Aya 26-27: Hakika Mwenyezi Mungu Haoni Haya Kupiga Mfano Wowote

Haya

Haya ikinasibishwa kwa mtu maana yake ni kubadilika hali yake ya tabia kuwa hali nyingine, kwa sababu fulani. Haya ya mtu inaweza kuwa nzuri au mbaya. Nzuri, ni ile kuona haya mtu kufanya mambo maovu na machafu.

Kwa hivyo ndio ikawa inasemwa kwa yule anayefanya uovu bila ya kujali: “Kama huoni haya fanya unavyopenda.” Imam Jafar Sadiq (a.s.) amesema; “Hana haya asiyekuwa na Imani.”

Ama ubaya wa haya, ni mtu kuacha kufanya yale yanayotakikana kwa kuogopa; kama vile mtu kuona haya kujifun-disha, kutafuta maarifa, n.k. Amirul Muminin amesema: “Woga uko pamoja na kushindwa; kukosa huletwa na haya, na wakati unapita kama mawingu (ya kiangazi).” Ilisemwa zamani: “Hakuna haya katika dini.”

Hiyo ni haya kwa upande wa binadamu. Ama ikinasibishwa kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), inakuwa makusudio yake ni kuacha kitendo.

Kama ilivyoelezwa katika hadith: “Hakika Mwenyezi Mungu anamuonea haya mzee, yani anaacha kumwadhibu.”

Makusudio ya kupiga mfano ni kuiweka wazi fikra na kuondoa mikanganyo. Makusudio ya ahadi ya Mwenyezi Mungu ni hoja iliyosimama kwa waja wa Mwenyezi Mungu; ni sawa iwe matokeo ya hoja hiyo ni maumbile na akili au kunakili kwenye kuthibiti kutoka katika kitabu chenye kuteremshwa au kutoka kwa Mtume.

Makusudio ya kufunga hapa ni kukata na kuhukumu. Ahadi kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu iliyopitishwa ni kumfanya peke Yake na kumfanyia ikhlas jambo ambalo linafahamika kutokana na akili na kuthibitishwa na sharia.

Makusudio ya kukata aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu kuungwa ni maamrisho yake na makatazo yake. Kwa mujibu wa irabu za kinahaw (sarufi) inawezekana kuwa maana yake ni, “Hakika Mwenyezi Mungu haachi kujaalia mbu kuwa mfano”. Pia inawezekana, kuwa maana yake ni, “Hakika Mwenyezi Mungu haachi kujaalia kitu chochote kuwa mfano, hata kama kitu hicho ni mbu”.

Uongofu Na Upotevu

Uongofu una maana nyingi; kama ifuatavyo:-

• Kubainisha na kuongoza. Aya nyingi katika Qur’an zina maana hiyo; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: Na hapana lililozuilia watu kuamini ulipowajia uongofu(17:94)

Vile vile kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَلَقَدْ جَاءَهُمْ مِنْ رَبِّهِمُ الْهُدَىٰ {23}

“Hakika umewajia uongofu kutoka kwa Mola wao(53:23)

Yaani; wala hapana ubainifu wa Mwenyezi Mungu isipokuwa ule waliokuja nao Mitume au uliohukumiwa na hukumu ya wazi isiyokuwa na shaka.

• Kukubali mtu nasaha na kunufaika nayo; kama asemavyo Mwenyezi Mungu:

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَكُمُ الْحَقُّ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا ۖ{108}

“Sema: Enyi watu! Haki imekwisha wajia kutoka kwa Mola wenu, basi anayeongoka anaongoka kwa nafsi yake na anayepotea anapotea kwa nafsi yake.(10:108).

• Tawfiq na msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia mahsusi; kama anavyosema Mwenyezi Mungu:

وَلَٰكِنَّ اللَّهَ يَهْدِي مَنْ يَشَاءُ ۗ{272}

...lakini Mwenyezi Mungu humuongoza amtakaye...” (2:272)

Na kauli yake:

وَأَنَّ اللَّهَ يَهْدِي مَنْ يُرِيدُ {16}

“...na hakika Mwenyezi Mungu humuongoza amtakaye... (22:16)

Yaani anamwafikisha kwenye amali kwa uongofu na kumwandalia njia ya kuendea. Kimsingi ni kwamba uongofu kwa maana ya ubainifu tu haulazimishi kuwafikisha kwenye amali; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.): “Si juu yako uongofu wao. (2:272)

Yaani si juu yako wafanye amali kwa uongofu wako au wasifanye; isipokuwa ni juu yako kubainisha tu.

• Thawabu; kama kauli yake Mwenyezi Mungu: Hakika wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, Mola wao atawaongoza kwa sababu ya Imani yao; itakuwa inapita mito mbele yao katika mabustani yenye neema. (10:9)

Yaani atawapa thawabu kwa sababu ya imani yao.

• Mwenye Kuongoza na mwenye kubainisha, kwa kuangalia kwamba uongofu umepatikana kwa sababu yake. Hayo ndiyo maksudio katika Aya hii tunayoizungumzia. Akasema mwenye mwenye Majmaul- Bayan: Kauli yake Mwenyezi Mungu: “Huongoza wengi kwa mfano huo”.

Anakusudia wale ambao wameamini. Kwa kuwa uongofu umepatikana kwa sababu ya Mwenyezi Mungu, basi umetengenezwa kwake.

• Hukumu; kama kusema: “Kadhi amehukumu sawa sawa”; yaani amehukumu kwa uadilifu wake. Maana haya yanafaa kuyanasibisha kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

Upotevu, nao pia una maana nyingi: Miongoni mwayo ni haya yafuatayo:-

• Kutia mashaka, kuingiza katika ufisadi na kuizuilia dini na haki. Maana haya hayategemezwi kwa Mwenyezi Mungu kwa hali yoyote; bali hunasibishwa kwa Iblis na wafuasi wake;
kama asemayo Mwenyezi Mungu akimzungumzia Iblis, Firaun na Samiri:

وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ{119}

“kwa hakika nitawapoteza na nitawatamanisha...” (4:119)

وَأَضَلَّ فِرْعَوْنُ قَوْمَهُ وَمَا هَدَىٰ {79}

“Na Firaun akawapoteza watu wake na hakuwaongoza. (20:79)

وَأَضَلَّهُمُ السَّامِرِيُّ {85}

...Na akawapoteza Samiri” (20:85)

• Adhabu, Aya nyingi katika Qur’an zimekuja kwa maana haya; kama vile:

كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّهُ الْكَافِرِينَ {74}

“Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu huwapoteza makafiri “(40:74)

وَيُضِلُّ اللَّهُ الظَّالِمِينَ ۚ{27}

...Na Mwenyezi Mungu huwapoteza madhalimu...” (14:27)

كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّهُ مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ مُرْتَابٌ {34}

“Kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza aliyepita kiasi mwenye shaka” (40:34)

Yaani anawaadhibu waongo, makafiri na madhalimu:

• Kukusudiwa jina la mpotezaji, kama kusema “Amepotezwa na fulani” Ukikusudia kumnasibisha kwenye upotevu na kumzingatia kuwa ni katika wapotevu.

• Kujitenga mtu na nafsi yake. Mwenye kumpuuza mtoto wake bila ya malezi yoyote au usaidizi wowote, inafaa kuambiwa amempoteza mtoto wake.

• Kupoteza kitu. Husemwa: “Fulani amepoteza ngamia wake”. Maana haya vile vile hayanasibishwi kwa Mwenyezi Mungu.

• Majaribio na mitihani, kwa namna ambayo hupatikana upotevu kwenye ubainifu ambao Mwenyezi Mungu humtahini mja wake. Mwenye Majmau anasema:”Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anawatahini kwa mifano hii waja wake, kwa hiyo huwapoteza watu wengi na huwaongoza watu wengi.”

Maelezo

Maana yanayopatikana kutokana na Aya mbili hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu haachi kupiga mifano kwa vitu ambavyo wajinga wanaviona ni duni; kama buibui, nzi, mbu na wengineo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Muumba na Mola wa kila kitu; kwake bawa la mbu na ulimwengu mzima ni sawa tu.

Zaidi hayo kupiga mifano kunapatikana katika lugha zote ili kuziweka wazi fikra kwa kuzikutanisha na vyenye kuhisiwa. Kwa hivyo, kila linalohakikisha kupatikana kwa lengo hili linafaa kufanywa ni mfano, liwe dogo au kubwa; na kwalo inatimu hoja kwa kila mpinzani.

Mwenyezi Mungu amewatahini watu kwa mifano hii, kama alivyowatahini kwa mambo mengine miongoni mwa dalili na ishara. Wengi wakaitumia na wengi wakapinga.
Wale walioitumia ni wale wema walio waumini na waliopinga ni wale mafasiki waliopotea.

Kumesihi kuutegemeza uongofu na upotevu kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kuangalia kuwa Yeye ndiye aliyepiga mifano ambayo imekuwa ni rehema kwa aliyewaidhika na ni mateso kwa asiyewaidhika.

Ni vizuri kuleta mfano ili kufafanua fikra hii: Mwanachuoni alipata elimu na ikamwinua, halafu akahusudiwa na hasadi ikadhuru kiwiliwili na akili yake; kama alivyosema Imam Ali (a.s.) “Siha ya mwili ni husuda kuwa chache.”

Inafaa kusema kuwa mwanachuoni huyu ndiye aliyemfanya hasidi kufanya uovu huu; au kama vile unavyosema: “Uzuri wa mwanamke fulani umeharibu akili ya mwanamume fulani.” Pengine wawili hao hata hawajuani.

Kwa mtazamo huu ndipo umenasibishwa upotevu kwa Mwenyezi Mungu kimajazi. Kwa vile Yeye ndiye aliyebainisha hoja na kuziweka wazi, na mhalifu alipozikhalifu akapotea. Lau Mwenyezi Mungu asingelibainisha, basi kusingekuwepo na suala la utiifu na uasi na asingelikuwako mpotevu na mwongofu.

Mwenyezi Mungu amemwita yule asiyepata onyo kwa mifano: Fasiki, mvunja ahadi na mkataji wa yale aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu ya ungwe, ambayo ni kufuatilia mambo ya heri na kuungana na watu wa heri na mengineyo ya kusaidiana kwenye heri.

Kuumba Na Kuweka Sharia

Mwenyezi Mungu ana matakwa mawili: Matakwa ya kuumba ibara yake ni “Kun fayakun” (kuwa na ikawa). Kwa matakwa haya kinapatikana ambacho hakikuweko.

Matakwa ya pili, ni ya kuweko sharia ambayo yanakuwa katika ibara ya kuamrisha na kukataza na kulingania kwenye heri na kuacha shari. Mja akifanya heri huifanya kwa matakwa yake na hiyari yake bila ya kulazimishwa. Vile vile akifanya shari na kuacha heri.

Ikiwa utekelezaji wa hukumu zote za dini unafungamana na matakwa ya wale wenye kukalifiwa na hukumu hizo na hiyari, wala kusiweko mwenye kuwachunga isipokuwa wao wenyewe, basi itakuwa ni kosa kusema kuwa dini imeathiri katika kuanguka wafuasi wake na wenye kunasibika nayo.

Ndio, lau wangeliitumia dini na wakaifuata kwa ukamilifu kwenye vitendo vyao, ingelifaa kufanywa dini ni kipimo cha kupanda na kuanguka kwao. Kwa hali hiyo basi ndio inabainika hasadi na chuki dhidi ya Uislamu katika kauli ya aliyesema; “Unyonge wa Waislamu ni dalili ya unyonge wa Uislamu na mafundisho yake.”

Kutokana na matamko ya mkosaji, inajuzu kwetu kunasibisha katika dini ya Kikristo kila ufasiki, uovu, na kuvunjiana heshima katika Ulaya na Amerika. Vile vile kunasibisha uharibifu wa vita vyote vilivyoathiri dola za Kikristo katika Mashariki na Magharibi ya dunia mpaka kulipuka bomu la Atomiki katika Hiroshima, na mabomu yaliyotupwa Veitnam; na hata kubadili maumbile1 na kuongezeka idadi ya makosa na maovu siku baada ya siku katika Ulaya na Amerika mpaka kufikia hatua ya kuhalalisha ulawiti katika Uingereza kikanuni na kikanisa.
Je, yote hayo na mengi mengineyo yanafaa kunasibishwa kwa Masih (a.s.)? Hapana! Ametakasika na uchafu wote huu.

Kama tungechukulia uzushi wa huyo mzushi, angelikuwa Myahudi wa Yemen ni sawa na Myahudi wa New York na Mkristo wa Misri ni sawa na wa Paris kimaendeleo.

Kuacha kuendelea miji kuna sababu nyingi sana zisizokuwa za dini; hasa ujinga, Historia ya kubakia katika unyonge na matatizo ya mazingira, na kukosa kuchangayika miji iliyoendelea na ile isiyoendelea.2 Lau kama si kuchanganyika Waislamu wa kwanza namataifa mengine isingebaki athari yoyote ya maendeleo ya kiislamu. Naam! Uislamu ulikuwa ndio msukumo wa mchanganyiko huo.

Kwa ufupi sababu za kutoendelea hazitokani na tabia ya Uislamu wala ya Ukristo au wasiokuwa na dini, bali ni kutokana na hali za kijamii.

Tutarudia kufafanua zaidi tutakapofika kwenye Aya za maudhui ya Jabri na Tafwidh (kutenzwa nguvu na kuachiwa). Na hayo tumeyaelezea kwa ufafanuzi katika kitabu Maalimul Falsafatul Islamiya na kitabu Maa’shiatul Imamiya.

كَيْفَ تَكْفُرُونَ بِاللَّهِ وَكُنْتُمْ أَمْوَاتًا فَأَحْيَاكُمْ ۖ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {28}

Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu akawafufua! Kisha atawafisha tena atawafufua, kasha kwake mtarejeshwa.

هُوَ الَّذِي خَلَقَ لَكُمْ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا ثُمَّ اسْتَوَىٰ إِلَى السَّمَاءِ فَسَوَّاهُنَّ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ ۚ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ {29}

Yeye ndiye aliwaumbia vyote vilivyomo katika ardhi tena akakusudia kuumba mbingu na akazifanya saba. Naye ni mjuzi wa kila kitu.
  • 1. Sehemu kubwa ya Hiroshima na Nagasaki zilizopigwa bomu la Atomiki ardhi yake haimei kitu, na watoto wengi hadi leo huzaliwa na kasoro mwilini kutokana na athari ya bomu hilo - Mfasiri
  • 2. Dini ni sawa na baraza la kutunga sharia. Ama utekelezaji ni wa mwingine. Umoja wa mataifa umefeli katika maazimio yake mengi muhimu na baraza la usalama nalo likafeli kuyatekeleza. Vile vile haikufaulu mikutano ya uongozi wa siasa zisizofungamana na upande wowote na wengineo. Mara ngapi wameshindwa, lakini lawama halikuwa lao. Sasa itakuwaje Uislamu ulaumiwe kwa sababu ya wanaoitwa W aislamu.