read

Maneno Mawili

Bismillahir Rahmanir Rahiim.

Namshukuru Allah swt pamoja na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. pamoja na Ahlul Bayt a.s. kwa kunijaalia tawfiqi ya kuweza kukitayarisha kitabu hiki.

Mimi binafsi nimekuwa na shauku kubwa ya kusoma hadithi na visa mbalimbali kuanzia utoto wangu na kwa hakika ndiyo maana nimeweza kuwa na faida kubwa kiilimu kwani mafundisho yanayopatikana katika maandiko haya matakatifu na ya wahenga wetu, yanakuwa yamejaa nasiha na mafundisho ambayo si rahisi kuyapata kwengineko. Lakini vitabu vingi vipo ambavyo vinavyo hadithi za uchimvi na vinavyosababisha watu kumomonyoka maadili yao na hivyo kupotoka. Na ndivyo maana inatubidi kujiepusha navyo.

Hadithi hizi nimezitoa kutoka mchanganyiko wa vitabu mbalimbali ili kuwanufaisheni nyinyi wasomaji muvisome na kuwaelezea wananyumba wenu ili nao wafaidike na kuweza kuelewa kuwa Dini na Qur’an Tukufu si kitabu cha kuchosha, bali kama tutasoma ipasavyo, basi sisi tutafaidika mno kwani ndani mwake kuna hazina kubwa ya ilimu na hekima.

Vile kuna vitabu vinginevyo vinavyozungumzia visa, masimulizi kama haya, yaani Visa vya Bahlul, Fadhail na Hukumu zilizotolewa na Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.

Ni matumaini yangu kuwa kitabu hiki na vinginevyo nilivyovikusanya na kuvitarjumu vitawasaidieni nyote. Iwapo utakuwa na maoni yoyote yale nitashukuru iwapo utanitumia ili kuweza kusaidia katika siku za mbeleni.

Wakati huo ninaendelea kutayarisha masimulizi na hadithi nyinginezo za kuongezea hapo mbeleni.

Wabillahi Tawfiq,

Amiraly M.H.Datoo, 4 April 2002
P.O.Box 838
BUKOBA – Tanzania ( datooam@hotmail.com )