Aya 60:Alipowaombea Maji

Maelezo

Na alipowaombea maji watu wake.

Hakuna maelezo katika Aya hii, kwani makusudio yake yanafahamika upesi, Razi amesema: “Wamesema kwa pamoja wafasiri, kwamba tukio hilo lilikuwa katika jangwa la Sinai.”

Vyovyote ilivyo ni kwamba Mwenyezi Mungu baada ya kuwafunika na kivuli na kuwalisha Manna na Salwa, vile vile aliwanywesha maji akawapitishia chemchem kumi na mbili kulingana na koo zao, kila ukoo ukawa na chemchem yake ili kusitokee mzozo kwenye maji.

Ubepari Na Ujamaa

Waisrail walipata kivuli, chakula na kinywaji bila ya taklifu wala mashaka yoyote; hakukuwa na tajiri wala maskini; wala mwenye njaa na mwenye kushiba; wala hakukuwa na mwenye kumiliki nyenzo za uzalishaji, wala hakuna ugawaji. Vile vile hakuna kuwa kila mtu atapata kutokana na nguvu zake; au kutokana na kazi yake. Hakukuwa na chochote isipokuwa usawa katika maisha bila ya kufanya kazi yoyote au kuwa na mali.1

Hilo ndilo taifa la mwanzo na la mwisho kupata kuonekana kwa maisha kama hayo, pamoja na kuwa na umoja katika lugha, maendeleo na historia. Tutathibitisha kwamba Mwenyezi Mungu alilifanyia taifa hilo mambo maalum kwa ajili yao tu na si kwa watu wote.
Ikiwa siyo sababu ya kiuchumi au ya kikabila inayoleta chuki na ufisadi, basi kwanini kuleta uharibifu na kumwasi mtoaji nasaha aliye mwaminifu, Musa bin Imran (a.s.)? Na vipi wachoke na maisha ya usawa katika utajiri na kusema, hatuwezi kungojea bali tunataka baadhi yetu wawaombe wengine; na wakaukabili mfululizo wa neema kwa ukafiri na uasi?

Wajamaa wanadai kwamba ubepari ndio kitovu cha uovu, na kwamba ujamaa ndio chimbuko la ubora. Mabepari nao wakasema umuhimu ni kuwa jinsi moja katika akili na sifa za kiroho...

Hitler anasema: “Hakuna kitu chochote isipokuwa watu wa aina ya Aria (Arian)” Lakini maadui wengi wa Hitler walikuwa (kama yeye) Aria; kisha nadharia yake hiyo ndiyo iliyoyaondoa maisha yake, ikidhalilisha taifa la Ujerumani na ikaangamiza mamilioni ya watu wengine. Pia ndiyo iliyovunja miji na maendeleo kwa ujumla.

Ama dola za kijamaa zimepita kiasi kwa kubishana. Mzozo wa Moscow na Beijing ulikata matumaini yote ya maafikiano; na kabla yake, kulikuwako na mzozo wa Stalin na Tito.

Hakika binadamu ana nguvu za ajabu zisizoweza kuhisabika, lakini hali ya mazingira yanayomzunguka kwa nje ni nyingi. Mwenye kujaribu kuyadhibiti hayo atakuwa ametafuta muhali, kila moja ina athari yake na kazi yake, na binadamu yuko kati ya kupwa na kujaa. Kwa hiyo kuchukulia kuwa athari inakuwa katika maada peke yake au katika roho peke yake, si sawa.

Ndio, ni kweli kwamba ‘ufakiri unakaribia kuwa ni ukafiri’ lakini hata hivyo binadamu akipata anayoyahitajia katika uhai wake, hautatimia kwake utulivu na upole mpaka aamini na kutegemea kwenye dini iliyo sawa itakayomhifadhi na makosa na dhambi.2

Kitu Kutoka Kusiko Na Kitu

Unaweza kuuliza vipi mawe yachimbuke chemchemi? Je, muhali unaweza kuwa? Je, kinaweza kupatikana kitu kutoka kusiko na kitu? Au mtu anaweze kuchimba maelfu ya mita ardhini na yasitoke maji ikiwa hayapo pale palipochimbwa. Sasa vipi yabubujiike maji kutoka katika jiwe lisilo na chemchemi wala athari yoyote ya maji?

Hakuna maelezo kutoka katika Sayansi kwa hili kabisa, isipokuwa kwa miujiza tu, ambayo kawaida yake ni kukhalifu ada; na isipokuwa kwa kauli yake ambaye umetukuka uweza wake: “Kuwa ikawa”; kama ilivyo katika kupasuka bahari na kusimama maji yake kama majabali, kushuka Manna na Salwa kutoka mbinguni na kuujalia moto kuwa baridi na salama kwa Ibrahim (a.s.). Vile vile kuzaliwa Isa bila ya baba, kufufua wafu, na kuumba ndege kutokana na udongo na mengineyo mengi.

Kwa hivyo mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na uweza wake atatosheka na haya, na mwenye kukanusha na akafanya inadi, itakuwa hakuna haja ya maneno katika matawi baada ya kukanusha shina.

Mimi nina yakini kabisa kwamba wale ambao wanataka maelezo ya kielimu na ya kiundani kwa kila kitu, kuwa katika maisha yao wanapitiwa na matukio kadhaa ambayo hawawezi kupata maelezo yake, isipokuwa katika ghaibu na matakwa ya Mwenyezi Mungu, lakini wao hawajui.

Inahakikisha hilo kauli ya Mulla Sadra3 mwanafalsafa mkubwa, ambaye wakati wake hakukuwa na vipimo vyovyote, aliposema katika kufasiri Aya hii: “Hakika asili ya maada haina sura ya kukoma kuendelea, kwa hiyo inawezekana baadhi ya sehemu ya jiwe kugeuka maji.”

Ushahidi hapo ni kauli yake “Inawezekana kugeuka baadhi ya sehemu ya jiwe kuwa maji.”

Hii inatilia nguvu nadharia ya kukua na kubadilika (evolution), ambayo aliibainisha kabla ya Darwin kwa karne tatu ambapo Darwin mwenyewe alihusisha nadharia yake kwa mnyama mwenye viungo tu, ama Mulla yeye amekusanya vitu vyote hata vitu vikavu, kama ulivyoona katika uwezekano wa kugeuka jiwe kuwa maji. Ni ukubwa ulioje wa uvumbuuzi huu. Lau Mulla angelikuwa ni mzungu, basi Einstein asingelikuwa na umaarufu wowote, lakini Einstein ni mtu wa Magharibi tena Myahudi na Mulla Sadra ni wa mashariki tena Mwislamu!

Ametangulia mtukufu huyu kuielezea nadharia ya kukua kwa upana. Na nadharia hii ilimzidishia imani juu ya kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Ugunduzi wake huu umeleta dalili mpya, kuweko Mwenyezi Mungu ambayo hakuwahi kuielezea yeyote mpaka akaitwa kiongozi wa wataalam wa kuthibitisha Mungu. Na ameleta nguvu ya hoja juu ya ujinga wa Gladstone na mamilioni ya wafuasi wake katika madai yao kwamba kuweko Mwenyezi Mungu, muumba wa ulimwengu huu, kumebatilika kwa nadharia ya kukua. Bali ni kinyume na hivyo.

وَإِذْ قُلْتُمْ يَا مُوسَىٰ لَنْ نَصْبِرَ عَلَىٰ طَعَامٍ وَاحِدٍ فَادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُخْرِجْ لَنَا مِمَّا تُنْبِتُ الْأَرْضُ مِنْ بَقْلِهَا وَقِثَّائِهَا وَفُومِهَا وَعَدَسِهَا وَبَصَلِهَا ۖ قَالَ أَتَسْتَبْدِلُونَ الَّذِي هُوَ أَدْنَىٰ بِالَّذِي هُوَ خَيْرٌ ۚ اهْبِطُوا مِصْرًا فَإِنَّ لَكُمْ مَا سَأَلْتُمْ ۗ وَضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ وَالْمَسْكَنَةُ وَبَاءُوا بِغَضَبٍ مِنَ اللَّهِ ۗ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَانُوا يَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّهِ وَيَقْتُلُونَ النَّبِيِّينَ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۗ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوْا وَكَانُوا يَعْتَدُونَ {61}

Na mliposema: Ewe Musa: Hatuwezi kuvumilia kwa chakula cha namna moja tu, basi toumbee Mola wako atutolee vile vinavyooteshwa na ardhi miongoni mwa mboga zake, na matango yake na ngano yake na adesi zake na vitunguu vyake. Akasema: Mnabadili vitu duni kwa vile vilivyo bora? Nendeni kwenye mji, huko mtapata mlivyoviomba: “Na ikapigwa juu yao (chapa ya) udhalili na umaskini; na wakastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na hayo ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya Mwenyezi Mungu na wakiwaua Manabii pasipo haki. Basi haya ni kwa sababu ya kuasi kwao na kupituka mipaka.
  • 1. Katika yaliyoelezwa na baadhi ya tafsir na ya kushangaza ni kwamba aliyekuwa mtoto katika wao alikuwa akikua na nguo; yaani kila anavyokua na nguo nayo hukua naye kwa urefu na upana, Hayo yanawezekana, lakini hakuna dalili juu yake.
  • 2. Katika mwaka 1936 Edward (VIII) alijiuzulu kiti cha ufalme wa Uingereza, ambao haukuchwewa na jua wakati huo. Alijiuzulu kwa sababu ya mwanamke aitwaye W allis, ambaye alikuwa amekwishaolewa na kuachwa mara mbili. Akaamua aishi naye kama mkimbizi na kuhangaika katika miji akitafuta kazi. Hiyo yote ni kutokana na kuchukulia maisha yote kuwa ni ya kimaada tu!
  • 3. Mulla Sadra ni katika wanavyuoni wakubwa wa karne ya kumi na sita (A.D.) na Darwin alikuwa mwishoni mwa karne ya kumi na tisa.