Aya 89-91: Kilipowafikia Kitabu

Maelezo

Mayahudi wa Madina walikuwa wamejipa tumaini la kujiwa na Mtume na walikuwa wakimtaja Muhammad, wakiwaambia Aus na Khazraj: “Kesho atakuja Mtume ambaye sifa zake tumezikuta katika Tawrat na atawashinda waarabu na washirikina wote.”

Mayahudi walikuwa wakifikiria kuwa huyo Mtume ni Mwisrail sio Mwarabu. Basi Mwenyezi Mungu alipomtuma Muhammad Mwarabu, waliona unyonge, wakaingiwa na ubaguzi na kuupinga Utume wake na kukanusha yale waliyokuwa wakiyasema kwa Muhammad. Ikawa baadhi ya Aus na Khazraj wanawambia: “Enyi Mayahudi, jana mlikuwa mkitutisha kwa Muhammad (s.a.w.) kuwa sisi ni watu wa shirk: mlikuwa mkimsifu na kumtaja kwamba yeye ni Mtume. Sasa mbona sisi ndio tunaomwamini na nyinyi mmegeuka na kurudi nyuma?

Wakajibu Mayahudi: “Hakutujia na kitu tunachokijua na wala yeye siye yule tuliyekuwa tukiwatajia”. Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii.

Na kilipowajia kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu kisadikishacho yaliyo pamoja nao.

Yaani ilipowajia Qur’an walikanusha. Qur’an waliyoikanusha ndani yake mna usadikisho wa yale yaliyo katika Tawrat yao iliyobashiri kuja Muhammad (s.a.w.). Kwa hiyo wanamfanya mwongo yule anayewasadikisha wao, bali wanajikadhibisha wenyewe.

Hili si geni wala si ajabu kwa yule anayefanya matakwa yake na mapenzi yake ndiyo kigezo cha kuhalalisha, kusadikisha na kukadhibisha. Kila mwenye kujihalalishia yale yaliyo haramu kwa wengine, basi anaingia katika mkumbo huu. Ewe Mwenyezi Mungu tukinge na shari ya kutojifahamu sisi wenyewe.

Na hapo mbele walikuwa wakiomba ushindi juu ya makafiri lakini yalipowafikia yale waliyokuwa wakiyajua waliyakataa.

Mayahudi kabla ya kuja Mtume Muhammad (s.a.w.) walikuwa wakiwaonya Aus na Khazraj kwa Muhammad. Lakini alipokuja mambo yaligeuka, Aus na Khazraj wakamwamini na wakamsaidia mpaka wakaitwa Ansar (wasaidizi) na Mayahudi wakamkanusha; wakaangamizwa na kufukuzwa na hao Ansar kupitia kwa Muhammad; kama vile walivyokuwa wao wakiwaonya Ansar. Namna hii wanapata wenye vitimbi vibaya, na balaa humshukia yule anayemtakia mwenzake hiyo balaa.

Unaweza kuuliza: Kwa nini Mayahudi waligeuza imani waliyokuwa nayo kwa Muhammad?

Jibu: Walikuwa wakiitakidi kwamba Mtume atakayekuja atakuwa Mwisrail kutoka katika kizazi cha Ishaq, kwa kufikiria wingi wa Mitume Waisrail. Walipomwona ni Mwarabu kutoka katika kizazi cha Ismail, walimkanusha kwa uhasidi na ubaguzi tu wa Kiyahudi. Na kila mwenye kuipinga haki kwa ubaguzi wa kikabila au vinginevyo, basi huyo ni sawa na Mayahudi hao ambao walikataa kumkiri Muhammad, si kwa lolote isipokuwa kwamba yeye ni Mwarabu tu.1

Kibaya kabisa walichokiuzia nafsi zao ni kule kukataa alichokiteremsha Mwenyezi Mungu.

Qur’an tukufu mara nyingi hutumia tamko la kuuza na kununua na biashara, kuhusu amali njema na mbaya. Kwa vile mtu akiamini na akafanya amali njema, ni kama kwamba amefanya biashara ya nafsi yake na kuiokoa; na kama akikufuru na kuacha kunufaika, ni kama kwamba ameiuza nafsi yake kwa shetani kwa thamani duni kabisa.
Kuziuzia nafsi zao hapa ni kwa maana ya kuwa Mayahudi wameziuzia shetani nafsi zao na wamejiangamiza; wala hapana thamani ya nafsi zao isipokuwa hasadi na ubaguzi wa Kiyahudi tu. Kwa hivyo ndiyo Mwenyezi Mungu akasema:

Kwa kuona maya kuwa Mwenyezi Mungu humteremshia fadhila zake amtakaye katika waja wake.

Yaani walimkanusha Muhammad (s.a.w.) si kwa jingine isipokuwa wao walitaka kuhodhi wahyi na fadhila kwao tu peke yao. Hawakubali kutoka kwa Mwenyezi Mungu wala kwa mwengine isipokuwa yale yanayoafiki mapenzi na manufaa yao. Kwa hiyo wao wanastahili adhabu mara mbili, kwa kukanusha na kwa ubinafsi wao.

Na wanapoambiwa: Yaaminini aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu.

Yaani aminini wahyi kama ulivyo bila ya kuangalia utu wa mwenye kuufikisha wahyi huo. Kwa sababu Mtume ni wasila tu wa kufikisha. Ama sharti lenu la kuamini wahyi kuwa uteremshwe kwa taifa la Kiisrail tu, na kama ukiteremshiwa mwengine basi hamwamini, sharti hili linafichua kukosa kuamini wahyi kimsingi. Isitoshe, itakuwa nyinyi mnatoa hukumu kwa Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yenu. Maana yake nyinyi mnataka Mwe-nyezi Mungu awanyenyekee na mnakataa kumnyenyekea.

Husema: Tunaamini yaliyoteremshwa juu yetu.

Huku ni kukiri wazi kwamba wao hawaamini wala hawataamini isipokuwa kwa sharti la kuteremshwa wahyi kwao, na hawataamini wahyi utakaoteremshwa kwa mwingine, hata kama kutakuwa na dalili elfu.

“Sema: Mbona mliwaua Mitume wa Mwenyezi Mungu hapo zamani kama mlikuwa mkiamini.

Hakuna hoja yenye nguvu zaidi ya hii; yaani sema ewe Muhammad kuwaaambia Mayahudi: Nyinyi ni waongo katika madai yenu ya kuamini wahyi kwa kuuhusisha na taifa la Kiisrail, bali nyinyi hamwamini wahyi kabisa, hata ule uliowahusu nyinyi! Dalili ya hayo ni kwamba Mwenyezi Mungu amepeleka Mitume kutoka kwenu na kwa ajili yenu na akawajibisha muwasadiki na kuwatii, lakini pamoja na hayo wengine mliwafanya waongo; kama vile Isa (a.s.) na wengine mkawaua kama vile Zakaria na Yahya. Hii inafahamisha uongo wenu na kugongana vitendo vyenu na maneno yenu na kujidaganya wenyewe.

Imekuwa sawa kuuelekeza msemo wa kuua kwa Mayahudi wa Madina pamoja na kuwa walioua ni mababu zao. Hiyo ni kwa sababu umma wao ni mmoja kwa kushiriki kuridhia kuua.

Waliofanana Na Mayahudi

Mayahudi walimkataa Muhammad (s.a.w.), kwa sababu alikuwa si Mwisrail; Naye Abu Sufian alimkanusha na kuongoza jeshi kumpinga kwa sababu Mtume ni katika ukoo wa Hashim. Alikataa kwa sababu ukoo wa Hashim utapata utukufu wa Utume kuliko ukoo wake yeye Abu Sufiani wa Umayya.

Vile vile Maquraish waliukana ukhalifa wa Ali (a.s.), kwa sababu walichukia kukusanyika Utume na Ukhalifa katika nyumba ya Hashim. Baadhi ya wasiokuwa Waarabu wanaona uzito kuwa Marjaa (Mufti) wa kwanza awe Mwarabu; kama ambavyo baadhi ya waarabu nao wanaona uzito kuwa Marjaa (Mufti) ambaye si Mwarabu.

Mimi nawajua watu ambao wako tayari kubaki kwenye upotevu lau wanahiyarishwa kuifuata haki kwa wasiokuwa wao. Vile vile lau wanahiyarishwa kati ya kusikiliza sifa za mwingine, basi wangeona bora kusikiliza za Yazid. Kwa ajili hiyo ndipo ukaona mtu anafanya juhudi ya kutafuta aibu ya mwenzake akipata chembe tu, huikuza na kuifanya jabali, na akiikosa huizusha.

Mwenye kuona fadhila kuwa ndio msingi, huikuza vyovyote iwavyo na njia yoyote itakavyokuwa na humwonyesha mwingine kama anavyoona yeye; bali hufanya kazi ya kuieneza. Ama mwenye kuikanusha, hutumia muundo huo ambao wameutumia Mayahudi kwa inadi.

وَلَقَدْ جَاءَكُمْ مُوسَىٰ بِالْبَيِّنَاتِ ثُمَّ اتَّخَذْتُمُ الْعِجْلَ مِنْ بَعْدِهِ وَأَنْتُمْ ظَالِمُونَ {92}

Na aliwajia Musana hoja zilizo wazi wazi, kisha mkafanya ndama baada yake na hali nyinyi ni madhalimu.

وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَكُمْ وَرَفَعْنَا فَوْقَكُمُ الطُّورَ خُذُوا مَا آتَيْنَاكُمْ بِقُوَّةٍ وَاسْمَعُوا ۖ قَالُوا سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا وَأُشْرِبُوا فِي قُلُوبِهِمُ الْعِجْلَ بِكُفْرِهِمْ ۚ قُلْ بِئْسَمَا يَأْمُرُكُمْ بِهِ إِيمَانُكُمْ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ {93}

Na tulipochukua ahadi yenu na tukauinua mlima juu yenu: Kamateni kwa nguvu haya tuliyowapa na sikilizeni. Wakasema: “Tumesikia na tumekataa” na wakanyweshwa nyoyoni mwao (imani ya) ndama kwa kufuru yao. Sema: Ni kibaya kabisa kilichowaamrishia imani yenu; mkiwa ni wenye kuamini.

قُلْ إِنْ كَانَتْ لَكُمُ الدَّارُ الْآخِرَةُ عِنْدَ اللَّهِ خَالِصَةً مِنْ دُونِ النَّاسِ فَتَمَنَّوُا الْمَوْتَ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {94}

Sema: Ikiwa nyumba ya akhera iliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni yenu nyinyi tu bila ya watu wengine, basi tamanini mauti kama nyinyi ni wa kweli.

وَلَنْ يَتَمَنَّوْهُ أَبَدًا بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ {95}

Wala hawatayatamani kabisa kwa sababu ya yale yaliotangulizwa na mikonoyao, na Mwenyezi Mungu anawajua madhalimu.

وَلَتَجِدَنَّهُمْ أَحْرَصَ النَّاسِ عَلَىٰ حَيَاةٍ وَمِنَ الَّذِينَ أَشْرَكُوا ۚ يَوَدُّ أَحَدُهُمْ لَوْ يُعَمَّرُ أَلْفَ سَنَةٍ وَمَا هُوَ بِمُزَحْزِحِهِ مِنَ الْعَذَابِ أَنْ يُعَمَّرَ ۗ وَاللَّهُ بَصِيرٌ بِمَا يَعْمَلُونَ {96}

Na Utawaona wanapupia zaidi maisha kuliko watu wengine na kuliko wale wamshirikishao Mwenyezi Mungu. Kila mmoja katika wao anapenda lau angelipewa umri wa miaka elfu. Na huko kupewa kwake umri mwingi hakuwezi kumwondoshea adhabu; na Mwenyezi Mungu anayaona wanayoyatenda.
  • 1. Haya ndiyo waliyoyataja wafasiri kwa kuangalia dhahiri ya Aya. Utakuja ubainifu wa sababu za hakika za kumkanusha kwao Muhammad (s.a.w.) katika Aya ya 91 ambazo ni manufaa na chumo lililotokana na uasherati, udanganyifu, riba, na mengineyo yaliyoharamishwa na Uislamu.