Aya 58 – 59: Ingieni Mji

Maelezo

Na tuliposema: Ingieni mji huu kuleni kumo maridhawa popote mpendapo.

Mwenye Majmaul-Bayan amesema: Wamekongamana wafasiri kwamba maana ya mji hapa ni Bayitul-Maqdis: na kwamba hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Ingieni ardhi takatifu”.

Na ingieni katika mlango (wake) kwa kunyenyekea.

Yaani ingieni hali ya kuinamisha vichwa kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Katika tafsir Bahrul-Muhit ya Abu Hayan Al-Andalusi anasema: Makusudio ya mlango ni mmojawapo wa milango ya Baitul Maqdis unaoitwa “Hitwa” (mwanachuoni huyu wa Kihispania alikufa mwaka 754 Hijriya)

Na semeni: Tusamehe

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwaamrisha kuingia kwa unyenyekevu, vile vile aliwaamrisha kuambatanisha kunyenyekea na kutamka kauli ya kujidhalilisha, mfano kusema astaghfirullah, ili kauli na kitendo vilingane; kama unavyotamka:”Subhana rabbiyal adhwiimi” katika kurukuu na; Subhana rabbiyal aala” katika kusujudu.

Ilikuwa si lazima kutamka neno lenyewe Hitwa kwa njia ya kuabudu kama walivyosema wafasiri wengi, wala sio kuwa makusudio ya “Hitwa” ni amali inayokata dhambi, kama ilivyo katika tafsiri ya Al-Manar kwa kunukiliwa Muhammad Abduh aliposema: “Hakika Mwenyezi Mungu hakuwakalifisha kutamka, kwa sababu hakuna kitu rahisi kwa binadamu kama hicho.”

Itakumbukwa kwamba Mwenyezi Mungu amewakalifisha waja wake kutamka maneno katika swala, amali za Hijja, kuamrisha mema, kurudisha salam na kutoa ushahidi, bali kuzitoa herufi kwa makhraji yake katika baadhi ya sehemu.
Wakabadilisha wale walio dhulumu kauli isiyokuwa ile waliyoambiwa.

Yaani wao waliamrishwa waseme yale yanayostahiki msamaha na thawabu, lakini walikhalifu wakasema yale yanayostahili adhabu na mateso.

Nilishangaa kuona baadhi ya wafasiri wakubwa miongoni mwao ni wanafalsafa wawili! Razi na Mulla Sadra, wameingilia masuala ya kuganda kwenye dua na dhikri, kwamba je, inapasa kuganda kwenye herufi au inajuzu kubadilisha tamko kwa tamko pamoja na kuchunga maana? Na wala wasiingilie pale walipofasiri ‘wakabadilisha wale waliodhulumu.’ kuwa inawaelezea wale ambao wameifanya dini biashara, na hali wao ndio waliokabidhiwa dini ya Mwenyezi Mungu, lakini wakafanya hiyana na wakazibadilisha Aya na mapokezi, kama walivyofanya Maquraish.

Tukateremsha juu ya wale waliodhulumu adhabu kutoka mbinguni.

Mwenyezi Mungu ameinyamazia aina na hakika ya adhabu yake wala hakutubainisha kuwa ni maradhi ya tauni, kama walivyosema baadhi, au ni theluji, kama walivyosema wengine. Vile vile amenyamazia idadi ya wale walioangamizwa na adhabu. Kuwa je ni elfu sabini, zaidi ya hapo au chini ya hapo? Pia hakueleza muda wa adhabu yenyewe kuwa ni saa au ni siku nzima? Kwa hivyo nasi tunanyamazia yale aliyonyamazia Mwenyezi Mungu, Wala hatutajikalifu, kama wengine, kwa kutegemea kauli dhaifu au Hadith zenye kuachwa.

وَإِذِ اسْتَسْقَىٰ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ فَقُلْنَا اضْرِبْ بِعَصَاكَ الْحَجَرَ ۖ فَانْفَجَرَتْ مِنْهُ اثْنَتَا عَشْرَةَ عَيْنًا ۖ قَدْ عَلِمَ كُلُّ أُنَاسٍ مَشْرَبَهُمْ ۖ كُلُوا وَاشْرَبُوا مِنْ رِزْقِ اللَّهِ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ {60}

Na Musa alipowaombea maji watu wake, tukasema: Lipige jiwe kwa fimbo yako. Mara zikabubujika humo chem chem kumi na mbili; kila kabila ikajua mahali pake pa kuywea. Kuleni na kunyweni katika riziki ya Mwenyezi Mungu wala msiasi katika ardhi mkifanya ufisadi.