Najilinda Kwa Mwenyezi Mungu Na Shetani Aliyefukuzwa

Kujilinda Na Shetani

Mwenyezi Mungu (S.W.T.) anasema:

فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ {98}

Unaposoma Qur’an jilinde kwa Mwenyezi Mungu na shetani aliyefukuzwa.(16:98)

Amesema tena:

وَإِمَّا يَنْزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {200}

Na kama wasiwasi wa shetani ukikusumbua basi jilinde kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mwenye kusikia mjuzi. (7:200)

Maana Ya Kujilinda

Kujilinda huku kwa Mungu hakutoshi kwa kusema: Au’dhubillahi minash-shaytwanir rajim” tu, isipokuwa linalotakikana ni kumwamini Mwenyezi Mungu, kumtegemea na kumwogopa; hata kama mtu hakutamka hivyo.

Mwenye kutenda umuhimu wowote kwa kuitakidi kuwa nyuma yake kuna nguvu inayomsaidia kutenda amali njema; mwenye kupondokea kufanya haramu, lakini twaa ya Mwenyezi Mungu ikamzuia na mwenye kuchanganyikiwa akaifanya sharia ndio kipimo, wote hao ni katika wale wanaojilinda kweli kwa Mwenyezi Mungu na shetani aliyefukuzwa.

Hakuna kitu kinachofafanua zaidi ‘kujilinda’ kuliko mtu kumtegemea Muumba wake, kuwa na yakini kwamba mja mwingine hawezi kumdhuru wala kumnufaisha na kwamba kabisa hakuna kitu kitakachozidi hifadhi ya Mwenyezi Mungu.

Majaribio yametufundisha kwamba mwenye kumtukuza asiyekuwa Mwenyezi Mungu, amedhalilika; na mwenye kutaka uokovu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ameruka utupu; na matarajio hayawezi kupatikana kwa kuwakimbilia viongozi, chama, wala kwenye hazina za matajiri, bali Mwenyezi Mungu tu peke yake ambaye hana mshirika.

Shetani Ni Nani?

Sisi hatujamwona Shetani ana kwa ana lakini ametolewa habari zake na wahyi. Kwa hivyo ni wajibu kusadiki kuwa yupo, na si wajibu kujua alivyo.

Mwenyezi Mungu amemtaja katika Qur’an kwa sifa ya kupoteza watu na kuwaepusha na twaa ya Mwenyezi Mungu na amali ya heri. Kwa hiyo kila wazo linalokupitia moyoni au mtu anayejaribu kukuhadaa kukuweka mbali na twaa na kheri ya Mwenyezi Mungu, kukuhadaa kuasi sharia na kuuvika uovu na ubatilifu nguo ya uongofu, basi huyo ni Shetani wa hisia au wa kimaana.

Jambo la kushangaza ni kuwa “mashetani watu” nao wanaomba walindwe na shetani, hali wao wenyewe ni mashetani lakini hawajijui. Ni sawa na mtu anayesoma Qur’an na huku inamlaani mwenyewe; kama ilivyoelezwa katika hadith.

Qur’an inamlaani mwongo aliye haini. Kwa hivyo huyo mwongo anapoisoma huwa amejitamkia laana yeye mwenyewe.

Mwenyezi Mungu anasema:

أُولَٰئِكَ جَزَاؤُهُمْ أَنَّ عَلَيْهِمْ لَعْنَةَ اللَّهِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ {87}

“Hao malipo yao ni kushukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote.” (3:87)

Hukumu

Kusoma Au’dhu... kabla ya kusoma Qur’an ni sunna, wala si wajib; ni kama vile kuosha mikono na kusoma Bismillah kabla ya kula. Lau hiyo Au’dhubillahi ingelikuwa ni wajibu ingeliwajibishwa katika swala, mahali pa fatiha na Sura. Wanavyuoni wote wamesema kuwa si wajib.

Mwenye Miftaahul-Karaama amesema:”Hawakuhitalifiana katika hilo isipokuwa Ibn al-Junaid ambaye mafakihi wamemwita: ‘aliyejitenga’.”

Mantiki Ya Iblis

Kwa mnasaba wa Au’dhu (kujilinda na Shetani) tutadokeza vigano alivyonasibishwa navyo Ibilisi.

Kwa sababu ingawaje ni vigano, lakini vina picha wazi kwa watu wengi wa zama hizi; hasa wale wanaotaka kujinufaisha bila ya kuangalia maslahi ya wengine, kwa kufanya mbinu za kujaribu kila njia ya kucheza na maneno na kuficha haki.

Tutayaonyesha hayo kwa matamko tu; bila ya kudhihirisha madhumuni.

Inasemekana kuwa Ibilisi alimwambia Mwenyezi Mungu (s.w.t): “Haijuzu kuniadhibu kwa kuacha kumsujudia Adam.” Mwenyezi Mungu akamuuliza, “Kwa nini?”

Akajibu: “Kama ungelitaka hasa nimsujudie ungenifanyisha kwa nguvu.”

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamuuliza: “Wakati gani ulijua kwamba sikukutaka umsujudie Adam? Je ulilijua hilo baada ya kukuamrisha na kuasi amri yangu? Au kabla ya kukuamrisha kusujudu?”

Akasema: “Ni baada ya kuniamrisha”.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Akasema: “Basi umejishinda. Kwa sababu ulihalifu kabla ya kujua kuwa Mimi niliyataka yale uliyoacha kuyafanya. Zaidi ya hayo kama ningekufanyisha kwa nguvu, basi isingelikuwa amri.”

Utaona katika mantiki ya Ibilisi sura iliyo wazi kwamba Mwenyezi Mungu hawafanyishi wenye kuwajibikiwa na sharia kama vile anavyofanya katika kuumba kwa njia ya “kun fayakun” (kuwa, ikawa). Isipokuwa anawafanyisha kwa njia ya kuongoza matakwa ya mtu kwa sharia inayoelezwa ya kuamrisha mema na kukataza mabaya.

Inasemekana kuwa siku moja Ibilisi alikutana na Mtume Muhammad (s.a.w.) akamwambia: “Hakika Mwenyezi Mungu amekusifu kwa jina la kiongozi, na mimi amenisifu kwa jina la mpotezaji. Lakini uongozi na upotezaji vyote vinatokana na Yeye, kwa hiyo wewe na mimi hatuna chochote.”

Mtume akasema: “Hapana! Mimi hubainisha batili na kuikataza na kuitolea kiaga kibaya; hali wewe una unafiki na hadaa ya ubatilifu; na mtu ana uwezo, upambanuzi na hiyari. Kwa hivyo mwenye kufanya hiyari nzuri (akaongoka) anajifanyia mwenyewe, na mwenye kuifanya mbaya (akapotea) pia anajifanyia mwenyewe.”

Imesemekana kuwa Ibilisi alimwendea Nabii Isa (a.s.) akamuuliza: “Si unadai kuwa wewe una daraja kubwa kwa Mungu? Basi hebu jitupe kutoka juu tuone, je atakuokoa?”

Masihi akasema: “Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anayemjaribu mja wake na sio mja kumjaribu Mola wake.” Imesemekana kuwa baada ya gharika na kukauka maji, Ibilisi alimwendea Nuh (a.s.) akamwambia: “Hakika wewe umenisaidia, kwa hiyo ninataka kukulipa.”

Nuh (a.s.): Akasema: “Mungu apishe mbali! kumsaidia na kiumbe kama wewe.”
Akasema Ibilisi: “Ndio hivyo.”
Nuh (a.s.): Akasema “kwa nimekusaidia nini?

Akasema Ibilisi:“Umewaapiza watu wako ili waangamie wakaangamia, na nilikuwa nikijishughulisha usiku na mchana kuwapoteza kwa muda huo. Baada ya kuaangamizwa watu wako, sina kazi ya kufanya; sipati wa kumpoteza.”

Nuh (a.s.) akasema: “Utanilipa nini?

Akasema: “Ninakunasihi usikasirike, kwa sababu hasira ya mtu inarahisisha kunifuata. Wala usihukumu kati ya watu wawili. Kama ukifanya hivyo, basi mimi nitakuwa wa tatu wenu. Wala usikae faragha na mwanamke kwani mimi hukuvutia kwake na yeye humvutia kwako.”

Kutokana na mantiki hii ya kishetani, inaonyesha kuwa Shetani ndiye mchochezi, na kwamba yeye huzipongeza silaha zenye kuangamiza.

Inasemekana kwamba Mtume (s.a.w.) na sahaba zake walimpitia mtu mmoja akirukuu na kusujudu kwa unyeyekevu. Wakasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni uzuri ulioje wa swala ya mja huyu!” Mtume akasema: “Huyu ndiye aliyemtoa baba yenu peponi.”

Lengo la hekaya hii ni kuwa haifai mtu kughurika na kuhadaika kwa zuhudi na ibada ya dhahiri.

Inasemekana kuwa Nabii Musa (a.s.) alikuwa akienda kuzungumza na Mola wake, ikatokea kukutana na Ibilisi, akamwambia “Unakwenda wapi ewe uliyezungumza na Mwenyezi Mungu?”

Nabii Musa (a.s.) akasema: “Ninakwenda kwa Mola wangu kupokea maneno kutoka kwake na niko tayari kukuombea akusamehe kama utaniahidi kuung’oa upotevu wako.”

Ibilisi akasema: “Mimi sina haja ya kuombewa na wewe wala mwingine, bali ni juu Yake Yeye Mungu kutaka radhi yangu.” (Mungu apishe mbali).

Musa (a.s.) akamwambia: “Kafiri mkubwa we Mwenye laana!”

Ibilisi Akasema: “Kwani nina dhambi gani mimi? Mungu alinitaka nimsujudie Adam, na mimi kwa iIkhlas yangu, siwezi kumsujudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Sasa tangu lini Ikhlas ikawa ni dhambi?”

Musa (a.s.) akamjibu: “Hii ni kuchezea maneno tu nako hakuwezi kukufaa wewe hata chembe, utaona yatakayokupata Kesho (Kiyama).” Ibilisi akasema: “Na wewe utaona nitakavyofanya kesho.”
Akasema: “Utafanya nini?”
Ibilisi akajibu: “Nitamtaka Mwenyezi Mungu atimize ahadi Yake na nitamtolea hoja kwa kauli Yake:

وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ۚ {156}

“Na rehema yangu hukienea kila kitu.” (7:156)

“Nami ni ‘kitu,’ kwa hiyo ni wajibu rehema Yake inipate (inienee). Kama mimi si chochote, basi sitahisabiwa wala kuadhibiwa.”

Akasema Musa (a.s.): “Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu inamwenea yule mwenye mwelekeo nayo, na wewe uko mbali sana nayo.”

Ibilisi akasema: “Basi nitafanya njia nyingine. Nitawaita wafuasi wangu waliopotea na nitamtaka Mwenyezi Mungu (s.w.t.) naye awaite wafuasi Wake waumini, halafu ipigwe kura. Hapo atajulikana nani mshindi mwenye sauti ya wengi. Kama Mwenyezi Mungu akikataa kura, nitafanya maandamano makubwa mpaka nipate ninayotaka.”

Kigano hiki kina lengo la kwamba watu wa batili ni wengi zaidi kuliko watu wa haki, kwa sababu haki ni nzito na batili ni nyepesi; kama alivyosema Amirul Muminin, Ali (a.s.): “Yapasa mwenye akili kutoangalia wingi kuwa ni kipimo cha haki, wala uchache kuwa ni kipimo cha batili.”

Katika Nahjul-Balagha, amesema: “Hakika kundi kubwa ni watu wa batili hata wakiwa wengi; na kikundi kidogo ni watu wa haki hata wakiwa wachache.”

Qur’an tukufu nayo inasema: “Na wengi wao ni wenye kuchukia haki.(23:70)

وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {21}

Lakini watu wengi hawajui.” (12:21)

وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ {38}

Lakini watu wengi hawashukuru.” (12:38)

وَأَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ {103}

“Na wengi wao hawatumii akili.(5:103)

بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ {100}

“Bali w engi wao hawaamini.(2:100)

Kuna Hadith inayosema: “Wakikutana wasaidizi wa Ibilisi wanaweza kujaza Mashariki na Magharibi.”

Ni kwa madondoo haya, na mengineyo mengi, ndipo Shia wakasema: Khalifa wa Mtume ni kama Mtume; huchaguliwa na Mwenyezi Mungu; siye yule anayechaguliwa na watu.
Huyo anayechaguliwa na watu ni Mfalme wa watu; si Khalifa wa dini. Ama mkuu wa dini, kwa Shia, ni yule mwenye sifa zilizoelezwa. Sio yule anayechaguliwa na watu wala si yule anayewekwa na kiongozi wa kidunia.

Na kwa nini isiwe hivyo? Je, watu wenye matamanio ya dunia wanaweza kuaminika kuongoza dini ya Mwenyezi Mungu? Basi kama ni hivyo na wawachague na kuwapigia kura Mitume, na walifaradhishe hilo kwa Mwenyezi Mungu. Ametakata kabisa Mwenyezi Mungu na yale wayasemayo madhalimu.

Natija ya kimantiki ni kwamba Khalifa wa Mtume hawi, na hatakuwa, isipokuwa kwa usimulizi unaotokana na Mtume mwenyewe, na kwamba mkuu wa dini ni yule mwenye sifa zilizosimuliwa.
Mwenye kujipachika ukuu wa dini bila ya kuwa na sifa zilizotajwa, basi atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na ameruka patupu mwenye kuzua.

Kwa hivyo basi, yote hayo yanafahamisha kuwa suala lolote haliwezi kuwa la kweli mpaka liwe limefuata haki; na kwamba mbinu za kucheza na maneno, haziwezi kuifanya batili iwe haki, au haki iwe batili, wala kisichoingia akilini kiingie akilini; hata kama hizo mbinu zitakuwa za hali ya juu kiasi gani.

Tutakalolifahamu ni kuwa mwenye mbinu hizo ni mwanafunzi hodari wa Ibilisi katika kuificha haki, na kuifunika na moshi wa hadaa.