Aya 80-82: Walisema Hautatugusa Moto Wa Jahannam

Na walisema: Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu

Mayahudi wanadai kwamba wao ni watoto wa Mungu na taifa lake teule na kwamba watu wote ni watoto wa shetani, isipokuwa wao tu, na ni mataifa yaliyotupiliwa mbali.

Kwa hivyo ati Mwenyezi Mungu hatawaweka milele motoni, isipokuwa atawaadhibu kwa adhabu hafifu tena kwa muda mfupi, kisha atawaridhia. Yaani kwamba Mwenyezi Mungu anawaendekeza na kuuendekeza ukoloni wa kizayuni ambao unaikalia ardhi ya Palestina.

Sema: Je, mmepata ahadi kwa Mwenyezi Mungu

Yaani waambie ewe Muhammad, kwamba madai yao haya ni porojo tu, na kama si hivyo, basi ni ahadi gani mliyowekeana na Mwenyezi Mungu? Madai yao haya, hayafahamishi chochote zaidi ya kudharau kwao madhambi na kufanya uovu.

Mtume mtukufu (s.a.w.) anasema: “Hakika mumini anaona dhambi yake ni kama jiwe anaogopa lisimwangukie na kwamba kafiri anaona dhambi yake ni kama nzi tu aliyepitia kwenye pua yake...”. Anasema Amirul Muminin (a.s.):” Dhambi kubwa zaidi ni ile iliyodharauliwa na mwenye kuifanya.”

Kauli yake Mtume mtukufu (s.a.w.): “Kama kwamba dhambi ni nzi anayepita juu ya pua ya mwenye dhambi.” Inafanana kabisa na ya Mayahudi ambao wanadai kwamba wao ni watoto wa Mwenyezi Mungu wenye kutendekezwa. Huenda haya yakamnufaisha na kumzindua yeyote ambaye anapuuza dhambi kwa kutegemea utukufu wa nasabu.

Mwenye kujitegemea yeye mwenyewe tu wala asihisi makosa ya nafsi yake, na asikubali nasaha za mwingine, basi ni muhali kuweza kuongoka kwenye heri. Hakika mwenye akili hajiangalii mwenyewe tu kwa kujihadaa na ndoto zake, bali daima anakuwa na msimamo wa kujilaumu makosa yake na kupambanua yale aliyonayo na yale anayotakiwa awe nayo.

Vile vile huitoa nafsi yake na fikra za kitoto na mawazo ya kishetani. Kwa hali hii pekee ndio atakuwa anafaa kuitwa mtu kwa maana sahihi. Kuna hadith tukufu inayosema: “Mwenye kujiona kwamba yeye ni mwovu, basi ni mwema.”

Ndiyo, wanaochuma ubaya na makosa yao yakawazunguka, hao ndio watu wa motoni na humo watadumu.

Ubaya ni shirk na madhambi mengineyo, lakini makusudio yake hapa yanahukumu shirk tu! Kwa kulinganisha na kauli yake Mwenyezi Mungu hao ndio watu wa motoni humo watadumu.

Mwenye Majmaul-Bayan anasema: “Makusudio ya ubaya kuwa ni shirk ndiyo yanayoafiki, kwa sababu dhambi nyingine yoyote haiwajibishi kudumu motoni.”

Na wale walioamini na kutenda mema hao ndio watu wa peponi watadumu humo.

Aya hii tukufu inafahamisha kuwa kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu kesho kutatokana na imani sahihi ikiambatana na matendo mema. Hadith tukufu inasema: “Abu Sufyani Athaqafiy, alisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niambie neno katika Uislamu ambalo sitamuuliza yeyote baada yako.” Akasema Mtume: “Sema: Nimemwamini Mwenyezi Mungu, kisha ufuate unyoofu (msimamo).”

Katika hadith yake hii Mtume (s.a.w.) anaelezea Aya inayosema:

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنْتُمْ تُوعَدُونَ {30}

Wale waliosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu kisha wakawa na unyoofu hao huwateremkia malaika (wakawambia): Msiogope wala msihuzunike, na furahini kwa pepo mliyokuwa mkiahidiwa.(41:30).

Makusudio ya kuwa na unyoofu katika Aya na Hadith, ni kuwa katika msimamo wa kufanya amali kwa mujibu wa Qur’an na hadith za Mtume (s.a.w.).

Mwislamu Na Muumini

Mwislamu kwa kuangalia muamala wake na kuthibiti Uislamu wake, anagawanyika kwenye mafungu mawili:

Kwanza, kumkubali Mwenyezi Mungu kuwa ni mmoja na kukubali Utume wa Muhammad bila ya kuangalia itikadi yake na amali (matendo) yake. Lakini ni sharti asikanushe zile dharura za dini, kama ulazima wa swala na uharamu wa zinaa na pombe. Huyu ndiye anayejulikana kwa Waislamu kuwa yeye ni Mwislamu atafanya na kufanyiwa mambo ya Kiislamu; kama kurithi, kuoa, na kuzikwa kiislamu, ikiwa ni pamoja na kumwosha, kumtia sandani, kumswalia na kumzika katika makaburi ya Waislalmu, anafanyiwa hayo kwa vile amepiga shahada.

Pili, ni kuamini na kushikamana na Uislamu kwa misingi na matawi; hakanushi hukumu yoyote katika hukumu za Kiislamu, wala hafanyi uasi wa hukumu katika hukumu za sheria. Huyu ndiye Mwislamu wa kweli (muumin) mbele ya Mwenyezi Mungu na watu, bali ni Mwislamu mwadilifu ambaye zimethibiti kwake athari zote za uadilifu wa Kiislamu duniani na akhera.

Athari za dunia ni kukubaliwa ushahidi wake, kufaa kuswalisha, kuchukua hukumu zake na fatwa zake akiwa ni mujtahidi. Ama athari za kiakhera ni kule kuwa juu hadhi yake na thawabu. Mumin ni yule mwenye kukiri kwa ulimi na kusadikisha kwa moyo wake shahada mbili, wala haitoshi kukiri kwa ulimi tu au kusaidikisha kwa moyo tu, bali hapana budi yote mawili yaende sambamba. Kwa hivyo kila mumin ni Mwislamu, lakini si kila Mwislamu ni mumin.

Hapa inatubainikia kwamba amali njema haiitwi imani, kwa dalili kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta kiunganishi baina ya imani na amali njema kwa maana ya kuwa ni vitu viwili tofauti. Hata hivyo amali njema inaingia katika ufahamu wa uadilifu kama tulivyoonyesha. Utakuja ufafanuzi wake mahali pake.

Mafaqihi wa kishia wanahusisha tamko la mumin kwa yule anayeamini Maimamu kumi na wawili, wakisema zaka inapewa mumin, na mwenye kuswalisha awe mumin, basi wanakusudia yule mwenye kuamini maimamu kumi na wawili tu. Istilahi hii wanahusika nayo mafaqih tu. Lakini hata huyo fakihi wa Kishia kama akizugumzia mumin katika mswala yasiyokuwa ya kifikihi, basi huwa anakusudia kila mwenye kukiri shahada mbili na kuzisadikisha kwa moyo; hata kama siye mwenye kuamini Maimamu kumi na wawili.

Kwa vyovyote ilivyo Uislamu na imani kwa maana tuliyoyaelezea, hautamuokoa mtu na adhabu ya Mwenyezi Mungu kesho, isipokuwa uwe pamoja na unyoofu ambao ni kufanya amali kulingana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume Wake (s.a.w.).

Mwenye Madhambi Makubwa

Mafakihi wameyagawanya madhambi katika mafungu mawili: Makubwa; kama kunywa pombe. Na madogo kama kukaa mwenye meza ya pombe bila kunywa. Utakuja ufafanuzi wa madhambi makubwa na madogo Inshallah, katika Aya isemayo:
“Ambao wanajiepusha na madhambi makuu na vitendo vichafu; isipokuwa makosa hafifu...”25

Wamehitalifiana Waislamu katika yule mwenye kukiri shahada mbili na akafanya madhambi makubwa, Je, yeye ni kafiri atakayebakia milele motoni au yeye ni mwislamu fasiki ambaye ataadhibiwa kiasi anachostahili, kisha atiwe peponi?

Khawarij wamesema kuwa atabakia milele motoni. Shia, Ash’ari, Masahaba wengi na Tabiin, wamesema atatolewa motoni. Mu’tazila wamezusha fikra ya tatu ya kuthibitisha mawili, yaani hatakuwa kafiri wala Mumin.

Allama Hilli ametoa dalili katika sherehe ya Tajrid juu ya ushahidi wa kauli ya kuwa mwenye madhambi makubwa ni fasiki hatokaa milele motoni, kuwa: “Lau atabakishwa milele motoni, ingelazimika mwenye kumwabudu Mwenyezi Mungu muda wa umri wake wote; kisha akamuasi mwisho wa umri wake mara moja tu, pamoja na kubakia na imani yake, aingie motoni milele, awe sawa na yule aliyemshirikisha Mwenyezi Mungu katika umri wake wote. Na hilo ni muhali na haliingii akilini.”

Hapana mwenye shaka kwamba ovu moja haliwezi kuondoa mema yote, bali ni kinyume; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Kwa ajili hiyo basi, inapasa kulichukulia neno ubaya katika Aya (Na wanaochuma ubaya na makosa yao yakawazunguka, hao ndio watu wa motoni, watadumu humo), kuwa na maana ya shirk. Kama ambavyo Aya inayofuatia hiyo (Na wale walioamini na kutenda mema hao ndio watu wa peponi, watakaa humo milele) inafahamisha kwamba mwenye kufanya madhambi makubwa ataingia peponi, wala hatakaa milele motoni. Kwa sababu Aya ile inamhusu pia mwenye kuamini na akafanya amali njema kisha akafanya madhambi makubwa na wala asitubie.

Mayahudi Tena

Madai ya Mayahudi kwamba wao ni watoto wa Mungu na taifa teule, ni kwamba dini na maadili yake, katika itikadi yao, ni kazi ya kibiashara na manufaa ya kiutu. Vinginevyo itakuwa ni bure tu.

Unaweza kusema, hayo hayahusiani na Mayahudi tu, bali wako watu wa namna hiyo. Jibu, ndio, lakini tofauti iliyopo ni kwamba Mayahudi wana hasadi kwa watu wote isipokuwa wao.

وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَ بَنِي إِسْرَائِيلَ لَا تَعْبُدُونَ إِلَّا اللَّهَ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَقُولُوا لِلنَّاسِ حُسْنًا وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ ثُمَّ تَوَلَّيْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا مِنْكُمْ وَأَنْتُمْ مُعْرِضُونَ {83}

Na tulipochukua ahadi na wana wa Israil: Hamtamwabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na maskini; na semeni na watu kwa uzuri na simamisheni swala na toeni zaka. Kisha mkageuka isipokuwa wachache tu katika nyinyi mnakengueka.