Aya 28 – 29: Vipi Mnamkanusha Mwenyezi Mungu

Mwanadamu Ni Hoja

Kwa dhahiri ya mfumo wa maneno inaonyesha kwamba msemo katika Aya mbili hizi unaelekezwa kwa yule ambaye hanufaiki na chochote katika kupigiwa mfano, lakini ilivyo hasa msemo unamhusu kila anayemkufuru Mwenyezi Mungu pamoja na kuweko dalili hizi zisizokuwa na idadi ambazo ni pamoja na huyo kafiri mkanushaji.

Kwani yeye kwa dhati yake ni dalili iliyo wazi ya kupatikana aliyemuumba. Kama si hivyo ni nani basi aliyemfanya katika nidhamu hii kali kabisa, akakiweka kila kitu mahala pake panapohusika, kuanzia chembe hai za ubongo na moyo mpaka kwenye utumbo na maini, kwenye usikizi na uoni na mpaka kwenye miishilio isiyokuwa na mwisho. Kila kimoja kinatekeleza umuhimu wake kwa uangalifu bila ya usimamizi wowote kutoka kwa kiumbe.

Vile vile ni kutoka wapi umekuja ufahamu huu na akili ambayo mtu analikurubisha lililo mbali, kulisahilisha zito na kukusanya yaliyo katika ardhi katika nyumba moja, kisha akaendelea zaidi na kuweka athari zake mwezini.

Je haya na mengineyo yamekuja kibahati na (kisadfa) tu? Je kuna vitu hasa vinavyoendesha mpangilio huo? Je Sayansi inaweza kujibu hayo? Na je majibu yatatokana na kuhusika na majaribio ya Kisayansi? (14:34)

Walijaribu wenye kujaribu kujibu, lakini yakajitokeza maelfu ya maswali. Sisi hatukanushi kabisa kwamba wataalamu wa kisayansi wamefikilia kwenye ukweli wa kushangaza katika tiba, ukulima na viwanda, lakini wataalamu wa uhai wameambulia patupu wakitafuta siri ya uhai na asili yake; na hawana chochote isipokuwa dhana tu, ambayo haitoshei haki.

Kimsingi, kila Sayansi inaposhindwa kutafsiri jambo hulihukumia kwa kinyume chake.
Ikawa kupatikana mtu ni nguvu ya hoja kuhusu kuwapo Mwenyezi Mungu (s.w.t.), inakuaje hoja hii ipinge hoja inayolazimiana nayo? Vipi mtu aliye na fasihi aweze kupinga fikra ya fasihi na balagha? Basi hapo ndio inakuwa siri ya kustaajabisha katika kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

Vipi mnakanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu akawafufua.

Yaani ni maajabu yaliyoje ya kumkanusha kwenu Mwenyezi Mungu na hali nyinyi kwa dhati kabisa ni dalili wazi ya kuwepo Mwenyezi Mungu. Vyovyote mtakavyokanusha, je, mnaweza kukanusha kwamba nyinyi hamkuwa kitu chochote kisha ndipo mkawa kitu kinachosikia, kuona, kuhisi na kutambua, pamoja na kusema na kutenda? Je, hiyo si dalili inayoeleza kupatikana nguvu iliyoumba?

Kweli kabisa. “Hakika binaadamu ni dhalimu mkubwa mwenye kukanusha mno!” Hakukuwa kumkanusha Mwenyezi Mungu isipokuwa ni kukanusha na kutojijua huyo mkanushaji.1 Na asiyejijua, basi ndio hamjui mwingine. Kwa hali hiyo ndiyo tunapata tafsiri ya hadith tukufu: “Anayejijua zaidi ni yule anayemjua zaidi Mola wake.”

Unaweza kuuliza: Ni akili gani inayoweza kujikanusha yenyewe? Je hayo yanaingia akilini? Tunajibu: Hakika hoja inalazimian na chenye kutolewa hoja; na kukanusha ulazima kunapelekea kukanusha chenye kulazimiwa. Kwa hivyo mwenye kukanu-sha dalili ya matamko, kwa mfano, kutokana na maana iliyowekwa, atakuwa ameyakanusha matamko yenyewe atake asitake, wala hakumfalii yeye kuyakubali wakati anakanusha dalili zake.

Hivi ndivyo ilivyo kwa mwenye kumka-nusha Mwenyezi Mungu. Kwani kuwapo kwake ni dalili ya kuwapo muumbaji, na kupatikana muumbaji kunatolewa dalili na kupatikana kwake yeye mkanushaji. Basi akikanusha chenye kutolewa dalili ndio amekanusha dalili yenyewe, ambayo ndiyo huyo mkanushaji kwa dhati yake bila ya kujijua wala kujitambua.

Hivyo ndivyo anavyofanya mjinga anayejiepusha na maumbile anayoishi nayo na kumpa uhai, kupinga dalili zilizo wazi na kuamini vigano na mambo ya kijinga.

Mauti Na Uhai Mara Mbili

Makusudio ya kufa kwa kwanza kunak-oonyesha na neno “Mlikuwa wafu” ni kutokuwapo kwa mara ya kwanza, Na makusudio ya uhai wa kwanza, “Akawafufua” ni kuumbwa baada ya kutokuwapo.

Mauti ya pili, Kisha atawaua, ni mauti haya yaliyozoeleka; na kufufuliwa mara ya pili ni kufufuliwa kwa ajili ya hisabu na malipo.

Tena Atawafufua

Unaweza kuuliza, je roho inafarikiana na mwili baada ya kwisha nguvu zake za uhai, kwa namna ambayo lau nguvu zingebakia, basi roho ingelibaki na bina -damu milele? Au ni kwamba inawezekana roho kufarikiana na mwili hata ukiwa na nguvu za kuishi kwa ukamilifu bila ya kutokea uharibifu wowote mwilini?

Jibu: Watu wa kimaada wamechukulia kauli ya kwanza na wengine wamechukulia kauli ya pili. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ لَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً ۖ وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ {34}

...Utakapofika muda wao hawatakawia (hata) saa moja wala hawatatangulia” (7:34)

Inaweza kuchukuwa njia zote mbili. Kwani haikubainisha sababu ya kufika muda wao. Je ni kuharibika mwili au ni kitu kingine.

Kauli yake Mwenyezi Mungu:

الَّذِينَ خَرَجُوا مِنْ دِيَارِهِمْ وَهُمْ أُلُوفٌ حَذَرَ الْمَوْتِ فَقَالَ لَهُمُ اللَّهُ مُوتُوا{243}

...ambao walitoka katika majumba yao nao walikuwa maelfu wakiogopa mauti? Mwenyezi Mungu akawaambia ‘Kufeni’ (2:243)

Na kauli yake:

قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَٰذِهِ اللَّهُ بَعْدَ مَوْتِهَا ۖ فَأَمَاتَهُ اللَّهُ مِائَةَ عَامٍ{259}

Akasema Mwenyezi Mungu atuuhuisha vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu alimfisha kwa miaka mia... (2:259)

Aya mbili hizo zinahusu matukio fulani tu. Haziingii katika matukio mingine.

Vyovyote iwavyo hatuna kitu kinachotuthibitishia, lakini tunayoshuhudia ni kwamba watu wengi wanafikiwa na mauti nao bado wabichi wakiwa na afya nzuri na kwamba wengi wanatembea na kufurahi nao wako katika umri mkubwa na magonjwa tele.

Madaktari wengi mahodari wanamwambia mgonjwa utakufa baada ya saa chache tu, lakini akaishi muda mrefu!

Ufufuo

Ufufuo katika Uislamu ni msingi wa tatu baada ya Tawhid na Utume, misngi ambayo tumeshaielezea. Mwenyezi Mungu ameyatolea habari marejeo (ufufuo) aliposema:

Kisha atawafufua kisha kwake mtarejeshwa.

Ametoa dalili au kuukurubisha uwezekano wa ufufuo katika Aya nyingi. Miongoni mwazo ni:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَلَمْ يَعْيَ بِخَلْقِهِنَّ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَنْ يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ ۚ{33}

“Je! hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi na hakuchoka kwa kuziumba, ana uwezo wa kuwafufua wafu?” (46:33)

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنْ كُنْتُمْ فِي رَيْبٍ مِنَ الْبَعْثِ فَإِنَّا خَلَقْنَاكُمْ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ مِنْ نُطْفَةٍ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍ{5}

“Enyi watu! Kama mmo katika shaka juu ya ufufuo, basi kwa hakika tuliwaumba kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na kipande cha damu...” (22:5)

Hakuna anayetia shaka kwamba Mwenye kuumba kitu huwa rahisi kwake kuvikusanya viungo vyake baada ya kuwa mbali mbali; bali kukusanya ni rahisi zaidi kuliko kuumba tena.

Mwenye kujenga jumba kubwa ni rahisi kwake kujenga kibanda.2

Ninacho kitabu maalum nilichoandika cha maudhui haya kinachoitwa ‘Al-akhira wal aql’ kisha nikayalinganisha na kitabu ‘Al-Islam wal aql’ ambavyo vimechapishwa mara nyingi sana.

Yaliyo Katika Ardhi

Baada ya Mwenyezi Mungu kumkumbusha mtu neema ya kupatikana kwake, anamtajia wingi wa neema alizonazo, ikiwa ni pamoja na kula na kunywa, mavazi, vipando, mandhari na mengineyo katika starehe za ardhi na heri zake zisizohisabika.

Wametoa dalili mafakihi kwa kauli ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.): “Yeye ndiye aliyewaumbia vyote vilivyo katika ardhi.” Kwamba vitu vyote kabla ya kuja sharia ni halali, na kwamba haimfailii kiumbe kuharamisha kitu isipokuwa kwa dalili. Mwenyezi Mungu anasema:

قُلْ أَرَأَيْتُمْ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ لَكُمْ مِنْ رِزْقٍ فَجَعَلْتُمْ مِنْهُ حَرَامًا وَحَلَالًا قُلْ آللَّهُ أَذِنَ لَكُمْ ۖ أَمْ عَلَى اللَّهِ تَفْتَرُونَ {59}

“Sema: Je, mnaonaje zile riziki alizowateremshia Mwenyezi Mungu kisha mkafanya katika hizo (kuwa) haram na (nyingine) halali. Sema, Je, Mwenyezi Mungu amewaruhusu au mnamzulia Mwenyezi Mungu tu?(10:59)

Pengine hutolewa dalili kwa Aya hii kwamba ardhi haimilikiwi. Kinachofaa kumilikiwa ni kile kinachozalishwa na ardhi. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: “Amewaumbia vilivyomo ardhini na hakusema amewaumbia ardhi.”

Mbingi Saba

Maana ya neno istawa hapa ni kukusudia. Kuzihusisha mbingu saba hakufahamishi kuwa ndio hizo hizo tu wala hakukanushi kabisa kuwapo nyinginezo. Wamethibitisha wanavyuoni wa elimu ya usul na lugha kwamba idadi sio ufahamisho, mwenye kusema mimi ninamiliki vitabu saba haimaanishi kwamba hamiliki vingine. Analitilia nguvu hilo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipomwambia Mtume wake (s.a.w.):

إِنْ تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ سَبْعِينَ مَرَّةً فَلَنْ يَغْفِرَ اللَّهُ لَهُمْ ۚ{80}

“Hata ukiwaombea msamaha mara sabini, Mwenyezi Mungu hatawasamehe.” (9:80)

Mtume (s.a.w.) akasema: “Lau ningelijua kuwa Mwenyezi Mungu atawasamehe nikizidisha sabini ningelifanya.”

Huenda ikawa sababu ya kutaja saba ni kwamba hizo saba zina mambo maalum yasiyopatikana katika mbingu nyingine.

وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي جَاعِلٌ فِي الْأَرْضِ خَلِيفَةً ۖ قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَنْ يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ وَنَحْنُ نُسَبِّحُ بِحَمْدِكَ وَنُقَدِّسُ لَكَ ۖ قَالَ إِنِّي أَعْلَمُ مَا لَا تَعْلَمُونَ {30}

Na Mola wako alipowaambia Malaika mimi nitaweka Khalifa katika ardhi. Wakasema (Malaika) utaweka humo watakaofanya uharibifu humo na kumwaga dmau, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na kukutaja kwa utakatifu wako?”Akasema Mwenyezi Mungu: Hakika mimi nayajua msiyoyajua.

وَعَلَّمَ آدَمَ الْأَسْمَاءَ كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلَى الْمَلَائِكَةِ فَقَالَ أَنْبِئُونِي بِأَسْمَاءِ هَٰؤُلَاءِ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {31}

Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika akasema Niambieni majina ya vitu hivi

قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنْتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ {32}

Wakasema: Utakatifu ni wako hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha; hakika wewe ndiwe mjuzi, mwenyw hekima.

قَالَ يَا آدَمُ أَنْبِئْهُمْ بِأَسْمَائِهِمْ ۖ فَلَمَّا أَنْبَأَهُمْ بِأَسْمَائِهِمْ قَالَ أَلَمْ أَقُلْ لَكُمْ إِنِّي أَعْلَمُ غَيْبَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَأَعْلَمُ مَا تُبْدُونَ وَمَا كُنْتُمْ تَكْتُمُونَ {33}

Akasema: Ewe Adam waambie majina yake. Alipowaambia majina yake. Alisema (Mwenyezi Mungu): Sikuwaambia kwamba mimi ninajua siri za mbinguni na za ardhini; tena najua mnayoyadhihirisha na mliyokuwa mkiyaficha.
  • 1. Anasema Charlie Champlin, mchezaji sinema mashuhuri wa kimataifa, ambaye umashuhuri wake umezidi ule wa Gandi: “Katika mamlaka isiyojulikana kuna nguvu isiyokuwa na mpaka.” Na anasema Kierkegaard “Hakika Mwenyezi Mungu anajitokeza kwenye nafsi yenye kukata tamaa katika wakati mgumu wa kukata tamaa na katika lindi la makosa.”
  • 2. Mnamo mwaka 1959 Mustafa Mahmud, Mmisri, alitunga kitabu Allahu W al-insan (Mungu na mtu) katika kitabu hicho alikana Mungu na ufufuo, nami nikamjibu kwa kutunga kitabu Allahu wal-Aqli (Mungu na Akili) mpaka sasa kimechapishwa mara tano. Ilipofika tarehe 10.4.1967 nilimsomeya makala Mustafa Mahmud katika jarida la Ruz Al-Yusuf, inayosema: Imani yangu inashikilia kwamba mimi nilikuwako kabla ya maisha yangu haya kwa jina jingine, na kwamba mimi sitaisha baada ya kufa kwangu isipokuwa nitarudi kwenye uhai kwa namna nyingine, na maisha yanaendelea.