Sura Ya Kumi

Baada ya kifo cha Mtume, wale masahaba ambao hawakuridhika kwa kitendo chake cha Ghadir Khum ambao walimpinga Ali, haraka sana walikusanyika Saqifah Bani Sadah mahali ambapo palitayarishwa maalumu kwa mashauriano yasiyofaa (Ghayathul Lughaat) na watu wachache wapatao 200 ambao walikuwemo Muhajirina na Ansar waliokubali na wasikubali walikuwemo, walianzisha msingi wa serikali ya mtu binafsi. Waliporudi Madina kutoka Saqifa, baada ya maziko ya Mtume, walianza kudai kiapo cha utii kutoka kwa watu kwa lengo la kupatia serikali hiyo ya kibinafsi sura ya pamoja na aina ya kidemokrasia. Ili kukamilisha lengo hili walionesha tabia ambayo katika ubinadamu wa kawaida inatetemesha si tu kwa masahaba wa kuheshimiwa lakini pia kwa Ahlul-Bait.

Kiini hasa cha hadithi hiii inayoumiza ya kipindi hiki ni kwamba, Ali alilazimishwa kutoa kiapo cha utii (Rauzatul Ahbab) na alipokataa, jeshi la Khalifa lilimpeleka mahakamani, huku shingo yake ikiwa imefungwa kwa kwamba (Bin Abil Hadid Motazali). Nyumba ya Fatimah ilichomwa moto (Tarikh Tabari, Tarikh al-Imamuah wa as-Siyasah Miratul Uqul) Mlango wa nyumba ulimwangukia Fatimah na kusababisha kuharibika kwa mimba ya mtoto wake wa kiume.(al-Milal wan Nahl of Shahristani).

Allamah Mukkah Muin Kashifi ameandika kwamba Fatimah aliugua kwa sababu ya mshtuko wa tukio hili, na hatimaye alifariki. (Maarij un-Nabuwwah Juz. 4, Sura ya 3, uk. 42). Halafu wale watu ambao walikataa kula kiapo cha uaminifu kwa Abu Bakr walilazimishwa kwa ukali, na wengine walipigwa sana. Salman Farsi ambaye Mtume alikwisha mjumuisha kwenye Ahlul Bait wake, pia alikuwa mmoja wapo wa majeruhi wa udikteta wao. Alipigwa sana hivyo kwamba shingo yake ilitenguka na hali hiyo ilidumu hadi kifo chake.

Majina ya wale waliokuwepo Madina na ambao walikataa kula kiapo cha uaminifu kwa Abu Bakr yameorodheshwa chini:

Imamu Ali, Abu Dharr, Salman Farsi, Ammar bin Yasir, Miqdadi bin al-Aswad Khalid bin Said, Burayda Aslami, Ubay bin Kab, Huzayma bin Thabit, Suhayl bin Harrif, Uthman bin Hanif, Abu Ayyub Al-Ansari, Hudhayfa bin al-Yamani, Sad bin Ubaydah, Qays bin Sad, Abdullah bin Abbas, Abbas bin Abdul Muttalib, Abdul Haytham bin Tayhan, Jabir bin Abdullah, Abdullah bin Thamit, Ubaydah bin Thamit, Abu Said Khidri (Tabsaratul Awam, uk. 24, Ainul’Hayat, uk. 5).

Imeandikwa kwenye ukurasa wa 43 wa kitabu hicho hicho (Tabsaratul Awam) kwamba baada ya siku chache Sad bin Ubaydah alipigwa mshale na akafa kwa sababu ya kukataa kwake kutoa kiapo cha utii.

Vyovyote vile uhuni huu wa kisiasa uliendelea baada ya kifo cha Mtukufu Mtume. Waandishi wa historia wameandika kwamba kiunga cha Fadak, rasilimali ya Ahlul bait kilinyang’anywa kwa sababu tu ya kukataa kutoa kiapo cha utii. Watu hawa walisema kwamba Ukhalifa ni haki isioondolewa kwa Ali na lazima apate. Maelezo marefu ya madai haya bado yapo kwenye hotuba ya Ali ya Shiqshiyyah iliyopo kwenye Nahjul Balaghah.
Ali amesema wazi kwamba Ukhalifa ilikuwa haki yake ambayo iliporwa kutoka kwake. Pia amesema jaribio lake la kuanzisha madai yake kama inavyoonekana kwenye ukurasa wa 231 katika kitabu cha an-Nihayah cha bin Athir.

Sasa tunanukulu kutoka kwenye Tarikhi Ahmadi kuhusu msiba wa tukio hili la maangamizi ambalo liliwatokea Ahlul-Bait na masahaba waaminifu baada ya kifo cha Mtukufu Mtume, hivyo kwamba msomaji aweze kujua nini kilitokea baada ya yote kwa uzao wa Mtume na masahaba wake waaminifu majuma mawili tu baada ya kifo cha Mtume na Abu Dharr aliwajibika vipi kwa hali mambo yalivyokuwa.

Kwa mujibu wa Tarikh bin Jasir, Umar alikuwepo wakati wa kifo cha Mtukufu Mtume lakini Abu Bakr hakuwepo. Alikuwa kwenye kijiji kiitwacho Sakh. Mtume alipokufa, Umar alisema, “Kufuatana na dhana ya wanafiki, Mtume amekufa, lakini ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba yu hai.”

Kwa mujibu wa al-Milal wan Nihal cha Shahristani, Umar alitishia kumuua kwa upanga wake endapo mtu anasema Mtume amekufa. Tukio hili pia limeandikwa kwenye vitabu vingine kama (Tarikh Abul Fida, Juz. 1, uk. 164, Tabaqatul Kubra Juz. Ya 2, uk. 271, Sunan bin Maja Juz. 1, uk. 571, Hadith ya 1618, Musnad Ahmad bin Hanbal Juz. 1).

Kwa mujibu wa Rauzatul Alhbab watu walianza kuwa na shaka kuhusu kifo cha Mtume waliposikia tishio hili la Umar. Wakati huo, Abu Bakr alikuwa nyumbani kwake Sakh. Alipopewa taarifa ya kifo cha Mtume haraka sana alikwenda Madina na alipofika kwenye msikiti wa an-Nabi aliona kwamba watu walikuwa katika ghasia nyingi.

Kwa mujibu wa Tarikh Abul Fida, Abu Bakr alipoona hali hii ya watu, akakariri Aya ifuatayo:

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِنْ مَاتَ أَوْ قُتِلَ انْقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُم {144}

“Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwisha pita kabla yake Mitume. Je, akifa au akauawa ndiyo mtageuka mrudi (Ukafirini)?” (Qurani 3:144).

Waliposikia hivi watu wakasadiki kuhusu kifo cha Mtukufu Mtume. Baada ya hapo watu wote waliondoka kwenda Saqifah Bani Sadah.

Kwa mujibu wa Tarikh Bin Khaldun, baada ya kufika Saqifah Abu Bakr alisema, “Sisi ni sahaba na ndugu wa Mtume na kwa hiyo tunastahili zaidi kudai Ukhalifa wa Mtume kuliko mtu mwingine yeyote.”

Kwa mujibu wa Tarikh Tabari cha Bin Jarir, Umar alimwambia Abu Bakr; “Nyoosha mkono wako ili niweze kutoa kiapo cha uaminifu kwako” Abu Bakr alisema, “Hapana; wewe ndiye unyooshe mkono kwa sababu katika kila hali wewe ni mwenye uwezo zaidi kuliko mimi.”

Pambano hili liliendelea kwa kipindi fulani. Hatimaye Umar aliunyoosha mkono wa Abu Bakr na akatoa kiapo cha uaminifu kwake na pia alisema, “Pia uelewe kwamba nguvu zangu zimeunganishwa.”

Kwa mujibu wa Tarikh Kamil cha Bin Athir, Umar na watu wengine waliapa kuwa waaminifu kwa Abu Bakr, lakini Ansar wote au baadhi miongoni mwao walisema, “Hatutatoa kiapo cha uaminifu kwa yeyote isipokuwa Ali.”

Kufuatana na Tarikh Khamis, wakati Abu Bakr alipomaliza kazi ya kupokea viapo, aliondoka Saqifa na kwenda Msikiti wa Nabi na akaketi kwenye mimbari. Hapa, pia, aliendelea kupokea viapo hadi mwisho wa siku na watu walishindwa kuhudhuria mazishi ya Mtukufu Mtume. Ilikuwa siku ya Jumanne usiku.

Kwa mujibu wa Kanzul Ummal imesimuliwa na Urwa kwamba Abu Bakr na Umar hawakuwepo kwenye mazishi ya Mtukufu Mtume, lakini walikuwepo kwenye kundi la Ansari (huko Saqifa bani Sadah) na Mtume alizikwa kabla ya kurudi kutoka huko.

Kwa mujibu wa Nihayah cha Bin Athir Jazari, Majma al-Bidar cha Mulla Tahir Qutni na al- Milal wa Nihal cha Shahristani, baadaye Umar alisema kwamba kutoa kiapo cha uaminifu kwa Abu Bakr ni jambo lisilotegemewa lakini Mwenyezi Mungu alitunusuru kutoka kwenye uovu wake.

Kufuatana na Tarikh Abu Fida kundi la Bani Hashim na pia Zubayr bin al-Awam, Miqdadi bin Amr, Salman Farsi, Abu Dharr, Ammar al-Yasir, Bara bin Azib na wengine waliokuwa upande wa Ali, walikaa pembeni wakati wa kutoa kiapo cha uaminifu kwa Abu Bakr.

Imeandikwa kwenye Istiab cha Abdul Barr kwamba wakati kiapo cha uaminifu kilikuwa kinatolewa kwa Abu Bakr, Ali hakuapa uaminifu kwake na alikaa nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa Muruj uz-Zahab cha Masudi, ambapo mnamo siku ya Saqifah kiapo cha uaminifu kilitolewa kwa Abu Bakr, Ali alimwambia Abu Bakr; “Umeharibu mambo yetu, ulituona kwa ushauri na hukufikiria haki yetu.” Abu Bakr akasema, “Lalamiko lako ni halali lakini nimefanya hivyo kwa kuhofia maasi.”

Kwa mujibu wa Rauzatul Ahbab, Abu Bakr alipomaliza kazi ya kutafuta kiapo cha uaminifu kwake, alimwita Ali kupitia kwa Wahajirina na Ansari kadhaa. Ali alikwenda na akauliza kwa nini nimeitwa? Umar akasema, “Umeitwa ili kutoa kiapo cha uaminifu kama ambavyo wengine wamekwisha fanya”. Ali akasema, “Ninaiweka mbele yako hoja ile ile, ambayo umewaambia Ansari kupata Ukhalifa. Niambie kwa uaminifu mtu ambaye yu karibu zaidi na Mtume.”

Umar alisema, “Hatutakuachia hadi hapo utakapotoa kiapo cha uaminifu.” Ali alisema, “Jibu swali langu kwanza halafu niambie suala la kutoa kiapo cha uaminifu.” Abu Ubaydah bin Jarrah akasema, “Ewe Abul Hasan! Ni wewe tu ndiye unayestahili Ukhalifa na utawala kwa sababu ya kutangulia katika Uislamu na ukaribu wako kwa Mtume, lakini kwa kuwa masahaba wamemkubali Abu Bakr, ni vema wewe pia uungane nao,” Ali akasema Abu Ubaydah! Unataka kuhamisha neema kubwa ambayo Mwenyezi Mungu ameipatia familia ya Mtume na kupeleka kwingineko. Tazama! Sisi ni mahali palipoteremshwa Wahyi, mahali ambapo ziliwasili amri na makatazo, chanzo cha uadilifu na maarifa, na mgodi wa akili na ustahamilivu.

“Aliposikia hivi, Bashir bin Said akasema, “Ewe Abu Hasan! Tulidhania kwamba kukaa kwako nyumbani ulikuwa tayari kujitoa katika kinyang’anyiro cha Ukhalifa.” Ali akasema, “Hivi nyinyi watu mnaona ni sawa kuacha maiti ya Mtume bila kukafiniwa, kuvishwa sanda na kuzikwa, na kwa hiyo ningejiingiza kwenye kugombania na kukirimu watu kwa kutafuta Ukhalifa?”

Imeandikwa kwenye Usudul ul-Ghibah kwamba Ali alimnukuu Mtukufu Mtume akisema, “Ewe Ali! Wewe ni kama Ka’abah ambapo kila mtu huenda kuzuru, ambapo yenyewe haiendi kuzuru mtu yeyote. Kwa hiyo, endapo watu wa kundi lako wanakuja kwako kutoa kiapo cha uaminifu kwako kubali. Usiende kwao hadi wao waje kwako.”

Kwa mujibu wa Rauzatul Ahbah, Abu Bakr aliposikia mambo haya na kuona kwamba kila sababu na hoja ya Ali, Ilikuwa haipingiki, thabiti na dhahiri kama hoja elfu moja, alisema kwa upole, “Ewe Abul Hasan! Nilidhani kwamba hungekataa kutoa kiapo cha uaminifu kwangu. Kama ningejua kwamba ungekataa, nisingekubali kuwa Khalifa. Sasa, kwa kuwa watu wametoa kiapo cha utii kwangu, nafikiri ni vema uungane nao, kama utapenda. Lakini, kama unasita kwa sababu hii, sitakulaumu.” Baada ya Ali kusikia haya alinyanyuka na kwenda nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa Iqdul Farid, cha Shahabuddin bin Abd Rabbihi Undlusi, watu waliokataa kutoa kiapo cha uaminifu kwa Abu Bakr walikuwa; Ali, Abu Dharr, Zubayr na Sad bin Ubadah. Miongoni mwao, Ali Abbas na Zubayr walikaa nyumbani kwa Bibi Fatimah hadi Abu Bakr alipomtuma Umar aende kuwatoa nje watu hao na kutumia upanga endapo wangekataa. Kwa hiyo, Umar alifika hapo akiwa na moto kwa lengo la kuchoma nyumba hiyo. Fatimah alipotambua nini kinachoendelea, alisema; “Ewe mwana wa Khattab! Umekuja kuchoma moto nyumba yangu!?” Umar alisema, Bila shaka nimekuja kwa nia ya hiyo, au vinginevyo, watu waliomo ndani ya nyumba hii watoke na watoe kiapo cha uaminifu kwa Abu Bakr.”

Kwa mujibu wa Tarikh Abul Fida, Umar alikwenda na moto kwa nia ya kuchoma moto nyumba ya Fatimah. Fatimah alipotambua, alisema, “Ewe mwana wa Khatab! Umekuja kuchoma moto nyumba yangu!?” Umar akajibu, “Ndio, vinginevyo watu waliopo ndani watoe kiapo cha uaminifu kwa Abu Bakr.”

Kufuatana na Tarikhut Tabari cha bin Jarir, Umar alikwenda nyumbani kwa Murtaza (Imamu Ali) ambamo walikuwemo Talha, Zubayr na muhajirina kadhaa na akasema, “Kwa jina la Mwenyezi Mungu! Nitachoma moto nyumba hii vinginevyo mtoke nje kwa ajili ya kutoa kiapo cha uaminifu.”

Imeandikwa kwenye Al-Imamah wa as-Siyasah cha bin Qutaybah Dinuri kwamba Abu Bakr alipogundua kwamba wale waliokuwa na Ali hawakuwepo wakati kiapo cha auaminifu kilipokuwa kinatolewa, alimtuma Umar awaite. Watu hao walikuwa ndani ya nyumba ya Ali. Walikataa kutoka nje. Umar aliagiza apewe kitita cha kuni zilizowashwa moto na akasema, “Tokeni nje au vinginevyo kwa jina la Mwenyezi Mungu nitawachoma watu waliomo ndani kwa moto!” Watu wakasema, “Fatimah, binti yake Mtukufu Mtume na yeye pia yupo ndani ya nyumba hii.”

Umar akajibu, “Haidhuru kitu,” Waliposikia hivi watu wote waliokuwa ndani ya nyumba walitoka nje isipokuwa Ali aliyekuwa anawapa maelezo watu ambao walitumwa wamwite, akasema; “Enyi kundi la Muhajirina! Ninayo haki zaidi ya kuchukua Ukhalifa kuliko nyinyi katika hali zote. Sitatoa kiapo cha uaminifu kwenu. Kwa usahihi zaidi, nyinyi mnatakiwa kutoa kiapo cha uaminifu kwangu.

“Tazama! Mmepata Ukhalifa kwa hoja mliyowapa Ansari kwamba nyinyi ni ndugu wa Mtume na jambo la kushangaza ni kwamba sasa mnajaribu kuchukua isivyo halali Ukhalifa kutoka kwa Ahlul-Bait wa Mtume.

“Hamweki madai yenu katika msingi kwamba nyinyi ni bora zaidi kuzidi Ansari kwa kisingizio kwamba Mtume alikuwa wa kabila lenu? Sasa nakupeni hoja hiyo hiyo ambayo mliwapa Ansari kwamba, uhusiano wetu na Mtume ni mkubwa na karibu zaidi kuliko wenu wakati wa uhai wake na baada ya kifo chake.

“Sasa mnatakiwa kutenda haki bila upendeleo endapo nyinyi mnamwanini Mwenyezi Mungu na kumwogopa Yeye.

“Kuhusu kundi la wahajirina! Mkumbukeni Mwenyezi Mungu na msichukue uongozi wa Mtume kutoka kwenye nyumba yake na kupeleka nyumbani kwenu.”

Baadhi ya hapo, Fatimah alisema akiwa kwenye ngazi za mlango wake, “Enyi watu! Mlituachia maiti ya Mtume, mkatatua jambo la Ukhalifa kwa kujipendelea nyinyi na hamkuzingatia haki yetu.”

Kwa mujibu wa Tarikh bin Qataybah Umar alipokwenda kwa Abu Bakr alisema, kwa nini hutoi amri ya kukamatwa Ali ambapo anapinga kutoa kiapo cha utii kwako?

Kwa mara nyingine Abu Bakr alimtuma mtumwa wake Qanfaz amwite Ali. Qanfaz alimwambia Ali, “Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu anakuita wewe.” Ali akasema, ‘Mmemkashifu Mtume haraka kiasi hicho nyie watu.”

Qanfaz alirudi kwa Abu Bakr na akarudia maneno aliyoambiwa na Ali. Baada ya kusikia Abu Bakr aliendelea kulia kwa kipindi fulani. Umar akamwambia Abu Bakr kwa mara ya pili, “Usimpe muda Ali ambaye hataki kutoa kiapo cha utii kwako.” Abubakr akamuagiza tena Qunfaz kwenda kwa Ali na kusema, Amiri wa Waumini anakuita ili utoe kiapo cha uaminifu. Qanfaz aliwasilisha ujumbe wa Abubakr kwa Ali. Ali akasema kwa sauti kubwa “Mwenyezi Mungu na asifiwe! Bwana wako amedai uhusiano huo ambao hana uwiano nao.”

Qafaz akaenda kwa Abu Bakr na kurudia maneno ya Ali. Baada ya kusikia hivi, Abu Bakr alianza kulia tena. Halafu Umar akasimama na akifuatana na kundi la watu, alikwenda nyumbani kwa Fatimah na akagonga mlango. Aliposikia kelele za watu, Fatimah alianza kulia kwa sauti kubwa, “Ewe Baba! Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni tatizo gani hili lenye uzito mkubwa ambao limeletwa kwetu na mwana wa Khattab na Abu Quhafah!” Watu waliposikia kilio cha Fatimah, wengi wao walirudi huku wanalia na wachache tu ndio waliobaki nyuma na Umar. Halafu Ali akatoka nje ya nyumba na akaenda nao kwa Abu Bakr. Ali aliambiwa atoe kiapo cha uaminifu kwa Abu bakr. Alisema, “Endapo sitatoa kiapo cha utii itakuwaje?” Akasema, “Endapo hutatoa kiapo cha uaminifu, kwa jina la Mwenyezi Mungu tutakuua.”

Ali alisema, Mtamuua mtu ambaye ni mja wa Mwenyezi Mungu na ndugu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Umar akasema, “Tunakiri kwamba wewe ni mja wa Mwenyezi Mungu, lakini hatujui kama pia wewe ni ndugu yake Mtume.” Abu Bakr alikuwa kimya wakati huo. Umar akamwambia, “Kwa nini hutoi amri, umekaaa tu?” Abu Bakr akasema, “Sitamlazimisha Ali wakati Fatimah bado hai.” Halafu Ali alinyanyuka na alikwenda kwenye kaburi la Mtume ambapo alilia, kwa uchungu na akasema, “Ewe ndugu! Watu wa kabila wamenitukana sana na walikaribia kuniua.”

Abu Dharr alikuwa anayaona mambo haya kwa macho yake. Alikuwa na kumbukumbu ya yele aliyoyaona humo Ghadir al- Khum. Alishangaa sana kuona yaliyokuwa yanatokea.

Akiwa bado yupo katika mshangao, ghafla imani yake ilitikisa hisia zake na alikimbia hadi kwenye Msikiti wa Nabi. Akili yake ilipatwa na fadhaa na kusumbuliwa na damu yake ilichemka kwa shauku. Alikuwa anangoja apate fursa ili atoe mawazo bila woga. Alipofika msikitini aliona kundi la masahaba wakiwemo Abu Bakr na Umar miongoni mwao.

Ujasiri wake wa kiume ulisisimuka na akaanza kutoa hotuba akiwa amesimama kwenye sehemu iliyoinuka.

Alisema: “Enyi watu wa Qurayshi! Nini kimetokea? Mmekuwa wazembe kiasi gani! Mmedharau kabisa ndugu wa karibu zaidi wa Mtume! Kwa jina la Mwenyezi Mungu kundi la Waarabu limeamua kuasi, na kutengeneza nyufa za mashaka katika imani. Nisikilizeni! Ukhalifa ni haki ya Ahlul Bait. Vurugu hii na ugomvi wa kelele ni mambo yasiyo na maana. Nini kimewapateni? Mnawaita wenye uwezo hawana uwezo na mnawasifu wasio na uwezo. kwa jina la Mwenyezi Mungu wote nyinyi mnatambua kwamba Mtume ametangaza tena na tena, ‘Baada yangu Ukhalifa na uongozi ni wa Ali, halafu Hasan halafu Husein na halafu uzao wangu ambao ni maasum ndio watakao shika nafasi hii.’

“Hamjali neno la Mwenyezi Mungu! Mlisahau mkataba ule na amri ile ambayo inawapa masharti. Mnaisujudia dunia hii ambayo inaandamia na mnauza Pepo ambayo inadumu milele, na ambamo vijana hawatazeeka na neema hazitapungua, na wakazi wake hawatapata huzuni au kufadhaika na ambamo malaika wa kifo hatafika. Mmeuza kitu cha thawabu kubwa sana kwa bei ndigo sana. Mmefanya kitu kile kile walichofanya watu wa Mitume wa zamani. Walivunja kiapo chao cha uaminifu na waliasi pindi Mtume wao alipokufa!

Walitangua mikataba yao, walibadilisha amri na kugeuza imani. Sasa mnathibitisha kwamba mpo sawa na wao. Kundi la Quraishii! Baada ya muda mfupi sana mtapata malipo ya makosa yenu na adhabu kwa maovu yenu. Kile mlichokichuuma kupitia na tabia yenu kitakuja kwenu kumbukeni! Vyovyote itakavyotokea itakuwa haki, kwa sababu Mwenyezi Mungu hawadhulumu waja Wake (al-Ishtiraki az-Zahis, uk. 113).

Ujasiri wa kiume wa Abu Dharr unaweza kudhihirishwa na hotuba iliyojaa ushawishi. Ni wazi kwamba alikuwa na moyo ulio mwepesi kuhisi na alijaalia kuwa shupavu na jasiri.

Abu Dharr alitoa hotuba hii wakati ambapo hakuna hata mtu mmoja ambaye angeweza kusema neno. Jeshi la Khalifa lilikuwa linawasonga masahaba wa Mtukufu Mtume. Yeyote aliyeonesha dalili za kukataa kutoa kiapo cha uaminifu aliuawa. Yeyote aliyesita kutoa kiapo cha Uaminifu alisongwa. Mtu jasiri kama Ali alifungwa kwamba shingoni na sahaba kama Salman alikabwa koo na kupigwa sana hivyo kwamba maumivu yake yalisababisha kifo chake.

Shaykh Abbas Qummi ameandika kwamba Fatimah binti yake Mtume baada ya kupata maumivu kwa kuangukiwa na mlango, aliugua kwa kipindi fulani na alifariki dunia. Kwa mujibu wa wosia wake, Ali hakutangaza kifo chake kwa watu walioshiriki katika kusababisha umateso yake. Baada ya kumaliza kuosha maiti, Ali alimtuma Imamu Hasan kumwita Abu Dharr ili aisalie maiti, na alikwenda akamwambia. (Safinatul Bihar, cha Shaykh Abbas Qummi, Juz. ya 1, uk. 483).

Hafidh Muhammad bin Ali bin Shahr Ashob (alifariki dunia mwaka 588 A.H) ameandika kwamba, maiti ya Fatimah ilisaliwa na Ali, Hasan na Husein, Aqil, Salman, Abu Dharr, Miqdad, Ammar na Buraydah.

Hadith nyingine imejumuisha majina ya Abbas bin Abdul Muttalib, Fazal, Huzayfah na bin Masud pia (Manaqib bin Shahr Ashob, Juz. ya 2, uk. 65 kimechapishwa Multan).