Aya 21-22: Mwabuduni Mola Wenu

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja waumini, makafiri na wanafiki kwa alama zao na sifa zao na yale yanayofafanua hali zao, aligeukia kuwaambia wote waliobaleghe wenye akili, wawe waumini au la, waliokuwepo wakati wa maneno na watakao kuwepo baadaye, wote aliwaamrisha kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake.

Amri hiyo kwa waumini ni kutaka uthabiti na kuendelea na imani na twaa. Kwa upande wa makafiri na wanafiki ni kuwataka watubie.

Unaweza kuuliza, kwa nini umewajumlisha watakaopatikana, wakati ambapo maneno ni ya ana kwa ana, hayawezi kumhusu asiyekuwepo?

Jibu: Kila jambo lina pande mbili: Upande wa nje ambao unahusika na yule aliyepo tu; kwa mfano kusema: “Ameangamia yule aliye katika jahazi.” Upande wa pili ni wa maana ya undani; kama kusema: “Fanyeni uadilifu enyi watawala.” Hapa amri itakuwa inafungamana na kila mtawala. Kwa hiyo Aya iko katika upande huu wa pili.

Tawi Hufuata Shina

Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an na akazifikiria vizuri kwa undani ataona kuwa zikitaja msingi wowote katika misingi ya itikadi; kama Tawhid, Utume au Ufufuo, basi huuambatanisha na hoja na dalili, lakini kama zikitaja hukumu za sheria kama kuharamisha zinaa huwa bila ya dalili yoyote, je kuna siri gani?

Jibu: Kukithibiti kupatikana kwa Muumba na Utume wa Muhammad (s.a.w.) kwa hoja ya kiakili, basi kauli zao zinatosha kuwa ni hoja, wala haijuzu kuzikhalifu kwa hali yoyote.

Kwa sababu kukhalifu kauli ya Mwenyezi Mungu na Mtume ni kupinga dalili ya kiakili juu ya Tawhid na Utume.

Yeyote mwenye kuamini na akakubali mashina haya mawili, basi ni juu yake kukubali kila lilothibitishwa na Qur’an na Hadith katika hukumu za sharia na tanzu zake bila ya maswali. Mwenye kuzikanusha hapana haja ya kujadiliana naye katika sharia na tanzu zake.

Kwa ajili hiyo Qur’an imejihimu zaidi kuleta dalili juu ya Tawhid, Utume na Ufufuo (mambo ya msingi - shina). Imeanza kwa Tawhid kwa sababu ndio msingi mkubwa. Kwa hiyo anayeamini shina ni lazima aamini tawi la shina hilo.

Tawhid

Dini za Mwenyezi Mungu zote zinasimamia misingi mitatu: Tawhid, Utume na Ufufuo. Hakuna Mtume yeyote kuanzia Adam (a.s.) mpaka Muhammad (s.a.w.) ambaye hakusimamia mambo matatu haya. Yale yanayofuatia yanatokana na hayo.

Kwa hiyo uadilifu, kudura na hekima zake ni sehemu ya Tawhid; Uimamu na Qur’an ni sehemu ya Utume; na hisabu pepo na moto ni sehemu ya Ufufuo.

Qur’an tukufu imeanza na msingi wa Tawhid na ikaongoza kwenye dalili Zake; ikiwaambia watu: Mwabuduni Mola wenu ambaye amewaumba.

Kimsingi ni kwamba kumwabudu Mwenyezi Mungu kunataka kumjua kwanza kwa njia ya mkataa, sio njia ya kudhani kwa sababu dhana haiwezi kuitoshea haki na chochote; kwa ushahidi wa hiyo Qur’an yenyewe.1

Ni njia gani inayopelekea kumjua Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa uwazi kabisa?

Wanavyuoni wanahitilafiana katika namna ya njia hii, kila mmoja amethibitisha kwa vile alivyoona ni sawa. Kuna wale waliotegemea dalili ya kilimwengu ambayo wameielezea kwa namna hii ifuatayo:

Hakika maumbile na matukio yake yenye kukaririka na yenye kutokea upya yanahitaji kuweko na sababu yake, na haiwezekani kuwa sababu iwe ni maumbile hayo yenyewe.

Kama ingekuwa hivyo, basi ingelikuwa sababu na chenye kusababishiwa ni kitu kimoja; na huo ni mzunguko ulio batili kama tulivyoonyesha katika vifungu vilivyotangulia katika Aya ya 4 ya Surah hii.

Ikiwa sababu iko nje ya maumbile tutauliza; je, sababu hiyo ni natija ya sababu iliyotangulia au ni kwamba imepatikana yenyewe bila ya sababu? Kama kuna sababu, je na hiyo sababu nayo imepatikana na sababu ipi? Hivyo yataendelea maswali; na mlolongo huu wa maswali ni muhali.

Kwa hiyo, inakuwa ni sababu ya pili ambayo ni kupatikana kwa dhati yake na kwake zinaishia na kukoma sababu zote; wala yenyewe haishilii kwa nyengine, nayo ni tamko la Mwenyezi Mungu, kukiambia kitu “kuwa kikawa” kun fayakun.

Dalili hii inasimamia kukubali nadharia ya sababu (Al-illiyyah) kwamba kila athari lazima iwe na mwenye kuileta athari hiyo na kila sababu ni lazima iwe na mwenye kuisababisha; kama vile elimu lazima iwe imetokana na mwenye elimu, na maandishi lazima yawe yameandikwa na mwandishi.2

Ili tuiweke wazi zaidi fikra ya ubatilifu wa mlolongo, na kulazimika kukomea kwenye sababu isiyokuwa na sababu, tutakupigia mfano: Hii michoro waliyoweka wahandisi wa michoro kwa ajili ya ndege, magari majengo, n.k. haina budi ikomee kwa mgunduzi wa kwanza ambaye ameweka huo mchoro; hata kama wengine wameuchukua kutoka kwake, na wala yeye hakuuchukua kutoka kwa mwingine.

Lau tukikadiria kuwa hakuna mgunduzi wa kwanza wa mchoro, basi lazima kusingekweko na ugunduzi wala mchoro.

Kwa hivyo basi haifai kwa yeyote kusema na kuuliza: Mgunduzi wa kwanza aliuchukua wapi huu mchoro? Kwa sababu, maana ya ugunduzi ni kwamba, amegundua yeye mwenyewe bila ya kuchukua kutoka kwa mwingine. Hakika hii inajifahamisha yenyewe, kama linavyojifahamisha jua kwa mwanga wake.

Basi hivyo ndivyo ilivyo kwa upande wa Mwenye kuumba na Mwenye kuruzuku. Maana yake ni kuwa Yeye anaumba, lakini hakuumbwa, anaruzuku lakini haruzukiwi. Ndio ikawa Leibnitz anamwita Mwenyezi Mungu Mhandisi yaani mvumbuzi; Plato naye anamwita Mtengenezaji. Yote hayo ni kuonyesha kuwa yeye ni Muumbaji lakini si Mwenye kuumbwa.

Wengine wanatolea dalili ya kuweko Mwenyezi Mungu kwa nidhamu ya ulimwengu na kupangika kwake kunakaoendelea. Dalili hiyo inaitwa dalili ya ukomo ‘Al-ghai’.

Maelezo

Wataalamu wengi wapya wa elimu ya maumbile wanaona dhahiri ya maumbile haifai kuifasiri kwa sababu ya ukomo wake, bali ni lazima kuifasiri kwa sababu za kiutendaji.

Jibu: sisi tunagundua kupatikana sababu ya kitendo kwa kupatikana sababu ya ukomo wake sawa na vile tunavyogundua seremala hodari kutokana na kupangika kitanda kifundi. Jibu linaweza kufunuka zaidi kutokana na maelezo yajayo.

Kuna wengine waliotegemea wataalamu wa elimu ya maumbile na wengineo katika kugundua hakika nyingi. Kutokana na makadirio haya ndio ikaja nadharia ya mvutano (Force of gravity) aliyogundua Newton kutokana na kuanguka tofaa juu ya ardhi. Kwamba makadirio yote yasiyokuwa mvutano ni batili na makadirio ya mvutano ni sahihi.

Ama kuifuatilia dalili hii juu ya suala tulilonalo, ni kwamba sisi tunashuhudia nidhamu ya ulimwengu na mshikamano wake unaoendelea; kila tunavyokadiria kuwa nidhamu hii imepatikana bila ya Muumba mwenye hekima, basi hayo ni makadirio ya kipuuzi yasiyokubaliwa na akili, wala haikubali akili isipokuwa lazima awepo Muumbaji mwenye hekima na kuwa yeye ndiye ambaye amepangilia. Hebu angalia mfano huu:

Kama ukiona jina lako limeandikwa angani kwa herufi za nuru; halafu usimwone mtu yeyote, huna budi kukadiria kuwa kuna mtu mwenye akili ana chombo kinachomwezesha kuchora herufi za nuru zenye kushikamana katika anga. Ni makadirio gani yasiyokuwa haya yanayowezwa kukadiriwa? Sadfa au kugongana gari mbili au kupatikana volkano, yote hayo yanakupeleka kwenye makosa. Akili yako haiwezi kutulia isipokuwa utakadaria tu kuwa kuna aliyefanya hivyo. Basi hivyo ndiyo ilivyo kuhusu ulimwengu.

Neno la kufikiria na lililo wazi zaidi ni lile la Voltaire aliposema: “Hakika fikra ya kuwepo Mwenyezi Mungu ni dharura. Kwa sababu fikra inayopinga hiyo ni upumbavu.”

Nimesoma kitabu “Adhahiratul-Qur’aniyya” ukurasa wa 91 chapa ya 1958. “Kuna aina fulani ya sisimizi katika Amerika huondoka nyumbani mwao kabla ya kulipuka moto kwa usiku mmoja.”

Vyovyote utakavyokadiria katika makadirio yote na tafsiri zote, haiwezi kutulia nafsi yako milele isipokuwa kwa kukadiria kupatikana mwenye kuzingatia vizuri mambo, mwenye hekima aliyeipa kila nafsi mwongozo wake.

Wengine wanategemea dalili ya kimaumbile na wanasema: “Lau si Imani ya kupatikana Mwenyezi Mungu yangeliangamia makadirio yote ya kimaumbile na kusingelikuwa na wa kuwaepushia watu shari wala kusingelikuwa na wa kuwafahamisha heri.”

Dalili hii iko karibu zaidi na kukanusha kuliko kuthibitisha, kwani inaonyesha kuwa kumwamini Mwenyezi Mungu na hali hii ni wasila na sio lengo, kiasi ambacho lau ingekadiriwa kupatikana mtu anayefanya yale yanayotakikana kuyafanya na kuacha yale yasiyotakikana kuyafanya, basi asingelikuwa na wajibu wa kumwamini Mwenyezi Mungu. Hakuna mwenye kutia shaka kuwa kumfanya Mwenyezi Mungu ni chombo tu ni kubaya zaidi kuliko kumkanusha.

Wengine hutegemea dalili ya hisia ya moyo; nayo ni hisia za moyo moja kwa moja. Wanasema kuwa moyo wa mtu unapata kumjua Muumbaji moja kwa moja bila ya dalili yoyote, sawa na vile unavyohisi mapenzi na chuki. “Yamekw-ishatangulia maelezo kuhusu hayo katika tafsiri ya Aya ya 3, kifungu cha maarifa.

Njia bora zaidi ya zote ni ile aliyoitolea dalili Mwenyezi Mungu juu ya kupatikana Kwake. Kwa ufupi ni kuangalia na kufikiri katika kuumbwa mbingu na ardhi, mtu, mauti na uhai na neema kubwa. Na mengineyo yaliyokuja katika Qur’an tukufu, hadith za Mtume na Nahjul-Balagha.

Ingawaje dailili hii hakika yake inarudi kwenye dalili ya Kawni (kupatikana ulimwengu) na dalili ya Al-ghai (ya ukomo), lakini mpangilio wa maelezo unafahamika upesi na unaweka karibu zaidi kufahamu vitu mahsusi na vya kiujumla. Asiyekinaika na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa dalili za kupatikana Kwake alizozileta yeye mwenyewe, je anaweza kukinaishwa na mtu aliye mfano wake?

Ajabu ya maajabu ni kwamba anayemkanusha Mungu anaamini kabisa na kuitakidi kuwa shati alilolivaa - kwa mfano - limetokana na mbegu aliyoipanda mkulima kwa mpangilio; akaifuma mfanya kazi kwa umakini, akaiuza mfanya biashara kwa maarifa, baadaye mshonaji akaipasua na akaishona kwa kipimo kinachohitajika. Lakini haamini kupatikana aliyetengeneza vizuri huu ulimwengu na kila kitu.

Kwa kuongezea dalili ya kuweko Mwenyezi Mungu ambayo inaingia kwa ujumla, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa kila mtu dalili ya kuwepo yeye Mungu inayomuhusu yeye tu bila ya kushirikiana na mwingine. Mtu yeyote, vyovyote vile atakavyokuwa, akikumbuka mambo na majaribio yaliyompitia, na kama akiyapeleleza ni lazima atakuta katika maisha yake amepitiwa na vitu visivyo na vitu visivyo na maelezo yoyote isipokuwa matakwa ya Mwenyezi Mungu tu.

Mimi sikubali kabisa kuwa kuna mtu yeyote vyovyote alivyo, ijapokuwa ni kafiri, kuwa anaweza kuishi kipindi fulani cha maisha bila ya kupitiwa na kipindi kimoja katika maisha yake asiweze kumrejea Mwenyezi Mungu tena bila ya kukusudia wala kutambua.

Atamwuelekea nani katika kipindi cha shida? Bila shaka atarudi katika maumbile ya Mwenyezi Mungu aliyowaumbia watu na yakapiga chapa kwa kila mwenye kuzaliwa, ambayo si baba anayeyajua wala mama.Mzandiki mmoja alimuuliza Imam Jafar Sadiq (a.s.):

“Ni ipi dalili ya kuweko muumbaji?” Imama akamwambia: “Lau unapanda chombo na mabaharia wote wakafa ukabaki wewe peke yako, je utakuwa unataraji kuokoka?” Mzandiki akasema: “Ndio” Imam akasema: “Hakika muumbaji (Mungu) ndiye Yule utakayemtarajia wakai huo.”

Basi mimi ninampa nasaha yule anayetia shaka ya kuweko Mwenyezi Mungu asome dalili za wakanushaji na watu wa maada, bila shaka yoyote ataishilia kwenye kumwamini Mwenyezi Mungu; ambapo atakuta dalili ya kukanusha ni kwamba wao wanataka kumwuona Mwenyezi Mungu kwa macho na kumgusa kwa mkono na kumnusa kwa pua.

Nimetaja dalili nyingi sana katika maudhui haya katika kitabu Mwenyezi Mungu na akili na Falsafa ya mwanzo na marejeo ambacho nilikihusisha na kujibu Falsafa ya kimaada Vile vile katika kitabu Baina ya Mwenyezi Mungu na Mtu, Elimu ya Falsafa, Uislamu pamoja na Maisha, Uimamu wa Ali na Akili na mengineyo katika vitabu na makala.

Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuombwa kuzitwaharisha nafsi zetu na shaka na kuzikinga radhi zake.
Tumerefusha maneno katika msingi wa kwanza ambao ni Tawhid, ili uwe kama mdhibiti wa yote ambayo yatarudia kwake katika Aya zinazoambatana nao.

وَإِنْ كُنْتُمْ فِي رَيْبٍ مِمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِنْ مِثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {23}

Na ikiwa mna shaka kwa (hayo) tuliyomteremshia mtumwa wetu, basi leteni sura moja iliyo mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.

فَإِنْ لَمْ تَفْعَلُوا وَلَنْ تَفْعَلُوا فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ {24}

Na msipofanya, na hamtafanya basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, uliowekewa makafiri.

وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِنْ ثَمَرَةٍ رِزْقًا ۙ قَالُوا هَٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِنْ قَبْلُ ۖ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {25}

Na wabashirie walioamini na wakafanya vitendo vizuri, kwamba watapata mabustani yapitayo mito chini yake; kila mara watakapopewa matunda humo kwa riziki, watasema: Haya ndiyo yale tuliyopewa mwanzo, kwani wataletewa hali yakuwa yamefanana na humo watapata wake waliotakasika; na watakaa milele humo.
  • 1. Uislamu ni itikadi na Sharia. Itikadi ni kama kumwamini Mwenyezi Mungu na sifa zake; utume na isma yake, ufufuo na mengineyo katika mfano wake yaliyo katika ghaibu. Halithibiti jambo lolote katika masuala ya kiitikadi isipokuwa kwa njia ya mkataa: Ndio maana Ijtihad haiko katika itikadi. Ama sheria; kama vile ibada, mahusiano ya jamii, hukumu za makosa nk,inajuzu kuzithibitisha kwa njia ya dhana na ijtihad kwa sharti ya kuwepo dalili mkataa ya kusihi amali kwa njia hii hasa.
  • 2. Mwanafalsafa mmoja wa Kiingereza anayeitwa Hume anakanusha misingi ya sababu kwa kusema: “Hakuna dalili kwamba kupatikana kitu lazima kuwe na sababu.” Hatuna la kujibu kauli hii zaidi ya kusema kuwa kuondoa msingi wa sababu nikuondoa msingi wa akili za watu wote. Hakuna yoyote anayeweza kufikiria kupatikana kitu bila ya sababu.