Aya 121-123: Wakakisoma Kama Inavyostahiki

Maelezo

Wale tuliowapa Kitabu wakakisoma kama inavyostahiki kukisoma, hao ndio wanaokiamini.

Baada ya Mwenyezi Mungu kumbainishia Mtume wake, Muhammad (s.a.w.) kwamba Wakristo na Mayahudi hawamwamini, bali hawatamridhia mpaka afuate mila yao, sasa anawavua wale wema wanaoichunga haki katika wao; wale ambao wamesilimu na wakamwamini Muhammad (s.a.w.) na akawaeleza kuwa ni wale ambao wanakisoma kitabu inavyostahiki.

Makusudio ya Kitabu ni kila kitabu alichokiteremsha Mwenyezi Mungu, kiwe ni Qur’an, Tawrat au Injil, kama vilivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu. Kuacha kukihusisha kitabu maalum katika maelezo yake Mwenyezi Mungu ni dalili ya kuwa ni vitabu vyote alivyoviteremsha.

Maana ya kukisoma inavyostahiki, ni kuzingatia vizuri maana yake na kufuata amri na makatazo yake; sio kusoma vizuri, kudhibiti matamko, na kuzitoa herufi sawa sawa (tajwidi tu). Kwani hilo si chochote ikiwa hakuna kuzingatia vizuri na kuongoka. Kuna Hadith tukufu inayosema: “Hakuiamini Qur’an mwenye kuhalalisha yaliyoharamishwa.”

Jumla ya maneno ni kwamba Tawrat na Injil vyote vimebashiri Utume wa Muhammad (s.a.w.); kama ambavyo Qur’an imefahamisha ukweli wake. Ndio maana wengi walisilimu miongoni mwa Mayahudi, Wanaswara na Washrikina ambao walizingatia vizuri Aya na wakaifuata haki kama ilivyo.

Na wanaokikanusha, basi hao ndio wenye hasara.

Yaani mwenye kukanusha aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu ambayo yanalazimisha kumkanusha Muhammad (s.a.w.), huyo ni katika wenye kuhasirika, kwa sababu ni sawa na mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu. Ni wazi kwamba hapana hasara kubwa zaidi kuliko hasara ya akhera na neema yake yenye kubaki.

Enyi wana wa Israil! Kumbukeni neema yangu niliyowaneemesha na hakika nimewafadhilisha kuliko viumbe wengine.

Tafsir ya Aya hii imeshatangulia katika Aya 40. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekariri kuwakumbusha Mayahudi neema yake katika Aya nyingi kwa lengo la kuwatahayariza kwa namna ya ufasaha zaidi na hekima; kama alivyotumia katika kauli yake: “Na iogopeni siku ambayo nafsi haitafaa kitu nafsi nyingine” ambayo pia tafsir yake imepita katika Aya 48.

Mujtahidi Na Muqallid

Sheikh Muhammad Abduh alitoa mwito wa ijtihad (kujitahidi) na kuwakemea watu wa Taqlid wenye kufuata tu, na alikuwa na darasa ya kufasiri Qur’an alipofika kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.): “Wakakisoma kama inavyostahiki.”

Alisema: “Yule ambaye anasoma Qur’an kwa kusoma tu, mfano wake ni kama punda aliyebeba vitabu vikubwa, hana imani kwa sababu hafahamu siri yake wala hajui uongofu wa Mwenyezi Mungu ulio ndani yake.

Kusoma matamko tu, hakuna faida yoyote, hata kama msomaji atajua maana ya hayo matamko. Kwa sababu itakuwa kama picha; na picha ni mawazo, yanakuja kisha yanapotea.
Hakika fahamu sahihi ni kufahamu kwa imani na kusadikisha, kwa yule anayezingatia vizuri kitabu na kutaka kuongoka akijua kuwa anasoma Aya zake ili aongoke na kupata uongofu kutokana na maana yake.”

Basi baadhi ya masheikh wa Taqlid wakamwingilia kati kwa kusema “Wanavyuoni wanasema: ‘Quran ni ibada kwa kuisoma.’Sheikh Abduh akajibuLakini Mwenyezi Mungu amesema: Kitabutumekiteremsha kwako, kilicho barikiwa ili wazizingatie Aya zake, na wenye akili wawaidhike. (38:29)

Na katika rai za Sheikh Abduh, kama ilivyo katika Tafsir Al-Manar ni kwamba, ni juu ya kila Mwislamu asome Qur’an au kuisikiliza yote ijapokuwa mara moja tu katika umri wake.

وَإِذِ ابْتَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ رَبُّهُ بِكَلِمَاتٍ فَأَتَمَّهُنَّ ۖ قَالَ إِنِّي جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَامًا ۖ قَالَ وَمِنْ ذُرِّيَّتِي ۖ قَالَ لَا يَنَالُ عَهْدِي الظَّالِمِينَ {124}

Na Mola wake alipomjaribu Ibrahim kwa matamko, naye akayatimiza. Aliwambia: Hakika mimi nimekufanya Imam wa watu. Alasema: Na katika Kizazi changu (pia) Akasema: Ahadi yanguu haiwafikii madhalimu.