Aya 127-129: Na Alipoinua Ibrahim Misingi Ya Ile Nyumba

Historia Ya Al-Ka’aba

Wafasiri na wanahistoria wametofautiana katika historia ya Al-Ka’aba, kwamba je, ilikuako kabla ya Ibrahim, kisha ikaharibika ndipo akaijenga upya yeye na mwanawe Ismail kwa amri ya Mwenyezi Mungu mtukufu; au yeye (Ibrahim) ndiye aliyeanza kuijenga?

Wafasiri wengi na wanahistoria wa Kiislamu wamesema kuwa ilikuwako kabla ya Ibrahim kwa miaka mingi. Baadhi wamesema ilianzishwa na Ibrahim (a.s.); wengine wamenyamaza na kusema: “Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi. Nasi tuko pamoja na hawa. Kwani akili haina nafasi hapa, na njia ya kujua itategemea athari au Aya za Qur’an au Hadith mkato.1

Na mimi sikupata kauli yoyote ya watafiti wa athari na uvumbuzi, na Qur’an haikuelezea waziwazi historia ya Al-Kaaba, bali inaelezea tu kwamba Ibrahim na mwanawe Ismail waliijenga na kusaidiana. Na hii haifahamishi kuwa ilikuwako au haikuako kabla ya Ibrahim. Na Hadithi mkato hakuna isipokuwa Hadithi Ahad (pwekesho).2
Na Hadithi pwekesho ni hoja katika hukumu ya sheria tu.3
Kwa vyovyote iwavyo sisi hatutaulizwa na Mwenyezi Mungu mtukufu wala hatuna wajibu wa kuijua historia ya kujengwa Al-Kaaba au kujua wakati ilipoanzishwa.

Vile vile hatuna taklifa ya kujua kwamba hiyo ni sehemu ya pepo au ni ya ardhi na kwamba je, Adam na Mitume baada yake walihiji au la! Au kwamba hiyo Al-Ka’aba ilipandishwa mbinguni wakati wa Tufani kisha ikateremshwa ardhini.?

Pia hatuna taklifa ya kujua kwamba Hajarul-Aswad (jiwe jeusi) lililetwa na Jibril kutoka mbinguni au lilikuja pamoja na Adam kutoka peponi au lilibanduka kutoka Jabal Abu Qubays na kwamba je lilikua jeusi kwa sababu ya kuguswa na wenye dhambi. Na mengineyo ambayo hayana mapokezi yoyote isipokua Hadithi Ahad au visa visivyokuwa na ukweli.

Sisi hatutaulizwa vitu vyote hivyo wala hatuna taklifu yoyote ya kujua si kwa njia ya wajibu, wala sunna; si kiakili wala kisheria. Wala hakuna faida yoyote ya kidini au dunia katika kuifanyia utafiti. Utafiti huu ulikuako kisha ukaenda na upepo; na yeyote anayetaka kuufufua, ni sawa na yule anaejaribu kurudisha nyuma mishale ya saa.

Kitu ambacho tutaulizwa na kutakiwa kukifanya kuhusu Al-Ka’aba ni kuikusudia kwa ajili ya Hijja na Umra kwa anayeweza kuiendea. Na vile vile kuiheshimu na kuitukuza na kuihami kwa kufuata nyayo za Mtume (s.a.w.) Ahlul Bait wake (s.a.w.), masahaba, wafuasi, wanachuoni na Waislamu wote. kwani hao wanaamini bila ya tashwishi yoyote kwamba kuiadhimisha nyumba ya Mwenyeezi Mungu ni kumwadhimisha Mwenyezi Mungu, na kuihami ni kuihami dini ya Mwenyezi Mungu.

Amirul Muminin amesema: “Amewawajibisha Mwenyezi Mungu kuhiji nyumba yake tukufu ambayo ameifanya ni kibla cha viumbe,wanaingia kama wanavyoingia wanyama na wanaingia makundi makundi kama njiwa. Ameijaalia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni alama ya kumnyenyekea yeye (Mungu) na kuukubali Utukufu Wake. Ameijaalia ni alama ya Waislamu, na nikinga ya wenye kutaka hifadhi.”

Ewe mola wetu!Tutakabalie

Hii ni dua kutoka kwa Ibrahim na Ismail ya kutaka thawabu kutokana na amali hii, kwa sababu maana ya kutakabaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kupata thawabu kutokana na amali atakayoikubali, kama vile ambavyo kukosa thawabu kunamaanisha kukataliwa amali. Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu ameitakabali dua yao na amewalipa thawabu kutokana na twaa hii. Kwa sababu yeye ndiye aliyefungua mlango wa dua, na hawezi kumfungulia mja mlango wa dua, hasa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, kisha amfungie mlango wa kutakabaliwa, kama alivyosema Amirul Muminini.

Ewe Mola wetu! Utufanye tuwe ni wenye kusilimu kwako.

Makusudio ya kusilimu hapa ni kufanya ikhlas katika itikadi na amali (matendo). Hapana mwenye shaka kwamba mwema mwenye kusifiwa, ni yule anayemnyen-yekea Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mambo yake yote.

Na miongoni mwa kizazi chetu (pia ufanye) umma uliosilimu kwako.

Ameikubali dua yao na akajaalia katika kizazi chao mamilioni na mamilioni ya waislamu.

Shia Na Mababu Wa Mtume

Shia wamehusika na kauli ya kuwa baba wa Muhammad, na mababu zake, mama yake na nyanya zake wote hawa-kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote na kwamba Muhammad tangu alipoumbwa alikuwa akigura (akihama) katika migongo mitakatifu mpaka kwenye tumbo la mfuko wa uzazi mtakatifu na hadi ilipotimu saa ya kuzaliwa kwake.

Sheikh wa Shia mwenye kujulikana kwa jina la Sheikh Al-Mufid amesema katika sherhe ya Aqaid Aswaduq chapa ya mwaka 1371 A.H. uk 67: “Hakika mababa wa Mtume (s.a.w.) kuanzia baba yake Adam, walikuwa ni watu walio na imani, na Mwenyezi Mungu amemwambia Mtume wake Muhammad:

وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ {219}

“Na mageuko yako kati ya wale wanaosujudu.” (26:219)

Mtume (s.a.w.) amesema: “Niliendelea kugurishwa katika migongo mitakatifu kwenda kwenye matumbo matakatifu mpaka Mwenyezi Mungu akanidhihirisha (kwa kuzaliwa) katika ulimwengu wenu huu.” Kwa hiyo kauli ya Mtume inafahamisha kwamba mababu zake wote walikuwa wenye imani. Kwani lau baadhi yao wangekuwa makafiri isingelistahiki kusifiwa na utwahara kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:

إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ{28}

“Hakika washirikina ni najisi”.(9:28)

Mtume alipowasifu mababu zake kwa utakatifu imefahamisha kwamba wao walikuwa waumini

Utukubalie toba

Sio lazima kwa mwenye kutaka msamaha awe na dhambi hasa ikiwa mwenye kutaka ni Mtume au wasii. Kwa sababu watu watukufu hawa wanajiona hawajafikia kuitekeleza haki ya Mwenyezi Mungu sawa sawa kadiri watakavyojitahidi katika ibada ya Mwenyezi Mungu. Kwani wao ndio wanaojua zaidi utukufu wa Mwenyezi Mungu. Na kwamba ibada ya mtu, vyovyote itakavyokuwa haiwezi kutekeleza haki ya utukufu huo usiokuwa na mwanzo wala mwisho.

Ewe, Mola wetu! Wapelekee Mtume anayetokana na wao

Ombi hili alilikubali Mwenyezi Mungu kwa kuleta Mtume wa mwisho na bwana wa Mitume wote. Zimekuja Hadith kwa upande wa Shia na Sunni kwamba Mtume amesema: “Mimi ni ombi la Ibrahim na ni bishara ya Isa.”

Katika Qur’an Mwenyezi Mungu amesema:

هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِنْ كَانُوا مِنْ قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {2}

“Yeye ndiye aliyemuinua Mtume katika wasiojua kusoma atokaye miongoni mwao anawasomea Aya zake na kuwatakasa na kuwafunza kitabu na hekima. Na kabla ya hayo walikuwa katika upotofu ulio dhahiri.” (62:2)

Amirul Muminin Ali (A.S.) amesema: “Alimpeleka Mwenyezi Mungu Muhammad kuwa ni Mtume na hakuna yeyote katika waarabu aliyekuwa akisoma kitabu au kudai Utume wala wahyi.”

Bishara Ya Mahdi Mwenye Kuongtojewa

Kama walivyotoa Mitume bishara ya Muhammad, yeye naye alitoa bishara ya Mahdi kutoka katika kizazi chake. Mimi nimetunga kitabu juu ya suala hilo nilichokiita Al Mahdil Muntadhar Wal-aql (Mahdi mwenye kungojewa na akili) katika kitabu hicho nimenakili Hadith nyingi kutoka upande wa Shia na Sunni; na zimetoka nakala nyingi na kurudiwa na wachapishaji ‘Daarul-malayin’ pamoja na kitabu ‘Allahu wal-aql’, ‘Al- akhira wal-aql’ na ‘Annubuwwat wal-aql’. Vitabu hivyo vine vimekusanywa kuwa kitabu kimoja kwa jina Al Islamu wal-aql (Uislamu na akili).

Kitabu kilichokusanya zaidi kuhusu suala hili katika nilivyovisoma ni kitabu kinachoitwa Muntakhabul-athari fil - Imam thani ashar cha Sayyid Lutfillah Assafi kilichokuwa na kurasa zaidi ya 500, ambacho ni rejea bora zaidi. Baada ya kuchapishwa kitabu ‘Al-Mahdil muntadhar wal-aql’ nilisoma maneno marefu ya Muhyiddin aliye mashhuri kwa jina la Ibnul Arabi, nanukuu sehemu ya maneno hayo. “Mwenyezi Mungu anaye Khalifa atakayetoka ikiwa nchi imejaa dhulma na jeuri ili aijaze uadilifu...na khalifa huyo ni kutoka katika kizazi cha Mtume (s.a.w.) kutoka katika kizazi cha Fatima (a.s.), jina lake linafanana na jina la babu yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu ...Atafanyiwa baia kati ya ukni na maqam, anafanana na Mtume kwa umbo naye atakuwa na uso mwangavu mwenye pua ndefu... Atawaongoza watu kwa desturi ya Mtume (s.a.w.). Na babu yake alisema kumhusu yeye: Atafuata athari yangu bila kukosea na hiyo ndiyo Isma.” Hayo amo katika kitabu Futuhatil-Makkiyya kilichochapishwa na Darul-kutubil-Arabiya uk 327 na kuendelea.

وَمَنْ يَرْغَبُ عَنْ مِلَّةِ إِبْرَاهِيمَ إِلَّا مَنْ سَفِهَ نَفْسَهُ ۚ وَلَقَدِ اصْطَفَيْنَاهُ فِي الدُّنْيَا ۖ وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ {130}

Na ni nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipokuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na hakika sisi tulimtakasa (Ibrahim) katika dunia; na hakika yeye katika akhera atakuwa miongoni mwa watu wema
.

إِذْ قَالَ لَهُ رَبُّهُ أَسْلِمْ ۖ قَالَ أَسْلَمْتُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ {131}

Mola wake alipomwambia silimu; akasema Nimesilimu kwa Mola wa walimwengu wote.

وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنْتُمْ مُسْلِمُونَ {132}

Na Ibrahimu akawausia haya wanawe, na pia Yaqub: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu
.

أَمْ كُنْتُمْ شُهَدَاءَ إِذْ حَضَرَ يَعْقُوبَ الْمَوْتُ إِذْ قَالَ لِبَنِيهِ مَا تَعْبُدُونَ مِنْ بَعْدِي قَالُوا نَعْبُدُ إِلَٰهَكَ وَإِلَٰهَ آبَائِكَ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ إِلَٰهًا وَاحِدًا وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ {133}

Je, mlikuwapo yalipomfikia Yakub mauti, alipowaambia wanawe: Je, mtaabudu nini bada yangu? Wakasema: Tutamwabudu Mola wako na Mola wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is-haka; Mungu mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake.

تِلْكَ أُمَّةٌ قَدْ خَلَتْ ۖ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَلَكُمْ مَا كَسَبْتُمْ ۖ وَلَا تُسْأَلُونَ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ {134}

Huo ni umma uliokwisha pita. Utapata Uliyoyachuma nanyi mtapata mtakayoyachuma; wala hamtaulizwa waliyokuwa wakiyafanya.
  • 1. Hadithi iliyokubaliwa na wote katika maana na matamshi.
  • 2. Hadith ambayo silsila (mfuatano) ya upokezi wake imekatika au Hadith ambayo haikubaliwi na wengi.
  • 3. La Kushangaza zaidi ya niliyoyasoma kuhusu maudhui haya ni kauli ya Sayyid Tabatabai katika Tafsir Al-Mizan J1 Uk 196 “Kukosekana kusihi mapokezi ya hadith hakuwajibishi kuitupa Hadith hiyo maadamu haihalifu akili au Hadith sahihi”. Inajulikana wazi kwamba kutohalifu akili na Hadithi thabiti ni sharti la yasiyothibiti, kwa sababu kutothibitika kusihi mapokezi kunatosha kuitupa Hadithi bila ya kuongeza sharti jengine; kama si hivyo basi itabidi kuitumia kila Hadithi isiyokuwa sahihi mpaka itakapohalifu akili au hadithi thabiti.