Aya 40 – 46: Zikumbukeni Neema Zangu

Mwenyezi Mungu amewataja Mayahudi katika Aya nyingi za Qur’an tukufu. Zimebainisha Aya hizo neema za Mwenyezi Mungu na kuua kwao Mitume bila ya haki.

Vile vile zimebainisha uadui wao kwa Musa na Harun (a.s.), kuabudu kwao ndama na kufanywa watumwa na Mafirauni, kisha kukombolewa. Vile vile Aya zimeeleza walivyookoka wasife maji na kuteremshiwa Manna na Salwa. Pia zimeelezea chuki yao hao Mayahudi kwa Mtume Muhammad (s.a.w.), au njama zao dhidi yake na uadui wao mkubwa kwa Waislamu, kuchukia kwao haki na mengineyo ambayo yatakuja maelezo yake kwa ufafanuzi. Surah ya Ng’ombe, waliyemchinja, hii inaelezea kwa upana sifa na matendo yao.

Dhahiri Ya Maisha

Aina nyingi za hali ya maisha wanayoishi watu ni natija ya Historia ndefu. Aina ya mavazi tunayovaa, mapishi ya chakula tunachokila na ujenzi wa nyumba tunazokaa, vyote hivi ni kutokana na usanifu wa waliotangulia.

Hata meli zinazotumia mashine zimeundwa baada ya majahazi yanayotumia matanga, baada ya kupita vipindi vya maendeleo.

Hakika maigizo ya kihistoria yanafanya kazi kama desturi za kitabia.; sawa na mawimbi yanayotulia kutokana na msukosuko wa kupwa maji na kujaa.

Kwa hivyo matukio yanayotumika katika maisha yetu ya kila siku na mfungamano tunaokuwa nao na watu wengine, mbaya au mzuri, ni natija ya yaliyopita zamani sana au hivi karibuni.

Hapa ndipo wanafalsafa wakasema: “Historia ni miongoni mwa njia za maarifa. Na Aya hizi ambazo Mwenyezi Mungu anawazungumzia Mayahudi, zina mfungamano mkubwa na Historia yao, kama tutakavyoona.

Israil

Israil ni jina jingine la Yaqub bin Is-haq bin Ibrahim (a.s.), Khalilullah. Ishaq ni ndugu wa Ismail, babuye Mtume Muhammad (s.a.w.). Waarabu na Wayahudi wote wamekutana kwa Ibrahim. Mwenyezi Mungu amesema:

لَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ ۚ{78}

“Mila ya baba yenu Ibrahim. (22:78)

Katika Majmaul-Bayan imesemwa kwamba Waarabu wote ni uzao wa Ismail; na wengi wasiokuwa Waarabu ni uzao wa Is-haq. Maana ya Israil katika lugha ya Kiebrania ni Abdullah (mja wa Mungu) Isra ni mja il ni Mwenyezi Mungu.

Alitumia upole Mwenyezi Mungu katika kuwazungumzia Wayahudi kwa kuwategemeza na Mtume mtukufu Israil ili kuwakumbusha nasaba hii tukufu. Huenda wakahisi utukufu ikiwa umo ndani ya nafsi zao; sawa na kusema: “Ewe mtoto wa watu wema! Kuwa kama baba zako na babu zako”.

Ama sababu ya kuitwa kwao Yahudi ni kwamba ukoo mmoja kati yao unatokana na Yahudha ambaye ni mtoto wa nne wa Nabii Yaqub. Sehemu ifuatayo tutaeleza kwa muhtasari historia ya Mayahudi kutokana na Aya tuliyonayo.

Historia Ya Mayahudi

Yatakuja maelezo katika Sura ya Yusuf kwamba Mtume Yaqub (a.s.) alihama na watoto wake kutoka Palestina kwenda Misri, alipo mtoto wake Yusuf (a.s.), akiwa waziri wa Firaun wakati huo. Firaun akawakatia kipande cha ardhi yenye rutuba kwa heshima ya Yusuf.

Kikaendelea kizazi cha Yakub kwa muda kiasi. Lakini Mafiraun waliokuja baadaye waliwakandamiza na kuwapa adhabu na mateso; waliwachinja watoto wao wa kiume wakawaacha wa kike; na wakawafanya watumwa.

Kisha Mwenyezi Mungu akawapelekea Mtume aliyekuwa mmoja wao ambaye ni Musa bin Imran, kuwakomboa na dhulma na utumwa; akawataka warudi Palestina kupigana na akawaahidi ushindi.

Wakakataa kwa woga. Mwenyezi Mungu akawapangia kutangatanga katika jangwa la Sinai miaka arobaini. Utakuja ufafanuzi Inshallah.

Katika kipindi hiki Harun alikufa kisha Musa pia akafa. Akachukua uongozi mpwawe Yashua bin Nun.
Ilipofika karne ya 13 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (a.s.) walivamia ardhi ya Palestina wakiongozwa na Yoshua wakawafukuza wenyeji; kama kilivyofanya kizazi chao (Wazayuni) katika Palestina mwaka 1948.1 Baada ya Yoshua Mwenyezi Mungu alituma mitume wengi waliotokana na wao.

Mnamo mwaka 596 kabla kuzaliwa Nabii Isa (a.s.), Mfalme wa Babil Nebukadnezzar aliwashambulia akaondoa utawala wao katika Palestina, akawachinja wengi na kuwachukua mateka wengi.

Wakaendelea kuwa chini ya utawala wa Nebukadnezzar mpaka mwaka 538 kabla ya kuzaliwa Isa (a.s.) aliposhindwa na mfalme wa Fursi (Iran ya sasa), ndipo Mayahudi wakapumua. Wakaendelea kuwa chini ya utawala wa Fursi kiasi cha miaka mia mbili, baadaye wakatawaliwa na makhalifa wa Alexandria mkuu. Kisha wakawa chini ya utawala wa Roma.

Ilipofika mwaka 135 kabla ya kuzaliwa Isa (a.s.), Mayahudi walifanya mapinduzi kwa Warumi, lakini hayakufanikiwa. Walifukuzwa Palestina, wakakimbilia sehemu mbali mbali za mashariki na magharibi; wengine Misri na wengine Lebanon na Syria, wengine wakaenda Iraq na wengine Hijaz. Ama Yemen walikujua Mayahudi na kuhamia huko kwa ajili ya biashara tangu zama za Nabii Suleiman ambaye alimwoa Malkia wa Yemen, Bilqis (Malkia wa Sheba).

Neema za Mwenyezi Mungu kwao ambazo Mwenyezi Mungu amezitaja kwa kauli yake; Zikumbukeni neema Zangu nilizowaneemesha, ni nyingi; zikiwa ni pamoja na kuwachagua Mitume kutoka katika kabila lao; kama Musa, Harun, Yoshua, Daud, Suleiman, Ayub, Uzair, Zakaria, Yahya n.k. Ama Maryam, mama yake Isa pia ni Mwisrail, nasaba yake inaishia kwa Nabii Daud (a.s.), lakini Mayahudi hawamkubali Masih mwana wa Maryam na wanadai kwamba Masih aliyetajwa katika Tawrat hajakuja bado.

Muhammad Na Mayahudi Wa Madina

Mtume (s.a.w.) alipohamia Madina kutoka Makka, Mayahudi walikuwa na koo tatu: Bani Qaynuqa, Bani Quraydha na Bani Nadhir. Walikuwa wana vilabu vya pombe, madanguro na sehemu za kufugia nguruwe. Na walikuwa wakihodhi dhahabu na fedha, kutengeneza silaha na kufanya biashara ya riba. Kwa ujumla wao ndio waliokuwa wakuu katika mambo ya uchumi mjini Madina, kama walivyo sasa (duniani).

Alipofika Mtume (s.a.w.), Mayahudi walihisi hatari kwa faida zao na mapa to yao ya kibiashara, kwa sababu vijana wa Madina wasingekwenda kwenye maduka na mabucha yao na watu wa Madina wasingekula nyama za nguruwe. Maana yake ni kwamba mayahudi wangepoteza vitega uchumi vyote.

Kwa ajili hiyo wakawa wanamchimbia vitimbi Mtume mtukufu (s.a.w.) na kupanga njama pamoja na makafiri dhidi ya Waislamu, kama zinavyofanya leo nguvu za dola kubwa zinavyolinda maslahi yake.
Mtume naye ni kama aliyejua hilo pale alipoingia Madina, akataka kuwatafutia hoja na kuwaadhibu kwa kauli zao. Kwa hiyo akawachukulia upole, akawekeana nao mkataba: kwamba wao wana uhuru katika dini yao na Mahekalu yao kwa masharti ya kuwa wasimsaidie adui na kama wakiamua kupigana pamoja na Waislamu, basi watapata fungu katika ngawira. Ni juu yao kushirikiana na Waislamu, kuulinda mji wa Madina, kwa sababu mji ni wa wote sio wa kundi maalum.

Lakini walivunja ahadi upesi sana. Tangu lini ahadi ikasimama mbele ya maslahi? Je inaingia akilini usalama na hadaa kuwa pamoja? Vipi anaweza kuishi mbwa mwitu pamoja na punda kwa amani? Kutafaa nini kukumbushwa neema, hadhari na nasaha kama zikigongana na maslahi ya kiutu na mapatano ya kibiashara?

Imeelezwa katika kitabu Muhammad Rasullul-huriyya (Muhammad Mtume wa Uhuru) hivi: “Mtume aliwaambia wafanyabiashara wa Kiislamu waanzishe soko jipya mjini Madina, wakaanzisha; likawa na nguvu soko hilo; wafanyi biashara wageni wakawa wanaelekea huko, na soko la Mayahudi likaathirika. Kwa sababu biashara katika soko la waislamu ilikuwa ya uadilifu sana kwa muuzaji na mteja.”

Hiyo peke yake ilitosha kujaza nyoyo za Mayahudi hasadi na chuki kwa Muhammad (s.a.w.) na kuwafanya wavunje ahadi.

Maelezo

Mwenyezi Mungu ameanza kuwaambia Mayahudi kukumbuka neema zake kwao. Miongoni mwa hizo neema ni kuwaletea Mitume wengi na kuwatukuza kwa Tawrat na Zabur.

Vile vile kuwakomboa katika utumwa wa Firaun, kuokoka kwao kutokana na kufa maji, kuwateremshia Manna na Salwa, kuwapa milki na ufalme katika zama za Mtume Suleiman na mengineyo ambayo yanawajibisha kuamini na kushukuru na wala sio kukanusha na kukufuru.

Unaweza kuuliza: Kwa nini msemo unawaelekea Mayahudi wa Madina pamoja na kujua kuwa neema zinazoelezwa zilikuwa kwa baba zao na sio kwao?

Jibu: Neema kwa baba ni neema kwa watoto vile vile; ambapo mtoto anapata utukufu kutokana na baba yake. Zaidi ya hayo ni kwamba umma wote ni mmoja.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuwakumbusha neema zake aliwaambia: Tekelezeni ahadi yangu nitatekeleza ahadi yenu.

Ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kuchukua yale yanayofahamiwa na maumbile na yale ambayo vimeteremshwa vitabu kwayo, ikiwa ni pamoja na kumwamini Mwenyezi Mungu na Mitume yake na kufanya amali kwa hukmu zake.

Mwenye Majmaul-Bayan anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu aliwaahidi katika Tawrat kwamba Yeye atawapelekea Mtume anayeitwa Muhammad. Fikra hii ndiyo wanayoielezea wafasiri wengi nayo ndiyo inayotolewa ushahidi na Qur’an.”

Ama ahadi ya Mayahudi ni ile ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao. Na, kila mwenye kuamini akafanya amali njema basi Mwenyezi Mungu atamlipa thawabu siku ya Kiyama.

Imesemekana maana yake ni kwamba kama wakimcha Mwenyezi Mungu, basi atawainua katika maisha haya ya duniani. Tutaeleza fikra ya malipo katika dunia mahali pake Inshaallah.

Kisha Mwenyezi Mungu amewaamrisha kuamini Qur’an na wasifanye haraka kuikanusha, kumkanusha Muhammad na kutaka maslahi tu. Na kwamba ni juu yao kuisimamisha swala na kutoa zaka ili wazitakase nafsi na mali zao.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: “Je, mnawaamrisha watu kutenda mema na mnajisahau, hali mnasoma kitabu,” inawaelekea viongozi na wakubwa, sio kwa watu wote, kwa sababu watu wengine ni wafuasi, na viongozi ndio wenye kufuatwa. Wao ndio wanaoficha haki na hali wanaijua na wanatoa mawaidha lakini hawayafuati.

Tunakariri tena kwamba mawaidha na nasaha haziendi pamoja na kutaka maslahi; na hayawezi kuacha athari yoyote isipokuwa katika nafsi isiyotaka maslahi na isiyokuwa na lengo lolote zaidi ya haki.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) “Na takeni msaada kwa kusubiri na kwa kuswali” Imeelezwa tena katika Aya ya 153 ya Sura hii, kwa hivyo utakuja ufafanuzi wake huko Inshallah.

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ {47}

Enyi wana wa Israil, ikumbukeni neema yangu niliyowaneemesha, na nikawatukuza kuliko viumbe wengine.

وَاتَّقُوا يَوْمًا لَا تَجْزِي نَفْسٌ عَنْ نَفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا هُمْ يُنْصَرُونَ {48}

Na iogopeni siku ambayo nafsi haitafaa nafsi kwa lolote. Wala hayatakubaliwa kwake maombezi (shufaa), wala hakitapokelewa kikomboleo; wala hawatanusuriwa.
  • 1. Tutaje mifano miwili: kwanza, W azayuni waliwakusanya wanawake 25 wenye mimba katika kijiji cha Dair Yasin, wakawapasua matumbo yao kwa mabisu na mikuki. Pili, waliwakusanya watu wa kijii cha Zaituni msikitini, kisha wakawalipua kwa baruti.