Sura Ya 30: Baada Ya Shahada Ya Husein.

Hata baada ya Husein na wapenzi wake wote na ndugu zake walipokuwa wamekutana na vifo vyao vya kishahidi, uonevu wa Yazid, bin Ziyad na vibaraka wao haukufikia mwisho. Ni zile namna tu za ukandamizaji na uonevu ndizo zilipata mabadiliko; mauaji yalibadilishwa na unyang’anyi, kuchoma mali moto na kuning’iniza vichwa vya mashahidi kwenye ncha za mikuki.

Wanawake wa familia ya Husein, iliyokuwa salama kutokana na ufedhuli na kushushiwa heshima wakati wa uhai wa Husein, walikuwa sasa wanaondolewa hata stara za nguo walizozitumia kufunika vichwa vyao, na wanaachwa kukutana na matusi mengi na walichukuliwa kutoka sehemu na kupelekwa sehemu nyingine kama wafungwa wa kawaida tu.

Maiti ya Husein iliibiwa kilemba chake, shati lake, shuka yake kutoka Yemen, na nguo zake za ndani ambazo alikuwa amezivaa kwa mara ya mwisho.

Upanga wake pia ulichukuliwa. Kisha jeshi lilifanya uporaji na unyang’anyi kwenye mahema yaliyokuwa na wanawake wa familia1 ya Husein ambao kutoka kwao walinyang’anya hata nguo ambazo zilifunika vichwa vyao.2

Kisha mahema yaliwashwa moto, na askari kumi waliopanda farasi walikanyaga juu ya maiti ya Husein chini ya kwato za farasi wao.3 Kichwa cha Husein kilichokatwa kilikuwa cha kwanza kupelekwa kwa Ibnu Yazid kupitia kwa Khawali bin Yaziud al-Asbahi. 4

Kisha vichwa vya baadhi ya mashahidi wengine vilipelekwa kwake pia. Miongoni mwa watu wa al-Husein waliopona alikuwa ni mwanawe aliye kuwa mgonjwa, Ali bin Husein, baadhi ya wanawake na baadhi ya watoto.

Tarehe 11 Muharram, 61 A.H Umar bin Sa’d aliizika miili ya watu wa jeshi lake, baada ya kukamilisha taratibu zote za mazishi. Hata hivyo, aliziacha maiti za Husein na wafuasi wake bila kuzikwa na bila kushughulikiwa kwa jambo lolote.

Wakati wa jioni aliwachukua watu waliobakia wa familia ya Husein kama wafungwa kuwapeleka Kufa na vile vichwa vya mashahidi ambavyo vilikuwa bado havijapelekwa kwa Ibn Ziyad vilichukuliwa pia na majeshi. Ilikuwa ni baada tu ya majeshi ya Yazid yalipoondoka kwenda Kufa kwamba maiti za mashahidi zisizokuwa na vichwa zilizikwa na baad- hi ya watu wa kabila la Banu Asad ambao waliishi karibu ya Karbala.

Vichwa vya mashahidi vilikabidhiwa kwa Ubaydullah bin Ziyad huko Kufa na kwa dharau na jeuri aliichokoachokoa midomo na meno ya Husein kwa fimbo.

Hili lilimuudhi sana Zayd bin Arqam, Sahaba wa Mtume, ambaye alikumbuka kuwahi kumuona Mtume akiibusu midomo hiyo na meno hayo. Kisha Zayd alianza kulia. Ubaydullah bin Ziyad alisamehe kutokumtolea amri ya kuuawa kwa sababu ya uzee wake.

Kabla ya kuwasili hapo Kufa kwa msafara huo wenye kuhuzunisha wa watu wa Husein waliobaki na kuporwa, ilitolewa ilani kwamba mtu yeyote asije akatoka nje ya nyumba yake, na askari doria walipelekwa kwenye sehemu mbalimbali kwa sababu ya wasiwasi fulani maalum.

Wengi wa watu waliamini kwamba wafungwa ambao kwa ajili ya kuwasili kwao sehemu ya sokoni ilipambwa, walikuwa wanawake wa maadui wa Uislamu walioshindwa, na idadi kubwa ya watazamaji walikuwa ni wenye furaha. Hata hivyo, baadhi yao walikuwa wamejawa na huzuni kwani walikwishaujua ukweli.

Vichwa vya mashahidi, vilivyotungikwa juu sana kwenye ncha za mikuki, viliwaongoza wafungwa wanaotokana na familia ya Mtume wakati msafara ulipoingia Kufa. Mwanamke mmoja ambaye alikuwa akilishuhudia hadhara hii kutoka juu ya ghorofa ya nyumba yake, aliwauliza wafungwa kuhusu familia zao na alipotambua kwamba walikuwa dhuria wa Mtume, yeye na watu wote wa kundi la watazamaji walilia na kuomboleza kwa sauti kubwa.

Ali bin Husein, kwa sauti dhaifu na ya kutetema aliwaambia watu, “Ni nyinyi ndiyo ambao mmemwaga damu yetu, na sasa wanawake wenu wanalia machozi juu ya msiba wetu. Mwenyezi Mungu ataamua kati yenu na sisi.” Umati huo, uliposikia maneno haya walishusha pumzi na wakalia sana kwa sauti za juu zaidi.

Katika hatua hii Zainab aliuhutubia mkusanyiko wa wanaume wengi akise- ma, “… Enyi watu wa udanganyifu na utapeli! Nyinyi mnalia? Kamwe Mwenyezi Mungu asikatishe machozi yenu. Nazisinyamazishwe sauti za vilio vyenu vya maombolezo.
Je, mnalia na kupiga mayowe kikweli katika kuomboleza? Kwa kweli ni vyema kwenu nyinyi kwamba mngelia zaidi na kucheka kidogo zaidi.

Je, mlijaribu kamwe kugundua ni kiasi gani mmeupasua moyo wa Mtume wa Mungu, mlivyowaweka wanawake waheshimiwa wa familia yake katika sura ya wageni, na kuwatukana? Je, mnastaajabishwa kwamba mbingu ilimwaga machozi? Hili si chochote kabisa ikilinganishwa na adhabu katika maisha yajayo ambayo kwa kweli itakuwa kali sana.

Kisha hakutakuwepo mtu yeyote yule wa kukusaidieni. Msifurahie muhula huu mfupi. Mwenyezi Mungu hana haja ya kufanya haraka kwani hatambui kwamba Angekosa nafasi ya kukuadhibuni. Bila shaka yeyote ile atakuachieni wenyewe mlivyo kwa muda kidogo.”

Imeelezewa kwamba wakati wa kutolewa hotuba hii yenye kugusa hisia, wote waliokuwepo walibakia wametingishwa mno na wote walikuwa wanalia. Kwa hotuba ya Zainabu, Bashir bin Huzaym al-Asad alisema, “Kamwe sijawahi kumwona mwanamke, ambaye ameishi katika faragha, akatoa hotuba yenye nguvu kama hii. Ilionekana kana kwamba baba yake, Ali bin Abi Talib ndiye alikuwa anatoa hotuba fasaha. Aliunyamazisha umati wa watu kwa ishira ya mkono wake na utulivu wa dhati ukapatikana hapo.

Kisha watu walihutubiwa na Fatimah bint Husein na Umm Kulthumu bint Ali na Ali ibn Husein. Hutuba hizi zilifungua macho ya wenyeji wa Kufa, na kuvunjavunja udanganyifu wa kuduwaza wa Bani Umayyah walioumwaga kwa watu wa Kufa.

Kisha Ibn Ziyad aliamuru kwamba wale wanusurika wa Husein waletwe kwenye Baraza lake. Ile tabia ya kijeuri na dharau ambayo kwayo amekitendea kichwa cha Husein, na uathirikaji wa Zayd bin Arqam kuhusu hilo umekwisha elezewa tayari. Baada ya kuuliza kwake, Zainab alitambulishwa kwa Ibn Ziyad, na majibizano yafuatayo yalitokea baina yao.

Ibnu Ziyad: “Mwenyezi Mungu ashukuriwe kwamba amekudhalilisheni, amekuuweni na kuufichua uwongo wenu.”

Zainab: Sifa zote njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu swt., ambaye ametunuku heshima juu yetu sisi pamoja na Muhammad mteuliwa, na ambaye ametutangaza sisi kuwa tohara, kama tohara yenyewe iwezavyo kuwa madai ya haki. Sisi hatuko kama usemavyo. Ameaibika na kudhalilika yule ambaye ni mwenye dhambi na mchafu. Uwongo umefichuliwa wa yule ambaye siku zote haiweki haki mbele kama lengo lake. Ni wengine, na siyo sisi, ndiyo watu wa namna hiyo.”

Ibnu Ziyad: Je, umeona ni kitu gani Mungu amekifanya kwa ndugu yako (Husein) na ndugu wengine?”

Zainab: “Nimeona kwamba Mwenyezi Mungu amewafanyia upendeleo tu. Walikuwa ni watu wateule wa Mwenyezi Mungu ambao walikuwa wamepangiwa kupata Shahada. Walikwenda kwenye madhabahu ya kuji- toa mhanga maisha yao kwa miguu yao wenyewe. Siku haiko mbali sana ambapo mtakapokuja kukabiliana nao mbele ya Mwenyezi Mungu kujibu makosa yenu mabaya na maovu.”

Ibn Ziyad: “Mungu ametimiza matakwa ya moyo wangu kwa kumuangamiza ndugu yako mpinzani na ndugu zako wengine wasiotii amri na walio waasi.”

Zainab: “Ndiyo, kwa hakika umewaua jamaa zangu, ndugu na marafiki. Kama hili limetosheleza matamanio yako basi jifurahishe nalo.”

Kisha Ubaydullah aligeukia kwa Ali bin Husein, na alipokuwa hakupata lolote lile lililokuwa zuri zaidi katika mahojiano aliamuru auawe. Zainab akamng’ang’ania mpwa wake na akataka auawe pamoja naye.

Ibnu Ziyad alitulia na akamuacha Ali bin Husein ambaye alitoa hotuba ifuatayo yenye maneno ya kukumbukwa kwake:
“Usijaribu kunitishia kwa kifo. Je, hujui kwamba kuuawa ni katika njia yetu na kwamba shahada (kujitoa mhanga) ndiyo sifa yetu.”

Akijisikia kuabika sana, Ibn Ziyad alivunja baraza kwa siku hiyo, akaamuru wafungwa wawekwe katika hali ya umateka mpaka kurudi kwa mjumbe wake kutoka Damascus, na kwamba raia wote wa hapo Kufa wakusanyike ndani ya msikiti mkuu wa mji, ambamo humo alipopanda katika mimbari alifanya rejea za kumuumbua na kumshushia mno hadhi yake Ali bin Abi Talib. Abdallah bin Afif, mmoja wa Shi’a wa Kufa, ambaye alipoteza macho yake yote mawili, wakati akipigana kwa ajili ya Ali katika vita mbalimbali, alisimama na akampinga Ibn Ziyad na akamkemea kwa ukali.

Aliamuriwa kukamatwa lakini askari mia saba watokanao na kabila lake walimwokoa na wakamchukua na kumpeleka nyumbani kwake. Hata hivyo, bila ya huruma aliuawa usiku uleule.

Siku iliyofuatia, kichwa cha Husein kilitembezwa katika eneo la sokoni kikatundikwa na kuning’inizwa katika mlango uingiao katika jumba la utawala wa Ibn Ziyad.5

Amri zililetwa kwa Yazid kwamba wafungwa wapelekwe Damaski. Ubaydullah bin Ziyad alielekeza kwamba kichwa cha Husein, kinyanyuliwe na kuwekwa juu sana katika ncha ya mkuki, kizungushwe katika mji na halafu vichwa vyote vya mashahidi vipelekwe Damascus.

Wanawake walipandishwa juu ya ngamia, na Ali bin Husein, bila kuridhika au kutaka na akiwa ametwikwa mnyororo mzito wa chuma kuzunguka shingo yake yote, aliwafuata chini ya ulinzi na uangalizi wa Shimr na Muhaffiz bin Thalaba al-Aidhi.6

Katika safari yake ya kwenda Damascus msafara huu wenye bahati mbaya wa familia ya Mtume ulipitia katika miji mingi na maeneo mengine yanayokaliwa na watu na katika sehemu chache sana maandamano ya watu wenye hasira yalifanyika kutokana na udhalilishaji waliofanyiwa wanusurika wa al-Husein, na hisia nzito za huzuni zilionyeshwa juu ya mauaji ya Husein na ndugu na wasaidizi wao.

Baada ya kupatwa na mateso makubwa sana, wanusurika wa Husein wali- ingia mjini Damascus wakati wa alfajiri.

Maduka makubwa ya mji yalipambwa makusudi kwa jambo hilo, na umati wa watazamaji ulikuwa mkubwa kiasi kwamba haikuwezekana mpaka wakati wa mchana ndipo msafara huu wenye kusikitisha ulipofikia jengo kubwa la kiutawala la Yazid.

Ibn al-Qiftii ameandika kwamba wakati vichwa vya mashahidi pamoja na familia ya Mtume walipokuwa wakisindikizwa kwenda kuiingia mji wa Damascus, Yazid alikuwa anawangalia kuingia kwao kwenye mlango wa jumba la kiutawala akiwa sehemu iitwayo Yahrum, na mara tu alipoviona vichwa vya mashahidi, alikariri aya ambazo kwazo fikra au wazo muhimu lilikuwa kwamba alifikiria ameyaweka mambo sawa na Mtume.

Ukumbi wa hadhara wa Yazid ulikuwa umepambwa makhususi kwa ajili ya jambo hilo na alikuwa anajishughulisha na uchezaji bao. Watu wa famil- ia ya Mtume walifikishwa kwa Yazid kama watumwa na wajakazi kutoka nchi ya Uhabeshi (Ethiopia) au Dailam au kutoka miongoni mwa Waturuki.

Maelezo ya kupotosha kabisa ya vita vya Karbala yalitolewa na Sahr ibn Qays, wakati ambapo Yazid alikuwa akisoma katika hali ya kuwa amelewa beti zenye maana ya: “Ingekuwa, kwamba wahenga wangu waheshimiwa waliopigana vita vya Badr wangeshuhudia jinsi gani vile wafuasi wa imani (dini) ya Muhammad walivyotupwa katika kuchanganyikiwa kwa michomo ya mikuki, hapo tena wangenisalimu kwa kunibariki, na pengine wangesema, ‘Tunaomba kamwe Yazid asipatwe na ugonjwa wa kupooza.’
Watu wa ukoo wa Bani Hashim walitumia kucheza mchezo wa hila kuupata utawala. Kwa kweli, hakuna habari za pepo au moto zilizokuja kwao, wala hakuna wahyi wowote ule uliteremshwa.”

Alipoyasikia maneno haya, Zainab alianza kutoa hotuba nzito ya kuvutia kufichua unyonge wa misingi ambamo juu yake utawala na mamlaka ya Yazid yalimojengewa. Alisema: “Ukweli ulioje ambao Mungu wangu ameueleza kwamba watenda mabaya hatimaye huja kubatilisha na kudhihaki alama za Mwenyezi Mungu.

Ewe Yazid, unafikiria kwamba kwa vile umetuzuia sisi milango yote, katika mbingu na juu ya ardhi, na umetushusha kwenye hali ngumu ya wafungwa, basi hata mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu sisi pia tumedharaulika, na wewe ni mheshimiwa, au kwamba kufaulu huku kusiko na mashiko halisi umekupewa kutokana na kuwa uko karibu na Mungu?

Ukiwa mwenye furaha kwa fikra hii huwa umetazama mabegani mwako kwa vile kwa sasa hivi unaona tu kwamba ulimwengu unanyenyekea chini ya amri zako, mambo ya nchi yako yakiwa katika mpango na hali nzuri, na utawala wako na serikali yako imewekwa katika usalama kutokana na hatari zote. Je, umesahau onyo la Mwenyezi Mungu lisemalo:

Makafiri wasilichukulie hili, kwamba muhula tunaowapa utawafaa chochote. Tunawapa muda ili kwamba waweze kujitumbukiza wenyewe katika kutenda dhambi mpaka kutosheka kwa mioyo yao, kwani mwishowe, adhabu yenye kufedhehesha imekwishaandaliwa kwa ajili yao.’

Je, ubora wa hali ya taadhima ya Kiislamu inakutaka wewe kuhifadhi faragha ya wanawake wenu na hata vijakazi wenu na kuwafunga wajukuu wa kike wa Mtume wako na kuwafanya wakimbie huku na huko na kupenda wapigwepigwe mabegani na wahenga wenu makafiri?

Usijisahau, kwani kipindi kifupi sana kijacho na wewe pia yatakutokea haya. Kisha utatamani sana kwamba mikono yako ingelikuwa imeondolewa uwezo wa kufanya kazi na ulimi wako kunyimwa uwezo wa kuongea, kwamba usingefanya yale ambayo umeyafanya na kwamba usingesema yale ambayo umeyasema.

Ni kipi kitakachokuwa kibaya zaidi kuliko kitu kingine katika Siku ya Hukumu, Mwenyezi Mungu atakuwa msuluhishi wa suala lako hili, Muhammad, mteule atakuwa ndiye mlalamikaji (kwa Mwenyezi Mungu) na (Malaika) Jibril atakuwa shahidi yake.

Kisha watafuatia pia wale ambao wamewasaida na wakashirikiana pamoja nanyi katika matendo yenu maovu na wakakuungeni mkono katika kuyapora madaraka (utawala) juu ya Waislamu, tambua jinsi kilivyo kikali kisasi kinachochukuliwa na Waislam juu ya madhalimu na wakandamizaji.

Ingawaje mabadiliko yaliyosababishwa na wakati yamenishusha hadi kwenye hali isiyotamanika ya kufanya nikuhutubie mtu kama wewe usiye na maana kabisa kama ulivyo mbele ya macho yangu, naliona hili kama sehemu ya balaa kubwa hata kule kukukemea tu, lakini nashindwa kujizuia mwenyewe. Huruma kubwa iliyoje kwamba wale ambao wanamwabudu Mwenyezi Mungu wapaswe kukutana na vifo vyao kwenye mikono ya makundi ya watu mashetani!

Ewe Yazid, kama unakula kiapo cha kufanya juu chini au kutoacha juhudi yoyote ile bila kufanywa, naapa kwa Mwenyezi Mungu hutaweza kufunika kumbukumbu zetu, wala kufutilia mbali kuwepo kwetu duniani, wala kufanikiwa katika kuharibu lengo letu halisi. Doa la umwagaji damu huu wa dhulma litabakia kwako mpaka Siku ya Mwisho na kamwe hutaweza kulisafisha kabisa.

Uamuzi wako hapana shaka yoyote ni ukaidi, maisha yako ni mafupi sana, na kundi la wale wanaokuzunguka kila upande litatoweka kabisa hivi karibuni. Siku imekaribia wakati itakaponadiwa, ‘Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.’ Shukurani zote ni kwa Mwenyezi Mungu ambaye amehukumu kwamba mwisho wa watangulizi wetu watukufu wa kuheshimika upaswe kuwa katika wema, na wenye baraka nyingi, na ile roho ya muadhama wetu wa mwisho kutoka katika shahada na rehema Zake. Yeye peke yake anatutoshelezea sisi na ndiye nguzo yetu bora na msaada wetu.”

Kisha Yazid aligeukia kwa Ali bin Husein, na ili amuumize hisia zake, alikariri aya ya Qur’ani, yenye maana, “Msiba wowote ule unakutokeeni ni kutokana na matendo yenu wenyewe.” Ali bin Husein akamwambia yeye kwamba aya hiyo haikumhusu yeye na kundi lake na kwamba aya ya Qur’ani ambayo ilimhusu yeye na wafuasi wake ilikuwa ni tofauti na hii nayo ina maana ya kwamba msiba ambao uliwapata ulikuwa ni katika kutimiza neno lililowekewa ahadi ambalo lilikuwa limeandikwa tokea mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, na ambalo kutimizwa kwake kulikuwa ni lazima.

Akichukulia kwamba hakuna mtu yeyote ambaye angekuwa na ujasiri wa kuudhishwa na utovu wa adabu wowote ule ambao angeuonyesha kwenye kichwa cha Husein hapo Damascus, aliyarudia yale Ibn Ziyad aliyoyafanya kule Kufa.

Aliigusa midomo na meno ya Husein kwa fimbo. Abu Barza al-Aslami mara moja akamkumbusha Yazid kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alitumia kuibusu midomo na meno ya Husein, na akaongeza kusema kwamba katika Siku ya Hukumu ni Ibn Ziyad tu pekee ndiye ataomba shifaa kwa niaba ya Yazid.

Hatua ilifikia wakati Yazid alitambua kwamba kila mtu katika baraza lake mwenyewe alimfikiria kwamba ana hatia. Katika jaribio lake la kujitetea, mbali na kuufichua uharibifu wake mwenyewe wa tabia na upotofu, alikubali kujifanya ameguswa sana na ulevi wa mafanikio kiasi cha kutoka kwenye sera za tangu zamani za Bani Umayyah za kuwaficha watu na kuwasahaulisha juu ya familia ya Mtume. Aliwauliza watu, “Je mnajua kwa nini janga limempata Husein?

Ni kwa sababu tu Husein alifikiria kwamba baba yake, mama na babu yake walikuwa bora zaidi kuliko baba yangu, mama na babu yangu. Sasa masuala haya yamewekwa sawa na ukweli wa kwamba wakati baba yake alipopigana dhidi ya baba yangu, ulimwengu unajua ni kwa manufaa ya upande wa nani uamuzi wa vita ulipotangazwa.

Ni kweli, hata hivyo kwamba mama yake alikuwa bora zaidi kuliko mama yangu na pia kwamba babu yake alikuwa bora zaidi kuliko babu yangu kwani hakuna Mwislamu awezaye kumfikiria mwingine yeyote yule kuwa sawa na Mtume.

Hata hivyo, walipotosha maana ya aya ya Qur’ani, wakimaanisha kwamba Mwenyezi Mungu ni Mola wa Ufalme na utawala. Humpa ufalme yeyote amtakaye na kumnyima ufalme yule amtakaye. Humtukuza amtakaye na humtweza yule amtakaye. Hakika, yeye ni mwenye uwezo juu ya kila kitu.”

Ingeonekana kutoka kwenye hotuba hii kwamba kuwa na sifa ambazo humtunukia heshima, Yazid aliikubali hali ya udhalili wake kwa Husein. Aliegemeza hoja yake ya mwisho kuthibitisha ubora wake juu ya ule wa Husein kwa kigezo cha kushinda na kuchukua madaraka. Hoja hii pia ingetumika kwa madhalimu na watesaji wengine wa wanadamu wenye kufahamika kuthibitisha uadilifu wao na kutokuwa na hatia kwao. Aya hiyo haifanyi mafanikio ya ushindi na kuchukua madaraka (utawala) kuwa vigezo vya uadilifu.

Yahya bin al-Hakam, mmoja wa Bani Umayyah, alikuwa amesikitishwa mno kwa maovu yaliyofanywa dhidi ya Husein na watu wengine wa famil- ia ya Mtume kiasi kwamba alianza kuonyesha huzuni yake waziwazi kutokana na kifo cha kishahidi cha Husein na kumsema vibaya Ubaydullah bin Ziyad pale hadharani. Yazid alimpiga Yahya kifuani mwake kwa mkono wake na akasema; “Je, hutanyamaza kimya?”7

Mke wa Yazid, Hind bint Abdallah bin Amir aliingia haraka sana mle barazani kwake huku akilia na kuomboleza akisema, “Ole, kichwa cha kipenzi cha Fatimah, binti ya Mtume, katika hali mbaya ya kuhuzunisha hivi.”

Watu wa Husein waliosalimika vitani hawakupelekwa haraka nyumbani kwao Madina, bali walibakia kwa muda mrefu katika hali ya umateka hapo Damascus.
Yazid aliwaachia huru na aliwapatia nyumba wakati tu alipoona dalili za kuongezeka kwa hali ya wasiwasi na kutoridhishiwa na utawala wake kulipojidhihirisha katika nchi na Bani Umayyah wakagundua makosa yao ya kisiasa. Kisha wanawake wa familia zilizochaguliwa wali- waendea wanawake wa familia ya Husein kwenda kuwapa pole na kuwafariji kutokana na vifo vya mashahidi, na maombolezo yakafanyika kwa muda wa siku tatu.

Al-Numan bin Bashir al-Ansar ambaye alikuwa ameondolewa kwenye ugavana wa Kufa kwa kutokumtendea Muslim bin Aqil ukatili baada ya kuwasili kwake pale Kufa, sasa alielekezwa kupanga kuwapeleka Madina watu wa Husein waliosalimika vitani kwa uangalizii unaostahili na kwa taadhima. Yazid aliwapeleka watu wake thelathini pamoja na al-Numan bin Bashir ambaye aliwatendea jamaa wa familia ya Mtume kwa heshima, taadhima na wema katika safari yote ya kwenda Madina.

Hii ilikuwa ni sehemu ya jaribio la Yazid lisilofanikiwa, la kujaribu kutaka kujikosha na kosa la mauaji ya Husein na sahaba zake na ndugu zake. Akiongea na Ali bin Husein katika faragha, alisema, “Mungu amlaani mwana wa Marjana kama ningewahi kukutana na baba yako moja kwa moja, ningelikubali kila jambo ambalo alikuwa amelipenda na kamwe nisingeridhia kifo chake. Vyovyote vile, lile ambalo limekadiriwa na Mungu limetokea. Sasa waweza kwenda Madina, fanya mawasiliano na mimi na nijulishe nijue ni kitu gani unahitaji.” 8

Jambo ambalo halijawahi kutokea katika uzito na urefu wa muda wake, lilikuwa ni vilio na maombolezo ambayo yalitokea katika mji wa Madina wakati wa kuwasili kwa msafara wa watu wa Husein waliosalimika katika vita.

Mwanamke atokanaye na familia ya Abdul Muttalib, nywele zake zikiwa timtim, alikuwa akikariri ibara zenye maana, “Jibu gani mtakalotoa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu wakati atakapokuulizeni katika Siku ya Hukumu, ‘Vipi mliwatendea dhuria wangu baada yangu?’ Wao sasa hivi wameshushwa katika hali kama hii kwamba baadhi yao ni mateka, na wengine katika wao, damu yao ilimwagwa chini na wamefunikwa na vumbi. Je, haya yalikuwa ndiyo malipo ya huduma zangu kwamba mpaswe kuwatendea kizazi changu katika mtindo huu?”9

  • 1. Akhbar al-tawal, uk. 256.
  • 2. Tabari, juz. 6, uk. 260
  • 3. Tabari, juz. 6, uk. 261-262 na Irshad, uk. 258.
  • 4. Akhbar al-Tawal uk. 256.
  • 5. al-Irshad, uk. 260.
  • 6. Tabari, juz. 6, uk. 264 al-Irshad, uk. 260.
  • 7. Tabari, juz. 6, uk. 265.
  • 8. Tabari, juz. 6, uk. 269/al-Irshad, uk. 263.
  • 9. Tabari, juz. 6, uk.221