Sura Ya Ishirini

Abu Dharr alikuwa anaona siku zinapita akiwa Rabzah katika hali ya upekee na upweke. Hapakuwepo na mtu wa kumtunza na kujua hali yake. Alikuwa hana njia ya kufarijika. Kama familia yake ingekuwepo naye, hangehisi uchungu wa upweke kiasi hicho. Familia yake ilikua bado ipo Syria na Abu Dharr akafukuzwa na kupelekwa Madina na halafu akafukuzwa kupelekwa Rabzah.

Abdul Hamid Jaudatus Sihar ameandika kwamba Muawiyah alipopata taarifa kwamba Uthman amemfukuza Abu Dharr na kumpeleka Rabzah, akamsafirisha mkewe na (wengineo) kwenda huko. Mke wa Abu Dharr alipotoka nje ya nyumba yake, alikuwa na sanduku tu. Muawiyah akawaambia watu, “Tazameni vitu anavyo miliki mhubiri wa maadili.” Baada ya kusikia hivi mke wa Abu Dharr akasema, Ndani ya begi hili zipo sarafu chache na si dinari na hizo pia zinatosha kwa matumizi tu.” Mkewe alipofika Rabzah aliona kwamba Abu Dharr alikwisha jenga msikiti.

Waandishi wa historia wengi wameandika kuhusu Abu Dharr kujenga msikiti huko Rabzah. Tunaona kutajwa kwa msikiti huo kwenye vitabu vya Tabari bin Athir na bin Khaldun. Kwenye nakala ya Kiarabu ya Tabari ipo sentensi isomekayo, ‘Abu Dharr alikuwa ameweka alama za msikiti, na mahali hapo ndipo ambapo alikuwa akisali, kama vile ilivyo leo, watu hukusanya udongo porini na kuuita msikiti, wala haingewezekana yeye kujenga msikiti kama wa siku hizi. Kwa mujibu wa Abdul Hamid, siku za Hija watu walipopita Rabzah walisali kwenye msikiti wa Abu Dharr.

Maana yake ni kwamba, sehemu hiyo haikuwa na watu. Endapo pangekuwepo na watu, ingeandikwa kwenye msikiti huo, kama vile ambavyo imetamkwa kwamba mahujaji walikuwa wanaswali kwenye msikiti huo.

Allamah Subaiti ameandika kwamba Abu Dharr alikuwa katika hali ya upweke na alikuwa akipitisha siku zake Rabzah katika hali ambayo hakuna binadamu angeonekana hapo isipokuwa mara chache ambapo mpita njia alipita hapo. Hapakuwepo sehemu yoyote ambapo angejihifadhi. Aliishi chini ya mti. Hapakuwepo na mpango wowote wa chakula chake, palikuwepo na majani yenye sumu sehemu yote iliyozunguka hapo na hayo ndio yaliyo sababisha kifo chake na cha mkewe.” (Abu Dharr al-Ghifari, uk. 165, chapa Najaf, 1364 A.H).

Baada ya hapo, mwandishi anaongeza kwamba, sababu ya kumpeleka Abu Dharr mahali kama hapo ilikuwa kusitishwa hotuba zake, ili pasiwepo na mtu wa kumsikia kwani alikuwa na ucheshi kwenye ulimi wake. Wakati wote aliposema, alisema ukweli, ambao ulitikisa misingi ya serikali.

Kwa ufupi, Abu Dharr alikuwa anaishi maisha yake na familia yake katika hali ya dhiki sana. Hapakuwepo na mtu wa kumliwaza huko.

Lakini wale watu waaminifu ambao walikua wanampenda na kumheshimu katika nyoyo zao walikuwa na desturi ya kwenda kumuona.

Kwa mujibu wa mwandishi wa historia, Waqidi, Abul Aswal Duayli anasema; “Nilikuwa nataka kumtembelea Abu Dharr kwa moyo wangu wote na kumuuliza kwa nini alifukuzwa. Kwa hiyo, nilikwenda kwake Rabzah na nikamuuuliza kama aliondoka Madina kwa chaguo lake mwenyewe au alifukuzwa kwa lazima. Akasema; “Ndugu yangu! Namna ya kukuambia kwamba nilipopelekwa Syria nilidhani kwamba nimekwenda mahali ambapo ni muhimu kwa Waislamu.

“Nilifurahi kuwa kule, lakini sikuruhusiwa kukaa huko na nikaitwa tena Madina. Nilipofika huko nilijiliwaza mwenyewe kwa fikra kwamba hiyo ilikwua ni sehemu ambayo ilikuwa nimehamia na ambapo nilipata heshima ya usahaba wa Mtukufu Mtume. Lakini, loo, pia nilifukuzwa kutoka hapo na nipo hapa unaponiona.” Baada ya hapo akasema, “Ewe Abul Aswad! Sikiliza, nikuambie. Siku moja nilikuwa nimelala kwenye msikiti wa Mtume.

Kwa bahati tu Mtukufu Mtume aliingia msikitini. Akaniamsha na akasema, “Ewe Abu Dharr! Kwa nini unalala msikitini?”

Abu Dharr, “Usingizi ulinizidi na ghafla nikalala.
Mtume, “Niambie utafanya nini utakapofukuzwa kwenye msikiti huu?

Abu Dharr, “Nitakwenda Syria, kwa sababu zipo ishara za Uislamu, huko. Pia sehemu hiyo ni mahali pa Jihadi.

Mtume, “Utafanya nini utakapofukuzwa huko pia?”

Abu Dharr, Wakati huo nitachomoa upanga wangu na kumuua mtu atakaye nifukuza.”

Mtume, “Ninakupa ushauri mzuri sana.” Abu Dharr, “Ushauri gani huo?”

Mtume, “Toa ruhusa ya kuburuzwa utakapoburuzwa, na kwamba ukubali kila unaloambiwa, na usipigane.

Ewe Abul Aswad! Kufuatana na ushauri wa Mtume, nilisikiliza nilivyoambiwa nao na nikakubali yale waliyoyasema. Bado ninaendelea kusikiliza wanayoyasema. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Atalipa kisasi kwa Uthman kwa yale ambayo amenifanyia na atathibitishwa kuwa mtenda dhambi mbaya kuzidi, kuhusu hili tatizo langu atakapofika kwenye mahakama ya Mwenyezi Mungu.”

(Sharh bin Abil Hadid, Juz. 1, uk 214; Murujuz Zahab Musudi, Juz. 1, uk. 238; Tarikh Yaqubi, Juz. 2, uk 148, Mustadirak Hakim, Juz. 3, uk. 343; Hulyah Abu Naima, Juz. 1, uk 162; Tabaqatul Kubra bin Sad, Juz. 1, uk. 166; Musnad Ahmad, Juz. 5, uk 156 na 180; Sunan Abi Daudi, Juz. 3, uk 213; Umdatul Qari Sharh Sahih Bukhari 8, Juz. 4, uk 291).

Wasimuliaji wa hadithi hii ya kuaminika ni watu wa kuaminika sana na kutegemewea kama ilivyo andikwa na Allamah Amini kwenye kitabu chake ‘al-ghadir.’

Mtu alimuuliza Abu Dharr wakati alipokuwa anaishi Rabzah, “ewe Abu Dharr unao utajiri wowote?” Akasema, “Utajiri wangu ni matendo yangu.”
Pia akasema, Ninaposema utajiri nina maana utajiri huu wa hapa duniani na ninataka kujua endapo unao utajiri wa kidunia au hapana.” Abu Dharr akasema; “Kamwe sijawahi kuwa na utajiri wa kidunia hata kwa siku moja au usiku moja nikiwa na hazina au tajiri wa kidunia na mimi. Nimesikia kutoka kwa Mtukufu Mtume kwamba utajiri wa mtu ni kaburi yaani utajiri wa kidunia haufai lolote, lakini mwenendo wa mtu lazima uwe mzuri kwa sababu utamtumikia kila mahali hususan Kaburini. Utajiri wa dunia hubaki duniani, na tabia njema hukunufaisha wewe huko Peponi.” (Hayatul Qulubi, Juz. 2, uk. 1046).

Allamah Majlis akimnukuu Shaykh Mufid anasimulia kutoka kwa Abu Ammah Bahili1 kwamba Abu Dharr baada ya kufika Rabzah alimuandikia mambo ya hatari yaliyo mpata Huzayfah bin al-Yaman,2 sahaba wa Mtukufu Mtume ambaye labda alikuwa Kufah. Kwenye barua hiyo, ametoa, ushauri wa aina mbali mbali na akaeleza kuhusu shida zake na matatizo yake. Ameandika’ Nuorullah Shustari kwamba wakati moja Huzayfah alimtembelea Abdullah bin Umar ambaye hakumheshimu. Wakati huo Huzayfah alimwambia kwamba wale ambao walikuwa bora zaidi yeye (bin Umar) walimhesabu kama mnafiki. Tukio la Uqbah lilitokea wakati watu wanarudi kutoka Vita ya Tabuk. Ali hakuwa na Mtume. Hatamu ya ngamia wa Mtume ilishikwa na Huzayfah na Ammar alikuwa anamwendesha ngamia. Ngamia alipofika kwenye mpasuko wa hatari baadhi ya wanafiki walijaribu kumuua Mtume kwa kumuogofya ngamia. Lakini aliokolewea na ujanja wa Ammar na Huzayfah. Huzayfah alikwenda kuishi Kufah siku arobaini baada ya kutoa kiapo cha uaminifu kwa Ali. Alikuwa anamuunga mkono kwa uaminifu. (Majalisul Monimi).

“Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu. Mpendwa Huzaifah, Ninakuandikia kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu kwamba kilio chako kimechupa mipaka. Ewe ndugu! Ikatae dunia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Usilale usiku kucha, ukeshe unamuabudu Mwenyezi Mungu na uweke mwili wako na roho yako katika taabu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Haya ni mambo yafaayo kufanya.

“Ewe Ndugu! Ni muhimu kwa mtu akatambua kwamba mtu ambaye amekasirikiwa na Mwenyezi Mungu atadumu Jahanamu, ili uondokane na starehe za dunia, kesho usiku kesha katika kumuabudu Yeye na uteseke kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Ewe Ndugu! Ni muhimu kwa mtu anaye tambua kwamba furaha ya Mwenyezi Mungu ni ujumbe kuishi Peponi, kujaribu kutafuta radhi Yake mfululizo ili upatikane ukombozi na kufuzu.

“Ewe Ndugu! Mtu asijali kufarakana na familia yake kwa ajili ya radhi ya Mwenyezi Mungu. Ni radhi ya Mwenyezi Mungu tu ndio usalama wa Peponi. Endapo Mwenyezi Mungu anaridhika mambo yetu yote yatatimia na Pepo itakubalika. Lakini, endapo Mwenyezi Mungu haridhiki ni vigumu sisi kuwa na mwisho wenye furaha.

“Ewe Ndugu yangu! Mtu anayetaka kuwa pamoja na Mtume na watakatifu huko Peponi, lazima abadili maisha kama ambavyo nimefanya na kama ambavyo nimesema hapo juu. Ewe Hudhayfah! Wewe ni mmojawapo wa watu ambao ninao furaha kuwaelezea kuhusu machungu na mateso yangu. Kwa kweli mimi ninajiliwaza kwa kukutaarifu wewe yale yanayonipata au yaliyonipata.

“Ewe Hudhayfah! Nimeona dhuluma ya madhalimu kwa macho yangu, na nimesikia maneno yao ya kuchukiza kwa masikio yangu. Kwa hiyo, ninalazimika kutoa maoni yangu kuhusu mazungumzo hayo karaha na kuwaambia wao kwamba vyovyote walivyo kuwa wanafanya haikuwa sahihi kabisa. Nilifanya kwa kutimiza wajibu na kwa hiyo watu hao dhalimu wakaninyang’anya haki zangu zote. Wakanifukuza kutoka jiji hadi jiji na kuniswaga kutoka sehemu hadi sehemu na wakaniweka mbali na ndugu na jamaa zangu. Ewe Hudhayfa! Walisababisha vurugu kubwa na baya zaidi kuliko yote, walinizuia hata kwenda kutembelea kaburi la Mtume.

“Ewe Hudhayfa! Ninakuelezea kuhusu mateso yangu, lakini nina hofu isije maelezo yangu haya yakageuka kuwa malalamiko dhidi ya Mwenyezi Mungu. Hudhayfah! Ninakubali kwamba uamuzi wowote wa Mola wangu Mlezi na Muumbaji atakao ufanya kuhusu mimi ni sawa. Ninainamisha kichwa changu mbele ya amri Yake. Maisha yangu na yawe mhanga katika njia Yake. Ninatamani kupata radhi Yake. Ninayoandika yote haya kwako ili uniombee na Waislamu wanaojitolea kwa Mwenyezi Mungu. Amani iwe kwako.” Abu Dharr.

Haijulikani Abu Dharr alipelekaje barua hii kwa Huzayfah bin al-Yamah. Huzayfah aliposoma barua hii macho yake yalijaa machozi. Akazikumbuka hadith za Mtume (s.a.w) kuhusu Abu Dharr. Kilichomshangaza yeye zaidi ni kufukuzwa kwa Abu Dharr na kupelekwa kwenye upweke. Alishika kalamu kwa uchungu mwingi na akaandika jibu la barua hii:

“Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye kuneemesha.

Mpendwa wangu Abu Dharr,

Niliipokea barua yako na nikajua yanayokusibu. Umeniogofya kuhusu kurudi kwangu siku ya Hukumu na umeshawishi nifanye mambo fulani, kwa ajili ya kujitengeneza na kujiboresha mimi mwenyewe.

“Ewe ndugu! Wewe umekuwa ukinitakia mema mimi na Waislamu wote kila mara na umekuwa na huruma na mwema kwa wote. Kila mara ulikuwa na shauku ya ustawi wa wote. Kila mara uliwaonesha watu njia ya uadilifu na ukakataza wasifanye uovu. Mambo kama yalivyo, uongozi ni haki ya pekee ya Mwenyezi Mungu. Humwokoa amtakaye na ukombozi unategemea radhi Yake. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Atoe msamaha kwa jumla na neema nyingi kwangu, kwa wateule na watu wa kawaida wa umma wote.
“Ninafahamu hayo mambo ya kushangaza, ambayo umeyataja kwenye barua yako, ni kwamba, ule uhamisho wako wa kufukuzwa kutoka mji wa nyumbani kwako na kuachwa kwenye nchi ya kigeni bila marafiki na wanao kuunga mkono, na kule kutupwa nje ya nyumba yako.

“Ewe Abu Dharr! habari kuhusu mateso yako zimevunja moyo wangu kabisa kabisa na mateso ambayo unayapata sasa yanasikitisha sana. Lakini ninasikitika kusema kwamba siwezi kufanya lolote nikiwa hapa. Kama ingekuwa inawezekana kununua mabalaa yako yote kwa fedha yangu yote, ningefanya hivyo. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, kama ingewezekana ningejitolea kila kitu changu kwa ajili yako. Ewe Abu Dharr! Umo katika dhiki na siwezi kufanya lolote.

“Kwa jina la Mwenyezi Mungu kama ingekuwa inawezekana mimi na wewe kugawana matatizo yako hakika ningefanya hivyo. Nina hisi uchungu ulioje kwamba siwezi kukutana na wewe. Ni vigumu kufika pale ulipo. Endapo watu hawa katili wakinifanya mimi mshirika sawa na wewe katika matatizo yako, nipo tayari kuchukua matatizo yako. Lakini, loo, haiwezekani iwe hivyo.

“Ewe Abu Dharr! Usiwe na wasi wasi. Mwenyezi Mungu ndiye anayekuunga mkono. Anayaona mambo haya yote. Ndugu! Ni muhimu kwetu sisi, mimi na wewe, kumwomba Mwenyezi Mungu na tumsihi Yeye ili atuzawadie thawabu nyingi na atuokoe kutoka kwenye adhabu. Ewe ndugu! Muda unakaribia sana ambapo mimi na wewe tutaitwa mbele ya Mwenyezi Mungu na tutaondoka kuelekea huko hivi karibuni. Ewe Ndugu! Usiwe na wasi wasi kwa matatizo ambayo umekuwa unayapata na usistaajabu. Mwombe Mwenyezi Mungu akupatie malipo yake.

“Ewe ndugu! Ninafikiria kifo ni bora zaidi kwetu sisi kuliko kuishi hapa. Sasa ni muhimu sisi kuiacha dunia hii ya kupita kwa sababu baada ya muda si mrefu ghasia3 zitatokea kwa mfuatano moja baada ya nyingine. Ghasia hizi zitaendelea kuongezeka na zitawagandamiza watu waadilifu wa dunia. Panga zitachomolewa kwenye vurugu hizi na kifo kitawazunguka watu pande zote. Yeyote ambaye atanyanyua kichwa chake kwenye vurugu hizi hakika atauawa.

“Ewe Abu Dharr! Ninakuombea wewe wakati wote. Mwenyezi Mungu na atuweke chini ya huruma Yake na atulinde tusiwe na kiburi wakati wa ibada. Mpangaji mkubwa wa mambo yetu. Siku zote sisi hutegemea ukarimu Wake. Amani iwe kwako.” Hudhayfah

(Shifa’us Sudur, Abu Dharr Gihfari, uk. 105 al-Fusul kilichoandikwa na Murtaza Alamul Huda).

Wasomi wanasema kwamba Abu Dharr aliishi na familia yake huko Rabzah ambapo ghafla mtoto wake wa kiume, Dhar aliugua. Hapakuwepo na daktari wa kumwendea huko jangwani kwa ajili ya tiba isipokuwa kumwamini Mwenyezi Mungu. Hatimaye maradhi yalizidi hadi wakati wake wa kufa ulikaribia. Mama mwenye huzuni alinyanyua kichwa cha mwanae kutoka kwenye mchanga na kukiweka juu ya goti lake.
Dhar alifariki. Mama na dada yake Dhar walianza kulia. Abu Dharr alishtuka sana lakini imani yake kwa Mwenyezi Mungu ilimliwaza. Alijizuia na hakulia. Kwa kuwa ilikuwa jangwa hapakuwepo na matayarisho kwa ajili ya mazishi.

Historia haituambii Abu Dharr alivyomzika mwanae, lakini inajulikana kutoka kwa chanzo cha kuaminika alichofanya baada ya hisia zake kwa maneno muhadithi Yaqubi Kulayni ameandika; “Wakati mtoto wa kiume wa Abu Dharr, Dhar alipokufa Abu Dharr aliweka mkono wake juu ya kaburi lake na akasema; “Ewe mwanangu! Mwenyezi Mungu na akuhurumie. Ulikuwa mtoto anaye jiweza sana. Umekufa wakati mimi nina furaha na wewe. Utambue kwamba, kwa jina la Mwenyezi Mungu, sikupata hasara yoyote kutokana na kifo chako na simhitaji mwingine yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu.

“Ewe mwanangu! Endapo hapangekuwepo na kufikiria mshtuko baada ya kifo ningefurahi kutamani kuchukua nafasi yako kaburini. Lakini sasa kwa kuwa mimi ninaomboleza kifo chako, hutaomboleza kifo changu. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sikulia kwa ajili ya kifo chako lakini mateso yako ndio yamenifanya nilie. Natamani ningejua nini ulichoulizwa na majibu yako. Ee Mwenyezi Mungu! Nimesamehe haki zangu ambazo nilikuwa ninamdai. Ee mstawishaji wangu! Ninakuomba umsamehe haki zozote ambazo ulikuwa unamdai. Mola wangu Mlezi! Wewe ni msamehevu zaidi kuliko mimi.” (Usudul Kafi).

Shaykh Abbas Qummi ameandika kwenye kitabu chake Safinatul Bahar Juzuu ya 1, ukurasa wa 438 kwamba maneno yaliyotamkwa na Abu Dharr juu ya kaburi la mwanae Dhar, pia yalitamkwa na Imamu Jafar Sadiq juu ya kaburi la mwanane Ismail.

Abu Dharr alikuwa hajasahau kifo cha mwanae kijana ambapo mke wake pia alipatwa na mauti na hakumuona tena hadi milele.

Kwa mujibu wa Allamah Abdul Hamid, Abu Dharr na watu wa familia yake walikuwa wanaishi katika hali ambayo haikuwa na mpango unaostahili kuhusu chakula isipokuwa walikuwa wanapata kipande kidogo cha nyama ya ngamia aliyechinjwa kwa ajili ya maafisa wa serikali. (Tabari, Juz. 5, uk. 67). Kwa kawaida walikula majani kama chakula chao kikuu au vitu vingine kipindi hicho. Siku moja mke wa Abu Dharr alikula majani yenye sumu ambayo yalisababisha apate maradhi ya hatari na alifariki dunia. (Hayatul Qulubi, Juz. 2, uk. 1049) Abu Dharr naye akaugua.

Baada ya kifo cha mke wake, Abu Dharr alihisi kuwa mpweke mno. Alibaki yeye na mwanae wa kike. Watu waliokuwa wanaishi Rabzah walipojua kuugua kwa Abu Dharr, baadhi yao walimtembelea na kumtaka hali. Kwa mujibu wa usemi wa mtoto wa kike wa Abu Dharr, watu hao walimwambia; “Ewe Abu Dharr!Unaumwa na nini na unalalamika kuhusu nini?”

Abu Dharr akajibu; “Nina malalamiko kuhusu dhambi zangu.” Watu hao wakasema, “Unatamani kitu chochote?” Akasema, “Ndio natamani huruma za Mwenyezi Mungu” Wakasema, “Kama unataka tunaweza kumwita daktari wa tiba.” Akasema, “Mwenyezi Mungu ndiye mganga wa uhakika. Maradhi na tiba yake vyote vimo kwenye uwezo Wake. Mimi sihitaji mganga wa tiba.” (Hayatul Qulubi) Alikuwa na uhakika wa kifo chake.

Majlis, kwa mamlaka ya Sayyid bin Taus, amemnukuu Muawiyah bin Thalabah anasema: Hali ya Abu Dharr ilipozidi kuwa mbaya huko Rabzah na tukapata taarifa, tuliondoka Madina kwenda Rabzah kwa lengo la kumuona yeye. Baada ya kuulizia kuhusu hali yake tulimsihi atengeneze wasia wake.

Akasema kwamba alikwisha tayarisha wasia wake, vyovyote itakavyo kuwa, mbele ya Amiri wa Waumini.

Tukauliza, “Kwa Amiri wa Waumini unamaanisha Khalifa Uthman?” Akasema, “Kamwe! Kwa Amiri wa Waumini maana yake ni kwamba yule ambaye ndiye anayestahili kuwa Amiri wa Waumini. Ewe bin Thalabah! Nisikilize! Abi Turab, (Baba wa Ardhi) Ali ndiye yeye ambaye ni maua ya dunia. Yeye ni msomi wa dini wa umma huu. Sikiliza! Utaona mambo mengi ya kuchukiza sana hapa duniani baada ya kifo chake.” Nikasema; “Ewe Abu Dhar! Tunaona kwamba unafanya urafiki na watu ambao Mtume aliwapenda.”

Sasa tunataka kusema kitu kuhusu mahali, Rabzar ambapo Abu Dharr alizuiliwa na hakuruhusiwa kuvuka mipaka yake.

Wasomi na waandishi wa historia wanakubaliana kwamba Rabzah ipo umbali wa maili tatu kutoka Madina karibu na Zate Araq kufuata njia ya kuelekea Hijaz na wakati huo huo haikuwa zaidi ya sehemu iliyotekelezwa na pweke maoni ukurasa wa 17 wa Juz. 2, ya Nahjul Balagha kwamba Rabzah ni sehemu iliopo karibu na Madina ambapo kaburi la Abu Dharr lipo. Bin Abil Hadid anasema kwamba Kufukuzwa kwa Abu Dharr na kupelekwa Rabzah ilikuwa sababu moja wapo ambayo iliwachochea Waislamu kumuasi Uthman.

Hapana shaka kwamba Abu Dharr alipata daraja la juu zaidi la imani. Alizingatia hadi dakika za mwisho za uhai wake kwamba aliapa kwa Mtume kusema kweli na bila kujali shutuma yoyote kwa ajili ya ukweli. Shah Walyullah Dehlavi ameandika kwamba katika utekelezaji kwa Mtume (s.a.w) ni kwamba alichukua viapo vya uaminifu vya aina mbali mbali kutoka kwa watu mbali mbali yaani kwenda Jihad, kukataa bidaa, kuanzisha sheria za Kiislamu, na kusema kweli. (Shifau alil).

Kiapo alichochukua kutoka kwa Abu Dharr ni kusema kweli. Abu Dharr alifanya kwa mujibu wa kiapo cha uaminifu baada ya kutambua vema maana yake na kwamba asingefanya hivyo, ambapo alikwisha sadiki sana hali ambayo iliondoa shaka kwake, kwamba chochote alichofanya kililingana na Ridhaa ya Mwenyezi Mungu na nia ya Mtukufu Mtume (s.a.w) (Futunatul Makkiyah bin Arabi, Sura ya 269).

Kuhusiana na hilo, kamwe hakujali nguvu za serikali wala kuogopa kupata matatizo. Alistahamili kila aina ya ukandamizaji na alibeba kila aina ya usumbufu lakini hakuacha kusema kweli, hadi akafukuzwa na kupelekwa uhamishoni mara mbili. Uhamisho wa Abu Dharr wa mara ya mwisho hauna mfano wake.

Alijitolea mhanga kwa kuzuiliwa kwenye jangwa ambalo ni pweke. Bila kuzungumzia habari za nyumba ya kuishi, alifanya kivuli cha mti kuwa makazi yake. Hakuwa na mpango wowote wa chakula na makazi ambapo angepumzika au kulala. Lakini kwa ujasiri wake wa hali ya juu na azima aliokuwa nayo, Abu Dharr aliyachukua matatizo yote kwa uchangamfu kwa sababu ya kumridhisha Mwenyezi Mungu. Mke na mtoto wake wa kiume walipokufa sasa muda ulikaribia ambapo alikuwa anangojea kifo chake mwenye we akiwa kwenye sehemu pweke kama hiyo akiwa na mtoto wake wa kike tu.

Loo! Siku ya mwisho ya uhai wa Abu Dharr kwenye sehemu hiyo pweke ilikaribia. Alikuwa anasali mara nyingi na binti yake alikuwa na wasi wasi na shauku kuhusu hali ya baba yake na mwisho wake uliokuwa unakaribia. Hapakuwepo na mtu. Hapakuwepo na hata mnyama. Muda wa kuwasili malaika wa kifo ulikaribia.

Muda ambao binadamu hulia na mtoto wa kike kunyang’anywa mapenzi ya baba yake.

Si tu kwamba alikuwa anaangalia kwa makini kwa kutokuwa na msaada kwa baba yake ambaye mapenzi yake yalisababisha mshtuko mara kwa mara.4

Hapa tunatoa maelezo ya historia ya hatari ya kifo cha Abu Dharr kama ilivyosimuliwa na binti yake kama ilivyoandikwa na Majlisi. Binti huyu anasema; “Siku zetu zilipita katika mateso yasiyo elezeka kwenye upweke. “Siku moja ilitokea kwamba hatukuweza kupata chochote chakula. Tulijitahidi kutafuta lakini hatukufanikiwa. Baba yangu aliyekuwa taabani akaniambia, “Binti yangu kwa nini una wasi wasi sana leo?”

Nikasema, “Baba, mimi nina njaa sana na wewe unazidi kudhoofika pia kwa sababu ya njaa. Nimejaribu kujitahidi kila nilivyoweza kupata chakula ili niweze kuhisi ninaheshimika kwako lakini sikufanikiwa.” Abu Dharr akasema, “Usiwe na wasi wasi. Mwenyezi Mungu ndiye mpangaji mkuu wa mambo yetu.” Mimi nikasema, “Baba! Ni sawa lakini hakuna kitu chochote sasa ambacho kinaweza kukidhi mahitaji yetu.”

Akasema; “Binti yangu! Nishike bega langu na unipeleke hapa na pale. Labda tunaweza tukapata chochote huko.” Nilimshika mkono wake na tukaanza kwenda kuelekea upande alikonielekeza. Wakati tupo njiani baba yangu aliniambia nimkalishe chini. Nikamketisha kwenye mchanga wenye joto. Akakusanya mchanga na akalaza kichwa chake juu ya mchanga huo.

Mara tu alipolala chini, macho yakaanza kuzunguka na akahisi uchungu wa kifo. Nilipoona hivi nikaanza kulia kwa sauti kubwa sana. Akajikaza kidogo na akasema, “Kwa nini unalia, binti yangu?” Nikasema, “Nitafanya nini baba yangu? Hapa ni jangwa na hakuna mtu yeyote. Sina sanda ya kukuvesha na pia hakuna mtu wa kuchimba kaburi hapa. Nitafanya nini mauti yakikufika hapa kwenye sehemu hii pweke.”

Akalia baada ya kuona jinsi nilivyokuwa sina jinsi ya kuwa na msaada wowote na akasema, “Binti yangu! Usiwe na wasi wasi. Huyo rafiki yangu ambaye kwa ajili ya kumpenda yeye na watoto wake ninavumilia matatizo yote haya, aliniambia kuhusu tukio hili mapema, Sikiliza, Ewe bint yangu mpendwa, alisema mbele ya kundi la masahaba wake wakati wa Vita ya Tabuk kwamba mmojawao angekufa lakini jangwani na kundi la masahaba wangekwenda kwenye maziko na mazishi yake.

“Sasa hakuna hata mmoja wao aliyehai isipokuwa mimi. Wote wamekufa wakiwa kwenye sehemu zenye watu. Ni mimi tu niliye baki na pia nipo kwenye upweke wa pekee.

Kamwe sijapata kuona jangwa la aina hii ambapo nimelala sasa na mwenye uchungu wa kifo. Binti yangu mpendwa! Nikifa nifunike joho langu na ukae kwenye njia inayoelekea Iraq. Kundi la watu waumini watapita hapo. Waambie kwamba Abu Dharr sahaba wa Mtume (s.a.w) amekufa. Kwa hiyo tafadhalini tayarisheni mazishi yake.”

Alikuwa anazungumza na mimi wakati malaika wa kifo alipofika na kumtazama uso wake. Baba yangu alipomtazama uso wake ukawa mwekundu na akasema, “Ewe Malaika wa Kifo! Umekuwa wapi hadi sasa? Nimekuwa ninakungojea wewe. Ewe rafiki yangu! Umekuja wakati ambapo mimi ninakuhitaji sana. Ewe Malaika wa kifo! Na asiokolewe mtu asiyefurahi kuonana na wewe. Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nichukue haraka sana na unipeleke kwa Mwenyezi Mungu mwenye Huruma sana ili niweze kupumzika na matatizo ya dunia hii.”

Baada ya hapo alimwambia Mwenyezi Mungu, “Ee Msitawishaji wangu! Ninaapa Kwako Wewe, na Unajua kwamba ninasema kweli kwamba kamwe sikuchukia kifo na kila mara nilitamani kukutana na wewe.”

Baada ya hapo jasho la kifo likatoka kwenye uso wa baba yangu na aliponitazama, aligeuza uso wake na kuiaga dunia daima milele. Sisi tunatoka kwa Mwenyezi Mungu na Kwake tutarejea.”5

Binti yake Abu Dharr aliendelea, “Baba yangu alipokufa nilianza kulia huku ninakimbia kuelekea kwenye njia inayoelekea Iraq. Nilikuwa nimeketi pale nikangojea kundi la watu linalokuja. Ghafla nilikumbuka kwamba maiti ya baba yangu ilikuwa haina mtu wa kuiangalia. Kwa hiyo, nilikimbia hadi ilipokuwa maiti. Tena nikarudi kwenye njia isije kundi likapita bila kulitaarifu. Kwa hiyo, ikawa ninakwenda kwenye maiti na kurudi njiani, mara kadhaa.

Sasa, ghafla nikawaona watu wanakuja wakiwa wamepanda ngamia. Walipokaribia, nikawaendea huku nikilia na kutokwa na machozi na nikawaambia; “Enyi masahaba wa Mtume! Sahaba wa Mtume amekufa.” Wakaniuliza sahaba huyo ni nani?” Nikajibu; “Baba yangu, Abu Dharr Ghifari.”

Mara waliposikia waliteremka kutoka kwenye ngamia na wakafuatana na mimi huku wakilia. Walipofika hapo wakalia sana kuhusu kifo chake cha kuhuzunisha na wakashughulikia ibada ya mazishi yake.

Mwandishi wa historia Atham Kufi, amesema kwamba kundi la watu waliokuwa wanakwenda Iraq, alikuwepo; Ahnaf bin Qays, Tamimi, Sasaah bin Sauhan al-Abdi, Kharijah bin Salat Tamimi, Abdulah bin Muslimah Tamimi, Halal bin Malik Nazle,
Jarir bin Abdullah bajali, Malik bin Ashtar bin Harith na wengineo. Watu hawa walimkosha Abu Dharr na wakafanya mpango wa kumvisha sanda. Baada ya mazishi Malik bin Ashtar alisimama pembeni mwa kaburi na akatoa hutuba ambapo ilirejea mambo ya Abu Dharr na kumwombea yeye. Baada ya kumsifu Mwenyezi Mungu Mweza wa yote akasema”

“Ee Mwenyezi Mungu! Abu Dharr alikuwa sahaba wa Mtume Wako na muumini wa Vitabu Vyako na Mitume Wako. Alipigana kishujaa sana katika njia Yako, alikuwa, mfuasi imara wa sheria Zako za Kiislamu na kamwe hakubadilisha au kugeuza amri yoyote miongoni mwa amri Zako.

“Ee Mola wangu Mlezi! Alipoona ukinzani unafanywa dhidi ya Kitabu na Sunna akapiga kelele na kuwatahadharisha wahusika kwa umma ili wajirekebishe, matokeo yake wakamtesa, wakamhamisha kutoka sehemu moja hadi nyingine, wakamfedhehesha, wakamhamisha kutoka katika nchi ya Mtume Wako mpendwa na kumweka kwenye matatizo makubwa sana, hatimaye amekufa akiwa katika hali ya upweke kabisa sehemu ambayo hawaishi watu.

“Ee Mwenyezi Mungu! Mpe Abu Dharr sehemu kubwa ya hizo neema za mbinguni ambazo Umewaahidi waaminio na umlipe kisasi yule ambaye amemfukuza kutoka Madina na umpe adhabu kamili anayostahiki.”6

Malik Ashtar alimwombea Abu Dharr kwenye hotuba yake na wote wale ambao walikuwepo hapo na akasema, “Amini” (Na iwe hiyo). Hata hivyo, walipokamilisha ibada ya mazishi ilikuwa jioni na wakawa hapo hadi asubuhi. Wakaondoka asubuhi siku iliyofuata.” (Tarikh kamil, Juz. 3, Izalatul Khifa Juz. 1, Tarikh Tabari, Juz. 4).

Hata hivyo bint yake Abu Dharr ambaye aliendelea kukaa hapo Rabzah kwa muda wa siku chache zaidi. Siku moja usiku alimuona Abu Dharr kwenye ndoto ameketi na anakariri Qurani Tukufu.

Akasema, Baba! Nini kimekutokea na umerehemewa kwa kiwango gani na Mwenyezi Mungu ambaye ni Mwingi wa Rehma? Akasema, Ewe binti yangu! Mwenyezi Mungu amenizawadia upendeleo usio na mipaka, amenipa starehe zote na amenipa kila kitu. Ninafurahia sana ukarimu Wake. Ni wajibu wako kujishughulisha na kumuabudu Mwenyezi Mungu kama kawaida na usiruhusu aina yoyote ya maringo na kiburi kuja kwako.” (Hayatul Qulubi, Juz. 2,).

Wasomi na waandishi wa historia wanakubaliana kwamba Abu Dharr alikufa tarehe 8, Zilhajjah, 32 A.H, Rabzah. Alikuwa na umri wa miaka 85.

  • 1. Jina lake alikuwa Sadi bin Ajlan Zaidi hujulikana jina lake la utani, Bahilah ni jina la kabila lake. Hadith nyingi zimesimuliwa na yeye. Aliishi Homs (Syria) ambako alikufa akiwa na miaka 91. Watu wengine husema kwamba huko Syria alikuwa sahaba wa mwisho wa Mtume (s.a.w) kufia huko. Lakini ukweli ni kwamba huko Syria sahaba wa mwisho kufa alikuwa Abdallah bin Bashir (Izalatul Khifa, Juz. 1, uk 285).
  • 2. Huyu alikuwa sahaba aliyeheshimiwa. Jina halisi la baba yake, Yaman lilikuwa Asal au Umail. Alikufa shahidi kwenye vita ya Uhud. Hudhayfah aliambiwa majina ya wanafiki na Mtume wa Uislamu. Kila mara Umar alikuwa akimuuliza Hudhayfah majina ya wanafiki. Hudhayfah pia alikuwa mtawala katika Madain wakati wa khalifa wa pili (Izatul Khifa, Juz. 1, uk. 282). Tabarsi anasema kwamba wanafiki walitayarisha njama ya kumuua Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenye bonde la Uqbah, lakini mpango huo ulivurugwa na Ammar yasir na wengineo. Mara tu baada ya tukio hilo, Mtukufu Mtume akafichua majina ya wanafiki kwa Hudhayfa. . . Kwa mujibu wa maandishi ya Abu Dharr orodha ya majina yaliyofichuliwa kwa Hudhayfa pia ilijulikana Ashrah Mubashirah (Masahaba kumi wa Mtume ambao walijulikana kwa cheo hiki baada ya kifo cha Mtume. Maandishi ya pembeni ya Ethtijaj Tabarsi, uk. 29).
  • 3. Labda anataja rejea ya utawala a Bani Umayyah na Bani Abbas. Hakuna Kabila la makabila yote ya miji na majangwa ya Arabuni ambalo halitaathiriwa. Wakati huo, watu katili watafikiriwa kuwa ndio wa kuheshimiwa, na wachamungu watadharauliwa. Mwenyezi Mungu na atunusuru kutokana na uovu a kipindi hicho.
  • 4. Waandishi wengi wa historia wamehusisha tukio la kifo cha Abu Dharr kwa mke wake Umm Dhar, lakini haioneshi kuwa sahihi kwa sababu waandishi wa historia kama vile Masudi na Yaqubi, wameandika kwamba mke na binti yake Abu Dharr walikwisha fika huko Rabzah. Majilisi ametoa maelezo ya kifo cha mke wake huko Rabza kama alivyoeleza bint yake. Tabari amesema kwamba mtoto wa kike alipelekwa Madina baada ya kifo cha Abu Dharr. Bin Athir pia amekiri kuwepo kwa mtoto wa kike (Kufuatana na Tarikh Kamil, Juz. 3, uk. 51) na hakuna hata mwandishi yeyote wa historia mwenye kuaminika ambaye ametamka kuhusu kuwasili kwa mke wa Abu Dharr Madina.
  • 5. Imetamkwa kwenye masimulizi ya kwamba Abu Dharr hakuhisi uchungu wowote wa kifo, na uhalali wake ulithibitika kwa sababu uchungu wa kifo anauhisi yule tu ambaye matendo yake yalikuwa ya kuchukiza au ambaye amefanya kitu ambacho kumbukumbu yake katika maisha husababisha kizuizi kwa roho kutoka. Mathalani Aishah alipohisi mateso makubwa alipokuwa kwenye uchungu wa kukata roho na alianza kupumua kwa nguvu sana watu wakamuuliza, Ewe Mama wa Waumini! Kwa nini imekuwa hivi? Nini kinachokusumbua" Akajibu, Vita vya Ngamia vinasonga roho (Rauzatul Akhyar anasimulia kutoka kwenye Rabiul Abrar).
  • 6. Upo uwezekano kwamba matokeo ya laana hiyo Uthman aliuawa baadaye kwa mfano wake. Historia inasema kwamba mwili wake ulilala juu ya lundo la kinyesi kwa muda wa siku tatu na mbwa walikula mguu wake mmoja. (Tarikh Atham Kufi). Baada ya mazishi ya Abu Dharr watu waliondoka Rabzah lakini mwanae wa kike aliendelea kukaa hapo kufuatana na wasia wake. Baada ya siku kadhaa, khalifa Uthman alimwita na akampeleka kwao. (Tarikh Tabari Juz. 4, uk 527)