Aya 102: Wakafuata Yale Yaliyofuatwa Na Mashetani

Maelezo

Wafasiri hapa wamerefusha maneno. Wengi wao hawana tegemeo lolote isipokuwa ngano ambazo hazikubaliki kiakili: Razi amechafua karibu kurasa ishirini katika kufasiri Aya hii, akazidisha mikanganyo. Mwenye Majmaul-Bayan naye akafanya hivyo hivyo. Ama Sayyid Qutb yeye ameingilia kuelezea mambo ya kuzugwa watu, ndoto, athari, n.k. Na huku hasa ndiko kukimbia.

Kwa hivyo nikabaki muda mrefu nikitafuta na kupekuwa vitabu na tafsir. Hakikutulia kiu changu hata kwenye tafsir ya Sheikh Muhammad Abduh na wanafunzi wake wawili - Al-Maraghi na mwenye Tafsir ya Al Manar, Bora zaidi ya niliyoyasoma katika mlango huu ni yale yaliyotajwa katika kitabu cha Annuwatu fi Haqli I-hayat cha Sayyid Ubaydiy, Mufti wa Musul (Iraq).

Na haya ndiyo aliyoyasema ninamnukuu: “Niliendelea kutofahamu maana ya Aya tukufu kiasi ambacho hakikunitosheleza kwa mfasiri yoyote, mpaka nilipotua kwenye historia ya Free Mason, ndipo nikajua maana yake.”

Kutokana na kugongana wafasiri kiasi ambacho walionyesha kuwa Aya ina vitu viwili vyenye kutofautiana na kuingiza katika Aya hii ngano za watu wa kale ambazo sharia iliyowazi inazikataa, nimeona ni wajibu nikitumikie kitabu cha Mwenyezi Mungu kuthibitisha haya.

Ulipotukuka Ufalme wa Suleiman, mfalme wa Babiloni alikuwa na chuki na tamaa katika Palestine na Syria, na akaingiwa na hofu badala ya tamaa yake. Wakafanya msafara watu wawili walio wajanja na werevu wakitafuta mafunzo yatakayowawezesha kuuharibu ufalme wa Suleliman.

Wakaingia dini ya Kiyahudi na kuonyesha utawa, kama kawaida wakapata wafuasi, wakawa wanaharibu fikra za watu na kuacha chuki kwa Suleiman mpaka wakamzulia ukafiri. Watu hawa walikuwa kama Malaika kwa wanavyoonyesha utawa.

Lakini walikuwa ni mashetani na mafunzo yao yalikuwa kama uchawi kutokana na ufasaha, na mara kwa mara walikuwa wakitumia neno mfalme kwa mtu mwema, na neno shetani kwa mtu mwovu na neno uchawi kwa ibara ya fitina. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu kumzungumzia Yusuf, alivyozungumziwa.

إِنْ هَٰذَا إِلَّا مَلَكٌ كَرِيمٌ {31}

...Hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu.” (12:31)

Na kauli yake:

شَيَاطِينَ الْإِنْسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا ۚ {112}

“Mashetani katika watu na majini wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupamba kwa udanganyifu.” (6:112)

Vile vile kauli yake Mwenyezi Mungu akimzungumzia Walid:

فَقَالَ إِنْ هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ يُؤْثَرُ {24}

إِنْ هَٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ {25}

“Hayakuwa haya ila ni uchawi ulionukuliwa, hayakuwa haya ila ni kauli ya binadamu.”(74:24-25)

Na kuna Hadith inayosema: “Katika ufasaha kuna uchawi.”

Tumeelezewa historia ya Nebukadnezzar, mfalme wa Babelon katika vita vya Palestin baada ya Suleiman na alivyoiharibu Baitul Maqdis. Na tunaiona Qur’an inatilia nguvu matukio ya historia katika Aya isemayo: Na tukawafahamisha wana wa Israil katika kitabu: Hakika nyinyi mtafanya uharibifu katika nchi mara mbili na kwa yakini mtatakabari kutakabari kukubwa. Basi ilipofika ahadi ya kwanza yake tukawapelekea watumishi wetu wenye mapigano makali, mno wakaingia majumbani kwa nguvu, na hii ilikuwa ahadi iliyotimizwa. (17:4-5)

Ukiyajua haya, basi tunasema: “Dhamiri katika kauli ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.), ‘na wakafuata’, “inawarudia Mayahudi wa Madina, ambao zimetangulia zaidi ya Aya sitini na mbili katika kuwaeleza wao tu.

Utakapoyajua haya, kisha ukazingatia vizuri Aya zinazoambatana na Aya ya Suleiman, na ukafikiria kwa ndani kauli yake Mwenyezi Mungu juu ya ufalme wa Suleiman na madhumuni yake, utajua kwamba maana ya Aya tukufu ni kwamba Mayahudi wa Hijazi walikuwa wakimfanyia Mtume wa Kiarabu vitimbi na propaganda kwa kufuata nyayo za mababu zao ambao waliwasaidia wajumbe wa Babilon katika kuvunja ufalme wa Suleiman.”

Ufafanuzi

Tutafasiri Aya kwa misingi ya alivyofahamu Ubaydiy.

Wakafuata.

Yaani walifuata Mayahudi wa Madina waliokuwa zama za Mtume Muhammad (s.a.w.).

Yale yaliyofuatwa na mashetani

Makusudio ya mashetani ni wadanganyifu; miongoni mwao ni wale watu wawili wa Babilon ambao walijionyesha kuwa ni watakatifu kumbe ni maibilisi.

Katika ufalme wa Suleiman.

Yaani Mayahudi wa Madina walitumia dhidi ya Muhammad, sawa na vile walivyokuwa mababu zao Mayahudi dhidi ya ufalme wa Suleiman.

Suleiman hakukufuru, bali mashetani ndio waliokufuru.

Yaani kila walilomnasibishia Suleiman alikuwa yuko mbali nalo ulikuwa ni udanganyifu na uzushi wao,

Wakiwafundisha watu uchawi.

Yaani wanawafundisha watu mambo ya ubatilifu.

Na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili.

Yaani watu wawili wa Babilon waliodhihirisha utakatifu na ucha Mungu. Makusudio sio kuteremshiwa Wahyi wa Mitume, bali ni kiasi cha kupewa ilham na kufundishwa.

Wala hawakumfundisha, yoyote mpaka wamwambie: Sisi ni fitna (mtihani) basi usikufuru’

Walikuwa wakisema hayo kwa unafiki ili wawapumbaze watu kwamba elimu zao ni za kutoka kwa Mungu na kwamba wao ni watakatifu, wasafi wa nia; sawa na anavyosema mlaghai kumwambia yule anayemfundisha kuandika chuki na mapenzi: “Tahadhari kuandika hivi usije ukawafarikisha waliooana kisheria, au kumfanya mke wa mtu kumpenda asiyekuwa mumewe.”

Wakajifunza kwao mambo ambayo kwayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe.

Yaani yale wanayofikiria kuwa yanaweza kutenganisha mtu na mkewe kama wanavyochukua watu kutoka kwa walaghai, maandishi ya mapenzi na chuki.

Kwa ujumla ni kwamba Aya haifahamishi kuthibiti athari ya uchawi wala kukanusha. Kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu “Wakijifunza kwao ambayo waliweza”, sio hukumu ya uhakika ya kutenganisha mtu na mkewe: Sawa na kusema kunywa kiponyesho, yaani kilichowekwa kwa ajili ya uponyeshaji. Kwa ufupi ni kwamba Aya haithibitishi wala haikanushi. Mara nyingi hekima ya kiungu hupitisha kubainisha kwa upande fulani na kwa ujumla kwa upande mwingine; hasa katika masuala yasiyo ya kiitikadi.

Wala hawakuwa wenye kumdhuru yoyote kwa hayo ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Yaani hawawezi kumdhuru yoyote vyovyote iwavyo kwa sababu ya kusoma na kuandika; kama akidhurika basi ni ku-tokana na sadfa tu, kwamba mtu amedhurika na sababu nyingine ya nje ikaon-ekana ni sababu hii. Makusudio ya idhini ya Mwenyezi Mungu ni sababu ya nje iliyodhuru.

Na wanajifunza yatakayo wadhuru wala hayawanufaishi.

Ni kiini macho tu, na kiini macho hudhuru wala hakinufaishi.

Na kwa hakika wanajua kwamba aliyenunua haya hatakuwa na sehemu yoyote katika akhera.

Wanajua wao kwamba mwenye kupendelea ulaghai hana fungu mbele za Mwenyezi Mungu.

Na bila shaka ni kibaya kabisa walichouzia nafsi zao.

Yaani wamebadilisha kitu cha thamani kwa kitu duni. Imepita tafsiri yake katika Aya ya 61 ya sura hii.

وَلَوْ أَنَّهُمْ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَمَثُوبَةٌ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ خَيْرٌ ۖ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ {103}

Na lau wangeamini na kuogopa,basi thawabu zitokazo kwa Mwenyezi Mungu zingekuwa bora kwao, laiti wangelijua.