6. Yaliyosemwa na Maimamu na Mashekhe

Wa kwanza ni Imam Ahmad bin Hambal. Yeye, kama ilivyonukuliwa katika uk. 440 wa Juzuu ya Nne ya Miizaanul I'tidaal ya Imam Dhahabi, amesema: "Haifai kupokea Hadith kwake (Yazid)." Na huyo Imam Dhahabi, yeye mwenyewe katika ukurasa huo huo, amesema kuwa Yazid "ni mtu ambaye uadilifu wake una walakini. Haifai kupokea Hadith kwake." Haya! Ikiwa mtu mwenyewe haaminiwi kadri hiyo, afaa kuitwa Amiirul - mu'minin?

Wala Imam Hambal hakuzuia tu kupokea Hadith kwa Yazid, bali alimlaani kamwe kwa sababu ya kumuuwa Imam Hussein a.s. kama ilivyoelezwa katika uk. 63 - 64 wa Al-It'haaf Bihubbil Ashraaf.

Wa pili ni Sheikh Muhammad Abduh. Yeye, katika tafsiri yake ya Qur'ani Tukufu iitwayo Tafsiirul Manaar (uk. 367 - 368 wa Juzuu ya Sita), baada ya kueleza jinsi Yazid alivyompinga Imam Hussein a.s., alisema: "Mwenyezi Mungu amshinde, na amshinde kila aliyemtetea miongoni mwa karaamiyya na nawaasib (wanaomchukia Imam Ali a.s.) ambao hawaachi kuendelea kupendelea kuabudu wafalme madhalimu katika kupinga kusimamishwa uadilifu na dini (ya Mwenyezi Mungu)."

Wa tatu ni Imam Shawkaani. Yeye, katika uk. 362 wa Juzuu ya Sabaa ya kitabu chake kiitwacho Naylul Awtwaar, baada ya kuwalaumu wanaomkosoa Imam Hussein a.s. kwa kumpinga Yazid, amemlaani Yazid na babake (Muawiya) kwa kusema "Mwenyezi Mungu awalaani!" Halafu akasema, kuhusu lawama hizo, "Ajabu iliyoje ya Mwenyezi Mungu, ya maneno hayo yanayoikausha damu na ambayo, kwa kuyasikia tu, majabali hupasuka!"

Wa nne ni Imam Taftaazaani, kama alivyonukuliwa katika uk. 12 wa Juzuu ya Kumi na Tano ya Irshaadus Saari, sherehe ya Sahih Bukhari. Imam huyo, baada ya kusema kuwa wanazuoni wameafikiana "kuruhusu kumlaani aliyemuuwa (Imam Hussein a.s.) au aliyeamrisha auwawe, au aliyeruhusu, au aliyeridhia"; na baada ya kueleza kuwa "ni jambo lililoenea kuwa Yazid aliridhia kuuwawa Hussein r.a. na kuitweza Nyumba ya Mtume s.a.w.w.", amesema: "Laana ya Mwenyezi Mungu imshukie yeye na answari wake na wasaidizi wake!"

Wa tano ni mtoto wake mwenyewe Yazid aliyempa jina la babake (Muawiya). Huyu alishika Ukhalifa baada ya babake (Yazid) kufa. Lakini yeye hakuendelea; baada ya siku 40 au, kwa kauli nyengine, baada ya miezi mitano alijiuzulu. Alipojiuzulu alipanda mimbari akatoa khutba. Katika khutba hiyo, miongoni mwa aliyoyasema, alitaja ugomvi uliotokea baina ya babu yake (Muawiya bin Abi Sufyaan) na "aliyekuwa bora kuliko yeye na wasiokuwa yeye (yaani Imam Ali a.s.)." Halafu akamtaja babake (Yazid) na "vitendo vyake viovu", na kwamba "hakuwa na sifa za kuwa Khalifa wa umma wa Muhammad (s.a.w.w.)"; akataja na "dhulma alizowafanyia watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w.w." Mwisho wa khutba yake alilia sana, na akawambia jamaa zake, Banii Umayya, kuwa hataweza kubeba dhambi zao. Kwa hivyo "shauri zenu! Uchukueni Ukhalifa huu mumpe mumtakaye. Mimi simo tena." Hayo yote yameelezwa katika uk. 301 wa Juzuu ya Pili ya Taariikhul Khamiis.

Haya!, Baada ya kuyasoma yote hayo (mbali mengi sana tuliyo yaacha) bado Yazid huyo angali Amiirul-mu'minin? Hata baada ya mwanawe mwenyewe kusema kuwa hakuwa na sifa za kuwa hivyo? Nani anayemjua zaidi baba wa mtu? Mwanawe au watu kando? Majibu ninakuachia wewe ndugu msomaji.