Aya 22 – 30: Sema Waiteni Mnaodai Kuwa Ni Waungu
Maana
Sema: Waombeni hao mnaodai kuwa ni badala ya Mwenyezi Mungu.
Washirikina waliabudu Malaika na masanamu, Mtume (s.a.w.) akawakataza lakini hawakusikia, akawaambia kwa amri ya Mwenyezi Mungu: iko wapi dalili ya mnaowafanya kuwa ni miungu? Waombeni manufaa au kukinga madhara, muone kuwa wanasikia na kuwajibu?
Lengo la matakwa haya ni kusimamisha hoja isiyoshindwa. Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُمْ مِنْ دُونِهِ فَلَا يَمْلِكُونَ كَشْفَ الضُّرِّ عَنْكُمْ وَلَا تَحْوِيلًا {56}
Hawamiliki hata chembe katika mbingu wala ardhini. Wala hawana ushirika wowote humo. Wala hawana msaidizi miongoni mwao.
Maneno yanaelekezwa kwa washirikina. Hata chembe ni kinaya cha kuwa hawamiliki hata kitu kilicho kidogo na duni. Maana ni kuwa hana mshirika wala msaidizi.
Wala hautafaa uombezi mbele yake ila kwa yule aliyempa idhini.
Hii ni kuwarudi washirikina na kauli yao:
مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّهِ زُلْفَىٰ{3}
Kwa maelezo zaidi Tazama Juz. 1 (47 – 48) kifungu cha ‘Shufaa.’
Hata itakapoondolewa fazaa kwenye nyoyo zao, watasema: Kasema nini Mola wenu? Watasema: Haki, naye ndiye aliye juu, Mkubwa.
Wafasiri wametofautiana kuhusu watakaoondolewa fazaa, watakaouliza na wataoulizwa.
Kauli yenye nguvu zaidi ni watakaoondolewa fazaa ni wote walioko mbinguni na ardhini; kwamba fazaa itawaenea wote isipokuwa atakaowataka Mwenyezi Mungu; kama ilivyoelezwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَيَوْمَ يُنْفَخُ فِي الصُّورِ فَفَزِعَ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَمَنْ فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَنْ شَاءَ اللَّهُ ۚ وَكُلٌّ أَتَوْهُ دَاخِرِينَ {87}
Mara kwa mara tumesema kuwa Qur’an inajifasiri yenyewe. Kwa hiyo maana yanakuwa kwamba wakati wa Kiyama, wa mbinguni na wa ardhini watagawanyika mafungu mawili: Kuna kundi litakalokuwa na fazaa kubwa na kundi jingine litakuwa na amani. Hawa ndio walioashiriwa na kauli ya Mwenyezi Mungu: “Ila amtakaye Mwenyezi Mungu.” Kundi la kwanza ikitulia fazaa yake, watauliza kundil la pili: Mola wenu amesema nini na mwisho wetu ni upi? Watakoulizwa watajibu kuwa Mwenyezi Mungu amesema haki naye ndiye aliye juu, Mkubwa.
Jibu hili kwa ujumla linaashiria kuwa Mwenyezi Mungu hana mshirika wala msaidizi. Pia hakuna atakayeombea kwake isipokuwa aliyempa idhini.
Sema: Ni nani anayewaruzuku kutoka mbinguni na ardhini?
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume (s.a.w.) awaambie washirikina. Riziki ya kutoka mbinguni ni mvua na mwangaza na riziki ya ardhini ni mazao ya porini na yanayopandwa.
Sema ni Mwenyezi Mungu, siyo masanamu au Malaika, wala sio Isa au Uzayr. Kwa vile hili ndio jibu pekee, ndio maana Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake mtukufu awajibie walioulizwa.
Na hakika sisi au nyinyi bila shaka tuko kwenye uongofu au upotofu ulio wazi.
Nabii ana uhakika kwamba yeye yuko kwenye uongofu na kwamba washirikina wako kwenye upotevu, lakini walipoukataa uwongofu na haki ndio akatumia mfumo huu wa hekima na kuwaambia kuwa mja wetu atakuwa kwenye haki na mwingine kwenye upotevu, basi zirudieni akili zenu muone ni nani aliye kwenye usawa?
Huu ndio mfumo wa Mtume wa uwongofu na rehema, kuongezea kuwa mwenye haki anajiamini hata wakimhalifu watu wote wa ardhini.
Sema: Nyinyi hamtaulizwa kwa makosa tuliyoyafanya wala sisi hatutaulizwa kwa mnayoyatenda.
Huu ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
وَإِنْ كَذَّبُوكَ فَقُلْ لِي عَمَلِي وَلَكُمْ عَمَلُكُمْ ۖ أَنْتُمْ بَرِيئُونَ مِمَّا أَعْمَلُ وَأَنَا بَرِيءٌ مِمَّا تَعْمَلُونَ {41}
Sema: Mola wetu atatukusanya kisha atatuhukumu kwa haki, naye ndiye Hakimu, Mjuzi.
Siku ya mwisho ina majina mengi; miongoni mwayo ni siku ya mkusanyiko. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
يَوْمَ يَجْمَعُكُمْ لِيَوْمِ الْجَمْعِ ۖ {9}
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atatukusanya sisi na na nyinyi ili tuangalie hisabu, malipo na matendo. Hapo pazia litafunuka na mtajua kundi gani ndio lililoelekea njia ya kunyooka.
Sema: Nionyesheni wale mliowaunganisha naye kuwa washirika.
Hapa kuna manaeno ya kukadiria kuwa nionyesheni dalili ya kuwa masanamu ni washirika wa Mwenyezi Mungu au watawajongeza kwa Mwenyezi Mungu. Hapana! Yeye hana mshirika wala msaidizi wala wa kuombea mbele yake isipokuwa aliyempa idhini.
Bali Yeye ni Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Hakuna enzi wala nguvu isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu. Ama dalili za hekima yake na utukufu wake zinajitokeza katika kuumba ulimwengu na maajabu yake.
Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mtoaji bishara na muonyaji, lakini watu wengi hawajui.
Tazama Juz. 7 (6:92) na Juzuu hii tuliyo nayo (33:40) Kifungu cha ‘Kwanini utume umeishilia kwa Muhammad (s.a.w.)?’
Na wanasema: Ni lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli?”
Imetangulia neno kwa neno katika Juz. 11 (10:48).
Sema: Mna miadi ya siku ambayo hamtaakhirisha saa wala hamtaitangulia.
Kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu ameahidi ufufuo, hisabu na malipo, naye bila shaka, ni mwenye kutekelza miadi yake, lakini kwa wakati alioupanga yeye ambaye hekima yake imetukuka, hatanguliwi wala hacheleweshwi. Basi yasiwahade mliyo nayo enyi washirikina, kwa sababu yatakwisha tu, muda mfupi au mrefu, kisha marejeo yenu nyote ni kwa Mwenyezi Mungu awajulishe yale mliyokuwa mkiyafanya.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَنْ نُؤْمِنَ بِهَٰذَا الْقُرْآنِ وَلَا بِالَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ ۗ وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ مَوْقُوفُونَ عِنْدَ رَبِّهِمْ يَرْجِعُ بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ الْقَوْلَ يَقُولُ الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا لَوْلَا أَنْتُمْ لَكُنَّا مُؤْمِنِينَ {31}
قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا أَنَحْنُ صَدَدْنَاكُمْ عَنِ الْهُدَىٰ بَعْدَ إِذْ جَاءَكُمْ ۖ بَلْ كُنْتُمْ مُجْرِمِينَ {32}
وَقَالَ الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا بَلْ مَكْرُ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ إِذْ تَأْمُرُونَنَا أَنْ نَكْفُرَ بِاللَّهِ وَنَجْعَلَ لَهُ أَنْدَادًا ۚ وَأَسَرُّوا النَّدَامَةَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ وَجَعَلْنَا الْأَغْلَالَ فِي أَعْنَاقِ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ هَلْ يُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {33}