Aya 3-5: Wanaoamini Ghaibu

Maarifa

Inasemekana kuwa mwanachuoni mmoja mkubwa aliyekuwa na heshima na cheo kikubwa huku watu wakimzunguka kwa kumuuliza maswali na kumnyenyekea, alionewa kijicho na mpinzani wake mmoja.

Akamuuliza swali la kutatiza kwa sauti kubwa, ili wote wasikie. Mwanachuoni akasema: “Sijui.” Muulizaji akasema: “Mahali ulipo ni pa anayejua sio pa asiyejua.” Akasema mwanachuoni: “Ole wako! Hapa ni mahali pa anayejua kitu sio kila kitu; anayejua kila kitu hana mahali.”

Ndio! ni muhali kwa mtu kujua kila kitu. Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا أُوتِيتُمْ مِنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا {85}

“Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.”(17:85)

Hakuna mtu yeyote anayezaliwa na ujuzi, isipokuwa hupata maarifa muda baada ya muda, kutokana na sababu fulani; hata hilo jina lake pia halijui, isipokuwa baada ya kuitwa mara kwa mara.

Wajuzi wa fani ya maarifa wametaja sababu nyingi za maarifa ambazo ni:

1. Kujua kutokana na hisia tano: Kujua rangi kwa kuona, sauti kwa kusikia, harufu kwa kunusa, ladha kwa kuonja na ugumu kwa kugusa. Vile vile kuna yale anayoyahisi mtu kwa hisia za kindani; kama njaa, shibe, mapenzi na chuki.

2. Kupata maarifa kutokana na uchunguzi na majaribio.

3. Kujua kwa misingi ya kikawaida; yaani kushirikiana na kukubaliana akili zote; mfano: Moja na moja ni mbili; na chenye kunufaisha ni bora kuliko chenye kudhuru. Au kujua kutokana na majaribio; kwa mfano kuamua kwamba kila kipande cha chuma ni kigumu, baada ya kujaribu kipande kimoja tu. Kwa hiyo hukumu inaenea kwa vyuma vyote lakini maarifa yametokana na majaribio ya kimoja.

4. Kujua bila ya kupata maalumati yoyote ya hisia, majaribio au nguvu ya akili; bali kupata moja kwa moja. Hilo ni baada ya jitihadi ya kuitakasa nafsi na uchafu; kama wasemavyo masufi. Kwa ufasaha zaidi ni kwamba moyo mbele za msufi ni kama akili kwa wengine. Kama ilivyo akili kutambua baadhi ya vitu vingine kwa kujitahidi na kuangalia vizuri, basi hivyo hivyo moyo nao hutambua baadhi ya vitu bila ya jitihadi ya nafsi; kama kuhisi mapenzi, na chuki. Na hutambua vitu vingine baada ya jitihadi ya nafsi; kama kujua kuweko Muumbaji.

Kwa hiyo jitihadi ya akili kwetu sisi inafanana na jitihadi ya nafsi kwa masufi. Wala hakuna yeyote anayeweza kubishana na sufi katika maoni yake na itikadi yake. Kwa sababu ukimuuliza dalili, atakujibu kwamba imani yangu na elimu yangu inatoka katika dhati yangu peke yake.

Na kama ukimuuliza: Kwa nini imani na elimu hii haitokei katika dhati za watu wote? Atakujibu: Kwa sababu wao hawakupitia majaribio ya kiroho niliyoyapitia mimi.
Sisi tunajiweka kando na msimamo wa kisufi, bila ya kufungamana na upande wowote. Hatuwezi kuuthibitisha, kwa sababu tuko mbali na tunavyoelewa na tulivyozowea. Pia hatuwezi kuukanusha, kwa sababu mamia ya wanavyuoni katika kila zama hata katika zama zetu wanaamini kuwako nguvu ya usufi; na kutofautiana kwao kihali, kidini, na hata kilugha.

Hatuna hoja yoyote inayokanusha majaribio ya kiutu kabisa. Inawezekana kuwa majaribio ya kisufi yanafanana na vipindi ambavyo anapata ilham (anafunukiwa) mshairi na msanii, lakini jambo hili linamuhusu yeye peke yake; wala hana hoja kwa mwingine.

Ghaibu

Kuna vitu ambavyo hakuna njia ya kuvijua kwa hisia, majaribio au nguvu ya akili, kama vile Lawhin Mahfudh (ubao uliohifadhiwa), Malaika, Iblis, Hisabu ya kaburi, Pepo na Moto.Vile vile miujiza ya Mitume; kama fimbo kugeuka kuwa nyoka, kufufua watu, n.k. Akili haiwezi kugundua mambo hayo wala hatujayaona. Yote hayo ni makusudio ya ghaibu katika neno lake Mwenyezi Mungu: “wanaamini ghaibu”.

Kwa hiyo ghaibu ni ile ambayo haijulikani isipokuwa kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia katika ulimi wa ambaye umethibitika Utume wake. Mwenyezi Mungu anasema:

وَعِنْدَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ{59}

“Na kwa Mwenyezi Mungu ziko funguo za siri hapana azijuaye ila Yeye” (6:59)

Kwa hali hii, inatubainikia kuwa kuamini ghaibu ni sehemu ya Uislamu, na kwamba asiyeiamini sio Mwislamu. Vile vile inabainika kuwa jambo ambalo halijulikani kwa kuona, majaribio au akili; au lisilosimuliwa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu wala mapokezi ya Mtume, basi litakuwa ni katika vigano. Na vigano vingi vinatokana na mapokezi ya Mayahudi na mfano wao.

Dini Na Elimu

Jambo la kushangaza ni kwamba hata wale wanaoamini kuwa ulimwengu umepatikana kibahati (sadfa), pia wanaamini ghaibu. Kwa sababu hakuna anayekataa kwamba kuamini sadfa ni ghaibu. Kwa vile hawakuiona hiyo sadfa kwa macho.

Kwani wao wamepatikana baada ya kuja ulimwengu. Vile vile hawawezi kuijua kiakili; kwa vile akili bado haijaifanyia majaribio ya kukanusha au kuthibitisha. La kushangaza zaidi ni kwamba wao wenyewe wanakadiria kuwa ulimwengu umepatikana kutokana na mada ndogo inayoitwa ether.

Na hilo wanaliamini kwa imani isiyokuwa na shaka yoyote; kisha wanawakataza wengine wasiamini kupatikana nguvu yenye hekima yenye kupangilia vizuri mambo kwenye ulimwengu huu; ingawaje huku ndiko kuliko karibu zaidi na akili na moyo kuliko kufikiria kitu kipofu na kiziwi.

Kwa vyovyote iwavyo, ghaibu inajieleza kwa jina lake; inafahamika kwa wahyi tu, na sio kwa majaribio wala kwa nguvu ya kiakili. Sharti lake pekee ni kutopingana na akili, sio kutambuliwa na akili. Kwa hali hiyo basi, elimu ya sayansi haina nafasi ya kuwa juu ya wahyi.

Umuhimu wa elimu ya sayansi unakuwa katika kumsaidia binadamu kujua hali ya maumbile na kuyatumia, na ni jawabu la kujua ni nguvu gani zinazofanya asili ya vitu, mimea na wanyama na vipi tutaunda ndege zinazokimbia kuliko sauti.

Sayansi haitambui ni nani aliyesababisha kupatikana maumbile (Nature) na utaratibu wake. Ama dini inatuambia sababu za kupatikana, na inatupa funguo kuu za kumjua aliyeumba ulimwengu na kutuongoza kwenye lile tunalohitajika kulifanya katika maisha haya, ili tuhakikishe kufikia lengo letu la kiroho na la kimaada (kimwili.)

Viwanda au kilimo peke yake, au vyote kwa pamoja haviwezi kutekeleza matakwa yote ya binadamu na malengo yake. Kwa sababu mtu sio mwili tu; bali ni mwili, roho, mawazo na fikra. Katika mwili wa binadamu kuna rehema yenye kuenea iitwayo utu, na nuru yenye kuenea iitwayo akili ambayo inaufanya ulimwengu mkubwa uwe mdogo mbele yake.

Mahitaji yetu ya hisia, kama vile kula kunywa na kulala yamekuwa ni lazima kwetu, wala hatuna hiyari ya kuyaacha. Kwa hivyo tutake tusitake ni lazima tuyahangaikie; wala hakuna tofauti katika hilo kwa mjuzi au kwa asiyekuwa na ujuzi, kwa Mtume au asiyekuwa Mtume.

Lakini mahitaji ya kiroho yanatofautiana kulingana na watu. Mara nyingi sana mtu huvunja matakwa yake, mapenzi yake na ghadhabu - jambo ambalo ni bora kabisa - lakini mtu hawezi kuacha mahitaji ya mwili wake.

Zaidi ya hayo, lau ingekuwa mtu ni mwili tu, ungeliweza kuhukumiwa na wataalamu wa sayansi, kama wanavyohukumu maada. Na wangeliweza kujua siri za nafsi na undani wake. Vile vile wangeliweza kubadilisha ukafiri kuwa imani na imani kuwa ukafiri; mapenzi kuwa chuki na chuki kuwa mapenzi; uzee kuwa ujana na ujana kuwa uzee, na mengineyo ambayo yanaweza kujaza kurasa. Natarajia kulifafanua zaidi suala hili katika sehemu zake zinazohusika nazo.

Makusudio ya maelezo haya ni kuonyesha kuwa maudhui ya elimu ya sayansi ni mbali na maudhui ya dini na wahyi. Sayansi ni maudhui ya kimaada yenye kuganda au kukua; na lengo lake ni kugundua nguvu za kimaada. Ama dini ni maudhui ya maisha ya binadamu kwa pande zake mbili za kimaada na za kiroho. Ukipenda unaweza kusema: maisha ya kiroho na ya kimatendo. Na lengo lake ni kutaka watu wote waishi maisha ya kuridhisha yenye ufanisi.

Ndio! Uislamu unaheshimu akili na elimu yenye manufaa, na unahimiza kuitafuta; bali unaizingatia kuwa ni wajibu kwa mwanamume na mwanamke. Elimu inawainua watu kupanda daraja. Kwa ajili hiyo basi ni wajibu juu ya Mwislamu kuitakidi kwamba hakuna kitu sahihi katika elimu au akili kinachopingana na Uislamu, wala hakuna kitu katika hukumu za Kiislamu kinachopingana na elimu au akili. Lakini sio kuwa akili inaweza kujua hukumu zote za dini.

Unaweza kuuliza:”Imethibiti Hadith kutoka kwa Mtume mtukufu (s.a.w.) aliposema: “Msingi wa dini yangu ni akili.” Je, hiyo si inaonyesha kwamba akili inajua hukumu zote za dini ya Kiislamu?”

Jibu: Uislamu unaanzia kwenye Uungu na Utume. Na kutokana na mawili hayo ndio yanachimbuka mafundisho yake na hukumu zake. Na njia ya kuyajua hayo ni akili. Kwa hivyo, maana ya Hadith tukufu ni kwamba Uislamu ambao misingi yake ni Uungu na Utume, unategemea akili kuuthibitisha huo Uungu na Utume, sio kuigiza na kufuata kama kipofu tu, au kufuata hekaya na vigano.1

Na Wanasimamisha Swala

Mara nyingine serikali inaweza kumhukumu mtu kubaki katika mji fulani bila ya kutoka, na humlazimisha kupiga ripoti kituoni kwa ajili ya kuthibitisha kuweko kwake.

Kama akihalifu basi atatakiwa kujibu. Uislamu umemwekea mumin sharti maalum, atakaloweza kwalo kuthibitisha imani yake kwa Mwenyezi Mungu Aliyeumba mbingu na ardhi kila siku mara tano, na kumfanyia ikhlas katika amali zake zote. Qur’an inasema:

إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا ۖ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ {79}

“Hakika mimi nimeulekeza uso wangu kwa yule Aliyeziumba mbingu na ardhi. Hali ya kuwa nimeacha dini zote za upotevu na mimi si miongoni mwa washirikina.”(6:79)

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ {162}

لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ {163}

“Sema hakika swala yangu na ibada zangu (zote) na uzima wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote. Hana mshirika, na hayo ndio niliyoamrishwa na mimi ni wa kwanza wa waislamu.” (6:162-163)

Mwenye kuiacha swala kwa kuikana, basi ameritadi; na mwenye kuiacha kwa kupuuza atakuwa fasiki mwenye kustahili adhabu. Ndipo tunaikuta tafsiri ya Imam Ali (a.s.) katika Nahjul-Balagha “Hakika Mtume ameifananisha swala na chemchemi ya maji moto iliyoko mlangoni kwa mtu; akiwa anaoga katika chemchemi hiyo mara tano kila siku hawezi kubakiwa na uchafu wowote.” Yaani kudumisha swala kunautakasa moyo kutokana na kuritadi na ufasiki; kama unavyotakasika mwili kutokana na uchafu. Je, kuna uchafu unaoshinda ukafiri na ufasiki?

Na Hutoa Katika Yale Tuliyowapa

Kutoa hapa, kunakusanya yote anayoyatoa mtu katika njia ya kheri, iwe ni zaka au kitu kingine. Hakuna mwenye shaka kwamba kutoa kwa njia ya heri ni jambo zuri. Lakini je, kunapasa katika mali kutoa kitu kingine zaidi ya zaka na khums?

Zimepokewa Hadith kwa upande wa sunni; kama vile kutoka kwa Tirmidhi, na kwa upande wa Shia; kama ilivyopokewa katika Al-Kafi; kwamba katika mali, iko haki nyingine. Imam Sadiq (a.s.) ameifasiri haki hiyo kuwa ni kitu anachotoa mtu katika mali yake akitaka atoe zaidi au kichache kwa kiasi cha vile anavyomiliki. Ametoa dalili Imam, kwa Aya isemayo:

وَالَّذِينَ فِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ مَعْلُومٌ {24}

لِلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ {25}

“Na ambao katika mali zao mna haki maalum (ya kupewa) masikini aombaye na anayejizuiya kuomba” (70:24-25)

Wanavyuoni wengi wamelichukulia hilo kuwa ni sunna na wala sio wajib; isipokuwa Sheikh Saduq katika Shia. Imenukuliwa kutoka kwake kwamba zaidi ya zaka na khumsi, kuna haki nyingine iliyo ya lazima katika mali, inalazimika kuitoa kwa kiwango anachomiliki mtu; kingi au kichache.

Vyovyote iwavyo, jambo ambalo halina shaka ni kuwa kutoa mali kwa njia ya kheri ni kujitwaharisha na uchafu na kujiokoa na adhabu ya moto. Mwenyezi Mungu anasema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِمْ بِهَا {103}

“Chukua sadaka katika mali zao uwasafishe na kuwatakasa kwazo.”(9:103)

Na ambao wanaamini yaliyoteremshwa kwako Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.). Makusudio ya yaliyoteremshwa kwako, ni Qur’an na Hadith. Kwa sababu, yeye Mtume (s.a.w.):

وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ {3}

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ {4}

Wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake). Hayakuwa haya (anayosema) ila ni wahyi uliofunuliwa (kwake). (53:3-4)

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا ۚ{7}

“Na anachowapa Mtume kichukueni, na anachowakataza jiepusheni nacho” (59:7)

Makusudio ya yaliyoteremshwa kabla yako, ni yale yaliyoteremshiwaMitume waliotangulia; kama vile Zabur ya Daud, Tawrat ya Musa na Injil ya Isa. Lakini hakuna athari yoyote hivi leo ya vitabu hivi kwa upande wa kiamali. Kwa sababu katika itikadi ya Waislamu ni kwamba, ama vitakuwa havipo au yale yaliyopo yamepotoshwa kabisa. Tuwaachie wenyewe wakristo mambo yanayofungamana na Injil.

Nimesoma katika kitabu kinachoitwa Voltar kilichotungwa na Johstone Lanson, na kufasiriwa na Muhammad Ghanimi Hilal ukurasa wa 193 chapa ya 1962. Ninamnukuu: “Inajulikana kuwa idadi ya Injili hizi ni hamsini na nne na Injili nne ziliandikwa baadaye na ya nne ya Luka, ndiyo ya mwisho.”

Amesema Elias Najma katika kitabu Yaasu’ Almasih (Yesu Masih) ukurasa 11 chapa ya 1962: Mitume (anakusudia wanafunzi wa Masih) walipoona kuwa ni dharura kukusanya mafundisho ya Mola na mafundisho mengine, ndipo wakaona waandike baadhi ya mafundisho, matendo na miujiza. Hiyo hasa ndiyo tunayoiita Injili iliyoandikwa. Kwa hivyo imekuja Injili moja katika sura nne.”

Huku ni kukiri wazi kwamba Injili nne sio kiini hasa cha wahyi wenyewe na herufi zake; kama ilivyo Qur’an; isipokuwa ni kunakili kwa mapokezi kutoka kwa Masih (a.s.); kama vilivyo vitabu vya Hadith kwa Waislamu, ambao wamekusanya kauli za Muhammad (s.a.w.), matendo yake na miujiza yake. Tofauti ni kuwa wapokezi wa Injil ni wanne: Mathayo, Yohana, Marko na Luka. Wao ni wenye kuhifadhiwa na kufanya madhambi na makosa, kama wanavyodai wakristo na kwamba haifai kutia ila mapokezi yao.2 Lakini Waislamu hakuna (Isma) kuhifadhiwa na dhambi kwa wapokezi wa Hadith; bali haifai kuchukua na kutumia mapokezi yao ila baada ya kuchunguza na kuhakikisha.

Hakuna tofauti katika mantiki ya kiakili kati ya Injili nne na vitabu vya Hadith. Inawezekana kuvitoa makosa, madaamu tu ni kunakili kutoka kwa mtu. Ama tofauti ya Qur’an na Injil iko wazi. Kwa sababu vizazi mbali mbali vimeshindwa kuleta angalau sura moja tu iliyofanana na Qur’an.

Elias amejaribu kuzuia mushkeli huu kwa kauli yake katika ukurasa wa 12: “Kanisa linatolea ushahid Injili, na Injili inalishuhudia kanisa. Vyote viwili vinathibitishiana.”

Ni wazi kwamba hivyo ni kuthibitisha madai kwa madai yenyewe. Ni sawa na anayesema: “Mimi ni mkweli katika madai yangu kwa sababu mtu fulani ananishuhudia kuwa mimi ni mkweli,” kama akiulizwa, “Ni nani anayeshuhudia kuwa huyo mtu fulani ni mkweli? Atasema: “Mimi ninashuhudia kuwa yeye ni mkweli.” Kwa maana hii anakuwa shahidi ndiye huyo huyo anayedai. Aina hii ya maneno wanafalsafa huiita ‘mzunguko wa kubabaisha akili.’Kama vile Mshairi mmoja alivyosema:

Kigeugeu kutuka, Kati yangu na muhibu
Lau si mvi kuzuka, Habiba singenighibu
Na asingeniepuka, Mvi singeniswibu.

Ubeti wa mwisho, kama unavyouona, unafanana na kupagawa na akili. Kwa sababu, maana yake ni kuwa kuondoka mpenzi wa mshairi kumetokana na huyo mshairi kuota mvi; na kwamba huko kuota mvi kwake kumesababishwa na kuondoka mpenzi wake.

Kwa hivyo kuondoka na kuota mvi ni visababishi kwa wakati mmoja; kama kusema: Nimeshona nguo ili niivae na nimeivaa ili niishone.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا سَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَأَنْذَرْتَهُمْ أَمْ لَمْ تُنْذِرْهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ {6}

Hakika wale ambao wamekufuruni sawa wao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.

خَتَمَ اللَّهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ وَعَلَىٰ سَمْعِهِمْ ۖ وَعَلَىٰ أَبْصَارِهِمْ غِشَاوَةٌ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ {7}

Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyozo zao na juu ya masikio yao; na juu ya macho yao pana kifuniko, basi watakuwa na adhabu kubwa.
  • 1. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hujulikana kwa akili kutokana na njia ya ulimwengu. Na utume hujulikana kwa akili kutokana na miujiza.
  • 2. Katika gazeti An-Nahaar la Beirut la tarehe 12.7.1964 kuna makala ndefu yenye maelezo kwamba wataalamu na wakikristo wamethibitisha kwa majaribio na kwa kompyuta kwamba barua nyingi zinazonasibishiwa Paulo, mwasisi mkubwa wa ukiristo, ni uongo.