Sura Ya Kumi Na Nane

Baada ya Abu Dharr kurudi Madina kutoka Syria, alijishughulisha na mahubiri yake ambapo tukio lingine la kupasua moyo lilitokea kwa mara nyingine na hilo lilikuwa la kuchomwa kwa Qurani.

Tayari alikwisha huzunika kuona Serikali ya Kiislamu ilikuwa inaharibiwa. Utajiri wa Waislamu ulikuwa unatumika kuwapa ndugu na jamaa wa Khalifa. Mlango wa Hazina ya Taifa ulifungwa kabisa kwa wanaohitaji, masikini, mayatima na wajane, lakini ulikuwa umefunguliwa wazi sana kwa uzao wa Umayyah. Watu masikini walikuwa wanateseka kwa njaa ambapo ndugu wa khalifa walikuwa wananunua nyumba, mabustani na ardhi. Ghafla akapata taarifa kwamba khalifa alikuwa na nakala tofauti za Qurani ambazo zilikusanywa kutoka sehemu mbali mbali na akazichoma moto. Kwa hiyo, tukio hili muhimu likawa lenye mahubiri yake. Mwandishi wa historia Abul Fida ameandika kwamba tukio hili lililotokea mwaka wa 30 A.H. (Tarikh Abul Fida, Juz. 2, uk. 100, chapa Amritsar, 1901 A.D).

Mwandishi wa historia Yaqubi (alifariki mwaka wa 278 A.H ) ameandika kwenye kitabu chake kwamba Uthman alikusanya Qurani na akazipanga kwa namna ambayo aliziweka sara ndefu pamoja na sura fupi pamoja mbali mbali, na akaagiza nakala kutoka kila sehemu, zikaoshwa kwa maji ya moto na siki na akazichoma moto. Matokeo yake ni kwamba hakuna nakala ya Qurani iliyobakia isipokuwa nakala iliyomilikiwa na Bin Masud ambayo alikuwa nayo Kufah. Abdullah bin Amir, gavana wa Kufah alipomuuliza bin Masud amwoneshe nakala yake akakataa. Uthman alipopata taarifa hii alimwandikia barua Amir amkamate bin Masud na ampeleke kwake Madina. Bin Masud alipoingia msikitini, Uthman alikuwa anatoa hotuba.

Alipomuona Bin Masud akasema; “Mnyama mbaya na katili amekuja.” Bin Masud naye alitoa jibu kali. Uthman aliposikia, akaamuru watu wampige. Kwa hiyo, watu wakampiga na kumburuza kwa namna ambayo kwamba mbavu zake mbili zilivunjika.

Imeandikwa kwenye tarjumi ya Kiajemi ya Tarikh Atham Kufi (imechapishwa Bombay, uk. 147 mstari wa 8) kwamba Uthman alipasua Quran na ikachomwa moto. Ni maelezo ya aina haya haya yapo kwenye kitabu ‘Successors of Muhammad’ (W. Iqving Uk. 160 chapa –London, 1850 A.D).

Kwa mujibu wa Majatul Mumin usemi wa Mulla Mohsin Kashmiri, Uthman akavunja mbavu za bin Masud na akamnyang’anya Quran na akaichoma moto. Kufuatana Raudhatul Ahad Juz. 2, uk. 229, chapa Luckanow), Uthman aliamuru Qurani yangu lazima ipewe nafasi ya kuenea kwenye utawala wangu na nakala zingine zichomwe moto. Kwa mujibu wa Tarikh al-Quran usemi wa Abdul Qadir Makki, uk. 36 chapa ya Jeddah, 1365 A.H Sahih Bukhari Juz. 6, uk. 26 chapa Bombay, Mishkar Shari chapa Delhi, uk. 150, na Tafsir Itqan Suyuti chapa Ahmads, Juz. 1, uk 84, Uthman alipeleka taarifa kwa Hafsah, mke wa Mtukufu Mtume, ili ampelekee Maandishi ili aweze kunakili na halafu amrudishie. Hafsah alimpekea nakala alizokuwa nazo na Uthman akamteua Zayd bin Thabit, Abdullah bin Zubayr, Said bin As, Abdul Rahman bin Harith kukusanya na kunakili maandiko hayo, na aliwataka watu hao wote watatu wa Quraishii kuandika Qurani kwa kutumia mazungumzo ya Quraishi endapo pangetokea tofauti fulani katika mambo kadhaa, kwa sababu Qurani iliteremshwa katika lugha yao. Watu hao watatu walifanya kufuatana na walivyoagizwa hadi mwisho na Uthman akayarudisha Maandiko hayo kwa Hafsah kama alivyoahidi na akampelekea nakala iliyotayarishwa upya. Sasa, nakala ya Qurani iliyobakia ni hiyo tu iliyotayarishwa na Uthman iliendelea kuwepo na nakala zingine zote zilichomwa moto. Kwa mujibu wa Fathul Bari, usemi wa bin Hajar Asqalani Juz. 4, uk 226, Uthman alirudisha Qurani ya Hafsah lakini Marwan alichukua kwa nguvu na akaichoma moto. Kwa mujibu wa Tarikh Khamis uk. 270, Istiab uk. 73 na Sawaiq Muhrizah uk. 68 Uthman alihakikisha nakala zote za Qurani zimechomwa moto isipokuwa ya kwake na aliamuru Abdullah bin Masud apigwe sana hivyo kwamba alipata maradhi ya henia (ngiri). Halafu akamfunga jela na akafia huko. Kwa mujibu wa Tuhfah Ithna Ashariyah, usemi wa Abdul Aziz, Ubayy bin Kab alimpa Uthman Qurani yake na hakupigwa. Qurani hiyo pia ilichomwa moto.

Kwa hali yoyote ile imeandikwa kwenye vitabu vingi sana kwamba Uthman alichoma maandiko matakatifu. Hizi ni nakala za Qurani zilizokusanywa wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr. Aishah Ummul Muminin alipopata habari ya Qurani kuchomwa moto alikuwa na wasi wasi. Akasema, “Enyi Waislamu! Muueni mtu huyu ambaye anachoma Qurani! Amefanya udhalimu mkubwa sana.”(Anwarul Qulub, Muhammad Baqir Majlis uk. 313).

Aishah hakuridhika na jambo hili alifululiza kudhihirisha kero dhidi ya Uthman. Alisema tena na tena; “Muueni Yahudi huyu, Na’thal. Mwenyezi Mungu na amuue. Amekuwa asi.” Rauzatul Ahbab, Juz. 3, uk. 12). Kwa mujibu wa Tazkirab Khawasul Ummah uk. 38, 40, 41 bin Athir Jazari alikwua akisema, “Muueni Na’thal huyu. Mwenyezi Mungu na amuue.” Kwa matamshi haya alikuwa anamaanisha khalifa Uthman. Halafu bin Athir anaeleza kwa nini Aishah alimuita Uthman Na’thal. Sababu ni kwamba Na’thal alikuwa yahudi wa Misri na ndevu zake zilifanana na zile za Uthman. Halafu tena anasema kwamba kufuatana na matamshi ya Shaykh ilimaanisha mpumbavu. Anaendelea kusema kwamba baadae Aishah alikwenda Makkah (Nihayah bin Athir).

Mwandishi wa historia Ibn Taqtaqi ameandika kwamba Uthman aliuawa kwa matokeo ya amri ya Aishah, ‘muueni Na’thal huyu.” Siku hiyo hiyo nyumba yake ilipozingirwa, Aishah alikwenda Makkah. (Tarikh Fakhri, uk. 62 chapa Misri).

Inaeleweka wazi kwamba Aishah akiwa mwanamke alishtushwa na tukio hili, kwa nini Ali asingeshtushwa na tukio hili la kutisha? Imejulikana kutokana na maandishi ya wasomi wa kuaminika kwamba Ali alishtushwa sana na tukio hili la kuchomwa Qurani. Kwa hiyo, aliona umuhimu wa kutaka ushauri wa Abu Dharr kuhusu suala hili. Allamah Majlis ameandika kwamba baada ya tukio hili Ali alimuomba Abdul Malik, mtoto wa Abu Dharr ampeleke baba yake kwake. Alipofika, alibadilishana mawazo naye kuhusu tukio hili, alionesha kuhuzunika kwake na akasema jambo hili limenyoshwa na kupasuliwa vipande vidogo. Inawezekana Mwenyezi Mungu atalipa kisasi kwake kwa jinsi ile ile. Abu Dharr akasema , “Ewe Ali! Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema kwamba wafalme dhalimu watawaua watu wa nyumba yake.” Ali akasema, “Ewe Abu Dharr! Unataka kunikumbusha kuhusu kuuawa kwangu?” Abu Dharr akasema, “Hapana shaka, hilo litatokea na wewe utakuwa mtu wa kwanza miongoni mwa uzawa wa Mtume kuuawa.” (Hayatul Qulubi, Juz. 2, uk. 104).
Kwa ufupi, inaonesha wazi kwamba Abu Dharr aliathirika sana na tukio hili la kuogofya. Pia aliongeza maudhui moja zaidi kwenye hotuba zake na kuliita tukio hili njia isiyo ya Kiislamu. Na itambulike kwamba kwa kuwa kitendo cha kuchoma Qurani kinatia jeraha moyo wa Kiislamu kwa baadhi ya waandishi wa siku hizi, wamebadilisha neno kuchoma pale ambapo maelezo ya kuchomwa Qurani yanatolewa. Shah Walyullah Dehlavi, kwenye matukio katika maisha ya Uthman ameandika. “Aliyaondoa maandiko mengine ambayo yalifikiriwa kusababisha migongano. (Izalatul Khifa Juz. 1, uk 274).