Aya 125-126: Na Tulipoifanya Ile Nyumba Iwe Mahali Pa Kuendewa

Lugha

Nyumba ni nyumba yoyote, lakini ikisemwa nyumba tu, basi itakuwa ni Al-Kaaba, kutokana na kutumika sana hivyo.

Maana

Na tulipoifanya ile nyumba (Al-Kaaba) iwe mahali pa kuendewa na watu na mahali pa amani.

Aya hii inaungana na Aya iliyotangulia (alipomfanyia mtihani Ibrahim). Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu ameijaalia nyumba yake ni mahali pa kuendewa na watu makundi kwa makundi kwa ajili ya kutekeleza ibada na baadaye warudi makwao; kisha yaje makundi mengine, n.k.

Vile vile ameifanya ni mahali pa kupata amani katika akhera. Kwa sababu mtu anapoifikia nyumba hiyo na akatekeleza ibada anajirudi na kutubia. Kwa hiyo nyumba ya Al-Kaaba inakuwa ni nyenzo ya kujitakasa na adhabu na mateso.

Kama vile ambavyo ameifanya ni mahali pa amani katika dunia. Kwa sababu mtu mwenye kwenda mahali hapo anakuwa salama wala haingiliwi na yeyote kwa ubaya.

Mtu anaweza kumwona mtu aliyemuua baba yake katika Haram (eneo la Al-kaaba) lakini akajitia hamnazo! Desturi hii imerithiwa tangu wakati wa Ismail (a.s.) mpaka leo.

Mkosaji Kukimbilia Haram

Katika kitabu cha Al-Jawahir ambacho ni tegemeo kubwa la Fiqh ya Shia Jafariyyah kuna maelezo haya, ninamnukuu: “Yeyote aliyekimbilia haram hapigwi haddi kwa kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.)”

وَمَنْ دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا ۗ {97}

“Na mwenye kuingia humo huwa katika amani” (3:97)

Bali atapunguziwa chakula na atapewa kidogo tu kiasi cha kuzuwia tumbo ili atoke akapigwe haddi nje.

Imepokewa riwaya sahihi kutoka kwa Imam Jafar Sadiq (a.s.) kuhusu mtu ambaye amefanya jinai mahali pengine pasipokuwa Haram kisha akakimbilia kwenye Haram. Akasema Imam: “Hatapigwa haddi, lakini hatalishwa, hatapewa maji wala hatasamehewa, kwani akifanyiwa hivyo, kuna uwezekano wa kutoka nje ya Haram na apigwe haddi. Kama akifanya jinai ndani ya Haram atapigwa haddi ndani ya Haram, kwa sababu hakuihishimu Haram.”

Abu Hanifa amesema: “Haifai kumwua aliyekimbilia kwenye Haram” ametoa dalili kwa kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na tulipoifanya ile nyumba (Al-Ka’aba) iwe mahali pa kuendewa na watu na mahali pa amani.”

Na pafanyeni alipokuwa akisimama Ibrahim ni mahali pa kuswali.

Hiyo ni amri ya kuswali (Maqamu Ibrahim) mahali aliposimama Ibrahim. Mafaqihi wamekubaliana kuwa inatakikana kuswali hapo rakaa mbili za Tawaf ikiwezekana. Maana ya (Maqam Ibrahim) mahali aliposimama Ibrahim ni pale mahali maarufu ndani ya msikiti. Ama mwenye kusema kwamba makusudio yake ni msikiti wote, basi na atoe dalili ya kuthibitisha kauli yake hiyo.

Na tuliagana na Ibrahim na Ismaili kuwa itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wenye kutufu na wenye kujitenga kwa ibada na wanaorukuu na kusujudu.

Maana yake, tulimwagiza Ibrahim na Ismaili kuiheshimu Al-Ka’aba na kuiepusha na kila lisiloelekeana nayo; kama vile masanamu, najisi, upuuzi, uovu, majadiliano n.k. Na wawaamrishe watu hilo “Wanye kutufu ni wale wanaoizunguka, wanaojitenga kwa ibada ni wanaokaa humo msikitini au wanaokaa karibu kwa ibada, na wanaorukuu na kusujudu, yaani wanaoswali.

Na aliposema Ibrahim Ewe Mola wangu! Ufanye mji huu uwe wa amani.

Hii ni dua na matamanio kutoka kwa Ibrahim kwa Mwenyezi Mungu kuijaalia Makka tukufu kuwa ni mji wa amani, yaani watu wake wasiwe na vita, mitetemeko, vimbunga n.k.

Kuna kikundi cha wafasiri wamesema kwamba Mwenyezi Mungu ameiitikia dua ya Ibrahim, ambapo hakuna yeyote anayeikusudia Makka kwa uovu ila Mwenyezi Mungu humwangamiza, na mwenye kuikusudia kwa uadui basi uadui wake hauchukui muda mrefu.

Na uwape wakazi wake matunda wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Ibrahim alipomaliza kujenga nyumba hiyo katika ardhi kame isiyokuwa na maji wala mmea wowote, alimwomba Mwenyezi Mungu s.w.t. aipe amani ardhi hii na iwe na rizki, wala hakuainisha aina ya riziki wala kule itakapotoka isipokuwa umuhimu ni kufikiwa na riziki vyoyote itakavyokuwa na popote itakapotoka.

Mwenyezi Mungu Mtukufu aliitikia maombi ya Ibrahim. Ikawa riziki ya namna namna inakuja Makka kutoka sehemu mbali mbali; ikawa Makka ni kituo cha wasafiri na cha biashara. Katika hali hii ndipo Mwenyezi Mungu akasema katika Aya hii: Je hatukuwakalisha mahali patakatifu na pa amani yanakoletwa matunda ya kila aina.(28:57)
Ibrahimu aliwahusisha waumini tu katika kutaka riziki, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikwisha mfahamisha kwamba katika kizazi chake kutakuwa watu madhalimu na Mwenyezi Mungu hakuuhaidi Uimamu kwa madhalimu.

Akasema (Mwenyezi Mungu s.w.t.): Na mwenye kukufuru nitamstarehesha kidogo.

Yaani Mwenyezi Mungu alimwambia Ibrahim: Mimi vile vile ninawaruzuku makafiri na hata mafasiki. Kwa sababu riziki ni kitu kingine na Uimamu ni kitu kingine, kwani Uimamu ni uongozi wa kidini na wa wakati, nao unahitajia imani, uadilifu na Isma.

Ama riziki inakuwa kwa mwema na mwovu; kama vile maji na hewa. Madhambi na maasi hayana dhara yoyote katika umri na riziki katika maisha haya, isipokuwa athari yake itadhirhirika kesho siku ya kiyama ambapo watu watapata malipo yao.

وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا ۖ إِنَّكَ أَنْتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ {127}

Na Ibrahim alipoinua misingi ya ile Nyumba (Al-Kaaba) na Ismail (wakaomba): Ewe mola wetu! Tutakabalie; hakika wewe ndiye Msikizi Mjuzi.

رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِنْ ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُسْلِمَةً لَكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَا ۖ إِنَّكَ أَنْتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ {128}

Ewe mola wetu! Utufanye tuwe ni wenye kusilimu kwako. Na miongoni mwa kizazi chetu pia ufanye umma uliosilimu kwako. Na utuonyeshe ibada zetu na utukubalie toba. Hakika wewe ndiye mwenye kukubali toba mwenye kurehemu.

رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولًا مِنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنْتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {129}

Ewe mola wetu! Wapelekee mtume anayetokana na wao, awasomee Aya zako, na kuwafundisha Kitabu na hikima na awatakase. Hakika wewe ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.