Jinsi Yazid Alivyotawalishwa

Kabla ya Yazid kutawala katika mwaka wa 60 BH, Waislamu walitawaliwa na babake aliyekuwa akiitwa Muawiya bin Abi Sufyan. Wote wawili hao, babake na babu yake, walisilimu kwa kukosa budi baada ya Makka kutekwa na (kabla ya hapo) baada ya kuongoza upinzani mkali dhidi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na kushindwa.

Huyo Muawiya ndiye yule aliyesimama kumpinga na kumpiga vita "Khalifa wa Nne" (Imam Ali bin Abi Talib a.s.) alipochaguliwa na Waislamu kuwa Khalifa wao; na baada ya Imam Ali (a.s) kuuliwa, akaingia kumpinga na kumpiga vita Imam Hasan (a.s) (ndugu yake Imam Hussein a.s.) ambaye, anavyotuambia Sheikh Abdalla S. Farsy, aliuliwa "kwa sumu" na yeye huyo Yazid tunayeambiwa kuwa ati ni "Amiirul-mu’minin"! (Tizama uk. 24 wa kitabu chengine cha Sheikh Abdalla S. Farsy kiitwacho Maisha ya Sayyidna Hassan (chapa ya 1999) kilichochapishwa na Adam Traders wa Mombasa vile vile).

Lakini kwa kiasi cha miaka kumi kabla ya kupawa hiyo sumu, Imam Hasan (a.s) na Muawiya, babake Yazid, baada ya vita vikali, walifanyiana suluhu na kuandikiana mkataba. Kati ya waliyokubaliana katika mkataba huo, anavyotueleza tena Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 16 wa kitabu chake hicho, ni kwamba Imam Hasan (a.s) amwachie Muawiya Ukhalifa. Lakini Muawiya akifa, basi Imam Hasan (a.s) ataukamata yeye. Na lau Imam Hasan (a.s) atakufa, basi ushikwe na Imam Hussein (a.s).

Kuona hivyo, Sheikh Abdalla S. Farsy anaendelea kutueleza katika uk. 24 wa kitabu chake hicho hicho cha Maisha ya Sayyidna Hasan, "akili ilimjia (Yazid) akaona kuwa huu ufalme wa baba yangu utanipotea kwani akifa baba yangu atatawala Hasan, wala haikuandikwa kuwa akifa nitatawala mimi. Akaona amuue kwa sumu. Akapeleka watu madhubuti kwa siri kwa mke wa mwisho wa Sayyidna Hasan, wala hakuzaa naye, akiitwa Jaada bint Ash-ath. Wamtumainishe kuwa akimuua huyu mumewe atamuoa Yazid na tangu sasa atampa dirham laki moja, na mengineyo makubwa kabisa anayoyataka. Bibi akavutika akampa sumu kali kabisa huyo mumewe. Akasononeka muda wa siku arbaini; kisha akakata roho hali ya kuwa shahidi…"

Na katika uk. 18 wa Maisha ya Sayyidna Hussein, Sheikh Abdalla S. Farsy anasema: "Kabla ya kufa Sayyidna Hasan … Muawiya aliona ajifungue na ahadi ya kumtawalisha Al-Hasan wala hana ahadi ya kumtawalisha mwengine. Basi aliona amfanye mwanawe anayempenda zaidi, naye ni Yazid, awe waliyyul ahdi (heir-apparent). Itangazwe kwa raia wote kuwa akifa yeye hakuna uchaguzi wowote ila kuwa mwanawe, Yazid ndiye Khalifa tu. Akiridhia Hasan asiridhie na mwengine yeyote yule akiridhia asiridhie." Akamalizia kwa: "Maliwali wake wengine, kwa ajili ya kutaka kujipendekeza ili waendelee na Uliwali wao walimtia nguvu katika fikira hii ijapokuwa siyo ya Uislamu…"

Baada ya Imam Hasan a.s. kufa kwa ile sumu, Muawiya alipanga mikakati yake ya kumtawalisha mwanawe (Yazid). Lakini, hata hivyo, haikuwa rahisi. Anavyosema Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 18 wa kitabu chake, Maisha ya Sayyidna Hussein, ni kwamba "aliona ni uzito kabisa kutaka kulivunja jambo hili, sharti alichukulie mbinu kwa taratibu, akaona awafundishe Maliwali wake watoe fikira hii, isiwe imetokana na yeye. Akawaambia walisemeseme wenyewe tu huko katika nchi wanazoziendesha kama mchezo tu hivi kwanza."

Baada ya hapo, aliwakusanya wote mahali pamoja na, kama alivyowafundisha, ikawa mmoja baada ya mmoja husimama na kupendekeza utawala aachiwe Yazid. Lakini hata hivyo, si wote walimkubalia Muawiya; wengine walipinga; mmoja wao akiwa Al Ahnaf bin Qays. Huyu, Sheikh Abdalla S. Farsy anatuambia (uk. 20 wa hicho kitabu chake), alisema hivi: "La! Sisi watu wa Iraq sote si radhi kwa haya, na watu wa Hijaz wote pia hawawafiki. Hatumridhii kattu Yazid kuwa Khalifa wa Waislamu. Na wewe unamjua zaidi mwanao, kuliko watu wengine, kuwa hafai. Usijitwike mzigo wa kukutia Motoni kwa khiyari yako. Sisi haturidhii ila kizazi cha Ali.”

Mambo yakakorogeka. Sheikh A. S. Farsy anasema (uk. 20): "Akainuka Abu Khunayf akatoa upanga wake akamwonyesha Muawiya akamwambia 'Asiyekubali mlishe huu atashika adabu yake'. Akainuka Muawiya akasema, 'Huyu ndiye khatibu barabara. Khatibu vitendo si maneno tu. Na huyu ndiye bora wa wote waliohudhuria hapa na wengineo'. Baraza ikavunjika."

Bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume s.a.w.w., aliposikia habari hiyo, Sheikh A. S. Farsy anaendelea (uk. 21), "alikasirika sana sana kuona vile; Muawiya anazivunja zile ahadi alizompa Sayyidna Hasan…"

Mambo yakamalizikia hapo, yasiende mbele zaidi. Lakini baada ya muda (mwaka wa 50 BH), Muawiya alikwenda Madina, asemavyo Sheikh A. S. Farsy (uk. 21), "kugonga gogo asikie vipi mlio wake". Huko alikutana na "watoto wa kisahaba wenye jina kubwa kabisa"; nao ni mabwana "Abdulla bin Abbas bin Abdul Muttalib (hakuwaita ndugu zake), Abdulla bin Jaafar bin Abi Talib bin Abdil Muttalib (hakuwaita ndugu zake), na Abdulla bin Zubeir bin Awam (hakuwaita ndugu zake) wala hakumwita Sayyidna Hussein." Akasema nao kwa ulatifu ili wamkubali Yazid, lakini wote wakapinga; na baada ya siku mbili tatu, akenda zake mtungi mtupu!

"Alipokufa Sayyidnal Hasan", Sheikh A. S. Farsy anazidi kutueleza (uk. 22), "…Muawiya aliwaamrisha watu wa Sham wote wamkubali Yazid kuwa ndiye Khalifa baada yake. Wakakubali wote kwa umoja wao." Akamwamrisha Liwali wa Madina awalazimishe watu wake nao wamkubali Yazid. Yeye, anavyosema Sheikh A. S. Farsy (uk. 23), "yakamuudhi haya akaona kwa nini tumkubali kijana asiyekuwa na mwendo mzuri atutawale sisi watu wazima na Masahaba". Kwa hivyo akamjulisha Muawiya msimamo wake, na Muawiya papo hapo "akamwandikia barua ya kumtoa katika Uliwali".

Alipopata barua hiyo, Liwali huyo (Marwan bin Hakam) alihamaki "sana sana na akachukua wakubwa wa jamaa zake wa kukeni, Bani Kinana, mpaka Sham kwa Muawiya kumtishia kuwa atafanya thaura (mapinduzi). Muawiya akamwogopa, akampa na akawapa na hao jamaa zake maneno mazuri na fedha nyingi na mshahara wa maisha. Yeye pauni mia tatu kila mwezi, na kila mmoja katika hao jamaa zake pauni khamsini kila mwezi."

Huko Madina, Liwali mpya aliifuata baraabara ile amri ya Muawiya ya kuwalazimisha watu wake wamkubali Yazid. Lakini hawakukubali; walipinga. Liwali akamjulisha Muawiya hilo pamoja na kumtajia waliokuwa mstari wa mbele katika upinzani huo. Naye akampelekea "barua za watu hao, akamwamrisha awapelekee na amletee jawabu ya kila mmoja katika wao. Nao ni mabwana hawa: Abdulla bin Abbas bin Abdil Muttalib, Hussein bin Ali bin Abi Talib bin Abdil Muttalib, Abdalla bin Jaafar bin Abi Talib bin Abdil Muttalib, na Abdalla bin Zubeir bin Safiyya bint Abdil Muttalib." Aliwaandikia "maneno makali kabisa", Sheikh A. S. Farsy anaeleza katika uk. 24 wa kitabu chake hicho, "na kuwahadidi (kuwatishia) kuwa atawaua wakikataa kumkubali Yazid awe Khalifa baada yake."

Walipozipata barua hizo, mabwana hao (anavyosema Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 24) walimjibu "kwa maneno makali kabisa na tahadidi (tishio) kubwa kabisa. Na aliyemwandikia maneno mengi kabisa ni Sayyidnal Hussein."

Alipozipata jawabu zao hizo, Muawiya alimwambia tena huyo Liwali wake "azidi kuwalazimisha kwa tashdidi kubwa zaidi kabisa. Akafanya", Sheikh Abdalla S. Farsy anasema (uk. 24), "zisifae kitu." Kwa hivyo akamwandikia Muawiya aende tena huko Madina akaonane nao yeye mwenyewe.

Alipofika Madina, na "baada ya kupumzika", Sheikh Abdalla anasema (uk. 25), Muawiya "aliwaita kila mmoja akamsemeza siri peke yake ili wasimjibu wote kwa jawabu moja." Wa kwanza alikuwa ni Imam Hussein a.s. "Akamwambia, 'Mwanangu! Usiutilie fujo umma wa babu yako. Watu wote wamekwisha kuridhia kuwa Yazid awe Khalifa baada yangu. Hakuna wanaopinga ila nyinyi tu, na wewe ndiye unayewaongoza. Ukikubali wewe na wao wataridhia, kama walivyoniambia.' (Imam Hussein a.s.) akamwambia, 'Waite mbele yangu hapa waseme hayo. Mimi sisadiki kuwa wamesema hivyo. Wakikiri mbele yetu hapa na mimi nitakuwa pamoja nao. Lakini nina yakini kuwa hawatakiri.' Akamwambia, "Basi nenda zako. Lakini usimhadithie yo yote lo lote katika tuliyoyasema." Hivyo ndivyo alivyoandika Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 25 wa kitabu chake hicho.

Baada ya Imam Hussein a.s., alimwita Bwana Abdalla bin Zubeir, kisha Bwana Abdulla bin Umar bin Al Khattab. Nao wakamjibu kama alivyojibu Imam Hussein a.s. "neno kwa neno". Hapo tena, Sheikh Abdalla anasema (uk. 25-26), "akapeleka mtu kumwita Bwana Abdur Rahman bin Abi Bakrinis Sidiqq. Akamsemesha maneno makali kabisa na yeye akamjibu makali kabisa. Wakaghadhibishana kweli kweli kwani yeye alikuwa mtu mzima kama yeye."

Baada ya hapo ilimbidi Muawiya abadilishe mbinu. Kwa hivyo "siku ya pili", Sheikh Abdalla anasema (uk. 26), " akapeleka mtu kumwita Sayyidnal Hussein bin Ali na Bwana Abdalla bin Abbas." Baada ya kuzungumza nao "mambo ya hali zao na hali za majumbani mwao", aliingia "kumsifu mwanawe Yazidi kwa aliyonayo na asiyokuwa nayo. Kisha akawaambia, 'Basi kwa hivi anastahiki kuwa Khalifa wa Waislamu…' " Imam Hussein a.s. akamjibu, Sheikh Abdalla anaendelea (uk. 26), kwa kumtajia "sifa mbovu za Yazid na akamwambia, 'Usizidishe madhambi kuliko uliyoyachuma. Yamekutosha hayo. ' Na akamwambia, 'Unaudhulumu Uislamu na Waislamu kwa hayo uliyoazimia kufanya.'"

Baada ya kutofaulu mbinu zake hizo, aliamrisha waitwe mabwana wote watatu: Abdur Rahman bin Abi Bakr, Abdulla bin Umar, na Abdalla bin Zubeir. Sheikh Abdalla anasema (uk. 27), "Akawakaribisha wote pamoja kwa wakati mmoja. Akawaambia, 'Hili jambo la kufanywa Yazid kuwa Khalifa kishalichagua Mwenyezi Mungu na watu wote wameliridhia isipokuwa nyinyi. Basi tahadharini na kuleta balaa. Itakufikeni wenyewe kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu na yangu …' Wakampinga wote… Akataka aseme faragha na Bwana Abdur Rahman bin Abi Bakr. Alipomwambia maneno hayo ya kutawalishwa Yazid, alimwambia, 'Hatutaki. Na ukiyapitisha kwa nguvu tutavirejesha upya vita vya mwanzo wa Uislamu; uwe na wenye shauri moja na wewe upande wa ukafiri kama alivyokuwa baba yako.' " Hapo Bwana Abdur Rahman akaondoka.

Baada ya siku tatu ikatoka amri ya kukusanyika watu wote wa Madina. Hapo Muawiya akawaweka wale wapinzani karibu yake, na akawaeleza waliohudhuria kuwa mikoa yote imemkubali Yazid kuwa Khalifa isipokuwa wao watu wa Madina, na kuwa lau yeye (Muawiya) angelikuwa anamjua aliye bora kuliko Yazid, angelimtawalisha; lakini hakuna bora kuliko yeye! Kisha akawaonya asisikie "kupinga kokote kule". Na akatangaza mkutano mwengine jioni.

Kabla ya huo mkutano, Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 28 - 29), aliwaita wale wapinzani "wote pamoja ili atoke nao waende mkutanoni. Walipofika akawaambia: 'Nimekwisha weka machakari (wauaji) huko mkutanoni. Na mimi nitawaambia watu wote huko kuwa nyinyi nyote sasa mmekubali kutawalishwa Yazid. Asiyetaka roho yake ainuke hapo anipinge. Papo hapo kitaonekana kichwa chake kinagaragara chini.' "Na huko mkutanoni alikuwa ameshawaambia "mbele hao maaskari kuwa ye yote atakaesema kitu muuweni. Na akafanya ijulikane habari hii kwa watu wote ili wote wawemo katika khofu."

Haya! Huyo ndiye Muawiya! Na hivyo ndivyo alivyopanga kumtawalisha mwanawe (Yazid) ambaye leo mawahabi wetu wasema kuwa mtu kama huyo ni Amiirul-mu’minin! Astaghfirullaah!

Kwenye mkutano huo, kama alivyowaonya kina Imam Hussein a.s., alipanda juu ya mimbari akasema, “Shuhudieni kuwa hawa waliokuwa wakipinga, sasa wameridhia. Na wenyewe hawa wote wako hapa. Na hawa ndio wazalendo wa Madina na wa Kisahaba. Hakuna lililosalia tena.” Hivyo ndivyo anavyoeleza Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 29 wa kitabu chake; na akaendelea kuandika, “Akatoa hapo mafedha kwa mafedha kuwapa kila wakubwa wa kila qabila za Kimuhajiri na Ansari na nyinginezo…” Na hivyo ndivyo Yazid alivyopatiwa utawala katika mwezi wa Rajab, mwaka wa 60 BH, baada ya babake kufa.

Ewe ndugu Mwislamu! Ikiwa mambo yalikwenda hivyo, kama yalivyoelezwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy, kweli Mwislamu yoyote anayeujua Uislamu wake, na anayetaka kubakisha jina jema la Uislamu, anaweza kujifakhiri kuwa mtu kama Yazid alikuwa ni kati ya viongozi wake wa Kiislamu, sambe (seuze) kumkubali kuwa ni Amiirul mu’minin?! Lakini hayo si aliyoyafanya Yazid, yeye mwenyewe; ni aliyofanyiwa na babake, Muawiya. Aliyoyafanya yeye mwenyewe, baada ya kutawala, ni makubwa zaidi! Ni yapi?