Sura Ya Kumi Na Nne

Abu Dharr alikuwa mtu mkweli. Alikuwa anawaonya watu wengine wafanye matendo mema. Muawiyah alikuwa mtu aliyependa mambo ya dunia. Kila mara Abu Dharr alikuwa anamwelekeza kufanya matendo mazuri hadi watu wa Syria walianza kuona aibu. Siku moja Muawiyah alimwambia Abu Dharr, “Wewe si muadilifu kiasi cha kunielekeza mimi kufanya matendo mema mbele ya umma.” Aliposikia hivi Abu Dharr akasema, “Nyamaza! Huoni hata aibu!”

Kwa ufupi, Muawiyah alipoona kwamba hangeweza kujirekebisha na hangemnyamazisha Abu Dharr, aliamua kumhamisha Syria. Kwa hiyo, aliamua kumpeleka Jabal al-Amul. Subaiti anasema kwamba Abu Dharr alipowaita watu wa huko kuwaelekea Ahlul-Bait, walikubali wito huo haraka sana! Kwa kuwa sehemu hiyo ilikuwa pana sana, wito wake haukubakia kwenye mipaka ya ndani ya Jabal al-Amul lakini ilifika hata kwenye sehemu za karibu.

Ni dhahiri kwamba Muawiyah alimpeleka Abu Dharr Jabal al-Amul kutoka Syria kwa sababu tu alidhani kwamba shughuli zake za kuhubiri miongoni mwa watu hao wageni zingesimama, lakini aliposikia kwamba Abu Dharr na hotuba zake kali aliwafanya watu wa Jabal al-Amul waelekee ukweli,1 alimwita arudi Syria haraka.
Abu Dharr alianza tena kazi yake alipofika Syria. Alikuwa na tabia ya kukaa mahali paitwapo Bab Damishq (lango la Dameski), baada ya Swala ya alfajiri na kila anapoona msururu wa ngamia uliobeba mali ya serikali aliita kwa sauti kubwa; “Watu! Msururu huu wa ngamia ambao unakuja haukubeba mali ile umebeba moto. Wamelaaniwa watu wanao waelekeza wenzao kufanya wema lakini wao hawafanyi hivyo, na iwaangukie laana watu wanaowakataza wengine wasifanye uovu lakini wao hufanya uovu.” (Tarikh Yaqubi, Juz. 2, uk. 148 na al-Ghadir, Juz. 8, uk. 299).

Halafu Abu Dharr aliondoka mahali hapo na kwenda kwenye lango la Ikulu ya Muawiyah na akatoa hotuba hiyo. Hili ilikwisha kuwa kawaida yake na alifanya hivyo mara kwa mara. Hatimaye Muayiyah alimkamata.

Abu Dharr aliizingatia hadith ambayo imenukuliwa na Khatib al-Baghdad na Almad bin Hanbal. Kufuatana na maelezo ya hadith hii Mtukufu Mtume aliwaambia masahaba wake; “Enyi masahaba wangu! Sikilizeni kwa makini.

“Baada yangu watawala wa umma wangu watakuwa kama makabaila. Wao hawatatofautisha haki na dhuluma na kweli na uwongo. Lakini, yeyote atakayekwenda upande wao na kuthibitisha uwongo wao na kuwaunga mkono katika udhalimu wao, hatakuwa na uhusiano na mimi, na hatakutana na mimi kwenye Haudhi ya Neema. Mtu ambaye hatakuwa na uhusiano nao, hatahalalisha uwongo wao, na hatawaunga mkono katika udhalimu wao, huyo atakuwa ametoka kwangu na mimi nitakuwa nimetoka kwake na atanikuta kwenye Haudhi ya Neema. (Tarikh al-Khatib al-Baghdad, Juz. 2, na Juz. 5, Musnad Ahmad bin Hanbal Juz.1)

Mtu yeyote mwenye akili ataelewa kwamba katika hali hiyo Abu Dharr hangejali mamlaka yoyote. Tabia ya Abu Dharr, zaidi ya kuwa mtu wa kawaida na wa hulka, yalikuwa matokeo ya mafundisho ya Mtukufu Mtume. Hakuna hata mfano moja uliotajwa kwenye historia za kuaminika kuonesha kwamba katika uhai wake Abu Dharr alisita kusema kweli.

Jalam bin Jandal Ghifari, Gavana wa Qiusarin anasema; “Wakati mmoja, wakati wa ukhalifa wa Uthman nilipokuwa Gavana wa Qiusarin nilikwenda kwa Muawiyah, Gavana wa Syria kwa shughuli za kikazi. Ghafla nilisikia mtu anasema kwa sauti kubwa kwenye lango la ikulu. Msururu wa ngamia unaokuja kwako umebeba Moto wa Jahanamu. Mwenyezi Mungu na awalaani wale wanao waambia wenzao kufanya matendo mema, lakini wao wenyewe hawafanyi hivyo. Mwenyezi Mungu na awalani wale wanaowakataza wenzao kufanya matendo maovu ambapo wao hufanya maovu.

“Wakati huo niliona kwamba uso wa Muawiyah ulibadilika rangi kwa sababu ya hasira. Aliniuliza kama nilikuwa humtambua mtu huyo, ambaye alikuwa analia. Nilimjibu hapana. Halafu Muawiyah akasema, ‘Huyu ni Jandab bin Janedah Ghifari. Huja kwenye lango la Ikulu yetu kila siku na kurudia maneno yale yale ambayo uliyasikia muda mfupi uliopita. Halafu akaamuru auawe.

“Ghafla nikamuona Yaqudunah anamleta Abu Dharr akimburuza na akamsimamisha mbele. Muawiyah akamwambia, ewe adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kila siku unakuja kwetu na kurudia rudia maneno hayo. Hakika ningekwisha kukuua kama ningeweza kumuua sahaba wa Mtume bila ruhusa ya Uthman. Sasa nitaomba ruhusa kuhusu wewe.”

“Nikataka kumuona Abu Dharr kwa sababu anatoka kwenye kabila letu. Nilipomtazama, nilimuona alikuwa amesinyaa, mwembamba na mrefu. Ndevu zake hazikuwa nyingi, na mgongo wake ulikunjika kwa sababu ya kuzeeka.

Abu Dharr alimjibu Muawiyah; “Mimi si adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake lakini wewe ndiye adui yake Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na baba yako pia alikuwa adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Nyinyi watu mlitangaza Uislamu kwa maslahi ya kibinafsi lakini katika nyoyo zenu mlikuwa makafiri. Mtume wa Uislamu alikulaani mara mbili na alikuapiza hivyo kwamba ule bila kushiba. Nimesikia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba Umma wake utateswa na fitina ya mtu mwenye macho makubwa na koo pana, ambaye hatosheki chakula ingawa hula sana, pale atakapokuwa mtawala wa umma huu.

Aliposikia hivi Muawiyah akasema; “Mimi sio yule Mjumbe wa Mwenyezi Munu alimsema” Abu Dharr akasema; ‘Ewe Muawiyah! Haina maana kukanusha kwa hakika wewe ndio mtu yule yule na sikiliza! Mtume ameniambia kwamba mtu huyo alimaanisha wewe na wewe peke yako. Ewe Muawiyah! Siku moja ulipokuwa unapita mbele ya Mtume, nilimsikia akisema; Ee Mwenyezi Mungu! Mlaani huyo na ulijaze tumbo lake vumbi. Ewe Muawiyah! Nimemsikia Mtume akisema pia kwamba upande mmoja wa Muawiyah upo kwenye Moto wa Jahanamu. Aliposikia hivi, Muawiyah alicheka kicheko cha aibu, akaamuru Abu Dharr akamatwe, akapelekwa jela na akamwandikia barua Uthman kuhusu jambo hili. (Hayat al-Qulubi, Juz. 2, uk. 1043, al-Ghadir, Juz. 8, uk. 299 kama ilivyo nukuliwa kutoka kwenye Tarikh Yaqubi).

Baada ya kumpeleka Abu Dharr jela Muawiyah katika barua aliyo mwandikia Uthman alilalamika kuhusu Abu Dharr kwamba aondolewa Syria na kurudishwa Madina. Kufuatana na Barua hiyo Uthman alimrudisha Abu Dharr Madina. Kwa mujibu wa tafsiri ya Tarikh Atham Kufi Shafii (Majlisul Muaminin uk. 119) Maudhui yake ni kama yafuatayo:

“Baada ya heshima ipasayo kwako Muawiyah bin Sakhr kwa unyenyekevu kwa kusema kwamba Abu Dharr anawachochea watu wa Syria waasi dhidi yako. Anawahamasisha watu wakuchukie wewe. Anawakumbuka Umar na Abu Bakr kila wakati na anakumbusha kuhusu mwenendo na uadilifu wao mzuri. Hukutaja wewe kwa kutumia maneno mabaya na husema maneno yako na matendo yako ni maovu na yenye makosa. Haifai kumruhusu aishi Syria, Misri na Iraq kwa sababu watu wa nchi hizi ni wapenda fitina na huungana na watu wachochezi haraka na kusababisha ghasia. Nimekutaarifu kuhusu yaliyo jitokeza. Sasa vyovyote khalifa atakavyo amua ni bora. Wasalam.”

Mpanda ngamia aliondoka na barua ya Muawiyah na kuiwasilisha kwa Uthman huko Madina. Mara baada ya Uthman kupokea barua hiyo alirudisha majibu kwa Muawiyah mara moja. “Ninayo barua yako; nimekwisha elewa ulichoandika kuhusu Abu Dharr. Mara upatapo barua hii msafirishe Abu Dharr aje Madina kwa kutumia ngamia wa mwendo wa haraka ambaye ataendeshwa na mtu mwenye moyo mgumu ambaye atamkimbiza ngamia mchana na usiku ili Abu Dharr achoke na alale ili asahau kusema mambo yako na yangu.”

Baada ya kupokea barua hii, Muawiyah alimwita Abu Dharr na akamsafirisha kwenda Madina kwa kupanda ngamia asiye na tandiko la kukalia na ambaye ni mtundu na mwendeshaji mbaya. Muawiyah alimwagiza mwendesha ngamia kumfanya ngamia akimbie usiku na mchana bila kupumzika hadi Madina.

Abu Dharr alikuwa mrefu na mwembamba na wakati huo tayari alikuwa mzee sana hivyo kwamba nywele na ndevu zake zilikuwa kijivu. Zaidi ya haya alidhoofu sana, hapakutandikwa nguo au tandiko la kukalia kwenye mgongo wa ngamia huyo. Mshika hatamu wa ngamia hakuwa na huruma naye. Kwa sababu ya matatizo yote haya na majeraha, mapaja ya Abu Dharr yalipata majeraha na alihisi maumivu makali na kuchoka.

Waandishi wa historia wanakubaliana kwamba Abu Dharr alipelekwa Madina peke yake. Familia yake haikuwa naye. Labda inaezekana hakuruhusiwa kwenda nyumbani kwake kuchukua familia yake. Lazima aliitwa kutoka jela na kusafirishwa kwenda Madina moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Allamah Majlis na Allamah Subaiti Abu Dharr alipokaribia kuondoka kwenda Madina, taarifa iliwafikia Waislamu ambao walikwenda kumuona na kumuuliza alikuwa anakwenda wapi. Abu Dharr akajibu; “Uthman ameniita Madina. Ninakwenda kuitika wito wake. Enyi Waislamu! Uthman alipohisi nimekosea, alinileta hapa kwenu. Sasa ninaitwa tena Madina. Ninatambua kwamba safari hii nimeitwa ili niteswe. Lakini ni muhimu mimi, kwenda, kwa vyovyote vile. Sikilizeni! Uhusiano wangu na Uthman utabakia hivi. Msisikitike na msiwe na wasi wasi kuhusu suala hili.”

  • 1. Vita hii ilitwa Zaat al-Ruqa (vita ya viraka vya nguo) kwa sababu njia ilikuwa na mawe mengi sana na mashimo, kwa sababu hiyo, miguu ya watu ilipasuka na kuifunga kwa vipande vya nguo. Zainul Ma’ad.