Aya 49 – 50: Na Tulipowaokoa

Lugha

Neno Aal lina maana ya kurudi; kwa hiyo kila mwenye kurudiwa kwa nasaba, rai au itikadi basi yeye ni Aal wa wale wanaomrudia, kisha likawa linatumiwa zaidi kwa maana ya watu wa nyumba ya huyo mtu atakayetajwa, lakini hawezi kuitwa mtu Al mpaka awe na utukufu fulani.

Makusudio ya Al-Firaun hapa ni wafuasi wake ambao walikuwa wakiwatesa wana wa Israil kwa amri yake. Abu-Hayan Al-Andalusi (Mhispania) amesema: Katika tafsir yake kubwa Al-Bahrul Muhit;

“Firaun ni lakabu (msimbo) ya wafalme wa Misri wakati huo; kama vile Kisra wa Fursi, Kaizari wa Roma, Najashi wa Uhabeshi, Tubba wa Yemen na Khaqani wa Uturuki.

Lakini alhamdulillah misimbo hii yote imebakia kuwa ni vigano tu!

Maelezo

Baada ya Mwenyezi Mungu kuwakumbusha neema zake kwao kwa ujumla, sasa anawakumbusha kwa ufafanuzi. Bora zaidi ya neema aliyoidokeza ni kuwaokoa na Firaun na wafuasi wake ambao waliwapa Mayahudi adhabu kali. Mwenyezi Mungu ameifasiri adhabu hiyo kwa kusema:

Wakiwachinja watoto wenu wakiume na kuwaacha hai wakike.

Yaani wanawaua watoto wanaume na kuwaacha wanawake waje kuwafanya watumishi.1 Zaidi ya hayo Wamisri walikuwa wakiwadhalilisha Wayahudi kwa kuwatuma kazi za kuvunja mawe, kuchimba mifereji na kazi nyinginezo za sulubu.Msemo umewaelekea Mayahudi waliokuwepo zama za Mtume Muhammad (s.a.w.), kwa sababu wao walikuwa kwenye dini ya mababu zao na waliridhia amali zao. Na, mwenye kupenda amali ya watu wengine anakuwa ameshirikiana nao.
Na katika hayo ulipatikana mtihani mkubwa uliotoka kwa Mola wenu:

Yaani, Enyi wana wa Israil, Mwenyezi Mungu amewatahini katika shida na raha, ili ijulikane kuwa je mtapigana jihadi na kuwa wavumilivi katika shida? Na je, mtashukuru raha? Au mtasalimu amri katika shida na mkufuru katika neema?

Kwa hakika Mwenyezi Mungu hamtahini mtu ili ajue, la! Yeye anajua lenye kuwa kabla ya kuwa; isipokuwa yeye anamtahini mtu kwa ajili ya kusimamisha hoja juu yake. Kwani hakuna madai kwa asiyekuwa na hoja, hata kama yenye kudaiwa yanathibiti katika elimu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.).

Mwenyezi Mungu amewaonyesha Waisrail neema ya pili aliposema:

Na tulipoitenga bahari kwa ajili yenu na tukawaokoa, na tukawazamisha watu wa Firaun.

Yaani tulitenga bahari na tukafanya njia kumi na mbili kwa hisabu ya wajukuu. Wajukuu katika wana wa Israil ni koo katika kizazi cha Yaqub (a.s)

Kwa ufupi Wayahudi walikuwa katika unyonge na udhalili wa hali ya juu; na adui yao alikuwa na nguvu za hali ya juu.

Lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akabadilisha hali hiyo kupitia mikononi mwa Mtume wake Musa (a.s.), wao wakawa ndio wenye nguvu; na adui yao akawa dhalili, hilo wakaliona kwa macho yao; kama inavyosema Aya: “Na hali nyinyi mnaangalia”.

Mwenyezi Mungu alimdhalilishia yule aliyewadhalilisha na akamwangamiza yule aliyetaka kuwaangamiza. Kwa hivyo basi wamelazimiana na hoja na imewalazimu kuwaidhika na kuzingatia, wala wasiwafanyie wengine yale waliyofanyiwa na wengine.

Lakini hivi leo mfano ule ule waliokuwa wakifanyiwa na Firaun ndio wanawafanyia Wapelestina. Na waendelee hivyo, lakini wajue hali itakuja wabadilikia tu, na yatawafika yale yaliyompata Firaun. Na waangalie ilivyokuwa kwa Nebukadnezzar na Warumi; na kwamba shujaa huvuma kisha akaisha.

Jambo la kustaajabisha sana kwa mtu ni kwamba anapokuwa kwenye shida, kisha akaokolewa na Mwenyezi Mungu, basi hupetuka mipaka akafanya uovu na kusahau kila kitu. Wafasiri wengi wamesema, kwamba bahari iliyotajwa ni Bahari nyekundu (Red Sea).

وَإِذْ وَاعَدْنَا مُوسَىٰ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً ثُمَّ اتَّخَذْتُمُ الْعِجْلَ مِنْ بَعْدِهِ وَأَنْتُمْ ظَالِمُونَ {51}

Na tulipomwahidi Musa masiku arobaini mkafanya ndama (kuwa Mungu) badala ya Mwenyezi Mungu mkawa madhalimu (wa nafsi zenu).

ثُمَّ عَفَوْنَا عَنْكُمْ مِنْ بَعْدِ ذَٰلِكَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ {52}

Kisha tukawasamehe baada ya hayo ili mpate kushukuru.

وَإِذْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَالْفُرْقَانَ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ {53}

Na tulipompa Musa kitabu na upambanuzi ili mpate kuongoka.
  • 1. Mwenye Majmaul Bayan anasema: Firaun aliota mambo yaliyomtisha. Wakamfasiria makuhani kuwa atazaliwa kijana wa kiume kutoka kwa wana wa Israil ambaye atakuja muua, ndipo Firaun akawafanyia hivyo wana wa Israil.