Aya 106-107: Aya Yoyote Tunayoifuta

Kufuata

Kwanza tutaeleza maana ya kufuta kwa ujumla katika hukumu za sheria, kisha maana ya kufuta katika Qur’an. Maana ya kufuta katika hukumu ya sheria ni kuja dalili inayofahamisha kuthibiti hukumu ya sheria kwa kudumu na kuendelea muda wote; baada ya kutumika hukumu hiyo kwa muda fulani, inakuja dalili nyingine ya kuthibitisha kwamba hukumu ile ilihusika na kipindi fulani tu; na kwamba masilahi yanahukumilia kutumika katika wakati fulani tu, sio kila wakati.

Lakini hekima ya Mwenyezi Mungu ilidhihirisha kudumu na kuendelea. Sawa na Daktari ambaye anaona masilahi ya mgonjwa ni kutokula nyama kwa muda wa wiki moja tu, lakini akaona ni vizuri amfiche ule muda wa kumkataza.

Baada ya kupita wiki moja akamruhusu kula nyama. Kwa hivyo kufuta kunakuwa kwa maana ya kufuta yale yaliyoonekana kuwa ni ya kudumu na wala sio kuwa ni kwa sababu ya kutojua au kubadili mawazo.

Hakuna mwenye kutia shaka kwamba kufuta kwa maana haya kumethibiti katika sheria ya Kiislamu; kwani sheria imefuta baadhi ya hukumu zake zilizotangulia; kama vile sharia za Musa na Isa. Bali hukumu za Qur’an zenyewe zinafutana; kama vile kugeuza Qibla kuwa Al-Ka’aba (huko Makka) baada ya kuwa Baytul-Maqdis (huko Jerusalem).

Ama kufuta katika Qur’an kunawezekana kukugawanywa katika njia tatu:

1. Kufuta Aya kisomo na hukumu, yaani kuondolewa tamko lake na hukumu yake.

2. Kufutwa kisomo tu; kufutwa tamko na kubaki hukumu.

3. Kufutwa hukumu tu, si kusomwa, yaani inasomwa lakini haichukuliwi dhahiri yake baada ya kutumiwa wakati fulani.

Lakini fungu la kwanza na la pili hayapo, kwa sababu yataleta upungufu na mageuzi katika Qur’an ambayo haifikiwi na batili mbele yake wala nyuma yake.

Ama fungu la tatu linawezekana na limethibiti; ndilo walilolikubali Waislamu wote na wafasiri wote, na limetungiwa vitabu mahsusi. Hivi sasa kimetolewa kitabu kikubwa kwa jina “Annasikh wal-mansukh” (Inavyofuta na inayofutwa) cha Dkt. Mustafa Zaydi wa Misri.

Kwa ujumla inaonyesha kuwa hukumu ya sharia ikithibiti kwa njia sahihi haiwezekani kufutwa isipokuwa kwa Aya ya Qur’an au kwa Hadith mutawatir. Kwa sababu kufuta ni jambo kubwa na la muhimu. Kwa hivyo kufuta hakuwezi kuthibiti kwa habari moja. Kwa sababu kila umuhimu hauna budi kuenea na kutangaa midomoni. Mtu mmoja tu akinakili tukio kubwa au watu wengi, lakini bila ya kuenea, itakuwa ni uwongo. Kwani huoni kifo cha mtu mashuhuri kinanukuliwa na watu wengi! Vile vile mapinduzi! Lakini kifo cha mtu wa kawaida hunukuliwa na baadhi ya majirani na ndugu tu! Ufafanuzi zaidi uko katika Usulul-fiqh (elimu ya misingi ya Fiqh).

Maana

Aya yoyote tunayoifuta au kuisahauliza, tunaleta iliyo bora kuliko hiyo au iliyo mfano wake.

Wafasiri wengi wanasema kwamba Mayahudi walikuwa wakisema kuwa: “Muhammad anawaamrisha masahaba zake jambo kisha anawakataza, leo anasema hili kesho anasema lile, lau anayoyasema kama yangelikuwa ni wahyi, kusingelitokea mgongano huu”. Ndipo ikashuka Aya hii, kuwajibu.

Makusudio ya Aya, ni Aya za Qur’an tukufu, kwani maana haya ndiyo yanayokuja haraka kwenye fahamu. Amenakili Sheikh Maraghi katika tafsir yake kutoka kwa mwalimu wake, Sheikh Muhammad Abduh, kwamba makusudio ya Aya ni muujiza unaofahamisha utume wa Mtume; kwamba Mwenyezi Mungu anampa Mtume muujiza wa Mtume mwingine, kisha anauacha na kuumpa Mtume mwingine muujiza mwingine.

Maana haya yenyewe yako sawa, lakini mpangilio wa Aya unayakataa.Maana yanayolezwa na wanavyuoni na kundi kubwa la wafasiri ni Aya za Qur’an.

Maana ya kufuta Aya ya Qur’an ni kubakia tamko na kisomo pamoja na kuacha hukumu iliyofahamishwa na Aya hiyo ambayo iliwahi kutumika wakati fulani.

Ama maana ya neno Nunsiha likisomwa bila ya harufi Hamza litakuwa lina maana ya kusahau; yaaani kuacha sio kwa kughafilika nayo yani twaiacha kama ilivyo bila ya mabadiliko. Kwani yafaa kusema kitu hiki nimekisahau kwa maana ya kukiacha kama kilivyo. Na likisomwa kwa Hamza, litakuwa na maana ya kuchelewesha na kuahirisha yaani tunaacha kuiteremsha mpaka wakati mwingine.

Vyovyote iwavyo kupatikana herufi ‘Ma’ ya sharti haifahamishi kutokea kufutwa hasa, bali inafahamisha kuwa lau inatokea, basi Mwenyezi Mungu angelileta bora kuliko ile iliyofutwa.

Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu, hujui kwamba Mungu ni wake ufalme wa mbingu na ardhi?

Inasemekana kwamba msemo ‘hujui’ unaelekezwa kwa Mtume na makusudio yake ni Waislamu ambao walidhikika kutokana na upinzani wa Mayahudi na wengineo kuhusu kufutwa.

Ilivyo hasa ni kwamba msemo unaelekezwa kwa kila anayeona ajabu kufutwa au yule anayeumizwa na upinzani. Maana yake ni kuwa kufutwa sio jambo geni.

Kimsingi ni kwamba Mwenyezi Mungu anamiliki kila kitu na anapanga na kupitisha anavyotaka, iwe ni kufuta au kubakisha bila ya kufutwa. Ama kuhusisha kutaja mbingu na ardhi kunafahamisha kukusanya vitu vyote. Kwa sababu mbingu na ardhi zinakusanya viumbe vyote vya juu na vya chini.

Nanyi hamna mlinzi wala msaidizi asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Yaani msijali enyi waumini kwa anayepinga suala la ‘kufutwa’ au kitu chochote katika dini yenu; kiumbe hawezi kuwadhuru maadamu Mwenyezi Mungu ndiye anayetia nguvu na ndiye msaidizi.
Kwa ufupi ni kwamba kufuta ni haki, hakuna kizuwizi cha kutoka akilini au kwenye sharia, kinyume na wanavyofikiri wakanushaji na wapinzani!

أَمْ تُرِيدُونَ أَنْ تَسْأَلُوا رَسُولَكُمْ كَمَا سُئِلَ مُوسَىٰ مِنْ قَبْلُ ۗ وَمَنْ يَتَبَدَّلِ الْكُفْرَ بِالْإِيمَانِ فَقَدْ ضَلَّ سَوَاءَ السَّبِيلِ {108}

Je mnataka kumuuliza Mtume wenu kama alivyoulizwa Musa zamani? Na anayebadilisha imani kwa ukafiri, hakika amepotea njia iliyo sawa.

وَدَّ كَثِيرٌ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَوْ يَرُدُّونَكُمْ مِنْ بَعْدِ إِيمَانِكُمْ كُفَّارًا حَسَدًا مِنْ عِنْدِ أَنْفُسِهِمْ مِنْ بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْحَقُّ ۖ فَاعْفُوا وَاصْفَحُوا حَتَّىٰ يَأْتِيَ اللَّهُ بِأَمْرِهِ ۗ إِنَّ اللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {109}

Wengi miongoni mwa watu wa kitabu wanatamani lau wangewarudisha nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa sababu ya husuda iliyomo nafsini mwao, baada ya kuwapambanukia haki. Basi sameheni na muwache mpaka Mwenyezi Mungu alete amri Yake. Hakika Mwenyezi Mungu Ni muweza wa kila kitu.