Aya 35 – 39: Adamu Peponi

Mwenyezi Mungu aliamwamrisha Adam na Hawa kukaa peponi; akawahalalishia kula yaliyomo ndani yake isipokuwa mti mmoja tu, waliokatazwa kuula. Lakini shetani aliwahadaa kwa kuwataka waule.

Walipokubaliana naye ilipita hekima yake Mwenyezi Mungu ya kuwatoa pepo ni kuwapeleka ardhini na akawatia mtihani kwa taklifa na kazi, uzima na ugonjwa, shida na raha, kisha mauti muda wake unapofika.

Adam alihisi msiba na akajuta. Akamwomba Mola wake kwa ikhlasi amtakabalie toba yake, akamkubalia na akamsamehe, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba Mwenye rehema.

Nadhani kwamba Hawa pia alitubia pamoja na Adam, lakini Mwenyezi Mungu hakuitaja toba yake. Hakuna tofauti kati ya Mwanamume na mwanamke. Mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na akafanya amali njema, Mwenyezi Mungu atamuweka peponi, na mwenye amali mbaya atamwingiza motoni awe mume au mke.

Wamejiingiza wafasiri wengi kuelezea pepo aliyotoka Adam, ilikuwa wapi? Mti ulikuwa mtini au ngano? Kuhusu nyoka ambaye aliingia Iblis ndani yake, na mahali aliposhukia Adam, je palikuwa India au Hijaz? Na mengineyo yaliyokuja katika hadithi za Kiisrail. Qur’an haikudokeza lolote katika hayo; wala haikuthibiti katika hadithi kwa njia sahihi. Pia akili haiwezi kujua chochote katika hayo, na hayo hayaambatani na maisha kwa karibu au mbali. Hata hivyo hakuma budi kutanabahisha mambo yafuatayo:-

Hawa Na Ubavu Wa Adam

Imeenea habari kwamba Hawa aliumbwa kutokana na ubavu wa Adam, lakini hakuna maelezo sahihi ya kutegemewa. Na habari zilizoelezea hilo si za kutegemewa. Ikiwa tutazichukulia kuwa ni sahihi basi ni kwamba makusudio yake ni kuonyesha usawa na kukosa kutofautisha kati ya mume na mke, yaani mke ametokana na mume na mume naye ametokana na mke.

Katika kitabu Malla yahdhur hul-faqih, imesemwa, Imam Sadiq (a.s.) wakati alipoulizwa usahihi wa uvumi huu, aliukanusha na akasema: “Mwenyezi Mungu Ametukuka na hayo kabisa. Je Mwenyezi Mungu alishindwa kumuumbia Adam mke isipokuwa kutokana na ubavu wake mpaka ikabidi Adam aoe sehemu yake ya mwili?”

Mtaka Yote Hukosa Yote

Hekima ya Mwenyezi Mungu ilipitisha kuwa Adam akae na mkewe peponi wakati fulani, kisha atoke kwa sababu maalum ambayo wao wawili ndio walioifanya kwa matakwa yao na hiyari yao; lau si hivyo wangelibaki peponi milele wakistarehe bila ya taabu yoyote.

Vile vile hekima yake Mwenyezi Mungu ilipitisha kuwa Adam na Hawa wabaki katika ardhi hii mpaka watakapozaana na kupatikana koo na vizazi, wakati ambapo wataulizwa wote, kauli na vitendo walivyovifanya. Kama ilivyohukumilia hekima yake kurudi Adam na mkewe peponi baada ya kufa na wadumu humo milele.1

Unaweza kuuliza: Kuna hekima gani ya kuingia Adam peponi na kutoka kuja ardhini, kisha kuitoka hiyo ardhi na kurudi tena peponi mara ya pili baada ya kufa?

Jibu: Huenda hekima iliyopo ni kuwa Adam apitie majaribio atakayonufaika nayo na kufaidika nayo, yeye na watoto wake, na kurudi kwenye pepo hii akiwa amejaa majaribio yenye kunufaisha.

Yaani ni kwamba mtu hawezi kuishi milele bure bure tu vile anavyotaka na kwamba mwenye kuyachunga hayo majaribio kwa kuyamiliki matakwa yake bila ya kukubali kusukumwa na matamanio yake, basi ataishi maisha mazuri ya wema usiokuwa na mwisho.

Na mwenye kuwa na msimamo hafifu na akawa mdhaifu mbele ya matamanio yake, atakuwa amepata aliyoyapata Adam majuto, kujaribiwa, taabu na mashaka.

Isma (Kuhifadhiwa Mitume)

Wameafikiana Waislamu wote kwamba Adam ni katika Mitume, na Mitume kama inavyofahamika ni wenye kuhifadhiwa na madhambi na makosa. Sasa nini maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu; “Akawahadaa shetani katika hali waliyokuwa nayo?”

Kwa ajili hiyo ndio wameonelea wanachuoni kuwa iko haja kubwa ya kufanya utafiti juu ya Isma ya Mitume; kisha kuifasiri Aya hii katika hali ambayo italeta natija. Nasi tunakusanya kauli juu ya hilo kama ifuatavyo ili iwe ni asili katika kila linaloambatana na maudhui haya.

Maana ya Isma ya Mtume ni kutakata na makosa katika kila jambo linaloambatana na dini na hukumu zake, kiasi ambacho atafikilia Mtume utakatifu na elimu na kumjua Mwenyezi Mungu na yale anayoyataka kwa waja wake; kwa hali ambayo inakuwa muhali kuikhalifu, iwe kwa makusudi au kwa kusahau.

Mwenye kuthibitisha Isma kwa Mitume kwa maana hayo na kwa mafungu yake yote yatakayokuja, ataifanyia taawil Aya inayopingana na dhahiri ya msingi huu, kwa kwenda na kanuni ya kiujumla ambayo ni wajibu wa kufanya taawil kwa kuafikiana na dhahiri ya akili. Na, mwenye kukanusha Isma kwa mitume, atabakisha dhahiri kwa dhahiri yake.

Wanavyuoni wa madhehebu mbali mbali wana kauli nyingi katika Isma, zenye kukhitalifiana kwa tofauti za mafungu yafuatayo:

1. Isma katika itikadi na misingi ya dini; yaani kutakasika kwa Mtume kutokana na ukafiri na ulahidi. Hilo ni lenye kuthibiti kwa kila Mtume kimisingi na kwa maafikiano. Kwani haiingii akilini kuwa Mtume amkanushe yule aliyempa Utume.

2. Isma katika kufikisha amri za Mwe-nyezi Mungu. Akisema, Mwenyezi Mungu anaamrisha hili na anakataza lile, basi amri itakuwa ile ile aliyoisema. Wameafikiana Shia Imamiya kuthibiti Isma hii kwa kila Mtume.

Kwa sababu lengo la kufikisha ni kuwachukua wale wanaokalifiwa na sharia kwenye haki. Akikosea mwenye kufikisha itakuwa lengo la kufikisha limebatilika. Hayo yanatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ {3}

Wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake)” (53:3)

Na kauli yake:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا ۚ{7}

“Na anachowapa Mtume kipokeeni na anachowakataza jiepusheni nacho. (59:7)

Kwa maneno mengine Isma ya Mitume haiwezi kuepukana kabisa na kusema kuwa kauli yao, kitendo na uthibittisho wao ni hoja na dalili.

Baada ya Razi kusema katika tafsiri yake: “Wameafikiana Waislamu kwamba kukosea katika kufikisha hakujuzu kwa kusudi au kusahau,” aliendelea kusema: “Wako watu wanaojuzisha hilo kwa kusahau.” Sijui aliwakusudia watu gani.

3. Isma katika Fatwa; yaani Mtume kufutu kitu cha wote; kama kuharamisha riba na kuhalalisha biashara. Razi ametaja kifungu hiki katika tafsiri yake kwa kusema: “Wameafikiana kwamba kukosea Mtume katika hilo hakujuzu kwa kukusudia ama kwa kusahau, wengine wamejuzisha na wengine hawakujuzisha.”

Kifungu hiki kinarudi katika kifungu cha pili cha kufikisha. Inatakikana kifanywe kifungu cha tatu ni Isma katika hukumu sio fatwa.2

Wameafikiana Imamiya kwamba Mtume ni mwenye kuhifadhiwa na makosa katika hukumu kama ilivyo katika kufikisha; pamoja na kwamba kwao wamenakili kutoka kwa Mtume mtukufu (s.a.w.) kwamba yeye amesema:

“Hakika mimi ninahukumu kati yenu kwa hoja (ushahidi) na yamini. Mimi ni mtu. Nyinyi mkiwa na ugomvi, huenda mmoja akawa mjanja kuliko adui yake - kwa hiyo nitahukumu kutokana na nilivyosikia kutoka kwake, basi kama mtu nikimpa haki ya ndugu yake asichukue; kwani ninamkatia kipande cha moto.” Kama ni kosa hapo katika hukumu yake, imetokana na hoja au kiapo n.k. yaani katika kutegemea hukumu sio katika hakimu mwenyewe.

4. Isma katika vitendo vya Mitume na mwenendo wao hasa. Amesema Iji katika Mawaqif Juz.5; “Hakika Hashawiya wanajuzisha kwa Mitume kufanya madhambi makubwa; kama uwongo, kwa makusudi au kusahau; na wamekataa Ash’aira - yaani Sunni - kwa kusudi sio kusahau. Ama madhambi madogo inajuzu kwao hata kwa kusudi wachilia mbali kusahau.”

Wamesema Imamiya: Hakika Mitume ni wenye kuhifadhiwa katika kila wanayoyasema na wanayoyatenda; kama vile ambavyo wamehifadhiwa katika itikadi na kufikisha. Ni muhali kwao kufanya madhambi madogo, wachilia mbali makubwa, na wala hayawezi kuwatokea kabisa, si kwa kukusudia wala kusahau, si kabla ya Utume wala baada yake.

Aya yoyote ambayo haiafikiani dhahiri yake na msingi huu, basi wameiletea taawil. Wakasema katika Adam kula tunda, kwamba kukatazwa kule hakukua ni kwa uharamu au kwa ibada, kama vile kukatazwa kuzini na kuiba, bali kulikuwa ni kimwongozo na nasaha tu; kama kumwambia mtu unayemtakia heri, ‘usinunue nguo hii kwa sababu sio nzuri,’ ikiwa hakukusikia, basi atakuwa hakufanya haramu wala hakumdhulumu mtu; atakuwa amejidhulumu yeye mwenyewe na amefanya jambo ambalo ilikuwa ni vizuri asilifanye.

Kimsingi kula tunda hakuambatani na kumdhulumu mtu yeyote isipokuwa kula tu. Kwa hivyo maana ya toba ya Adam inakuwa ni toba ya kuacha kutenda jambo lenye kupendekezwa na lililo bora. Na, jambo la toba ni jepesi sana, kwani mara nyingi Mitume na watu wema hulikariri neno “Namtaka msamaha Mwenyezi Mungu na ninatubia.”

Inatosha kuwa ni dalili juu ya hilo dua ya Imam Zainul-Abidin katika Sahifa Sajjadiyya yenye kujulikana kwa dua ya toba akisema: “Ninaomba msamaha kutokana na ujinga wangu.”

Ahlul-Bait

Amesema Muhyiddini anayejulikana kwa jina Ibnul Arabi katika kitabu chake Futuhatul Makkiya Juz. 1; Uk. 196 chapa ya zamani. “Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemtoharisha Mtume wake na kizazi chake kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا {33}

...Mwenyezi Mungu anawatakia kuwaondolea uchafu enyi watu wa nyumba (ya Mtume) na kuwatakasa kabisa kabisa.(33:33)

“Hakuna kitu kichafu zaidi ya dhambi kwa hivyo hakutegemewi kwa watu wa nyumba (ya Mtume) isipokuwa usafi na utohara, bali wao ni dhati ya utohara.”

Kisha akasema Ibnul Arabi kwamba Salmanul Farisi ni mwenye kuhifadhiwa na dhambi kwa ushahidi wa Mwenyezi Mungu, na imethibiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba yeye amesema: “Salman ni katika sisi Ahlul Bait.” Kwa hiyo Salman ni mwenye kuhifadhiwa na dhambi kwa ushahidi wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Katika juzuu ya pili ya kitabu hicho hicho Uk. 127, amesema: “Hatabaki katika moto mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika waliotumwa na Mwenyezi Mungu, kwa sababu moto kwao unakuwa ni baridi na salama kwa baraka ya Ahlul Bait katika akhera. Ni utukufu ulioje wa baraka za Ahlul Bait!”

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَوْفُوا بِعَهْدِي أُوفِ بِعَهْدِكُمْ وَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ {40}

Enyi wana wa Israil! Kumbukeni neema yangu niliyowaneemesha; na tekelezeni ahadi yangu nitatekeleza ahadi yenu; na niogopeni Mimi tu.

وَآمِنُوا بِمَا أَنْزَلْتُ مُصَدِّقًا لِمَا مَعَكُمْ وَلَا تَكُونُوا أَوَّلَ كَافِرٍ بِهِ ۖ وَلَا تَشْتَرُوا بِآيَاتِي ثَمَنًا قَلِيلًا وَإِيَّايَ فَاتَّقُونِ {41}

Na aminini niliyoyateremsha ambayo yanasadikisha mliyonayo wala msiwe wa kwanza kuyakataa, wala msiuze ishara zangu kwa thamani ndogo; na niogopeni Mimi tu.

وَلَا تَلْبِسُوا الْحَقَّ بِالْبَاطِلِ وَتَكْتُمُوا الْحَقَّ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ {42}

Wala msichanganye haki na batili, na mkaficha haki na hali mnajua.

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ {43}

Na simamisheni swala na toeni zaka na inameni pamoja na wanaoinama.

أَتَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبِرِّ وَتَنْسَوْنَ أَنْفُسَكُمْ وَأَنْتُمْ تَتْلُونَ الْكِتَابَ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {44}

Je, mnawaamrisha watu kutenda mema na mnajisahau, hali mnasoma Kitabu? Basi je, hamfahamu?

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ {45}

Na takeni msaada kwa kusubiri na kwa kuswali na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu.

الَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُمْ مُلَاقُو رَبِّهِمْ وَأَنَّهُمْ إِلَيْهِ رَاجِعُونَ {46}

Ambao wana yakini kwamba wao watakutana na Mola wao na kwamba watarejea Kwake.
  • 1. Kuna maelezo yanayosema kuwa Adam ana jina la kubandikwa peponi la Abu Muhammad kwa heshima na kutukuzwa, na hakuna mtu mwenye jina la kubandikwa peponi ispokuwa yeye tu.
  • 2. Tofauti ya hukumu na Fatwa ni kwamba maudhui ya hukumu yanakuwa ni mahsusi kama kadhi kuhukumu mapatano yaliyopita kati ya Zaid na Bakari ni batili. Ama maudhui ya Fatwa yanakuwa ni kwa wote kama kuhalalisha biashara na kuharamisha riba