Aya 62: Waumini Na Mayahudi

Lugha

Makusudio ya neno Hadu ni Yahudi kwa kunasibishwa kwa Yahudha mtoto mkubwa wa Yaqub. Israil ni jina la Yaqub, kama tulivyotangulia kueleza. Naswara ni wenye kunasibishwa na mji unaitwa Naswira katika nchi ya Palestina. Imepokewa Hadith: “Hakika wameitwa Manaswara kwa sababu Isa na mama yake Maryam (a.s.) wanatoka katika kijiji kinachoitwa Naswira katika mji wa Sham, Mara nyingi Bwana Masih (a.s.) huitwa Naswiri”.

Wasabai ni watu wanaomkubali Mwenyezi Mungu, siku ya mwisho na baadhi ya mitume, lakini wanaitakidi kuwa baadhi ya nyota zinaathiri heri na shari na uzima na ugonjwa, miongoni mwao wanaishi Iraq hivi sasa.

Neno Swabia lina maana ya kuchomoza; Yaani kuchomoza nyota. Watu wa kwanza kuabudu nyota ni watu wa Namrud ambao walipelekewa Mtume Ibrahim (a.s.); wao ndio watu wa dini ya zamani katika Historia.

Maelezo

Katika maana ya Aya hii kuna karibu kauli nane za baadhi ya wafasiri. Zilizo sahihi zaidi katika hizo ni mbili.

Kwanza: Makusudio ya Aya ni kwamba Mwenyezi Mungu anataka kubainisha kuwa Yeye hatilii umuhimu majina kabisa. Ni sawa iwe ni aina ya Mwislamu, Mumin, Yahudi, Naswara au Msabai. Kwa sababu matamko hayadhuru kitu wala hayanufaishi, ispokuwa umuhimu mbele ya Mwenyezi Mungui ni itikadi sahihi na amali njema.

Ufahamisho wa Aya ni yale yaliyoelezwa katika hadithi kwamba Mwenyezi Mungu haangalii sura isipokuwa huangalia vitendo.

Hapana shaka kwamba maana hii yenyewe ni sahihi, lakini tamko halitoi maana hiyo waziwazi. Wengine wamezowea kujipendekeza kwenye dini nyingine kwa kutolea dalili Aya hii kwamba hakuna tofauti kati ya Waislamu na wengine mbele ya Mwenyezi Mungu, na hali wao wanajua kwa yakini kwamba wao wanakanusha Utume wa Muhammad (s.a.w.) bali wanamzulia uongo na wanamnasibishia mambo yanayoweza kuitingisha ardhi.

Maana ya pili, ni kwamba watu ambao hawakumuwahi Muhammad (s.a.w.) lakini waliongoka kwenye imani ya Mwenyezi Mungu na wakaacha mambo ya haram; kama uwongo, kunywa pombe na kuzini, miongoni mwao ni Qas bin Saida, Zayd bin Amr na Waraqa bin Nawfal na wengineo; hao wanaitwa wenye kushikamana na dini sahihi. Kwa hiyo muulizaji aliuliza hukumu ya hawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Ikajibu Aya kwamba hakuna ubaya kwao.

Vile vile Wayahudi, Wasabai na Wanaswara ambao hawakumuwahi Muhammad (s.a.w.) kupata ufafanuzi; hakika wote hao hawana hofu kwao, madamu walikuwa na Imani ya Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na matendo mema. Nasi tunapondokea kwenye maana hii.
Unaweza kuuliza kwamba maana ya Aya hii inafanana kuwa ni maana ya hayo kwa hayo. Kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mwenye kuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho”, imekuja baada ya kusema: “Hakika wale ambao wameamini.” Kwa kujaalia maneno kuwa: “Hakika wale ambao wameamini mwenye kuamini katika wao” ambayo ni sawa na kusema: “Hakika Waislamu mwenye kusilimu katika wao” na “waliosimama mwenye kusimama katika wao” basi nini jawabu?

Jibu: Swali hilo linaweza kuja ikiwa tutaifanya herufi man ni ya mubtada (kuanzia) kwa kusema: Yeyote atakayemwamini.

Ama tukiifanya ni Badal (badili) ya namna tatu yaani katika Wayahudi, Wasabai na Manaswara atakayemwamini, basi itakuwa hakuna haja ya swali; yaani itakuwa maana yake ni: Hakika wale ambao wamemwamini Mwenyezi Mungu wasiokuwa Wayahudi, Wasabai na Wanaswara haitakuwa hofu juu yao; vile vile atakayeamini katika Wayahudi, Wasabai na Wanaswara haitakuwa juu yao hofu. Hukumu ya wote ni moja.

وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَكُمْ وَرَفَعْنَا فَوْقَكُمُ الطُّورَ خُذُوا مَا آتَيْنَاكُمْ بِقُوَّةٍ وَاذْكُرُوا مَا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ {63}

Na tulipochukua ahadi yenu na tukauinua mlima juu yenu: Shikeni kwa nguvu haya tuliyowapa na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kumcha (Mungu).

ثُمَّ تَوَلَّيْتُمْ مِنْ بَعْدِ ذَٰلِكَ ۖ فَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ لَكُنْتُمْ مِنَ الْخَاسِرِينَ {64}

Kisha mligeuka baada ya haya. Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Zake, mngelikuwa miongoni mwa wenye kuhasirika.

وَلَقَدْ عَلِمْتُمُ الَّذِينَ اعْتَدَوْا مِنْكُمْ فِي السَّبْتِ فَقُلْنَا لَهُمْ كُونُوا قِرَدَةً خَاسِئِينَ {65}

Na kwa yakini mmekwisha jua wale miongoni mwenu walioivuna Sabato (Jumamosi.) Basi tukawaambia: Kueni manayani wadhalilifu.

فَجَعَلْنَاهَا نَكَالًا لِمَا بَيْنَ يَدَيْهَا وَمَا خَلْفَهَا وَمَوْعِظَةً لِلْمُتَّقِينَ {66}

Kwa hivyo tukaufanya (umma huo) ni onyo kwa waliokuwa katika zama zao na waliokuja nyuma yao, na mawaidha kwa mwachao Mwenyezi Mungu.

Aya 63-66: Tulipochukua Ahadi

Na tulipochukua ahadi yenu.

Yaani tulipochukua ahadi kutoka kwa wahenga wenu kufanya amali kwa mujibu wa Tawrat. Walipoivunja ahadi, Mwenyezi Mungu aliwainulia jabali juu yao, akasema fanyeni la sivyo nitawaangushia jabali hili. Wakakubali na wakatubia; likatulia jabali mahali pake, lakini baadaye walirudia kuasi.

Ikiwa Wayahudi walikuwa hivi wakati wa Musa (a.s.) pamoja na kushuhudia waliyoyashuhudia katika miujiza, wala hakuna nguvu ya hoja kuliko kuona, basi si ajabu kwa mayahudi wa Madina kumkanusha Mtume (s.a.w.) na kuvunja mkataba naye.

Angalia kifungu cha Muhammad (s.a.w.) na Mayahudi wa Madina katika tafsir ya Aya 47.

Na lau si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Zake.

Yaani lau si kuwahurumia Mwenyezi Mungu, angeliwapa adhabu katika dunia na akhera. Mulla Sadra anasema: “Hakika Aya hii ni katika Aya zinazotoa matarajio zaidi na yenye dalili ya nguvu zaidi ya rehema ya Mwenyezi Mungu na vile asivyopatiliza maovu ya waja wake waasi.
Kwa sababu, kauli yake: “Lau si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu”, ni baada ya kukithiri uovu wao, ukiwa ni pamoja na kuabudu ndama, kuikufuru neema, kuwakana Mitume na kuwaua, kuvunja ahadi iliyotiliwa mkazo, na mengineyo; inafahamisha ukamilifu wa upole wake na msamaha wake.

Kisha akanakili Mulla Sadra, kutoka Kuffal, yale yanayoeleza kwa muhtasari, kwamba baada ya kuwaondolea adhabu ya jabali waliibadili Tawrat wakadhihirisha maasi wakamkhalifu Musa, wakamfanyia kila adha. Mwenyezi Mungu alikuwa akiwalipa hapa duniani ili waweze kuzingatia kiasi kwamba baadhi yao aliwapoteza katika ardhi, wengine akawaunguza kwa moto na wengine wakaadhibiwa kwa tauni. Yote hayo na yasiyokuwa hayo yameandikwa katika Tawrat wanayoikubali, ambayo hivi sasa anaweza kuipata kila anayetaka.

Kisha waliofuatia wakafanya makosa kama waliyoyafanya waliopita; wakamkanusha Bwana Masih wakadhamiria kumuua. Kwa hivyo si ajabu kukanusha yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad (s.a.w.).

Na kwa yakini mmekwishajua wale miongoni mwenu walioivunja sabato (Jumamosi).

Mwenyezi Mungu aliwaamrisha kuacha kufanya kazi siku ya Jumamosi (sabato) akawaharamishia kuvua samaki siku hiyo. Wakawa samaki wanakusanyika siku hiyo kwa usalama na utulivu, lakini kundi jengine la Mayahudi lilifanya hila ya kuwazuia samaki siku ya Jumamosi, mahali wasipoweza kutoka na kuwachukua siku ya Jumapili, wakisema: “Mwenyezi Mungu ametukataza kuvua samaki siku hiyo, lakini hakutukataza kuwazuia na kuna tofauti kati ya kuzuia na kuvua.”

Waongo hawa wenye hila wananikumbusha wale wanaoigeuza dini, ambao wanacheza na matamko; wanazivuruga haki ili waingize uwongo katika mitego yao.

Jambo la kushangaza ni kwamba baadhi ya masheikh wametunga vitabu maalum vya kuifanyia hila sheria; kama kwamba Mwenyezi Mungu ni mtoto mdogo anayedanganywa, asiyewajua wakweli na waongo. Kama Mwenyezi Mungu hakuwabadilisha hawa kuwa manyani hapa duniani, kama alivyowafanyia Mayahudi, basi atawafufua kesho kuwa majibwa, manyani na nguruwe. Ikiwa waongo hawakugeuzwa hivi sasa kwa dhahiri, basi wamegeuzwa kwa ndani; na hakuna hoja yenye nguvu zaidi inayofahamisha hilo kuliko vitendo vyao vinavyofahamisha kugeuzwa nafsi zao.

Basi tukawaambia kuweni manyani madhalili.

Wamehitalifiana wafasiri kwamba je, kugeuzwa manyani kulikuwa kwa uhakika kiasi ambacho sura zao na mili yao ilikuwa ya manyani ama kulikuwa ni kugeuzwa kwa kitabia tu; kama vile alivyosema Mwenyezi Mungu:

خَتَمَ اللَّهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ{7}

Amepiga muhuri Mwenyezi Mungu juu ya nyoyo zao.” (2:7)

Au...

كَمَثَلِ الْحِمَارِ يَحْمِلُ أَسْفَارًا ۚ{5}

“Kama mfano wa punda anayechukua mizigo?” (62:5)

Ambapo Aya hizi ni za majazi.

Wafasiri wengi wamesema kuwa walikuwa manyani wa kikweli kabisa, kwa kuchukulia dhahiri ya Aya ambayo haina haja kuiletea tafsiri nyingine. Kwa sababu kugeuzwa sura na kuwa sura nyingine ni jambo linalowezekana kihakika. Ikija Aya au hadith kuhusu jambo ambalo lawezekana, basi tutaipitisha kwa dhahiri yake bila ya kuhitajia tafsiri nyingine (Taawil).

Wafasiri wachache, kama Mujahid na Sheikh Muhammad Abduh wamesema kwamba mabadiliko yalikuwa katika nafsi si katika mwili. Anasema Sheikh Muhammad Abduh katika tafsiri yake ya Al- Maraghi: “Hakika Mwenyezi Mungu hambadilishi kila asi kumtoa katika umbile la mtu, kwa sababu hiyo siyo desturi yake katika kuumba kwake, na desturi ya Mwenyezi Mungu ni moja, analolifanya kwa karne ya sasa ndilo alilolifanya kwa karne iliyopita.”
Sisi tunakubaliana na wale wa kwanza waliosema kwamba mageuzo yalikuwa ya uhakika. Ama kauli ya Abduh ni sahihi kama msingi wa mambo yalivyo na kama kawaida ya vyote, lakini kuna mambo mengine yasiyofuata kawaida ambayo yanatokana na hekima ya Mwenyezi Mungu, kama miujiza na mengineyo katika karama zake Mwenyezi Mungu. Vitendo vya Mwenyezi Mungu pamoja na mayahudi wakati huo, ni katika mambo yasiyofuata desturi, kama itakavyobainika katika kifungu kifuatacho.

Mayahudi Hawana Mfano

Mwenye kuangalia vizuri Aya za Qur’an tukufu zilizowahusu Waisrail hasa wale waliokuwa katika zama za Musa, atatoka na natija iliyo wazi kama jua. Nayo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwafanyia mambo yasiyokuwa na mfano wala hayafanani na kitu chochote ambacho watu wamekizowea. Sio mbali kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na nikawatukuza kuliko viumbe wengine”, ni ishara ya muamala huo mahsusi.

Mwenyezi Mungu aliwakomboa kutoka katika ukandamizaji wa Firaun na utaghuti wake kwa kuipasua bahari, sio kwa jihadi wala kujitolea muhanga. Aliwalisha Manna na Salwa na kuwapa maji kwa muujiza bila ya taabu au kazi yoyote. Akawainulia jabali ili waweze kutii na kusikia.

Akamfufua mtu wao aliyeuliwa, ili abainike muuaji. Yote hayo na mengineyo yanaonyesha dalili kwamba matatizo ya Mayahudi wakati huo hayakutatuliwa kwa njia ya kawaida iliyozoeleka, bali hata hawakufikiria kufanya kazi ya kuyatatua; kila walipo kuwa wakipata tatizo, basi husema; “Ewe Musa tuombee Mola wako afanye hivi na awache hivi,” na Musa alikuwa akiwaombea na kukubaliwa.
Kwa hivyo basi inatufahamikia kwamba kukifananisha kizazi cha Waisrail cha wakati huo na vizazi vingine sio mahali pake; na kwamba kauli ya Sheikh Muhammad Abduh (analolifanya kwa karne ya sasa ndiyo analolifanya kwa karne iliyopita) ni sahihi katika watu wote isipokuwa watu hao tu!1

Vile vile inabainika kwamba Mwenyezi Mungu aliwainulia jabali kutaka kuwalazimisha waifuate Tawrat, na kwamba kauli ya Sayyid Tabatabai katika tafsiri Al-Mizan: “Hakika kuinuliwa jabali hakufahamishi kulazimisha kwa sababu hakuna kulazimisha katika dini,” kauli hii iko mbali na mnasaba wa watu wa Musa ambapo Mwenyezi Mungu aliwafanyia mambo yaliyo mbali na kawaida na desturi.

Mimi sina namna yoyote ninayoweza kutegemea kujua hekima ya Mwenyezi Mungu katika hilo. Huenda ikawa siri katika hilo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alitaka kupiga mfano kwa Mayahudi hao kwamba maisha hayawi mazuri ila kwa kutaabika na kufanya kazi. Na ni kutokana na hali hiyo tu, ndipo mtu anaweza kugundua mambo na kujua siri, na kupanda katika daraja ya juu ya kimaendeleo.

Lau binadamu angeliishi kivivu kwa kutegemea chakula kutoka mbinguni asingeliweza kutofautiana na mnyama aliyefungwa na kulishwa; wala asingelikuwa na haja ya akili na utambuzi. Hakika uvivu ni kuganda na ni mauti, ama ukakamavu ndio uhai.

Vyovyote iwavyo, historia ya Mayahudi kwa ujumla inaambatana na historia ya Wayahudi waliokuwa wakati wa Musa, wao ndio waliotangulia halafu ndio wakafuatiwa na wajukuu zao.

Kutokana na mazungumzo haya tutadokeza kuhusu jumuiya ya wazayuni wanaoishi Marekani katika mtaa uitwao Brooklyn mjini New York. Jina la jumuia hiyo ni Mashahidi wa Yehova ambayo lengo lake la kwanza na la mwisho ni kuleta vurugu na fitina za kidini katika pembe za ulimwengu hasa Uarabuni.

Wanatoa matoleo mengi sana ya vitabu kwa lugha zote, tena kwa majalada ya rangi ambayo yanamiminika kwa wingi katika miji yetu: Pia wanatoa jarida kwa jina la Mnara wa mlinzi. Miongoni mwa vitabu walivyotoa ni kile kinachomshutumu Mtume Muhammad (s.a.w.) na Qur’an. Jina la kitabu hicho ni Hal-khadama ddinul-Insaniyya (Je, dini inahudumia utu). Vingine ni Liyakunillah-Swadiqan (Mungu awe ni mkweli), Nidhamu dduhuril-ilahiy (Nidhamu ya zama za kiungu), Al- haqqu Yuharrirukum (Haki itawakomboa), Al-Maswaliha (Masilahi), na vingine chungu mzima, ambavyo vyote vimechapishwa Beirut.

Serikali ya Misri iliwagundua baadhi ya wanachama wa jumuia ya Mashahidi wa Yehova wakiwa katika mikutano ya siri. Ikawashika na kuwashtaki mnamo mwezi wa April mwaka 1967.

Miongoni mwa mafunzo ya jumuia hii ni kwamba kulikuwa na mzozo mkubwa kati ya Mwenyezi Mungu na shetani, ambao ulidumu kwa muda wa karne sitini; kisha Mwenyezi Mungu akajitoa akamwachia mamlaka shetani afanye vile anavyotaka. Shetani akamwachia Mwenyezi Mungu umma wa Kiisrail. Kwa ajili hii Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani:”

Chukua watu wote na uniachie umma huu”. Hivyo ndivyo yalivyotimia maafikiano kati ya Mwenyezi Mungu na Shetani, lakini mambo yatabadilika mwisho.

Kwa sababu umma wa Kiyahudi utatawala kuanzia mto Naili (Nile) mpaka Furati (Euphrates) na kwamba Mitume wa Kiisrail watafufuka na kuchukua madaraka ya juu katika dola ya Kiisrail; hatimaye ulimwengu wote utakuwa chini ya dola hii, Shetani atash-indwa na Mwenyezi Mungu atashinda. Kundi hili lina wafuasi na wawakilishi katika Beirut, Oman, Baghdad, Damascus, Cairo, Saudia na Morocco.

Lengo la kuyaeleza yote hayo ni kuwatahadharisha watu na nyoka huyu, na kuwahadharisha na vidole ambavyo vinawatekenya baadhi ya waandishi wa vitabu na magazeti kwa kufanya njama za kuleta vurugu na uharibifu, na kuleta ukabila na fitina za kidini.

وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ إِنَّ اللَّهَ يَأْمُرُكُمْ أَنْ تَذْبَحُوا بَقَرَةً ۖ قَالُوا أَتَتَّخِذُنَا هُزُوًا ۖ قَالَ أَعُوذُ بِاللَّهِ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْجَاهِلِينَ {67}

Na Musa alipowaambia watu watu :Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrisha mchinje ngombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: Najikinga kwa Mwenyezi Mungu kuwa miongoni mwa wajinga.

قَالُوا ادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُبَيِّنْ لَنَا مَا هِيَ ۚ قَالَ إِنَّهُ يَقُولُ إِنَّهَا بَقَرَةٌ لَا فَارِضٌ وَلَا بِكْرٌ عَوَانٌ بَيْنَ ذَٰلِكَ ۖ فَافْعَلُوا مَا تُؤْمَرُونَ {68}

Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie ni ngombe gani? Akasema: Hakika yeye anasema kwamba ngombe huyo si mpevu wala si mchanga, ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyoamrishwa.

قَالُوا ادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُبَيِّنْ لَنَا مَا لَوْنُهَا ۚ قَالَ إِنَّهُ يَقُولُ إِنَّهَا بَقَرَةٌ صَفْرَاءُ فَاقِعٌ لَوْنُهَا تَسُرُّ النَّاظِرِينَ {69}

Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie rangi yake ni ipi? Akasema: Yeye anasema ngombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imeiva sana, huwapendeza wanaomtazama.

قَالُوا ادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُبَيِّنْ لَنَا مَا هِيَ إِنَّ الْبَقَرَ تَشَابَهَ عَلَيْنَا وَإِنَّا إِنْ شَاءَ اللَّهُ لَمُهْتَدُونَ {70}

Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie ni vipi hali yake; hakika ng’ombe wamefanana na hakika sisi kama Mwenyezi Mungu akipenda (tutakuwa) ni wenye kuongoka.

قَالَ إِنَّهُ يَقُولُ إِنَّهَا بَقَرَةٌ لَا ذَلُولٌ تُثِيرُ الْأَرْضَ وَلَا تَسْقِي الْحَرْثَ مُسَلَّمَةٌ لَا شِيَةَ فِيهَا ۚ قَالُوا الْآنَ جِئْتَ بِالْحَقِّ ۚ فَذَبَحُوهَا وَمَا كَادُوا يَفْعَلُونَ {71}

Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo si ng’ombe anayefanyishwa kazi ya kulima ardhi wala kutilia maji mimea, mzima, hana kipaku. Wkasema: Sasa umeleta haki. Basi wakamchinja, na walikaribia wasifanye.

وَإِذْ قَتَلْتُمْ نَفْسًا فَادَّارَأْتُمْ فِيهَا ۖ وَاللَّهُ مُخْرِجٌ مَا كُنْتُمْ تَكْتُمُونَ {72}

Na mlipoiua nafsi, kasha mkahitilafiana kwa hayo, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyatoa hayo mliyokuwa mkiyaficha.

فَقُلْنَا اضْرِبُوهُ بِبَعْضِهَا ۚ كَذَٰلِكَ يُحْيِي اللَّهُ الْمَوْتَىٰ وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ {73}

Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo ngombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anawaonyesha ishara zake ili mpate kufahamu.
  • 1. Qur’an na Injil zimewalaumu Mayahudi kwamba wao ni maadui wa utu, na historia yao inashuhudia ukweli huu. Kwa ajili hiyo wanajaribu kufanya kila njia ionekane kwamba hakuna tofauti ya ukabila wala ya dini; ndio wakatunga vitabu kwa makusudio hayo na wakaeneza propaganda na wakaanzisha taasis, miongoni mwa hizo taasisi ni ile ya ‘Free Mason’ ya kimtaifa ambayo wameivika nguo ya ‘ubinadamu.’