Aya 118-120: Mbona Mwenyezi Mungu Husemi Nasi

Maana

Na walisema wale wasiojua; mbona Mwenyezi Mungu hasemi nasi au kutufikia ishara (tunazozitaka). Wale wenye inadi walimwambia Mtume (s.a.w.): “Hatutakuamini mpaka Mungu atwambie ana kwa ana kwamba wewe ni Mtume; au atuletee malaika atakayetufahamisha hilo au atakayeleta hoja tunazozitaka sisi; kama vile alivyowazungumzia Mwenyezi Mungu aliposema: Na walisema: Hatuwezi kukuamini mpaka utububujishie chemchemi katika ardhi... au upande mbinguni na hatutaamini kupanda kwako mbinguni mpaka ututeremshie kitabu tukisome... (17:90, 93)

Mwenyezi Mungu amewajibu hilo kwa kauli yake:

Hivyo hivyo walisema wale waliokuwa kabla yao mfano wa kauli yao (hii). Nyoyo zao zimefanana. Hakika sisi tumezibainisha ishara kwa watu wenye kuyakinisha. Yaani kung’ang’ania huku kwa mawazo ya ubatilifu hakuhusiki na waliyoyatoa kwa Mtume (s.a.w.) tu, kwani watu wa Nabii Musa walimwambia:

أَرِنَا اللَّهَ جَهْرَةً{153}

...Tuonyeshe Mwenyezi Mungu wazi wazi...” (4:153)

Kwa hoja na dalili ambazo hazileti shaka katika nafsi isiyokuwa na shaka na wasiwasi, na kusafika kwa haki kwa njia ya haki.

Mwenyezi Mungu amelifanya hilo na akabainisha dalili zenye kutosheleza juu ya Utume wa Muhammad. Ama kutaka zaidi ni kujitia mashaka na kutaka makubwa.

Kimsingi ni kwamba mpinzani mwenye inadi, haipasi kumjibu bali hupuuzwa na kuachiliwa mbali. Na watu wenye yakini ndio ambao wanatafuta yakini kwa njia yake.

Chenye Kutolewa Dalili Na Aina Ya Dalili

Tumetangulia kueleza katika kufasiri Aya ya 111: (“...Sema: Leteni dalili zenu, kama nyinyi ni wasema kweli”) Kwamba kila dai linahitaji dalili na dalili inahitaji dalili mpaka iishie kwenye asili iliyo wazi ambayo haipingani. Katika kifungu hiki, tutazungumza aina hiyo ya dalili.

Dalili inatofautiana kwa kutofautiana tabia ya kitu. Kwa mfano tukitaka kujua vitu ambavyo vinatengeneza kitu katika vitu vya maumbile tutategemea majaribio na mtaalamu mtafiti. Tukitaka kuthibitisha kuwapo kwa mwenye kupanga mambo mwenye hekima, tutarudia akili.

Tukitaka kujua hukumu yoyote katika hukumu za sharia tutarudia Qur’an na Hadith. Kama tukitaka kujua lugha ya Kiarabu na matamko yake ni lazima kuwarudia wajuzi na istihali za Waarabu wa mwanzo:

Ikiwa kuna masuala ya kikanuni tutarudia kanuni au masuala ya kihistoria tuatawarudia wanaakiolojia na wapokezi wenye kutegemewa.

Hivyo ndivyo zinavyotofautiana dalili kutokana na yanayotakiwa kuthibitisha. Kwa hivyo haifai kwa yeyote, vyovyote alivyo kutoa maoni yake kwa namna ya dalili anayoitaka au kutaka uthibitisho zaidi baada ya kukamilika dalili zote zinazowajibisha yakini na kukinaisha.

Kwa hivyo dalili ya kutosha ikipatikana kisha mwingine akatoa maoni ya dalili nyingine au zaidi, basi huyo ni mwenye inadi na mwenye kutaka makubwa.

Mtume Muhammad (s.a.w.) amewashinda wenye shaka na wapinzani kwa Qur’an; kukathibiti kushindwa kwao na hoja ikatimu. Basi wanapotaka zaidi baada ya kushindwa huko kwenye kufedhehesha, itakuwa matakwa yao hayo ni inadi. Kwani lau kama kusudio lao ni haki, kama ilivyo, basi wangelikinai na wengeliikiri baada ya kuwadhihirikia kwa sura ya ukamilifu iliyo wazi.

Hakika sisi tumekutuma kwa haki, uwe mbashiri na mwonyaji, wala hutaulizwa juu ya watu wa motoni.

Hiki ni kiwango cha kazi ya Mtume na jukumu lake na kwamba yeye ni mwalimu sio mtenza nguvu, na ni mwenye kubainisha haki sio mlazimishaji. Aya hii ni kama Aya inayosema: “Na sema: Ni ukweli uliotoka kwa Mola wako, basi anayetaka na aamini na anayetaka na akufuru... (18:29)

Aya hiyo ni kumuondolea uzito Mtume (s.a.w.) asipatwe na jaka moyo kwa sababu ya kufuru ya mwenye inadi na ya mwenye kufanya upinzani.

Hawatakuwa radhi nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila yao.

Mwenye Majmaul-Bayan anasema: Mayahudi na Wakristo walimwomba Muhammad (s.a.w.) kupatana nao kwa muda kisha watamfuata wamwamini. Ndipo Mwenyezi Mungu akamkatisha tamaa. Hii inafahamisha kuwa haifai kuwaridhisha Mayahudi na Wakristo kwa hali yoyote iwayo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ameambatanisha kuwaridhisha na kuwa Myahudi au Mkristo. Ikiwa haliwezekani hilo, basi haiwezekani kuwaridhisha.

Kwa hakika ni kwamba dini zote na vikundi vyote ni hivyo wala sio Mayahudi na Wakristo tu; bali baadhi ya watu hawawi radhi nawe mpaka uwe mtumwa kwao. Qur’an inapinga hali hii ya kuchukiza na ikatoa mwito kuishi kidini pamoja na dini zote, kuwatukuza Mitume wote na kuwataja kwa heri, na ikawajibisha kuamini Utume wao. Haya ndiyo yenye nguvu zaidi katika kuleta udugu kati ya watu wa dini na kusaidiana.

Mwenyezi Mungu amewahusisha kuwataja Mayahudi na Wakristo ili Mtume akate tamaa nao kuwa watamfuata kama alivyosema mwenye Majmaul-Bayan.

Sema: Hakika uongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uongofu (hasa).

Tumetangulia kueleza katika tafsir ya Aya 26, kwamba neno Huda (uongofu) lina maana nyingi; kama vile kubainisha haki, kuwafikisha kwenye uongofu, thawabu na mengineyo. Hapa lina maana ya Uislamu ambao Mwenyezi Mungu amempelekea Mtume wake Muhammad (s.a.w.); usiokuwa huo ni upotevu sio uongofu. Maana yake ni, sema ewe Muhammad, niliyonayo mimi ndiyo haki na mliyo nayo nyinyi ni upotevu na batili, vipi niache, niifuate upotevu?

Maadui Wa Dini Na Msingi Wake

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemfahamisha Mtume wake mtukufu kwamba Wayahudi na Wakristo hawatamridhia mpaka afuate mila yao; pamoja na kujua kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) isma ya Mtume wake Muhammad s.a.w.) kwamba yeye hatafuata mapenzi yao kwa hali yoyote. Lakini amempa tahadhari hii:

Na kama ukifuata matamanio yao baada ya ujuzi uliokufikia, basi hutapata mlinzi yoyote wala msaidizi kwa Mwenyezi Mungu.

Wafasiri wametaja kufaa hali mbili kutokana na tahadhari na katazo:

Kwanza, kwamba maasi yanawezekana kutokea kwa Mtume lakini anajizuia; yaani yeye anaacha maasi pamoja na kuwa anaweza kufanya; vinginevyo ingekuwa hakuna ubora wowote katika kuyaacha, na ndio yakaja makatazo na hadhari kwenye lile linalowezekana kufanyika bila ya kuangalia isma. Pili, kwamba kwa dhahiri msemo unaelekezwa kwa Mtume, lakini ni kwa watu wote.

Mimi nimefikiria hali ya tatu, kwamba huenda Mtume ilimpitia kuwa Mayahudi watasogea na kuongoka au wamsaidie katika mambo ambayo yataleta heri au yatakayopunguza ugoigoi wao na kuzuia baadhi ya shari zao; ndipo akabainisha Mwenyezi Mungu kwamba maadui wa dini na msingi wake hawawezi kuridhia chochote kwao isipokuwa uache haki uliyo nayo na ufuate upotovu walio nao; kisha akamkataza kupatana nao na kukurubiana. Kwa sababu hilo litawasaidia na kuwapa nguvu; na kutia nguvu huko ni haramu kwako ewe Muhammad na mwingine kama ilivyo haramu kufuata dini yao.

Zaidi ya hayo ni kwamba Mayahudi wana maumbile ya shari na ufisadi, kupinga haki na watu wake na kumfanyia uovu mwenye kufanyia wema; wala halifai kwao jaribio lolote la amani.

Jawabu bora ni kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kumwamuru na kumkataza masum; kama anavyoweza kumwamuru asiyekuwa masum kwa kuangalia utukufu wake na ukubwa wake.
Kisha makatazo haya na hadhari hii inawavunja wale wanaowabembeleza maadui wa dini wanaotoa udhuru kuwa wanafanya hivyo kwa masilahi ya Waislamu.

Kwa sababu adui wa dini na wa nchi, hataki usalama wowote isipokuwa kwa biashara ambayo yeye daima atakuwa ndiye mwenye faida; na nembo yake pekee ni ‘chukua wala usitoe, ukiweza chukua zaidi ya unavyotoa’,

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebainisha hakika hii ya wafanyi biashara hawa kwa ufasaha na uwazi aliposema:

وَلَتَجِدَنَّهُمْ أَحْرَصَ النَّاسِ عَلَىٰ حَيَاةٍ وَمِنَ الَّذِينَ أَشْرَكُوا ۚ{96}

“Na utawaona wana pupia zaidi maisha kuliko watu wengine na kuliko wale walioshirikisha” (2:96)

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلَاوَتِهِ أُولَٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۗ وَمَنْ يَكْفُرْ بِهِ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ {121}

Wale tuliowapa Kitabu wakakisoma kama inavyostahiki kukisoma, hao ndio wanaokiamini. Na wanaokikanusha, basi hao ndio wenye hasara.

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ {122}

Enyi wana wa Israil! Kumbukeni neema yangu niliyowaneemesha na hakika nimewafadhilisha kuliko viumbe wengine.

وَاتَّقُوا يَوْمًا لَا تَجْزِي نَفْسٌ عَنْ نَفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا تَنْفَعُهَا شَفَاعَةٌ وَلَا هُمْ يُنْصَرُونَ {123}

Na ogopeni siku ambayo nafsi haitafaa kitu nafsi nyingine, wala hakitakubaliwa kwake kikomboleo; wala maombezi (shufaa) hayatafaa, wala hawatanusuriwa.