robo tatu za usiku, watu arobaini waliizingira nyumba ile na kuchungulia kupitia kwenye tundu. Waliona hali ya nyumba ile kuwa ni ya kawaida na wakadhani ya kwamba yule mtu aliyelala kwenye kile chumba cha kulalia ni Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe.

Mtume (s.a.w.w.) aliamua kutoka mle nyumbani wakati maadui walipokuwa wameizingira katika pande zote, na walikuwa wakifanya mkesha kamili. Allah Mwenyezi alipenda kumwokoa yule kiongozi mkuu wa Uislamu kutoka makuchani mwa hawa watu wabaya. Mtume (s.a.w.w.) alizisoma zile aya za Surah Yasin zilizofaa katika hali yake ile katika wakati ule na baada ya kusoma hadi aya: “. . . . . hivyo hawaoni.” (Surah Yasin, 36:9), akatoka nyumbani mle upesi na kuelekea ile sehemu aliyodhamiria kwenda. Haieleweki vema jinsi Mtume (s.a.w.w.) alivyoweza kuyapita yale mazingira na ni kwa nini wale waliokuwa wakiizingira nyumba ile hawakuweza kumwona.

Tunajifunza kutoka kwenye Hadith iliyonukuliwa na mwanahadith maarufu wa Kishiah, marehemu Ali bin Ibrahim, alipokuwa akiifasiri aya isemayo: “Na walipokupangia mpango waliokufuru wakufunge, au wakuuwe au wakutoe. Wakapamga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango.” (Sura al-Anfal, 8:30), kwamba, Mtume (s.a.w.w.) alipotoka nyumbani mle, wote walikuwa wamelala, walitaka kuishambulia nyumba ile alfajiri nao hawakufikiria ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliutambua mpango wao ule.

Hata hivyo, wanahistoria wengine husimulia dhahiri2 kwamba wale maadui walibakia macho hadi ule wakati walipoishambulia nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) naye akatoka nje kimuujiza nao hawakuweza kumwona.

Hakuna shaka juu ya ukweli uliopo kwamba muujiza huo unawezekana. Lakini swali ni hili: “Je, muujiza huo ulikuwa muhimu kwenye tukio hili?” Udadisi wa hali hii ya kuhajiri unathibitisha ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliitambua makri ile ya madui kabla hawajaizunguka nyumba yake na ule mpango alioufanya ili kuweza kunusurika ulikuwa wa kawaida kabisa na haukuwa na chochote cha kimiujiza juu yake. Kwa kumfanya Sayyidna Ali (a.s.) alale kitandani mwake alitaka kujitenga na waabudu masanamu kwa njia ya kawaida na si kwa miujiza.
Hivyo, angeweza kuitoka nyumba ile kwa urahisi kabla ya kuzingirwa na hakuhitaji muujiza wowote katika lengo lile.

Hata hivyo, inawezekana kwamba Mtume (s.a.w.w.) kubakia nyumbani mle hadi ilipozingirwa ilikuwa ni kwa sababu tusizozifahamu kwa hivi sasa. Hivyo basi, mjadala juu ya jambo hili (la Mtume (s.a.w.w.) kuondoka nyumbani mle wakati wa usiku) haujafikia mwisho machoni mwa wanahistoria wote, kwa sababu, kwa mujibu wa baadhi yao, Mtume (s.a.w.w.) alitoka nyumbani mwake kabla ya kuzingirwa kwake na kabla ya kuchwa jua.3

Maadui Waishambulia Nyumba Ya Mtume (S.A.W.W.)

Askari wa ukafiri waliizingira nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) na walikuwa wakisubiri waamrishwe kuishambulia kwa ghafla na kumkata Mtume (s.a.w.w.) vipande vipande kwenye chumba chake cha kulala. Baadhi yao waling’anga’ania ya kwamba washambulie wakati wa usiku na kuutimiza mpango wao. Hata hivyo, Abu Lahab alisimama na kusema: “Wanawake na watoto wa Bani Hashim wamo nyumbani humo na hivyo, inawezekana kwamba wakadhurika wakati wa mashambulizi.” Wengine wanasema kwamba sababu ya kuchelewesha kwao ni kwamba walitaka kumwua Mtume (s.a.w.w.) kwenye mwanga wa mchana kabisa mbele ya macho ya Bani Hashim, ili wao (Bani Hashim) waweze kuona kwamba mwuaji wake hakuwa mtu maalum. Hatimaye waliamua kuutimiza mpango wao wakati wa alfajiri, kutakapokuwa na mwanga.4

Sasa imeshaingia alfajiri. Ghera na shauku vilionekana miongoni mwa makafiri. Walidhania ya kwamba wangeliweza kufikia lengo lao walilolidhamiria upesi sana. Mikono yao ikiwa kwenye mipini ya panga zao, waliingia ndani ya chumba kile cha kulala Mtume (s.a.w.w.) wakipiga makelele mengi. Wakati huo huo, Sayyidna Ali (a.s.) aliamsha kichwa chake kutoka kwenye mto wake, akaitupa kando shuka ya kijani na akasema kwa upole mno: “Kuna nini?” wakamjibu: “Tunamtaka Muhammad. Yuko wapi?” Sayyidna Ali (a.s.) akawajibu akisema: “Je, kwani mlinikabidhi Muhammad ili kwamba hivi sasa niwajibike kumrudisha kwenu. Hata hivyo, hayumo nyumbani humu hivi sasa.”

Nyuso za mawakala wale ziliwiva kwa hasira na makoo yao yakisongwa na jambo hili. Walijuta kwa kusubiri hadi alfajiri na wakamlaumu Abu Lahab aliyewazuia kufanya mashambulizi wakati wa usiku. Waquraishi wakazidishwa mshtuko kutokana na kuvunjika kwa mpango wao na kushindwa walikolazimika kukabiliana nako. Wakaanza kufikiria kwamba Muhammad asingeliweza kutoka nje ya mazingira ya mji wa Makka katika kipindi kifupi kiasi kile na wakaamua kwamba amejificha mahali fulani ndani ya mji wa Makka au alikuwa njiani akielekea Yathrib.
Hivyo, wakapanga wamkamate.

Mtume (S.A.W.W) Akiwa Kwenye Pango La Thaur

Ni ukweli uliothubutu kwamba aliutumia usiku wa kuhajiri pamoja na Abu Bakr (r.a) kwenye pango la Thaur, lililoko kusini mwa mji wa Makka (sehemu iliyo mkabala na mji wa Madina). Hata hivyo, haifahamiki ni vipi kufuatana huku kulifanyika na jambo hili halina maana ya dhahiri hata kidogo katika historia. Baadhi ya watu huamini ya kwamba kufuatana huku kulitokea tu kwa bahati na kwamba Mtume (s.a.w.w.) alipomwona Bwana Abu Bakar (r.a) njiani alimchukua akaenda naye.5

Wengine wanasema kwamba Mtume (s.a.w.w.) alikwenda nyumbani kwa Abu Bakr usiku ule na katika usiku wa manane wote wawili walitoka nyumbani mle na kwenda kwenye pango la Thaur. Kadhalika wengine wanasema kwamba Abu Bakr (r.a) alikuja kumuulizia Mtume (s.a.w.w.) na Sayyidna Ali (a.s.) alimuelekeza kwenye yale maficho yake.6

Vyovyote vile iwavyo, waandishi wa wasifa wa Mtume (s.a.w.w.) hukichukulia kitendo hiki cha kufuatana kuwa ni uthibitisho wa utukufu wa Abu Bakr (r.a) na hulinukuu tukio hili kwa umaarufu kuhusiana na ubora wake.7

Waquraishi Hawasiti Kumtafuta Mtume (S.A.W.W)

Kushindwa kulikowapata Waquraishi kuliwafanya wazibadili mbinu zao. Hivyo, wakaamua kuzifunga barabara zote, kuweka walinzi kwenye njia zote ziendazo Yathrib na pia kupata huduma za wenye uwezo wa kumtafuta mtu kwa njia ya nyayo zake, ili kwamba kwa njia hii, waweze kumpata Mtume (s.a.w.w.) kwa gharama zozote zile. Vile vile walitangaza ya kwamba yeyote yule atakayetoa taarifa sahihi kuhusu sehemu aliyojificha Muhammad atapata zawadi ya ngamia mia moja.

Waquraishi walishughulika na wakaenda upande wa kaskazini wa mji wa Makka na wakaenda barabara ielekeayo Madina, wakati ambapo Mtume (s.a.w.w.) ili kuuvuruga mpango wao, alijificha kwenye pango la Thaur. Abu Karz, mtaalamu wa kusoma tabia za watu kwa kuangalia tu, wa mjini Makka, alikuwa anazifahamu nyayo za Mtume (s.a.w.w.). Katika kumtafuta Mtume (s.a.w.w.) alifika karibu na pango lile na akasema: “Yaonekana kwamba Mtume alidhamiria kuingia kwenye sehemu hii. Inawezekana kwamba amejificha kwenye pango hili.” Hivyo, akamtuma mtu mmoja aingie pangoni mle.

Mtu yule alipolikaribia lile pango aliona utando mnene mno wa buibui umetandwa kwenye mlango wa pango lile na njiwa allikuwa ametaga mayai hapo.8 Alirudi bila ya kuingia pango lile na akasema: “Kuna utando wa buibui mlangoni mwa pango, jambo lionyeshalo kwamba hakuna mtu yeyote ndani yake.” Kazi hii iliendelea kwa muda wa siku tatu na mikesha mitatu na kisha Waquraishi wakapoteza matumaini yote na wakaacha kumtafuta.

Kujitoa Mhanga Katika Njia Ya Ukweli

Jambo muhimu zaidi kuhusiana na tukio hili ni kule kujitoa mhanga kwa Sayyidna Ali (a.s.) katika njia ya ukweli. Kujitoa mhanga kwa njia ya ukweli ni fadhila za wale waliounganishwa na jambo hili, watu wasio ujali uhai wao, mali zao na vyeo vyao, na wakatumia uwezo wao wa kiroho na kimaada kwa ajili ya kuuhuisha ukweli. Ni dhahiri kuwa watu hawa ndio wapenzi wa ukweli, na ukamilifu na matumaini wanayopata katika ufuatiliaji wake, yanawafanya wayatoe maisha yao haya yenye kupita na wayakumbatie yale yenye kudumu milele. Kulala kwa Sayyidna Ali (a.s.) kitandani kwa Mtume (s.a.w.w.) katika usiku ule wa vurugu ni mfano wa wazi mno wa huba yake juu ya ukweli. Hakikuwapo kichocheo chochote kingine kwa tendo hili la hatari ila ni mapenzi ya kuuhuisha Uislamu, ambao ni dhamana kwa ajili ya ustawi wa jamii.

Aina hii ya kujitolea mhanga ni yenye thamani mno kiasi kwamba Allah Mwenyezi amekuita mhanga uliofanywa kwa ajili ya kuitafuta radhi ya Allah na kama ilivyonukuliwa na wengi wa wafasiri wa Qur’ani, aya ifuatayo ilifunuliwa juu ya jambo hili: “Na miongoni mwa watu yuko ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Allah; na Allah ni Mpole kwa waja wake.” (Sura al-Baqarah, 2:207).

Ukuu na umuhimu wa kitendo hiki umewafanya watu mahodari wa Uislamu kukichukulia kitendo hiki kuwa ni moja ya fadhila kuu zaidi za Sayyidna Ali (a.s.) Amiri wa waumini, na wamemwelezea kuwa yu mtu shujaa na mwenye kujitolea mhanga. Na popote pale lilipotajwa tukio hili kwenye tafsiri ya Qur’ani na historia imekubaliwa kwamba aya tuliyoitaja hapo juu ilifunuliwa kuhusiana naye. Ukweli huu hauwezi kusahaulika. Daima sura ya ukweli inawaka kwenye boma za ndani zaidi za ushirikina na vipande vilivyotawanyika vya mawingu haviwezi kuizima nuru ya jua.

Uadui wa Mu’awiyah dhidi ya familia ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na hasa kwa Amiri wa waumini hauna hata haja ya kutajwa. Alipanga kuwahonga baadhi ya masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) ili kupata uwongo uliozushwa kwa lengo la kuzitia madoa kurasa za historia ziangazazo, lakini hakufaulu.

Samrah bin Jundab aliyeishi kwenye zama za Mtume (s.a.w.w.) na baadae akajiambatanisha na baraza la Mu’awiyah alikuwa na desturi ya kubadili mambo fulani fulani na alikuwa akilipwa kwa kufanya hivyo. Siku moja alipokuwapo mbele ya Mu’awiyah, Mu’awiyah alimwomba kwa bidii sana aipande mimbari na akane ya kwamba aya tuliyoitaja hapo juu haikufunuliwa kuhusiana na Sayyidna Ali (a.s.). Vile vile alimtaka awaambie watu kwamba kwa hakika aya hii ilifunuliwa kwa ajili ya muuwaji wa Sayyidna Ali (a.s.) (yaani Abdur Rahmani bin Muljam).

Kama tuzo yake kwa kitendo hiki ambacho kingaliweza kuivunja imani ya Samrah, Muawiyah alimuahidi kumpa dirham laki moja. Samrah hakukubali. Hivyo Muawiyah akakikuza kima kile na hatimaye biashara ile ikafanyika kwa dirham laki nne. Huyu mzee mroho akaanza kuyageuza mambo ya kihistoria kuwa uwongo na kuiharibu zaidi heshima yake iliyokuwa na madoa tayari. Mbele ya mkusanyiko mmoja alisema kwamba aya tuliyoitaja hapo juu ilifunuliwa kuhusiana na Abdurahmani bin Muljam na wala si kuhusiana na Saidiana Ali (a.s.).

Watu wajinga na wenye akili potovu waliyaamini yale aliyoyasema na haikutokea kwao ya kwamba wakati wa kufunuliwa kwa aya ile Abdur Rahmani hakuwako Hijaz na pengine alikuwa bado hajazaliwa. Hata hivyo sura ya ukweli haikufichikana kwa uzushi huu. Muawiyah na familia yake wakapatwa na matatizo ya mageuzi ya nyakati. Dalili za wale waliozusha uwongo kwenye wakati ule zilifutika.
Ukweli ukatawala tena. Wafasiri wakubwa na maarufu9 wa Qur’ani Tukufu na wanahadith wa zama zote wamekubali kwamba aya isemayo: “Na miongoni mwa watu yuko ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Allah; na Allah ni Mpole kwa waja wake.” (Sura al-Baqarah, 2:207) ilifunuliwa wakati wa ‘kukesha usiku’ juu ya kujitoa mhanga kwa Sayyidna Ali (a.s.).10

Maelezo Ya Ibn Taymiyah

Ahmad bin Abdul Halim Haraani aliyefariki kwenye jela ya Morocco katika mwaka 728 A.H. alikuwa mmoja wa wanachuoni wa Kisunni, na nyingi ya itikadi za Mawahabbi zinatokana naye. Yeye alikuwa na maoni maalum juu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), Sayyidna Ali Amiri wa Waumini (a.s.) na watu wengine wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) na ameziandika nyingi ya itikadi zake kwenye kitabu chake kiitwacho ‘Minhaajus Sunnah’. Kutokana na itikadi zake potovu, wengi wa maulamaa wenzake wa wakati uleule walimlaumu kwa uzushi na kuonyesha kuchukizwa kwao juu yake. Hata hivyo, mjadala juu ya mambo haya ni nje ya lengo letu.

Amesema jambo fulani juu ya sifa hii11 ambalo linaweza kuwekwa mbele yako pamoja na masahihisho kidogo. Wakati mwingine yaonekana kwamba watu wasio na uwezo wenye elimu haba au ya kijuu juu tu wanaathiriwa na maneno yake na wanayabalighisha maoni yake miongoni mwa watu wa kawaida bila ya uchunguzi na bila ya kutaka maoni ya wale wenye elimu pana juu ya jambo hilo, na kejeli iliyopo hapa ni kwamba watu wanaweza kuwachukulia wao kama ni wanachuoni watafiti. Hata hivyo, wao wanauona dhahiri ukweli uliopo kwamba maneno haya ni ya mtu mzushi yaliyokanushwa na wanadini wenzie na alishutumiwa kwa uzushi.

Anasema: “Kule kulala kwa Ali kwenye kitanda cha Mtume (s.a.w.w.) si fadhila juu yake, kwa kuwa Ali alijua kutokana na sababu mbili kwamba hatapatwa na madhara yoyote usiku ule. Kwanza, yalikuwa ni yale maneno ya Mtume (s.a.w.w.) ambayo yalikuwa kweli kabisa, kwa sababu usiku ule alimwambia: “Lala kitandani mwangu na hutapata madhara yoyote yale.” Na pili, Mtume (s.a.w.w.) alimpa vitu ambavyo watu waliviweka amana kwake, na kwa kawaida alijua ya kwamba mwakilishi wake hatauawa, kwani vinginevyo angalimpa mtu mwingine vitu hivyo. Na kutokana na mapendekezo haya, Ali yeye mwenyewe, naye alielewa kuwa hatapata dhara lolote na atafaulu kulitimiza jukumu alilopewa na Mtume (s.a.w.w.).

Majibu Kwa Tafsiri Hii Ya Uongo

Kabla ya kutoa majibu yenye maelezo marefu juu ya haya mambo mawili, tunaweza kusema kwa kifupi tu kwamba: “Kwa kuikana sifa moja Ibn Taymiyah atakuwa ameithibitisha sifa kubwa zaidi ya Sayyidna Ali (a.s.), kwa sababu itikadi yake juu ya ukweli wa Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa ni imani ya kawaida au ilikuwa ni itikadi yenye nguvu isiyo na kifani na maneno yote ya Mtume (s.a.w.w.) yalieleweka mbele yake.

Kwa mujibu wa dhana ya kwanza (yaani iwapo kama imani yake ilikuwa ya kawaida) itakuwa kwamba Sayyidna Ali (a.s.) hakuwa na ujuzi juu ya kusalimika kutokana na madhara yoyote. Hii ni kwa sababu maneno ya Mtume (s.a.w.w.) hayajengi ujuzi maalumu nyoyoni mwa watu kama hawa (na Sayyidna Ali a.s bila shaka hakuwa mmoja wao). Hata kama wakiyakubali maneno yake kuwa ni ya kweli bado husababisha uchungu mwingi nyoyoni mwao. Na kama wakilala kwenye sehemu yake wakati wa hatari mchafuko wao wa akili huzidi zaidi na kila mara kitisho cha mauti hutokea machoni mwao. Hivyo basi, kutokana na dhana hii alilitekeleza jukumu hili kwa mwezekano wa kuuawa na wala si kwa kujua ya kwamba atasalia salama.

Kwa mujibu wa dhana ya pili, Ibn Taymiyah ameithibitisha sifa kubwa zaidi ya Sayyidna Ali (a.s.), kwa sababu kama itikadi ya mtu ni thabiti mno kiasi kwamba maneno ya Mtume (s.a.w.w.) yanaeleweka wazi kabisa kwake na ubora wa itikadi kama hiyo unakipita kila kitu.

Basi matokeo ya itikadi ya aina hii ni kwamba, Mtume (s.a.w.w.) anapomwambia: “Lala kitandani mwangu hutapata madhara yoyote yale kutoka kwa maadui.”
Anakwenda kwa akili iliyotulia kabisa na analala kitandani mwake na aoni woga hata kidogo moyoni mwake. Na kama maoni aliyoyatoa Ibn Taymiyah (kwamba Saidina Ali a.s aliutambua usalama wake, kwa kuwa aliambiwa na Mtume (s.a.w.w.) aliye mkweli) yanakuwa uthibitisho wa itikadi ya daraja la juu kabisa, hana budi atambue ya kwamba bila ya kujitambua ameithibitisha hii sifa kuu kabisa ya Sayyidna Ali (a.s.).

Jibu Lenye Maelezo Ya Kina

Ama kuhusu hoja ya kwanza inaweza kusemwa kwamba sentensi isemayo: “Lala kitandani mwangu na hutapata madhara yoyote yale kutoka kwa maadui,” haikunakiliwa na mwanahistoria yoyote wa kutegemewa.12Bila shaka Ibn Athir (aliyefariki katika mwaka 630 Hijiria)13 na Tabari (aliyefariki dunia katika mwaka 310 Hijiriya)14 wameinukuu sentensi hii, lakini yaonekana kwamba wameipata kutoka kwenye Siiratu-Ibn Hisham15 aliyelinukuu jambo hili hivi - hasa kwa sababu maelezo ya wanahistoria hawa juu ya jambo hili, ni yale yale kabisa kama ya Ibn Hisham. Zaidi ya hapo, kwa kadiri tunavyotambua sisi, jambo hili halipatikani kwenye maandishi ya wanachuoni wa Kishia.

Shaykh Muhammad bin Hassan Tusi (aliyefariki katika mwaka wa 460 Hijiriyya) amelinukuu tukio hili la kuhajiri kwenye kitabu chake cha ‘Amaali’ kwa kirefu zaidi na pia ameitaja sentensi hiyo kwa mabadiliko madogo madogo. Hata hivyo, kile akizungumziacho ni tofauti na kile kilichonukuliwa kwenye maandishi ya wanachuoni wa Kisunni, kwa kuwa yeye ananakili wazi wazi kwamba ulipopita ule usiku wa kuhajiri, Sayyidna Ali (a.s.) na Hind bin Abi Hala (mwana wa Bibi Khadija na mwana wa kulea wa Mtume (s.a.w.w.) walikutana na Mtume (s.a.w.w.) katika mikesha iliyofuatia. Katika mmoja wa mikesha hiyo, Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Sayyidna Ali (a.s.): “Ewe Ali! Tangu sasa watu hawa katu hawataweza kukushinda nguvu.”

Kama itakavyoonekana, hivi karibuni ni sentensi ileile iliyonukuliwa na Ibn Hisham, Tabari na Ibn Athir. Hata hivyo, kwa mujibu wa nukuu za Shaykh Tusi, Mtume (s.a.w.w.) alimpa Sayyidna Ali (a.s.) uthibitisho huu katika usiku wa pili au wa tatu wala si kwenye usiku wa kwanza. Zaidi ya yote haya ni kuwa, maneno ya Sayyidna Ali (a.s.) mwenyewe ndio ushahidi ulio bora zaidi kwenye jambo hili. Kama ionekanavyo kwenye beti (zilizotafsiriwa hapa chini) yeye mwenyewe amekichukulia kitendo hiki kuwa ni aina fulani ya kujitoa mhanga katika njia ya ukweli:

“Kwa uhai wangu nilimlinda mtu aliye bora zaidi, aliyewahi kuitandika miguu yake katika ardhi, na mtu mtukufu aliyeifanya ‘Tawaf’ ya ‘Nyumba ya Allah’ na Hajar-i Isma’il.’ Mtu yule mtukufu ni Muhammad bin Abdullah. Nami nimefanya hivi wakati makafiri walipokuwa wakipanga makri dhidi yake. Katika muda ule, Allah Mtukufu alimhami dhidi ya makri yao.

Nilisalia kitandani mwake tangu usiku hadi alfajiri na nikaenda kuwasubiri maadui, na kujitayarisha kwa ajili ya kutekwa au kuuawa.” (Suyuti ameinukuu mistari hii kutoka kwa Sayyidna Ali (a.s.) kwenye tafsiri yake ya Qur’ani tukufu itwayo ‘Durr’ul-Manthur)

Mbele ya sentensi hizi zenye kujieleza na maelezo ya waziwazi hakuna haki tena ya kuyategemea maneno ya Ibn Hisham, kwa sababu ziko nafasi nyingine nyingi kwa yeye kufanya makosa. Na upo uwezekano mkubwa kwamba, kwa vile Ibn Hisham alipendelea kuyaelezea mambo kwa njia ya kuyabana, alitosheka na kuinakili sentensi yenyewe tu. Na kwa vile haikuwa na maana sana kwake, kuhusu ni lini sentensi hii ilitamkwa (ambapo kwa hakika sentensi hii ilitamkwa kwenye usiku wa pili) alidharau kuutaja ule wakati na akayaeleza mambo katika njia ionyeshayo kana kwamba matukio yote haya yalifanyika kwenye usiku uleule wa kuhajiri.
Ushahidi mwingine uthibitishao kauli hii ni ile Hadith maarufu iliyonukuliwa na wengi wa wanachuoni wa Kisunni na Kishia. Kwa mujibu wa riwaya hii, Allah aliwaambia wale Malaika Wakuu Jibriil na Mika’il kwenye usiku ule: “Kama nikiamua kumpa mmoja wenu uhai na mwingine nimpe kifo, ni nani kati yenu atakayekuwa tayari kukikubali kifo na kumwachia uhai mwenzie?” Hakuna yeyote kati yao aliyekubali mpango huu. Hapo Allah, Mwenyezi akasema: “Sasa Ali amekipendelea kifo na kautoa mhanga uhai wake kwa ajili ya Mtume.” Kisha akawaamrisha kushuka duniani na kuusimamiia usalama na ulinzi wa Ali.

Hoja nyingine aliyoitoa juu ya Sayyidna Ali kuwa alitambua hatima usalama wake ni ile amri aliyopewa na Mtume (s.a.w.w.) kuwarudisha kwa wenyewe vitu walivyoviweka amana kwake. Kufuatana na maoni yake, jambo hili laonyesha kwamba Mtume (s.a.w.w.) alijua ya kwamba Sayyidna Ali (a.s.) hatapatwa na madhara yoyote na hivyo basi, alimtaka avirudishe vitu vile. Hata hivyo, tunafikiria ya kwamba kama ukichunguza kwa makini ule mfuatano wa matukio, tatizo hili nalo laweza kutatuliwa. Na huu ufuatao hapa chini ndio ule mkondo wa matukio ya kuhajiri.

Mfuatano Wa Matukio Ya Hajira Ya Mtume (S.A.W.W)

Hatua za awali za kuponyoka kwa Mtume (s.a.w.w.) zilichukua sura ya kimatendo kwa msaada wa mipango. Mtume (s.a.w.w.) alikimbilia kwenye pango la Thaur wakati wa usiku na kuushinda mpango wa wale waliopanga makri dhidi yake. Hakuhisi mchafuko wowote wa akili, kiasi kwamba kwenye wakati mgumu alimfariji sahaba wake kwa maneno: “Usihuzunike. Allah Yu pamoja nasi.” Kwa siku tatu mchana na usiku walizifaidi baraka za Allah. Kufuatana na kauli ya Shaykh Tusi (kwenye kitabu chake ‘Amaali’) Sayyidna Ali (a.s.) na Hindi bin Abi Hala (mwana wa Khadija), na kwa mujibu wa wanahistoria wengi, Abdullah bin Abu Bakr na ‘Aamr bin Fuhayrah (mchungaji wa Abu Bakar) walikuwa na desturi ya kwenda kuonana na Mtume (s.a.w.w.).

Ibn Athr anaandika hivi:16 “Kwenye nyakati za usiku mwana wa Abu Bakar (r.a) alikuwa akimwarifu baba yake na Mtume (s.a.w.w.) juu ya uamuzi uliochukuliwa na Waquraishi, na mchungaji wake akiwapitisha mbuzi na kondoo wake karibu na pango lile walipokuwa wakienda Makka ili kwamba Mtume (s.a.w.w.) na yule sahaba wake waweze kuyatumia maziwa yao. Katika wakati wa kurejea kwake, Abdullah alikuwa akitangulia mbele ya kondoo wale ili kwamba nyayo zake ziweze kufuatwa na miguu ya wale kondoo.

Shaykh anasema katika ‘Amaali’: “Katika mmoja wa mikesha hiyo (baada ya usiku wa kuhajiri) wakati Sayyidna Ali na Hind walipopata heshima ya kufika mbele ya Mtukufu Mtume alimuamrisha Saidina Ali (a.s.) atayarishe ngamia wawili kwa ajili yao (yaani kwa ajili ya Mtume s.a.w.w na yule sahaba wake). Wakati uleule, Abu Bakr (a.s.) akasema: “Tayari nishatayarisha ngamia wawili kwa ajili yako na mimi mwenyewe.” Mtume (s.a.w.w.) akajibu akasema: “Niko tayari kuipokea zawadi hii kwa malipo.” Baada ya hapo alimwamrisha Sayyidna Ali (a.s.) alipe bei ya ngamia yule.

Miongoni mwa maelekezo aliyoyatoa Mtume (s.a.w.w.) usiku ule kwenye lile pango la Thaur baadhi yake yalikuwa haya: “Katika siku ya kesho yake Sayyidna Ali (a.s.) atangaze wakati wa mchana kabisa na kwa sauti kuu kwamba kama mtu yeyote kaweka amana kitu chochote kile kwa Muhammad au kama yeye (Muhammad) alikuwa akidaiwa na mtu yeyote yule, watu hao wahusikao waje wachukue vitu vyao.”

Kisha alitoa maelekezo kuhusu kuondoka kwa ‘Fawaatim’ (neno lenye maana ya binti yake mpenzi Bibi Fatimah a.s na Fatimah binti Asad na Fatimah bint Zubayr) na akamwamrisha Sayyidna Ali (a.s.) kuitayarisha safari yao pamoja na safari ya watu wengine wa ukoo wa Bani Hashim kwa kutegemea mwelekeo wao wa kuhajiri. Na kwenye tukio hili aliitamka sentensi aliyoitegemea Ibn Taymiyah kwa hoja yake ya kwanza. Alisema: “Ewe Ali! Tangu sasa watu hawa katu, hawataweza kukushinda nguvu.”
Kama uwezavyo kuona, Mtume (s.a.w.w.) alimwamrisha Sayyidna Ali (a.s.) kuvirudisha vitu vilivyowekwa amana kwake na watu, wakati ule ‘usiku wa mkesha’ umeishapita tayari. Amri hizi alizitoa akimpa Sayyidna Ali (a.s.) wakati yeye mwenyewe alikuwa akijitayarisha kutoka mle pangoni.

Halabi anaandika hivi: “Wakati usiku mmoja Ali alipokwenda mbele ya Mtume (s.a.w) kwenye Pango la Thaur, Mtume (s.a.w) akamwambia Ali pamoja na mambo mengine, kwamba awarudishie watu vitu walivyoviweka amana kwake (yeye Mtume s.a.w) na pia kuyalipa madeni yake.”

Kisha anayarudia yale maneno ya kwamba Ali hakukutana na Mtume (s.a.w.w.) baada ya ule usiku wa mkesha, lakini yeye mwenyewe halikubali hilo, na ananukuu kutoka kwa mwandishi wa kitabu ‘Ad-Durr al-Manthur’ kwamba Sayyidna Ali (a.s.) alikutana tena na Mtume (s.a.w.w.) baada ya usiku wa kuhajiri.17

Kwa kifupi, Shaykh Tusi amewanukuu wanachuoni wategemewao wakisema kwamba amri ya kuvirudisha vitu vilivyowekwa amana kwa Mtume (s.a.w.w.) kwa wenyewe ilitolewa na yeye Mtume (s.a.w.w.) baada ya ‘usiku wa mkesha’ hatuna haja kuyakana maelezo haya yaliyo sahihi na kujishughulisha katika kuwafurahisha watu.

Na kuhusu wale wanahistoria wa Kisunni kulinakili jambo hili katika jinsi ambayo kwa dhahiri hutoa dhana ya kwamba maelekezo yote yalitolewa na Mtume (s.a.w.w.) kwenye usiku mmoja ambao ni ule wa kuhajiri kunahitaji maelezo.

Kutoka Nje Ya Pango Lile

Kama alivyoelekeza Mtume (s.a.w.w.), Sayyidna Ali (a.s.) alipeleka ngamia watatu kule pangoni katika usiku wa nne pamoja na kiongozi wa kutumainiwa aliyeitwa ‘Urayqit’. Mtume (s.a.w.w.) aliisikia milio ya ngamia akatoka mle pangoni na yule sahaba wake. Waliwapanda wale ngamia na wakaondoka wakielekea Yathrib (Madina) kutoka upande wa chini wa mji wa Makka wakipitia njia ya pwani. Maelezo kamili ya safari hii yameandikwa kwenye vitabu vya historia.18

Ukurasa Wa Kwanza Wa Historia

Giza la usiku liliingia. Waquraishi waliokuwa wakizurura huko na huko mjini Makka na kwenye mazingira yake kumtafuta Mtume (s.a.w.w.), wakarudi majumbani mwao wakiwa wamechoka kabisa, na wakiwa wamepoteza matumaini yote ya kuipata ile zawadi kubwa sana (ya ngamia

100) iliyowekwa kwa ajili ya kumkamata Mtume (s.a.w.w.). Zile njia zinazoelekea Yathrib, zilizokuwa zimefungwa na wale walinzi waliowekwa na Waquraishi pia nazo zilifunguliwa19 Katika wakati huu, sauti ya chini ya yule kiongozi aliyekuwa na ngamia watatu na chakula iliyafikia masikio ya Mtume (s.a.w.w.) na sahaba wake. Alikuwa akisema kwa sauti ya upole: “Ni muhimu kujinufaisha na giza la usiku huu na kutoka nje ya eneo liwezalo kufikiwa na watu wa Makka upesi iwezekanavyo na kuichukua njia isiyopitiwa na watu mara kwa mara.”

Historia ya zama za Uislamu huanza kwenye usiku huu hasa. Tangu hapo waliweka tarehe za matukio yote kufuatana na kalenda ya Hijiriya na kuyaandika kwenye historia kwa mujibu wa tarehe hiyo.

Kwa Nini Ule Mwaka Wa Hijra Ukawa Ndio Mwanzo Wa Historia Ya Kiislamu?

Uislamu ni dini ya kimungu iliyo kamili zaidi nayo inafuata dini ya Mtume Musa (a.s.) na Isa (a.s.) katika mfumo kamilifu zaidi unaofaa katika hali na mazingira yote. Uislamu umemletea mwanadamu neema. Ingawa Nabii Isa (a.s.) na kuzaliwa kwake ni vitu viheshimiwavyo mbele ya macho ya Waislamu, hawakuchukua kuzaliwa kwake kuwa chanzo cha zama zao, kwa kuwa wao ni taifa huru na lenye kujipambanua na isingalifaa kwamba wawafuate watu wengine katika kutwaa zama zao.

Kwa kipindi kirefu mwaka wa Ndovu (mwaka ambao Abraha alikuja Makka na jeshi la ndovu na kutaka kuibomoa Ka’bah) ulitumiwa na Waarabu kuwa ndio chanzo cha historia, na kuzaliwa kwa Mtume (s.a.w.w.) nako kulitokea katika mwaka huo huo. Hata hivyo, Waislamu hawakuufanya mwaka ule kuwa ndio ukurasa wa kwanza wa historia ya Uislamu.

Mwaka wa Bi’that (kuteuliwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuishika kazi ya Utume) pia nao haukuchukuliwa kuwa mwanzo wa historia ya Waislamu, kwa sababu wakati ule hazikuwapo dalili za Uislamu na dini ya Kiislamu, na idadi ya Waislamu katika siku zile haikuzidi watatu. Hata hivyo, katika mwaka wa kwanza wa kuhajiri, Uislamu na Waislamu walineemeshwa kwa mafanikio makuu. Serikali huru ikapatikana mjini Madina.

Waislamu wakaondokana na kukosa maskani na kwa uhuru kabisa wakaweza kujikusanya katika sehemu muhimu. Hivyo basi, kutokana na mafanikio na ushindi huu, waliamua kuufanya mwaka ule kuwa ndio mwanzo wa historia yao.20 Na hadi hivi sasa, wao huhesabu tarehe ya kila kitu, kilicho chema au kiovu kufuatana na mwaka huo.

Mpango Wa Safari Ya Kwenda Yathrib

Safari ambayo ilibidi Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuichukua ilikuwa na umbali wa kiasi cha kilometa 400, na kuusafiri umbali huu kwenye joto kali la wakati wa kiangazi kulilazimu mpango ulio sahihi. Zaidi ya hapo, wao (yaani Mtume na masahaba zake) walikuwa pia wakiwaogopa Waarabu waliokutana nao njiani, kwani wangeliweza kuwapa Waquraishi taarifa za kule waliko, hivyo basi, walisafiri wakati wa usiku na wakapumzika wakati wa mchana.

Inaonekana kwamba mpanda ngamia mmoja baada ya kumwona Mtume (s.a.w.w.) na masahaba zake kwa mbali, aliwaendea Waquraishi upesi upesi na kuwaarifu juu ya njia ya safari ya Mtume (s.a.w.w.). Ili aweze kupata ile zawadi yeye peke yake, Saraqah bin Malik bin Ja’sham Madlaji aliwavunja moyo wenziwe katika kulifuatilia jambo lile na akawaambia kwamba wao (wale walioonwa na yule mpanda ngamia) walikuwa ni watu wengine. Kisha Saraqah akaja nyumbani mwake akazitwaa silaha zake, akampanda farasi mwenye mbio na upesi kwa kadiri ilivyowezekana akafika mahali alipokuwa amepumzika Mtume (s.a.w.w.) na sahaba zake.

Ibn Athir anaandika hivi:21 “Hali hii ya mambo ilimfanya yule sahaba wa Mtume (s.a.w.w.) ahuzunike mno, na ilimbidi Mtume (s.a.w.w.) amfariji tena kwa yale maneno: “Usihuzunike Allah Yu pamoja nasi.” Saraqah alijivunia mno nguvu zake za kimaumbile na silaha kali na alikuwa tayari kabisa kuimwaga damu ya Mtume (s.a.w.w.) ili aipate ile zawadi kubwa sana waliyoiweka Waarabu.

Wakati huo huo Mtume (s.a.w.w.) alijiombea yeye mwenyewe na masahaba zake kwa moyo uliokuwa ukibubujika imani na matumaini na kusema: “Ee Allah! Tuokoe kutokana na uovu wa mtu huyu.” Mara kwa ghafla yule farasi wa Saraqah akashtuka na kumtupa chini Saraqah kwa nguvu sana.

Saraqah alitambua ya kwamba mkono wa Allah ulikuwa ukifanya kazi na yale yaliyokuwa yakitendeka pale yalitokana na nia mbaya aliyokuwa nayo dhidi ya Muhammad.22

Hapo akamgeukia Mtume (s.a.w.w.) katika hali ya kumsihi na akasema: “Ninakupa mtumwa wangu na ngamia wangu na niko tayari kufanya lolote lile upendalo.” Hapo Mtume (s.a.w.w.) akamjibu akasema: “Sina chochote nikitakacho kutoka kwako.”

Hata hivyo marehemu Allamah Majlis anasema kwamba Mtume (s.a.w.w.) alimwambia: “Rudi na ukawazuie watu wengine na wasitufuate” Hivyo Saraqah alimwambia kila aliyekutana naye:
“Hakuna dalili zozote za Muhammad kwenye njia hii.”23

Waandishi wa Kisunni na Kishia wameinukuu miujiza iliyotendwa na Mtume (s.a.w.w.) wakati wa safari yake ya kutoka Makka kwenda Madina. Hata hivyo, ili kupunguza maneno, tunaacha kuisimulia.

Kuwasili Kwenye Kijiji Cha Quba

Kijiji cha Quba kilikuwa kiasi cha ligi mbili (kilomita 10 hivi) kutoka Madina. Kijiji hiki kilikuwa makao makuu ya Bani ‘Amr bin Auf’. Mtume (s.a.w.w.) na masahaba wake walifika kijijini hapa siku ya Jumatatu na akafikia nyumbani kwa Kulthum Ibnul Hadim, chifu wa kabila lile. Idadi fulani ya ‘Muhajir’ (wahamaji) na ‘Ansar (wasaidizi) walikuwa wakisubiri kuwasili kwa Mtume (s.a.w.w.).

Mtume (s.a.w.w.) alikaa kijijini pale hadi mwishoni mwa juma lile na katika wakati huu aliweka jiwe la msingi la msikiti kwa ajili ya kabila la Bani Awf. Baadhi ya watu walishikilia ya kwamba aendelee na safari yake ya kwenda Madina upesi iwezekanavyo. Hata hivyo, yeye alikuwa akimsubiri binamu yake Sayyidna Ali (a.s.) afike.

Baada ya kuhajiri kwa Mtume (s.a.w.w.) Sayyidna Ali (a.s.) alisimama mahali fulani mjini Makka na akasema: “Yeyote aliyeweka amana kitu kwa Muhammad na aje akichukue kutoka kwangu.” Wale waliohusika walikuja kuchukua vitu vyao baada ya kutoa maelezo ya utambulisho wa vitu vyao. Baada ya hapo, kufuatana na maelekezo ya Mtume (s.a.w.w.), Sayyidna Ali (a.s.) aliwachukua wanawake wa Bani Hashim na kwenda nao Madina ikiwa ni pamoja na Bibi Fatimah (a.s.), binti wa Mtume (s.a.w.w.) na mama yake Bibi fatimah bint Asad, na vile vile wale Waislamu ambao hadi wakati ule, walikuwa bado hawajaweza kuhama. Sayyidna Ali (a.s.) aliifuata njia ya ‘Dhi Tuwa’ na akaelekea Madina wakati wa usiku.24

Shaykh Tusi anaandika hivi:25 “Wapelelezi wa Waquraishi walipata habari za kuhajiri kwa Sayyidna Ali (a.s.) na kikundi chake. Hivyo wakamfuata na wakakutana naye uso kwa uso kwenye eneo la ‘Zajnaan’. Walibadilishana naye maneno makali. Wakati ule vilio vya wanawake vilifika angani. Sayyidna Ali (a.s.) alitambua ya kwamba hakuwa na uchaguzi wowote mwingine ila kuihami heshima ya Uislamu na Waislamu. Hivyo basi, aliwageukia wale wapinzani wake na akasema: “Yeyote apendaye kwamba mwili wake ukatwe vipande vipande na damu yake imwagwe, basi na ajitokeze.” Dalili za ghadhabu ziliweza kuonekana usoni mwake. Wale mawakala wa Waquraishi walihisi kwamba sasa jambo lile lishakuwa zito. Hivyo, wakachagua kufanya mapatano na wakaishika njia waliyoijia (wakarudi makwao).”

Ibn Athir anaandika hivi: “Ali alipofika Quba, miguu yake ilikuwa ikitoka damu. Mtume (s.a.w.w.) alielezwa kwamba Ali amefika, lakini hakuwa katika hali ya kuweza kufika mbele yake.

Mtume (s.a.w.w.) alikwenda upesi kule alikokuwa Ali na akamweka mapajani mwake na alipoiona hali ile ya miguu ya Ali ilivyovimba alianza kutiririkwa na machozi machoni mwake”.26 Mtume (s.a.w.w.) alifika Quba tarehe 12 Rabiul-Awwal na Sayyidna Ali (a.s.) alijiunga naye hapo katikati ya mwezi huo huo.27

Maoni haya yanaungwa mkono na Tabari kwa kusema hivi: “Ali alibakia Makka kwa muda wa siku tatu baada ya kuhajiri kwa Mtume (s.a.w.w.) na katika kipindi hiki aliwarudishia watu vitu vyao walivyoviweka amana (kwa Mtume (s.a.w.w.).28

Makelele Na Hoihoi Za Shangwe Mjini Madina

Kulikuwa na msisimko na shangwe miongoni mwa watu waliomwamini Mtume (s.a.w.w.) miaka mitatu ilioyopita na kumpelekea wawakilishi wao kila mwaka na kulitumia jina lake takatifu kila siku kwenye sala zao, pale walipopata taarifa ya kwamba kiongozi wao mkuu amefika kiasi cha mwendo wa ligi mbili tu na alitegemewa kuingia mjini mwao karibuni. Jinsi fikara na hisia zao zilivyokuwa, haziwezi kuelezwa kwa maneno.

Ansar walikuwa na kiu ya Uislamu na mpango wake mtukufu na wenye kuimarisha. Ili kuutoharisha mji wa Madina kutokana na ibada ya masanamu walikuwa wameshayachoma masanamu na kuziondoa dalili zote za ibada ya masanamu kutoka majumbani, mitaani na katika masoko ya mjini mle. Ingalifaa kama tungalinukuu hapa mfano wa moyo wa kupenda waliouonyesha Ansar katika Uislamu.

‘Amr bin Jumuh, aliyekuwa mmoja wa machifu wa kabila la Bani Salmah, alikuwa kaweka sanamu nyumbani mwake. Ili kumfanya atambue kwamba sanamu la mti ni kitu kisicho na faida yoyote, wanaume wa kabila lake walilichukua na kulitupa chini kwa kulipindua pindua juu chini; chini juu, katika shimo ambalo siku zile lilikuwa likitumika kwa kwendea chooni. Aliamka asubuhi yake na baada ya kulitafuta sana aliliona sanamu lile kwenye lile shimo. Aliliokota, akalisafisha na akalirudisha mahali pale. Mchezo huu ulirudiwa rudiwa kwa mara nyingi. Mwishowe ‘Amr aliufunga upanga shingoni mwa sanamu lile na akasema: “Kama wewe ndiwe chanzo cha nguvu yoyote ile hapa ulimwenguni, basi jihami.”

Hata hivyo, siku moja alilikuta sanamu lile kisimani likiwa limefungwa kwenye kiwiliwili cha mbwa aliyekufa, nalo halikuwa na ule upanga. Alipoyaona matukio haya, alitambua ya kwamba cheo cha mwanadamu kilikuwa kikuu zaidi kuliko kwamba yeye ainamishe kichwa chake mbele ya jiwe, mti au matope. Kisha akasoma beti fulani ambazo lengo lake ni hili: “Ninaapa kwa jina la Allah! Kama wewe ungelikuwa u mungu wa kweli, usingalilala kisimani ukiwa umefungwa kwenye mzoga wa mbwa. Sifa zote njema zamstahiki Allah Ambaye anamiliki neema zote. Yeye ndiye Mwingi wa rehema na Mwenye kustawisha na Mwenye kulipa thawabu. Yeye ndiye atupaye wokovu kabla ya kupelekwa kwetu kaburini.”29
Mtume (s.a.w.w.) aliendelea na akaingia Madina. Aliposhuka kutoka juu ya ngamia wake mahali paitwapo Thaniyatul Widaa’ na mnyama yule akauweka mguu wake kwenye ardhi ya Yathrib, watu wakamkaribisha kwa mikono miwili na kumsalimu na wakaanza kuimba nyimbo za furaha wakisema:

“Mwezi umechomoza kutoka ‘Thaniyatul Widaa’. Ni wajibu wetu kuwa wenye shukrani kwa baraka hizi hadi katika siku ambayo hakuna hata mtu mmoja usoni mwa ardhi asiyemwomba Allah na kumabudu. “Ewe uliyeletwa na Allah kwa ajili ya mwongozo wetu! Ni muhimu kwetu sisi sote kuzitii amri zako.”

Kabila la Bani ‘Amr bin Awf lilishikilia ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) abakie pale Quba, na wakasema: “Sisi ni watu wenye bidii nyingi, madhubuti na mashujaa.” Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) hakulikubali hilo. Wakati watu wa makabila ya Aws na Khazraji walipotambua kuhajiri kwa Mtume (s.a.w.w.) walichukua silaha na wakaharakisha kwenda kumpokea Mtume (s.a.w.w.).

Alipokuwa akiendelea na safari yake watu walimzunguka ngamia wake na machifu wa makabila wakazishika hatamu zake.

Kila mmoja wao alishikilia kwamba Mtume (s.a.w.w.) akae kwenye eneo lake, lakini aliwajibu wote akisema: “Musimzuie huyu ngamia. Mimi nitashuka popote pale atakapopiga magoti.” Yule ngamia alisimama na kukunja magoti yake kwenye uwanja mpana uliokuwa mali ya wavulana wawili yatima walioitwa Sahl na Suhayl waliokuwa wakiishi chini ya ulinzi na ulezi wa As’ad bin Zurarah30 Uwanja huu ulikuwa ukitumika kwa kukaushia tende na kilimo, nyumba ya Abu Ayub ilikuwa karibu na uwanja huu.

Hivyo basi mama yake (Abu Ayub) akaitumia nafasi ile na akaichukua mizigo ya Mtume (s.a.w.w.) nyumbani kwake. Hivyo yakaanza mashindano na maombi ya kumchukua Mtume (s.a.w.w.), hata hivyo, yeye aliyamaliza mashindno yale na akasema: “Iko wapi mizigo yangu?” aliambiwa kuwa ilichukuliwa na mama yake Abu Ayub na kuipeleka nyumbani kwake. Hapo akasema: “Mtu na aende kule iliko mizigo yangu.” Na As’ad bin Zurarah alimchukua ngamia wa Mtume (s.a.w.w.) na kumpeleka nyumbani kwake.

Mbegu Ya Mfarakano

Abdullah bin Ubay anachukuliwa kuwa yu chifu wa msonge wa madaraka wa wanafiki. Kabla ya watu wa Madina kufanya mapatano na Mtume (s.a.w.w.) waliamua kumchagua Abdullah bin Ubay kuwa mtawala wao kwa wote pamoja. Hata hivyo, kutokana na kuendelea kwa uhusiano baina ya Mtume (s.a.w.w.) na Aws na Khazraji, uamuzi huu ulikoma, na tangu hapo Abdullah akawa na mfundo dhidi ya huyu kiongozi mkuu wa Uislamu naye hakumwamini hadi kwenye dakika za mwisho za uhai wake. Alipoyaona yale mapokezi aliyopewa Mtume (s.a.w.w.) na watu wa makabila ya Aws na Khazraji, alipatwa mno na wasiwasi na hakuweza kujizuia kuitamka sentensi yenye kukidhihirisha kabisa kijicho na uadui wake dhidi ya Mtume (s.a.w.w.). Aliugeuzia uso wake kwa Mtume (s.a.w.w.) na akasema: “Nenda kwa wale watu waliokupokea na usitudanganye sisi hapa.”31

Sa’ad bin Ubadah, akichelea ya kwamba Mtume (s.a.w.w.) atayachukulia maneno yake kuwa ya kweli (yaani kuyaona kuwa ndio hisia za Ansar wote) au kuyaweka moyoni, aliomba radhi kwa maneno yake yale na akamwambia Mtume (s.a.w.w.): “Ameyazungumza maneno haya kutokana na mfundo na kijicho, kwa sababu iliamuliwa ya kwamba awe mtawala pekee wa Aws na Khazraji na sasa, kutokana na kuja kwako, utawala wake umekuwa si jambo lenye kufikiriwa tena”

Kwa ujumla wanahistoria wanasema kwamba Mtume (s.a.w.w.) aliwasili Madina mnamo siku ya Ijumaa na akaisali sala ya Ijumaa pamoja na masahaba zake mahali palipokuwa kwenye eneo la watu wa kabila la Bani Saalim.
Hapa alitoa hotuba yenye ufasaha iliyoibua hisia kali nyoyoni mwa watu ambao hawajapata kuyasikia maneno ya namna hiyo hapo kabla. Maandiko na hotuba hii yamenukuliwa na Ibn Hisham,32 Miqrizi kwenye Amtaa’ul Asmaa’ na Allamah Majlisi.33 Hata hivyo, maneno na maelezo yaliyomo kwenye hotuba hiyo, kama yalivyonakiliwa awali ni tofauti na yale yaliyonukuliwa na Allamah Majlis.

 • 1. Tabaqaatul Kubraa, Juzuu 1, uk. 222 -228; na Siirah-i Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 480 - 482
 • 2. Tabaqaatul Kubraa, uk. 228; na Tarikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 100.
 • 3. Siiratu Halabi, Juzu 2, uk. 32.
 • 4. A'lamu wara, uk. 39; na Bihaarul An'waar, Juzuu 19, uk. 50.
 • 5. Rai hii ndio tuichaguayo sisi, kwani ikumbukwe kuwa kuhama kwa Mtume (s.a.w.w.) kulikuwa ni siri nzito ambayo haikupasa kabisa maadui angalau kuweza kuinusa ukiachia mbali kuigundua, hivyo uzito wa siri ulipasa kuafikiana na uzito wa hatari, na kwa mantiki hiyo ilipasa siri hii aijue yule tu aliye mwaminifu kwa mujibu wa wahyi, naye si mwingine ni Ali (a.s.). Hivyo kwetu sisi rai hii ndio yenye nguvu - Mhariri.
 • 6. Ta'rikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 100.
 • 7. Lakini waweza kupima kati ya ubora huo utokanao na kitendo cha kusuhubiana na Mtume pangoni, na ule utokanao na kitendo cha kuchukua nafasi ya Mtume kitandani kwake ili adui anayekusudia kumuuwa Mtume amuuwe yeye kwa kud- hani yule aliyelala pale ndiye Mtume. Bila shaka wa pili ni bora zaidi mara dufu kuliko wa kwanza - Mhariri.
 • 8. Tabaqaatul-Kubra, Juzuu 1, uk. 229 n.k. wengi wa waandishi wa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.) wameunukuu muujiza huu. Hata na yale tuliyokwisha kuyasae- ma juu ya miujiza kuhusiana na masimulizi juu ya Abraha haionekani kwamba ni jambo lenye kufaa kwamba bila ya kuwapo haja yoyote ile tuelezee au tusahihishe silsila hii ya muujiza.
 • 9. Kwenye Sharh-i Nahjul Balagha ya Ibn Abil Hadid fadhila hii ya Sayyidna Ali (a.s.) imetajwa kwa maneno yenye kufaa (kwenye Juzuu 13, uk. 262.)
 • 10. Samrah bin Jundab alikuwa mmoja wa watenda majinai wa zama za Bani Umayyah. Hakuyabadili mambo kwa kadiri tulivyoitaja hapo juu tu, bali kama ilivyoelezwa na Ibn Hadid aliongeza mambo fulani fulani kwenye habari hizo na akasema kwamba kile hasa kilichofunuliwa juu ya Ali kilikuwa ni aya hii ifuatayo: "Na miongoni mwa watu yuko yule ambaye kauli yake kuhusu maisha ya dunia hii inakustaajabisha, naye humshuhudilisha Allah yale yaliyomo moyoni mwake, na hali yeye yu mpinzani mkubwa zaidi" (Sura al-Baqarah 2:204.)
  Kwenye zama za ugavana mkuu wa wa Ziyaad bin Abih nchini Iraq, Samrah alikuwa gavana wa Basrah. Moja ya majinai ya mtu huyu ni kwamba aliua Waislamu na wachamungu wafuasi wa nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) elfu nane. Na Ziyaad alipotaka maelezo yake na alipomwuliza: "Vipi wewe ulipata moyo wa kuwauwa watu wote hawa? Je, haikupita akilini mwako ya kwamba inawezekana kwamba miongoni mwao wamo watu wasio na makosa?" Samrah alijibu akisema "Sitajali kuuwa hata zaidi yao hawa." Matendo yake yaaibishayo ni mengi mno kiasi cha kutoweza kuwekwa kwenye kurasa hizi. Mtu huyu mkai- di alikuwa ndiye yeye yule aliyeyakataa maagizo ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) juu ya kuziheshimu haki za jirani, na Mtume (s.a.w.w.) alimwambia: "Wewe ni mtu mwenye madhara na Uislamu hauruhusu ya kwamba mtu awatendee wenzi- we madhara au ayavumilie madhara kutoka kwao."
 • 11. Kabla yake Jahiz aliitaja sehemu tu ya ukanusho huu kwenye kitabu chake kiitwacho ‘Al-Uthmaniyah'. Tafadhali rejea juu ya jambo hili kwenye Sharhi Nahjul Balagha, cha Ibn Abil Hadid, Juzuu 13, uk. 262.
 • 12. Kwa mfano sentensi hii haikutajwa mwenye Tabaqaatul Kubra uk. 227 - 228. Mwandishi wake alizaliwa katika mwaka 168 Hijiriya na akafariki dunia katika mwaka 238 Hijiria. Maqrizi nae hakuitaja mwenye kitabu chake. 'Al- Imta'a'.
 • 13. Tarikhul Kamil, Juzuu 2, uk. 72.
 • 14. Tarikhut- Tabari, Juzuu 2, uk. 99.
 • 15. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 483.
 • 16. Tarikhul Kamil, Ibn Athir, Juzuu 2, uk. 73.
 • 17. Siiratu Halabi, Juzuu 2, uk. 37.
 • 18. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 491; Tarikhul Kamil, juzuu 2, uk. 75 na mwenye maelezo ya chini ya ukurasa ya Ta'rikh Ibn Athir.
 • 19. Ta'rikhut-Tabari, Juzuu 2, uk. 104.
 • 20. Ibn Waazih Akhbari anaandika mwenye kitabu chake cha Historia kiitwacho 'Ta'rikhu Yaqubi' kwamba kwenye mwaka wa 16 wa Hijiria khalifa wa pili alid- hamiria kuweka mwanzo wa historia ya Waislamu. Alitaka iwe ile tarehe ya kuza- liwa Mtume (s.a.w.w.) au tarehe ya kuteuliwa kwake kuishika kazi ya Utume, lakini Ali (a.s.) hakukubaliana na maoni yake na akasema kwamba kuhajiri kuwe ndio mwanzo wa historia ya Kiislamu. (Ta'rikh Yaqubi, juzuu 2, uk. 135.)
 • 21. Ta'rikh Kamil, juzuu 2, uk. 74.
 • 22. Wengi wa waandishi wa wasifu wa Mtume (s.a.w) kama vile Ibn Athir (Tarikh Kamil, Juzuu 2, uk. 74) na Majlis (Bihaar Anwwar, Juzuu 9, uk. 88) wamelinuku tukio hili, kama tulivyolielekeza hapo juu, kutokana na asili yake itegemekayo. Hata hivyo, mwandishi wa 'Hayatu Muhammad' anasema: "Saraqah aliyachuku- lia matukio haya kuwa ni ndege mbaya na akafikiria ya kwamba miungu ilikuwa ikitaka kumzuia asiitende kazi ile.
 • 23. Bihaar Anwar, Juzuu 19, uk. 75.
 • 24. Baadhi ya wachambuzi wetu waaminifu hawakubaliani na kauli hii ya Imam Ali (a.s.) kuhama kwa msaada wa giza la usiku, na hivyo kiakili na kihistoria wanathibitisha ya kwamba alihama mchana peupe na kwa tangazo la wazi dhahiri shahiri bila kuficha kuwa yeye anahama kumfuata Mtume (s.a.w.w.), na yeyote awezaye kumzuia basi aweze kujitokeza kujaribu hilo. Ni kweli kabisa hiyo ndio hali ya kawaida ya yule simba wa Mungu asiyeshindwa, na ndio kauli yenye nguvu kwetu -Mhariri.
 • 25. Amaali, uk. 300.
 • 26. Tarikhul-Kamili, Juzuu 2, uk. 75.
 • 27. Imtaa'ul Asmaa', uk. 48
 • 28. Tarikhut-Tabari, Juzuu 1, uk. 106.
 • 29. Usudul Ghabah, Juzuu 4, uk. 99.
 • 30. Bihaarul Anwaar, Juzuu 19, uk. 108, lakini kwa mujibu wa baadhi ya vitabu, ikiwa ni pamoja na Tarikh-i Kamil, walikuwa chini ya ulezi wa Mu’aaz bin ‘Afraa’.
 • 31. Bihaarul Anwaar, Juzuu 19, uk. 108.
 • 32. Siiratu Ibn Hisham, Juzuu 1, uk. 500-501.
 • 33. Bihaarul Anwwar, Juzuu 19, uk. 126.