Sura Ya Kumi Na Moja

Abu Dharr, kwa sababu ya desturi yake, mwenendo wake, tabia na amri ya Mtume, alishindwa kunyamaza inapobidi alisema kweli na aliishi maisha ya kimya. Kazi kubwa zaidi ya kumuabudu Mwenyezi Mungu ilikuwa kukaa karibu na kaburi la Mtume na kuwasifu Aali Muhammad (Uzao wa Mtume).

Inaonekana na kwenye vitabu vingine vya historia kwamba Ali alimshauri afuate sera ya upole. (Nasikhul Tawarikh, Juz ya 2, uk. 803).

Baada ya muda kupita hadi mwaka wa 13. A.H., Abu Bakr alifariki dunia. Kwa mujibu wa Tarikh Tabari na Mujam Kabir ya Tabarani, Abu Bakr alisema kwa majuto na masikitoko; “Endapo nisinge fungua nyumba ya Fatimah hata kama ilifungwa kwa nia ya kupigana, na kama nisingekubali Ofisi ya Ukhalifa, lakini ni kwamba niliweka mkufu wa Ukhalifa kwenye shingo la Umar au Abu Ubaydah.”

Imeandika kwenye Tarikhi bin al-Wardi kwamba baada ya hapo alimteua Umar kuwa Mrithi wake. Kwa mujibu wa al-milal wan nahl cha Shahristani, Abu Bakr alipomteua Umar kuwa Khalifa muda mfupi kabla ya kifo chake, watu walipiga kelele, “Umemteua mtu mwenye hasira na moyo mgumu kama kiongozi wetu.”

Kwa mujibu wa Tarikh Abul Fida, Abu Bakr alikufa mwezi wa Jamadiul ukhra tarehe 22, mwaka wa 13 A.H, kati ya muda wa Swala ya magharibi (jioni) na Isha (usiku) na siku hiyo hiyo kiapo cha utii kilitolewa kwa Umar. Abu Dharr hakushiriki Swala ya kumsalia maiti au taratibu zingine za mazishi ya Abu Bakr kwa sababu hakuna kitabu cha historia kinachotaja jina lake katika tukio hili.

Wimbi la ushindi lilijitokeza bada ya kifo cha Abu Bakr. Chini ya hali iliyojitokeza wakati huo, Abu Dharr aliamua kuondoka Madina na kwenda Syria na kuishi huko kwa kipindi chote cha uhai wake. Kwenye kitabu cha Musnad cha Ahmad, anasema kwamba Abu Dharr alipendelea kuishi Syria kwa sababu ya wasia wa Mtume ambapo unasema ifuatavyo; “Ewe Abu Dharr! Ondoka Madina uende Syria wakati idadi ya watu itaongezeka na kuenea hadi Mlima Sala.”

Kwa vyovyote vile, kwa mujibu wa wosia wa Mtume, Abu Dharr aliondoka kwenda Syria akiwa na mke wake na mtoto wa kike mmoja. Shah Walyullah Dehlavi, ameandika kwamba Abu Dharr aliondoka kwenda Syria baada ya kifo cha Abu Bakr na akaloea huko. (Izalatul Khiofa Juz. ya I , uk. 282).

Abu Dharr alikuwa mkali sana kuhusu ukweli. Kwa hali hii, kamwe hakujali ukali wa mtu yeyote, wala hakuogopa serikali ya mtu yeyote au uwezo wa mtu yeyote.

Baada ya Abu Dharr kuondoka kwenda Syria, Umar alikwenda huko kwa madhumuni mengine alipokutana na Abu Dharr ambaye alimsimulia hadith moja ya Mtume. Abu Dharr alisema; “Nina shuhudia kweli kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema; “Mtu ambaye anafanywa kuwa mtawala au kiongozi, ataamuriwa kusimama kwenye daraja la Jahanamu. Atapata ukombozi kama yeye ni muadilifu, lakini kama ni mwovu, daraja litavunjika na kuanguka na mtu huyo ataanguka ndani ya Jahanamu.”
Abu Dharr alikuwa anampenda sana Mtume (s.a.w). Mapenzi haya yaliongezeka zaidi baada ya kufa Mtume na alikuwa akilia sana. Wakati alipokuwa anaishi Syria, watu walimshinikiza Bilal aadhini Adhana kwa ajili ya Swala.

Bilal akasema, “Nimeacha kuadhini Adhana baada ya kifo cha Mtume (s.a.w). Wala sewezi kukariri Adhana sasa na siwezi kuivumilia.” Kwa hali yoyote Bilal alikataa na kwa shida sana akalazimishwa na kukubali. Bilal alisimama ili adhini Adhana na akaanza kuadhini kwa sauti yake kubwa ambayo kipindi fulani ilisikika kwenye mitaa ya Madina wakati wa uahi wa Mtume (s.a.w). Abu Dharr aliinamisha kichwa chake kuelekea mbele. Machozi yalianza kutiririka kwenye machavu yake. Fikra zake zilimkumbusha Madina na akamuona Mtume kwa macho yake ya kiroho, akiwa amezungukwa na masahaba wake.

Akakumbuka mambo yaliyopita akaanza kulia kwa sauti kubwa huku machozi yakimtoka machoni pake.” (al-Ishtiraki az-Zahid).

Abu Dharr aliishi nje ya Madina kwa muda wa miaka kumi huko Syria na alirudi Madina baada ya kupata taarifa kwamba Umar ameuawa.

Abdul Fida ameandika kwenye historia yake kwamba mtu aliyeitwa Abu Lulu alimshambulia Umar mnano mwezi wa Dhil Hijjah tarehe 24, mwaka wa 23 A.H Tarikh Kamil bin Athir ameonesha kwamba Umar alipojeruhiwa, mganga wa kabila la Bani Harith aliagizwa. Alimpa Umar divai ya tende, uliotoka kwenye jeraha bila mabadiliko. Halafu akampa maziwa anywe, pia yalitoka bila ya mabadiliko; “Ewe Amiri wa Waumini! Tayarisha wosia wowote unaotaka.”

Imesimuliwa kutoka kwa Abu Wajiz kwenye Kanzul Ummal kwamba Umar aliuliza watu, “Mnataka nani awe Khalifa baada yangu?” Mmoja wao alisema: “Zubayr bin al-Awam.”

Umar akasema, “Mtamfanya mtu huyo kuwa Khalifa wenu ambaye ni bahili na hana staha.” Mtu mwingine akasema; “Tutamfanya Talha awe khalifa wetu,” Umar akasema; “Mtapenda kumpa Ukhalifa mtu ambaye aliweka rehani kwa mwanamke wa Kiyahudi aridhi iliyotolewa wakfu na Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Baada ya kusikia hivi, bado mtu mwingine akasema, “Tutamfanya Ali kuwa Khalifa wetu.”

Umar akasema, “Kwa niaba ya uhai wangu! Hamtamfanya Ali kuwa khalifa na endapo kwa jina la Mwenyezi Mungu, mtamfanya Ali kuwa Khalifa wenu, hatajizuia kuwawekeni katika njia iliyonyoka hata kama nyinyi hampendi.” Walid bin Uqbah aliposikia hivyo, akasema, “Namjua mtu atakayekuwa khalifa baada yako,” Umar alinyanyuka na akamuuliza, “Nani?” Walid akasema; “Uthman”. Huzayfa bin al-Yaman anasimulia kwamba Umar aliulizwa, alipokuwa na afya njema, kama nani angekuwa khalifa baada yake. Akajibu, “Uthman bin Affan.”

Mulla Ali Qari ameandika kwenye‘Sharah I-iaqh Akbar’ kwamba wakati wa muda wa kifo cha Umar ulipokaribia shughuli za Ukhalifa zilianza kufanywa na Uthman, Ali, Talha, Zubayr, Abdul Rahman bin Auf na Sad bin Abi Waqqas, na akasema kwamba Ukhalifa usivuke hawa watu sita.

Imeandikwa kwenye Tarikh Kamil kwamba Baada ya hapo Umar alimlaumu Suhayb, “Waongoze watu kwenye Swala kwa kipindi cha siku tatu wafungie ndani ya nyumba hawa watu sita ambao wengine miongoni mwao wanatekeleza kazi za ukhalifa halafu uwaangalie.

Kama watano miongoni mwa watu hawa wanamkubali mtu mmoja na mtu mmoja anapinga, auawe endapo watu wanne wanakubaliana na wawili hawakubaliani, wawili wanakataa wauawe na kama watatu wanakubaliana na watatu wengine wanakataa, Abdullah bin Umar ateuliwe kuwa mwamuzi wa kuamua, na kama watu hawa wanamkataa Abdullah bin Umar kuwa mwamuzi, kundi ambalo Abdullah Rahman yupo lishinde na kundi lingine la watu liuawe.”

Kwa mujibu wa Tarikh Abul Fida, Umar alikufa siku ya Jumamosi tarehe 30 mwezi wa Zil Hajjah. Kwa mujibu wa ‘Sharah Fiqh Akbar,’

Ambapo baada ya kifo cha Umar, na kufuatana na maagizo yake, kikao cha baraza la ushauri kilifanyika ndani ya nyumba ya Fatimah, dada yake na Ashath bin Qays. “Kwa mujibu wa Tarikh Aathama, uk. 112, watu wa kundi hilo la watu sita lilimpa Abdul Rahman bin Auf, haki ya kumteua khalifa.

Abdul Rahman akiwa amenyanyua mkono wa Ali aliuliza mara tatu, “Endapo tunakuteua wewe Walyyul Amir na Imamu upo tayari kufuata Kitabu cha Mungu, Hadith za Mtume na hadith za Shaykhain (Abu Bakr na Umar)?”

Ali alijibu, “Nitafanya hivyo, vyovyote vile itakavyokuwa, nitafuata Quran Tukufu na Suna ya Mtukufu Mtume (s.a.w) lakini (kuhusu suna za (shaikhain), nitapitia amri za kidini kufuatana na ujuzi wangu.” Baada ya kusikia hivi Abdul Rahman alimuuliza Uthman mara tatu, “Utafuata Kitabu cha Mungu, Suna za Mtume na Suna za Abu Bakr na Umar, endapo tunakuteua wewe kuwa Imamu?” Uthman alisema, “Ndio vyovyote vile itakavyokuwa, nitafanya.” Halafu Abdul Rahman alitoa kiapo cha uaminifu kwake na wengine wakafuata hivyo.

Imetamkwa kwenye Tarikh Kamil na Tarikh Abul Fida kwamba kiapo cha uaminifu kilipokuwa kinatolewa kwa Uthman, Ali alipoona hila katika jambo hili la kutoa kiapo cha uaminifu alisema, “Leo si mara ya kwanza kwamba mmepata ushindi kwa kutumia hila. Vema! Ni bora zaidi kuwa mvumilivu. Ewe Abdul Rahman! Kwa jina la Mwenyezi Mungu! Umetoa kiapo cha uaminifu kwa Uthman ili ukhalifa ukuelekee wewe,” Abdul Rahman alisema; “ewe Ali! Usijali hili.” Halafu akatoka nje ya nyumba huku akisema; Ilitakiwa iwe hivyo. Miqdad akasema; “Ewe Abdul Rahman! Ulimwacha Ali pamoja na kwamba, kwa jina la Mwenyezi Mungu, yeye ni miongoni mwa watu wasio achana na kweli na hutoa hukumu zenye haki.”

Tarikh Kamil na Tarikh Tabari ni maandishi yanayosema kwamba, Miqdad iliendelea kusema, ‘nilikuwa sijaona kitendo cha ukorofi kama hiki wanafanyiwa watu wa Nyumba ya Mtume baada ya kifo chake. Ninashangaa kuona kwamba Qurayshi wamemwacha mtu ambaye ninamfikiria kuwa mwanachuoni bora kuliko wote (Alim-i Rabbani) na jaji muadilifu kuliko wote (Adil). Kwa jina la Mwenyezi Mungu, endapo ningepata wa kuniunga mkono na msaidizi!” Miqdadi alisema hivi tu ambapo Abdul Rahman aliingilia kati, “Ewe Miqdadi! Muogope Mwenyezi Mungu. Ninahofu vinginevyo waweza ukajikuta upo kwenye matatizo.”

Imeandikwa kwenye Murujuz Zahab cha Musudi kwamba Ammar Yasir alisimama kwenye Msikiti wa Nabi na akasema; “Enyi kundi la Waquraishi! Mlipopora Ukhalifa kutoka kwa Ahlul Bait wa Mtume wenu na mkauondosha na kuupeleka mara hapa mara kule, pia lazima tuwe na matumaini kwamba Mwenyezi Mungu atauchukua ukhalifa kutoka kwenu na kumpatia mtu mwingine kama ambavyo mmechukua kutoka kwa anayestahili.” Halafu Miqdadi akasimama na kusema, Sijapata kuona kamwe aina hii ya mateso na maudhi ambayo Ahlul Bait wanapewa baada ya kifo cha Mtume.” Abdul Rahman akasema, “Ewe Miqdadi! Unafanya nini?” Miqdad akasema, “Kwa nini nisiseme?

“Mimi ni rafiki wa Ahlul Bait wa Mtume kwa sababu mapenzi niliyonayo kwa Mtume na hakika wao hawaachani na kweli na ipo kwao peke yao. Ewe Abdul Rahman! Ninawashangaa Waquraishi ambao unajaribu kuwasaidia wapate kuwazidi wengine na ambao wamekula nyama kutaka kupora upendo na ukuu wa Mtume (s.a.w) kutoka kwa Ahlul Bait wake baada yake. Ewe Abdul Rahman! Tambua! Kwa jina la Mwenyezi Mungu! Kama ningekuwa na watu wa kuniunga mkono na marafiki, ningepigana na Quraishii kama ambavyo nilivyofanya kwenye vita ya Badr.”

Kufuatana na Tarikh Tabari, Ammar Yasir alisema, “Enyi watu! Mwenyezi Mungu ametimiza jambo kubwa kwa kutupatia imani Yake na ametupatia ukuu kwa sababu ya Mtukufu Mtume. Mnataka kupeleka wapi Ukhalifa mnapowanyang’anya Ahlul-Bait wa Mtume wenu?”

Kwa mujibu wa Raudhatul Ahbab Abdul Rahman bin Auf alipotoa kiapo cha uaminifu kwa Uthman na wale waliokuwepo kwenye mkutano walifuata kufanya hivyo, Ali alisema baada ya kutua kwa muda, “Enyi watu! Ninawaulizeni mniambie kwa kiapo kama yupo hata mtu mmoja isipokuwa mimi miongoni mwa masahaba wa Mtume ambaye Mtume kwenye tukio la kutangaza ‘udugu’ baada ya kunitangaza mimi kuwa ndugu yake, kwamba mimi ni ndugu yake hapa duniani na Akhera.” Wasikilizaji wakajibu, “Hakuna.”

Ali akasema “Yupo mtu yeyote miongoni mwenu isipokuwa mimi ambaye Mtume angemteua kuitangaza Sura ya Baraat (Sura ya 9 ya Quran Tukufu) ikifuatiwa na tangazo kwamba kazi ya Utume wa Mwenyezi Mungu haiwezi kufanywa na yeyote yule isipokuwa na yeye au mojawapo wa Ahlul Baiti wake?” Wote walisema, “Hakuna.”

Ali akasema, ”Mnatambua kwamba kiongozi wa wanadamu, na mwombezi wa Siku ya Hukumu alinipeleka mimi kama kamanda wa Muhajirina na Ansari wote katika Siriyas (vita ambazo Mtume hakushiriki yeye binafsi) na akawaamuru wanitii na kamwe hakumteua mtu yeyote kama kamanda kunizidi mimi.” Watu wakasema, “Ndio, kwa vyovyote vile. Ni kweli.”

Ali akasema, “Mnatambua Mtukufu Mtume ametangaza elimu yangu kwa kusema; “Mimi ni jiji la elimu na Ali ni lango lake.” Watu wote walikiri, “Ndio tunajua.”

Ali akasema, “vita nyingi masahaba walikimbia na kuondoka kwenye uwanja wa vita na kumwacha Mtume ameelemewa katikati ya maadui lakini mimi kamwe sikumtekeleza kwenye vita yoyote ya hatari na nilibaki naye kujitolea maisha yangu kwa ajili ya maisha ya Mtume.” Watu wote walisema, “Ndio, hasa.”

Ali akasema, “mnajua kwamba mimi nilikuwa wa kwanza kuingia kwenye Uislamu.” Watu wakasema, “Ndio tunatambua.”

Halafu Ali akauliza, “Ni nani kati yetu ambaye yupo karibu zaidi na Mtume kwa sababu ya uhusiano wa undugu?” Wote kwa pamoja walisema, “Hapana shaka kwamba uhusiano wako wa nasaba na Mtukufu Mtume (s.a.w) unathibitishwa vema sana, rasmi na umeimarika kwa njia zote.”

Ali alipokuwa anazungumza hivyo naye Abdul Rahman bin Auf alisema, “Ewe Abul Hasan! Hakuna mtu anayeweza kukanusha sifa ambazo umezitaja na kuzieleza. Lakini, kwa kuwa sasa watu walio wengi wametoa kiapo cha utii kwa Uthman, na anayo matumaini kwamba wewe pia utaungana nao kwa jambo hili.” Ali akajibu, “Kwa Jina la Allah wewe unatambua vema sana ni nani aliyestahili Ukhalifa, lakini, inasikitisha kwamba umemwacha kwa kukusudia.”

Kwa mujibu wa Tarikh Tabari, Ali alikariri Ayah hii kutoka kwenyeQurani Tukufu:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ مِنْ نَفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا{1}

“Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaomba na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaangalia.” (Sura 4:1).

Mazungumzo ya tukio la kuchaguliwa kwa Uthman pia yameandikwa katika Iqdul Farid, Juz. 3 uk. 75, kimechapishwa Misri na Sharah Maqasid Taftazani, uk. 296.

Mwandishi wa historia Muhammed bin Ali bin Athman Kufi ameandika kwenye kitabu chake mnao mwaka wa 204 A.H kwamba Ali bin Abi Twalib (a.s) aliongezea kwa kusema, “Enyi watu! Mnatambua kwamba sisi ni Ahli Bit wa Mtume na njia ya ulinzi wa umma dhidi ya kila janga na dhiki. Endapo hamtatupatia haki yetu, itajifikisha yenyewe kwenye mhimili wake, na kama hamtatupata haki yetu, tutakwenda popote tunapoona panafaa kwa kupanda ngamia, bila kujali muda utakaotumika, na saa ya ahadi ya kuonana, tutarudi.

Ninaapa kwa Utukufu wa jina la Mwenyezi Mungu kwamba kama Muhammad hakuchukua ahadi kutoka kwetu na kutuambia kuhusu jambo hili, nisinge acha kupigania haki yangu, na nisingesita kufanikisha lengo langu hata kama ingemaanisha kupoteza uhai wangu. (kwa kupigana).”

Kufuatana na Tarikh Abul Fida kiapo cha uaminifu kwa Uthman kilifanyika mwezi wa Muharram tarehe 3, mwaka wa 23 A.H.

Baada ya kuchaguliwa kwake kwa kazi ya ukhalifa, Uthman alifuata utaratibu unaotakiwa kutawala kwa muda fulani. Lakini, muda ulivyozidi kupita ndivyo alivyondeleza kugeuka, akaacha kutenda haki na kuwa dhalimu, matokeo yake ni kwamba ilitokea vurumai ya kusisimua miongoni mwa masahaba wa Mtukufu Mtume.

Muhammad bin Ali bin Atham Kufi, mwandishi wa historia wa Uislamu wa karne ya tatu A.H amesema kwamba lolote lile walilosema watu kuhusu Uthman na maneno na matendo yake yoyote yale yaliyovumiliwa nao, yalisimuliwa kutoka kwa wahadithi wa kuaminika kwa maneno na mitindo tofauti, lakini kwa kuwa kiini chao kimoja, ameyafupisha maneno hayo katika neno moja.

Wasimulizi wanasema kwamba baada ya kuwa khalifa Uthman aliendelea nao watendaji wa Umar kwa muda wa siku chache ambapo baadaye aliwafukuza kazi na akawapatia Bani Umayyah ambao walikuwa binamu na ndugu zake mikoa yote. Alimteua Abdullah bin Amir Kurbuz huko Basrah. Walid bin Atabah aliteuliwa gavana wa Kufah, Muawiyah bin Abi Sufyani aliendelea kuwa gavana wa Syria, alimteua Abdullah bin Sad bin Abi Sarah kuwa gavana wa Misri, na Umar bin Aas aliteuliwa kuwa gavana wa Palestina.
Sehemu ya ngawira ilipelekwa kwa Khalifa baada ya kutoka Khurasan, Sijistan, Pars, Kerman, Misr, Syria na visiwa vya Iraq. Pia Khalifa Uthman alikuwa na tabia njema hadi wakati huo na alizingatia utoaji wa haki. Lakini ofisi ya ukhalifa ilipoanza kupelekewa utajiri mkubwa na ngawira nyingi, tabia ya Uthman ilibadilika.

Aliweka utawala wote chini ya udhibiti wa Bani Umayyah, na aliwapatia ndugu zake miji yote. Aliwapa ndugu zake idadi kubwa ya fedha bila sababu za msingi kutoka hazina ya taifa. Alimpa Abdullah bin Khalid bin Asas bin Aas bin Umayyah dinari 100,000 mara tu alipomtaarifu kwamba yupo pale ingawa hakuwepo kwenye orodha, alimpa mwanae Abdullah, Harith dinari 100,000 na alimpa mwanae Harith bin Hakim kiasi hicho hicho.

Watu hawakukubaliana na ugawaji wa namna hii wa fedha, walilalamika kwa Abdul Rahman bin Auf na wakasema, “Utawajibika kwa matokeo yake. Tunapata hasara hii kwa sababu yako. Siku hiyo ulipomfanya Khalifa, hatukutoa kiapo cha uaminifu kwa matendo haya mabaya na uovu. Sasa tunataka kujua tufanye nini.”

Abdul Rahman akasema, “Bado sijapata taarifa ya hayo mnayoyasema.” Siku iliyofuata Ali alimuona Abdul Rahman na akamuuliza endapo alikubaliana na matendo kama hayo. Abdul Rahman akasema, “Mimi sijui endapo mambo haya ni ya kweli na tabia ya Uthman imebadilika kama hivi, chomoa upanga wako na mimi pia nitafanya hivyo.”

Watu, pia nao walipeleka taarifa hii kwa Uthman ambaye alikasirika na akasema, “Abdul Rahman ni mnafiki na yeye kuniua mimi halitakuwa jambo gumu kwake.” Abdul Rahman pia alisikia maneno haya, alikasirika na akasema, “Kamwe nisingedhani kwamba Uthman angediriki kuniita mimi mnafiki.” Halafu akaapa kwamba hatasema na Uthman hadi mwisho wa uhai wake. Sasa mambo haya yakajulikana na kila mtu akawa anamshutumu Uthman.

Taarifa zilikuwa zinamfikia Uthman pia. Siku moja aliagiza Waislamu wote wakusanyike msikitini. Watu walipokusanyika Uthman alipanda kwenye mimbari, akamsifu Mwenyezi Mungu na kukariri Salawat na Salam kwa ajili ya Mtukufu Mtume. Baada ya hapo akasema; “Enyi watu! Endeleeni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ukarimu Wake ili kwamba neema na utajiri unaweza kuongezeka. Mkumbukeni Yeye wakati wote, chukueni Jina Lake, na mzingatie haki Zake. Nyinyi ni Waislamu na muwe nacho Kitabu cha Mungu ambamo kila kitu kimeandikwa.

“Tambueni kwamba kuweza kukalia kiti cha Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na kuendesha ukhalifa ni kazi ngumu sana. Pia cheo cha Ukhalifa kipo nje ya uwezo wenu wa kuelewa. Mwenyezi Mungu amewapa utawala Mawalii na Maamiri ili waweze kuamua ugomvi baina ya wanyonge na wenye uwezo na kuwazuia wenye uwezo wasiwakandamize wanyonge.

“Mjue kwamba ni amri ya Mwenyezi Mungu kumtii mtawala. Muwe na hofu kwa Mwenyezi Mungu. Mfuate maagizo Yake. Mjiepushe na upinzani na dhambi.

“Wapo wengi miongoni mwenu ambao wameona siku za Mtukufu Mtume, wamesikia mazungumzo yake matakatifu na wameshuhudia matendo yake. Zaidi ya hayo, Kitabu cha Mwenyezi Mungu kipo mikononi mwenu. Lazima mmezisoma amri zote na makatazo yote na matendo mema na maovu. Mwenyezi Mungu amekupeni tangazo Lake la mwisho, Ameahidi kuwazidishia neema wale watakao mshukuru Yeye kwa neema hizo. Watu waadilifu watapata thawabu na adhabu watapewa waovu.

“Tayari nimesikia ufahari na maonyesho na utukufu na uwezo wa wafalme na watawala. Wao walikuwa na uwezo zaidi kuzidi sisi na walikuwa na majeshi makubwa zaidi. Walikuwa na majiji makubwa na walikuwa wanaishi kwenye raha na starehe, lakini, kwa kuwa hawakutekeleza amri za Mwenyezi Mungu, walipenda zaidi dunia kuliko pepo, walipenda zaidi ugomvi na vurugu, na hawakutaka kumshukuru Yeye kwa ajili ya neema Zake. Aliwaweka kwenye uoza, na akawapeni nyinyi miji yao, nyumba zao na malisho yao na akawapeni neema zao zote. Neema zitabaki kwenu kama mkiendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwazo, au vinginevyo zitapunguzwa kwa sababu ya dhambi zako na kutokuwa mtiifu na hatimaye mtaangamia.

“Mwenyezi Mungu amenipa mimi Ukhalifa wa Mtume. Nina uwezo wa kufanya kazi hii leo. Nimechukua ofisi hii mkononi mwangu na ninafanya kazi muhimu na nzito.

“Mwenyezi Mungu huyu huyu ambaye amenipa Ukhalifa, hunipa uwezo unaolingana na ridhaa Yake, na pia nilitambua siri ya sentensi: Wote nyinyi ni walinzi na wote mtaitwa kuhesabu masuala yenu, na mmeelewa ukweli ulio wazi kwamba mtu ambaye amefanywa kuwa kamanda, amepewa dhamana kueleza kila tendo la watu wake na kuhesabu kila chembe na atomi.

“Watu wameniambia kwamba baadhi yenu waneweka pingamizi kuhusu fedha ninayotumia na wanaambizana kwamba ingelikuwa vizuri kama Uthman angeliwapa fedha hizi wapiganaji na watoto wao. Kwa vyovyote vile lingekuwa jambo la manufaa na lingekubaliwa na Mwenyezi Mungu. Ninakubali na nitaendelea kukubali siku zijazo. Nimewatuma watu wa kuaminika katika kila jiji na kuwagawia wapiganaji na watoto wao fedha nyingi kadiri watakavyokusanya na kuweka akiba zitakazobaki kwa matumizi wakati zitakapohitajika.

“Inshallah, nitakuwa ninawalipia haki zao wazee, fakiri, mayatima na wajane, nitataka ushauri wenu ninapokuwa na muda, kuhusu mambo yanayojitokeza na kuhitaji kufikiriwa na nitatekeleza kufuatana na ushauri wenu.

“Njooni kwangu mara kwa mara, zungumzeni na mimi matatizo na manufaa na nielezeni yale mnayoona yanastahili. Nitafanikisha kazi kama mnavyotaka na kufuatana na dharura itakayo kuwepo muda huo. Sina mlinzi mlangoni kwangu wa kuwakagua nyinyi. Mtu yeyote anaweza kuja wakati wowote na kuniambia lolote atakalo. Amani iwe kwenu!”

Baada ya kumsikia Uthman Waislamu wote walifurahi na walirudi kwao wakimsifu na kumwombea. Uthman alifuata njia ya haki, akazingatia usawa baina ya wapiganaji na raia, aliwafanya wema watu wote na aliwatimizia masikini na mayatima. Mwaka mmoja ulikwisha katika hali hii.

Kwa mara nyingine tabia yake ilibadilika kufuata taratibu ambazo zilikuwa kinyume na Sunna na uadilifu. Masahaba wa Mtume walikasirika sana. Walifanya mkutano na wakaamua kumuona Khalifa na wawasilishe kwake orodha ya maandishi ya mambo hayo ambayo yanachukiza katika Uislamu na ambayo yametokea tangu alipochukua cheo cha ukhalifa, kwa sababu mazungumzo ya mdomo yangeweza kusahaulika na hata kama wangekumbuka baadhi ya mambo muhimu lakini wangeshindwa kuyabainisha wazi wazi. Kwa hiyo ilionekena ni busara kuyaandika mambo hayo. Baada ya hayo, waloandika mambo yote matatu yanayopingana na dini ambayo yalitokea tangu mwanzo wa Ukhalifa wa Uthman hadi muda huo, na walitaka waende wote kwa pamoja kukabidhi Khalifa waraka huo.
Halafu, watu hawa walionana na Ammar bin Yasir, wakamwambia walichoandika na wakamwomba awasilishe waraka huo kwa Uthman.

Ammar akajibu kwamba alikuwa tayari kufanya hivyo. Halafu akaenda kwa Uthman na waraka ule. Wakati ambapo khalifa alikuwa anatoka nje ya nyumba yake, Ammar alikuwa amefika mlangoni na akamuuliza, “Ewe Abul Yaqzan! Unataka kuniona?” Ammar akajibu, “Sina jambo lolote la kibinafsi na wewe lakini masahaba wa Mtume kwa pamoja wameandika orodha ya matendo yako ambayo umeyafanya kinyume na sharia ya dini , ili ufafanue maoni yako.”

Uthman alichukua waraka huo akiwa amekasirika, alisoma mistari michache halafu akazitupa. Ammar akamwambia, “Usitupe kwa kuwa makaratasi haya yameandikwa na masahaba wa Mtume (s.a.w). Badala yake, soma kwa uangalifu na utoe jibu ipasavyo, ninakuambia mambo haya kwa maslahi yako.” Uthman akasema, “Ewe mwana wa Sumayyah! Unasema uwongo!” Akajibu, “Bila shaka mimi mtoto wa Sumayyah bin Yasir.”

Khalifa akakasirika. Akaamuru watumishi wake wampige Ammar, sahaba wa Mtume (s.a.w). Alipigwa sana hivyo kwamba alianguka chini na kupoteza fahamu. Halafu yeye mwenyewe Uthman alimpiga Ammar mateke kadhaa tumboni na sehemu za siri. Ammar akapoteza fahamu tena. Alipata mpasuko tumboni na kusababisha ngiri.

Watu wa bani Makhzum ambao walikwua ndugu zake Ammar, walikwenda na Hashim bin Walid bin Mughirah waliposikia habari hizo. Wakamchukua Ammar na kumlaza kitandani. Ammar alikuwa bado amepoteza fahamu ambapo watu wote waliapa kiapo kwamba endapo angekufa, kwa sababu ya kipigo wangemuua Uthman. Wakati Ammar bado hana fahamu, vipindi vya Swala vya adhuhuri na jioni vilipita. Alipopata fahamu wakati wa usiku aliamka, akatawadha na kusali Swala zake za vipindi vilivyopita.

Jambo hili la Ammar pia ni mojawapo ya matendo mabaya ya Uthman ambayo yalisababisha masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w) kuvunja kiapo cha uaminifu kwa hasira (Tarikh Aatham Kufi, uk. 126-130). Hili ni tukio moja tu ambalo limeandikwa kwenye vitabu vya historia. Ifuatayo ni mifano michache kutoka kwenye vitabu vya kuaminika na mashuhuri vya historia, ili ijulikane ni matendo gani aliyoyafanya wakati wa Ukhalifa wake na alifanya kwa umma na masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w).

Imeandikwa kwenye Tarikh Khulafa cha Suyuti, kwamba Uthmani alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha Adhan ya kwanza kabla ya Sala ya Ijumaa. Kufuatana na ‘al-Wasail Fi Marifatul Awail’ Uthman alikuwa mtu wa kwanza kufanya hotuba itangulie Swala ya Idd. Kamwe haikufanyika wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w) na wakati wa utawaka wa khalifa wa kwanza na wa pili. Kwa mujibu wa taarifa ya Masoud iliyopo kwenye, Murujuz Dhahab, Uthman alipopata Ukhalifa, mjomba wake Hakam bin al-Aas, Marwan bin Hakam na wengineo kutoka Bani Umayyah (ambao walifukuzwa Madina kwa amri ya Mtume) walikusanyika kwa Uthman. Marwan alikuwa ni yule yule aliyetengwa na kutolewa Madina na Mtume na alikatazwa kusogea karibu na Madina.

Pia magavana walioteuliwa na Uthman, alijumuishwa kaka yake upande wa kikeni, Walid bin Uqbah ambaye Mtume alikwisha sema habari zake kwamba angekwenda Jahanamu. Walid bin Uqbah alikuwa na tabia ya kunywa kilevi na marafiki zake wapiga muziki na Malaya usiku kucha, na muadhini alikuwa akimwamsha kwa ajili ya Swala, naye (akiwa amelewa) alikwenda msikitini kuongoza Swala ya alfajiri, na baada ya Swala kusalisha rakaa nne badala ya mbili, alionesha kutaka kuendelea na rakaa zingine endapo watu walitaka kuendelea.
Pia imeandikwa kwamba Walid akiwa kwenye rukuu ya Swala alikawia kunyanyuka na kusema; kunyweni na mnifanye mimi ninywe. Kwa hiyo, mara mmoja ilitokea watu waliokuwa mstari wa mbele nyuma yake walisema, ‘Hatukushangai wewe lakini tunamshangaa yule aliyekuleta wewe hapa ili uwe kamanda wetu.” Taarifa ya ufisadi wa Walid na kulewa kwake ilipoenea kwa watu wote, kundi la Waislamu, akiwemo Abu Jundab na Abu Zaynab, walimzonga Walid msikitini. Wakamuona amelala na hana fahamu.

Watu walijaribu kumwamsha, lakini aliposhindwa kupata fahamu, walichukua pete yake ya alama kutoka kwenye kidole chake na haraka walikwenda Madina na kutoa taarifa ya ulevi wa Walid kwa Uthman. Uthman alimuuliza Abu Jundab na Abu Zaynab walijuaje kama Walid alilewa mvinyo. Walisema huku wanampa pete yake kama ushahidi wa ulevi wake. Alikunywa mvinyo huo huo tuliokuwa tunakunywa wakati wa siku za ujahiliya (kabla ya Uislamu). “Badala ya Uthman kusikiliza mazungumzo yao yote, alianza kuwalaumu na kuwasukuma huku akisema, “Ondokeni hapa.” Waliposikia hivi wote wawili walirudi haraka.

Kwa mujibu wa Tarikh Abul Fida Uthman alimfukuza Amr bin al-Aas kwenye ugavana wa Misri na badala yake akamteua kaka yake wa kuchangia ziwa Sad bin Ali Sarh na ni mtu huyu huyu ambaye Mtume alikwisha toa ruhusa ya kuuawa siku Makah ilipotekwa na Waislamu.

Kwa mujibu wa Tarikh Kamil, Uthman alikwenda Hija mwaka 26 A.H. Marwan bin Hakim anasimulia kwenye Musnad Abu Daud Tialisi. Nilimuona Uthman na Ali wakati wa Hija. Uthman alikuwa anawakataza watu kufanya Hija ya Mut’a (kutekeleza Hija na Umra). Ali alipoona hivi alikariri Tahlil (La ilaha illallah) ya Hija na Umra kwa pamoja na akasema; “Nipo hapa kwa Hija na Umra pamoja,” Uthman akasema, “Ewe Ali! Unafanya jambo lile ambalo nimekataza watu wasifanye,” Ali akajibu, ‘Sitaacha Sunna ya Mtume kwa ombi la mtu.” (Hadith hii inaweza kuonekana kwenye Sahih Bukhari pia).