Sura Ya Ishirini Na Mbili

Jaun bin Huwi alikuwa mtumwa wa Abu Dharr ambaye historia ya maisha yake yanaonekana jinsi alivyofundishwa na Abu Dharr. Kwa mujibu wa Mama qani, nasaba ya Jaun ni kama ifuatavyo:

Jaun bin Huwi bin Qatadah bin Awar bin Saidah bin Awf bin Kab bin Huwi Habashi (Tanqihul Maqal Juz. 1)

Imeandikwa kuhusu mtu huyu kwamba alikuwa wa jamii ya Kiafrika na alikuwa anamilikiwa na Fadhl bin Abbas bin Abdul Muttalib, ambako Ali alimnunua kwa sarafu za dhahabu 150 na akamtoa kama zawadi kwa Abu Dharr. Ali alitaka Jaun amtumikie Abu Dharr.

Kama ilivyotarajiwa, Jaun alifanya kazi inayostahili sifa kwa Abu Dharr ambaye alikuwa akifurahi sana kuwa anaye. Jaun alimtumikia Abu Dharr na pia alipata faida ya kuwa naye. Alichunguza kila kipengele cha tabia ya Abu Dharr kwa uangalifu mkubwa na alipendezwa sana nayo.
Kwa mambo yalivyokuwa, Jaun alimtumikia Abu Dharr kwa kila jinsi alivyoweza. Pia hakuna mahali ambapo alikosa heshima ya kuwa na Abu Dharr isipokuwa huko Rabzah ambako kuwepo kwake huko hapatajwi na mwandishi yeyote wa kuaminika wa historia.

Hata hivyo, Jaun alimtumikia Abu Dharr kwa ufanisi kwa kadiri alivyoweza. baada ya Abu Dharr kuondoka kwenda Rabzah yeye alibaki na kuendelea kumtumikia Ali. Baada ya Ali kufa kishahidi aliendelea kumtumikia Imamu Hasan naye alipokufa kishahidi mwaka wa 50 A.H alianza kumtumikia Imamu Husein.

Kwa ufupi, aliwatumikia kwa uaminifu watu waadilifu maisha yake yote. Imamu Husein alipoondoka Madina na kwenda kwanza Makkah na halafu Karbalah wakati wa mwezi wa Rajabu, mwaka wa 60 A.H. Jaun alikuwa naye kwenye safari hii.

Allamah Majlisi na Allamah Samawi wameandika kupitia kwa mamlaka ya Sayyid Razi daudi kwamba mapigano yalipoanza Karbala tarehe 10, Muharram, mwaka wa 61, A.H. Jaun alikwenda kwa Imamu Husain na akaomba ruhusa apigane. Imamu Husain akasema unaruhusiwa.

”Lakini ewe Jaun! Umeishi na mimi kwa kipindi kirefu katika amani na sasa unataka kuuawa!” Aliposikia maneno haya, Jaun alianguka miguuni mwa Imamu Husain na akasema, “Ewe bwana wangu, mimi si mmojawapo wa wale wanaokudanganya wakati wa amani na na furaha, na kukuacha wakati wa dhiki. Ewe bwana wangu! Hapana shaka kwamba jasho langu hunuka harufu mbaya, nasaba yangu si ya watu bora na rangi yangu nyeusi, lakini ukiniruhusu, jasho langu litanukia harufu nzuri, nasaba yangu itakuwa bora na rangi yangu itakuwa nyeupe huko peponi. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sitakuacha hadi hapo damu yangu itakapo changanyika na damu yako.”

Hatimaye Imamu Husain alimpa ruhusa. Jaun akaingia kwenye uwanja wa vita, akaanza kupigana na akakariri rajaza ifuatayo:

“Enyi mliolaaniwa! Mliwahi kuona mtumwa Mwafrika anavyopigana? Angalieni anavyopigana akiwaunga mkono uzao wa Mtukufu Mtume!”

Baada ya kukariri ‘rajaz’ Jaun alifanya shambulizi kali kwa adui na aliendelea kupigana mfululizo hadi akawaua maadui ishirini na tano na yeye mwenyewe alikufa kishahidi (Muntahul Amal).

Muhammad bin Abi Talib Makki ameandika kwamba Jaun alikufa kishahidi, Imamu Husain alikwenda kwenye maiti yake, akaweka kichwa chake kwenye maiti yake, akaweka kichwa chake kwenye paja lake na akamwombea Mwenyezi Mumgu;

“Ee Mwenyezi Mungu! Tia nuru uso wa Jaun, fanya jasho lake liwe na harufu ya kupendeza na mpe mahali awe na waadilifu wa huko Peponi, ili aweze kuwa na Muhammad na uzao wake (Ahlul-Bait).”

Wasomi humnukuu Imamu Muhammad Baqir ambaye humnukulu baba yake Imamu Zaynul Abidin akisema kwamba siku chache baada ya Bani Asad kuzika maiti ya mashahidi na kuondoka, waliona maiti ya Jaun ambayo uso wake ulikuwa unang’ara na maiti yake ilitoa harufu nzuri ya manukato. (Absanul Ainu uk. 165; chapa Hyderabad Deccan, 1357 A.H Biharul Anwar, Juz 1).

Kwa ufupi, mtumwa huyu mwaminifu wa Abu Dharr aliyeweka mhanga maisha yake kwa ajili ya bwana wake, Imamu Husain, aliyekuwa anapigana na Yazid bin Muawiyah Dikteta wa Umayyad, kwa ujasiri ushujaa na ushupavu na akafa shahidi.

Ni ukweli uliothibitishwa kwamba mara tu baada ya kufariki Mtukufu Mtume, mafundisho yake yote na maonyo hayakutiliwa maanani na wanafiki, ambao lengo lao moja tu lilikuwa kupata manufaa ya kidunia na wakayadharau mafundisho ya Mtume.

Baadhi ya masahaba wa Mtukufu Mtume walikuwa waumini imara wa Uislamu na mapenzi yao kwake na Ahlul Bait wake yalijaa kwenye mioyo yao, walinyanyuka kupigana kufa na kupona na hizo nguvu za uovu. Walikuwa wafuasi wa kweli wa Mtume Muhammad na Ahlul-Bait wake na walichukua mwongozo kutokana na yale waliyoyasema na kuyatenda. Pia walipata masahaba wengine ambao walipata uwezo na mamlaka kwa jina la Uislamu. Lakini badala ya kutumikia njia ya Uislamu, wakalitumia vibaya jina la Uislamu na utajiri kwa maslahi yao binafsi na kujiongezea kifamilia.

Walifuja utajiri wa taifa kama vile ulikuwa rasilimali yao. Miongoni mwa masahaba alikuwepo mmoja ambaye alithubutu kutamka; “Kwa jina la Mwenyezi Mungu hadi hapo nitakapolifuta jina la Mtume Muhammad kutoka kwenye uso wa ardhi sitapata amani”. (Murujuz Zahab Andalus Press) Matokeo yake ni kwamba mfumo mpya wa utawala ulijitokeza yaani ufalme ambao ulisababisha matisho miaka iliyofuata. Kupotoshwa kwa Uislamu kwa namna hiyo haikuvumiliwa na masahaba wa kweli ambao hawakujizuia kusema kweli hata kama ilimanisha kupoteza maisha.

Abu Dharr ni mfano wa wazi wa kubeba dhiki za kila aina na uimara na ujasiri ambazo ni sifa alizozionesha alipokuwa anateswa na mateso hayo yalikuwa makali kiasi cha kusababisha kifo chake kama ambavyo ilikwisha tabiriwa na Mtukufu Mtume (s.a.w). Mfano wake ulifuatwa na mtumwa wake Jaun ambaye naye pia alijitoa mhanga kwenye mchanga wa Karbala ambapo aliamua kuutetea Uislamu bega kwa bega na mjukuu wa Mtukufu Mtume, Husein. (a.s).