Sura Ya Kumi Na Tano

Abu Dharr alipokuwa anaondoka, watu walimsindikiza kumuaga hadi walifika Dair Maran sehemu iliopo nje ya jiji. Hapo aliswali Swala ya jamaa. Halafu akahutubia watu na tafsiri yake ni kama ilivyotolewa na Hayatul Qulub.

“Enyi watu! Ninawaachieni wasia wa kitu ambacho kitakuwa na manufaa kwenu.” Baada ya hapo aliwaambia wamshukuru Mwenyezi Mungu. Wote wakasema, “Sifa zote zinastahiki kwake Mwenyezi Mungu.” Halafu Abu Dharr akashuhudiaa Upweke wa Mwenyezi Mungu na Utume wa Muhammad na wote wakasema kama alivyosema. halafu akasema; “Ninakiri kuwepo kwa Ufufuo na Siku ya Hukumu na kuwepo kwa Pepo na Jahanamu. Ninaamini yale ambayo Mtume alileta kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ninawatakeni mshuhudie hii imani yangu.” Wote wakasema, “Tunashahudia yale ambayo umeyasema.”

Baada ya hapo akasema, “Yeyote miongoni mwenu atakaye kufa akiwa kwenye imani hii atapata habari njema za huruma na wema wa Mwenyezi Mungu almuradi yeye si msaidizi wa watenda dhambi anayeunga mkono matendo ya wagandamizaji, mshirika wa madhalimu.

“Enyi kundi la watu! Ghadhabu na msononeko iwe pia sehemu ya Swala zenu na kufunga Swaumu, mnapowaona watu wanafanya dhambi kinyume na matashi ya Mwenyezi Mungu. Msiwafurahishe viongozi wenu kwa vitu ambavyo ni sababu ya hasira ya Mwenyezi Mungu. Endapo watu hao wanaingiza vitu katika imani ya Mungu ambavyo ukweli wake hamjui, waacheni na mfichue makosa yao hadharani, hata kama watawatesa na kuwaondoeni kwenye makundi yao, hata kama watawanyang’anya zawadi zao, na kuwahamisheni kutoka kwenye miji, ili Mwenyezi Mungu apate kufurahishwa na nyinyi.

“Hakika Mwenyezi Mungu ametukuka mno na yuko Juu sana. Haistahili kumkasirisha Yeye kwa sababu ya kuwafurahisha viumbe Vyake Mwenyezi Mungu na waghufirie nyinyi na mimi. Sasa ninawaacheni kwa Mwenyezi Mungu na ninawatakia amani na huruma za Mwenyezi Mungu.”

Wote wakajibu; “Ewe Abu Dharr! ewe sahaba wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na akuweke salama na akuridhie neema Zake! Hungependa tukuchukue tena tukurudishe jijini kwetu na tukuunge mkono mbele ya maadui.” Abu Dharr akasema; “Mwenyezi Mungu na akupeni rehema! Sasa mnaweza kurudi. Hakika mimi ni msitahimilivu zaidi kwenye mabalaa kuliko nyinyi. Kamwe msifarakane na msiwe na wasiwasi na msitofautiane miongoni mwenu.”

Waandishi wa historia wanasema kwamba Abu Dharr alipofika Madina akiwa ameiacha familia yake Syria, akiwa amenyong’onyea na kuchoka sana alipelekwa mbele ya mfalme wa wakati huo, Khalifa Uthman. Wakati huo watu wengi walikuwepo kwenye baraza. Mara Khalifa Uthman alipomuona Abu Dharr, alianza kumshutumu bila kujali heshima yake mbele ya Mtukufu Mtume. Inaonekana kwenye wasomi wa histoira kama vile Uthman alisema chochote kilichokuwa akilini mwake akiwa kwenye hasira na ghadhabu. Hata alisema, “Ni wewe ndiye ambaye amefanya matendo yasiyostahili.”

Abu Dharr akasema, “Mimi sikufanya lolote isipokuwa nilikupa ushauri na ukauwelewa vibaya ushauri wangu na ukanihamisha na kunipeleka mbali na wewe. Halafu nikamshauri Muawiyah. Na yeye pia hakupenda ushauri wangu na amenihamisha na kunipeleka mbali na yeye .” Uthman akasema; “Wewe ni mwongo. Wewe unaendekeza uhaini akilini mwako. Unataka kuichochea Syria iniasi mimi.”

Abu Dharr akasema; “Ewe Uthman! Fuata nyayo za Abu Bakr na Umar tu na hakuna mtu atakayesema lolote dhidi yako.” Uthman akasema, “Kuna umuhimu gani mimi kufuata nyayo zao au nisifuate nyayo zao. Mama yako na afe!” Abu Dharr akasema; “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, huwezi kunishutumu mimi kwa lolote isipokuwa mimi ninawaelekeza watu wafanye matendo mema na kuwakataza wasifanye matendo mabaya.

Aliposikia maneno haya Uthman alijaa hasira na akasema, “Enyi wazee wa baraza! Nipeni ushauri nimfanye nini huyu mzee mwongo. Nimpe adhabu ya kumtandika viboko, nimfunge jela, auawe, au nimpeleke uhamishoni. Amesababisha wasiwasi katika jamii ya Waislamu.”

Baada ya kusikia hivi, Ali ambaye alikuwepo hapo, alisema; “Ewe Uthman! Ninakushauri wewe kama muumini wa taifa la Firauni umwache mtu huyo alivyo. Endapo yeye ni mwongo basi atapata malipo yake na kama yeye ni mkweli hakika wewe ndiye utakayeumia. Mwenyezi Mungu hamwongozi yule ambaye ni mbadhirifu na mwongo.” Hapa palitokea mabishano makali kati ya Uthman na Ali ambayo sitaki kuyaeleza hapa. (Tabaqati bion Sad al-Waqidi, alifariki mwaka 230 A.H. Juzu. ya 4, uk. 168).

Muhammad bin Ali bin Atham Kufi, Ameandika kuhusu mzozo huo: Ali alimwambia khalifa Uthman, “Usimsumbue Abu Dharr. Endapo yeye ni mwongo atateseka kufuatana na matokeo ya matendo yake, na kama ni mkweli, yale anayoyasema yatatokeza dhahiri.” Uthman hakukubaliana na usemi huu wa Ali. Alimwambia Ali kwa hasira, “Usiingilie jambo lisilokuhusu! Ali pia alirudia maneno hayo hayo.

Halafu Ali akasema; “Ewe Uthman! Unafanya nini sasa? Ni dhuluma iliyoje unaifanya sasa! Haistahili wewe kutamka maneno kama hayo kuhusu Abu Dharr ambaye ni rafiki yake Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya mambo yasiyojulikana ambayo Muawiyah ameyasema. Hivi huna habari kwamba upo upinzani, ugandamizaji, maasi na uovu wa Muawiyah? Aliposikia hivi Khalifa Uthman alinyamaza.” (Tarikh Atham. Kufi na Majalisul Muminin).
Sayed Nurullah Shustari ameandika kwamba mara tu Abu Dharr alipomuona Khalifa Uthman mbele yake alikuwa na desturi ya kukariri Aya ya Qurani; “Iogope siku ambapo Moto wa Jahanamu utaunguza nyuso zao na zitapigwa chapa.” Akimaanisha kusema kwamba, ‘Ewe Uthman! Ni kosa kwako unapoacha kuwapa masikini utajiri unao hodhi lakini unapotoa, huwapa ndugu zako. Siku hiyo ipo karibu ambapo pande zako na uso wako utapigwa chapa huko Jahanamu.” (Mjalisul Muminin, uk. 94).

Kwa mujibu wa Tabari ilitokea Ali alimwambia Uthman; “Umeacha kufuata nyayo za wale waliokutangulia na sasa kwa urahisi tu unazidisha kuwapa mali uzao wa Umayyah na ndugu zako. Umewasahau masikini kabisa unavyofanya si sawa hata kidogo. Umepata wapi haki ya kugawa rasilimali ya Waislamu kwa njia ya dhuluma?” Uthman akakasirika aliposikia maneno haya ya Ali na akajibu, “Wale walio tangulia waliwakosea ndugu zao. Mimi sitaki kufanya hivyo. Nitawapa ndugu zangu masikini kile nitakachoweza.” Ali akasema; “Ndio hao tu watu wenye haki ya kuwapa maelfu ya dinari kutoka kwenye Hazina ya Taifa ya waislamu? Hakuna masikini mwingine?” (Tarikh Tabari, Juz. 2, uk. 272).

Waandishi wa historia kama Abul Hassan Ali bin Husein bin Ali al-Masudi (alifariki mwaka 346 A.H) Ahmad bin Abi Yaqubi na Ishaq bin Jafar bin Wahhab bin Wazeh Yaqubi (alifariki mwaka wa 278 A.H), na Muhammad bin Sad al-Zahri al-Basri, Katib al-Abbasi al-Waqidi (alifariki mwaka 230 A.H) wamesimulia tukio hili hivi: Abu Dharr alipofikishwa kwenye baraza, Uthman alimwambia Abu Dharr; “Nimeambiwa kwamba umewaambia watu hadithi ya Mtume kwamba wakati idadi ya wanaume wa Bani Umaayah itafikia thelathini kamili, wataifikiria miji yote ya Mwenyezi Mungu kuwa ngawira yao na waja wa Mwenyezi Mungu watumishi wao wa kiume na wakike na wataifanya dini ya Mwenyezi Mungu kama udanganyifu.”

Abu Dharr akasema, “Ndio, nimemsikia Mtume anasema hivyo.” Uthman akawauliza wasikilizaji wa baraza, “Mlimsikia Mtume anasema hivyo?” Wakasema, “hapana!” Halafu akamwita Ali na akasema, “Ewe Abul Hassan! Unathibitisha hadith hii?” Ali akasema; “Ndio.” Uthman akasema; “Nini uthibitisho wa ukweli wa hadithi hii?” Ali akajibu, Usemi wa Mtukufu Mtume kwamba hakuna msemaji chini ya mbingu na juu ya ardhi, ambaye ni mkweli kuzidi Abu Dharr.”

Abu Dharr alikaa Madina kwa siku chache tu baada ya tukio hili ambapo Uthman alimpelekea ujumbe kwamba, “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, hakika utahamishwa kutoka Madina.” (Murujuz Dhahab al-Masud; Juz. 1, uk. 438 na Tarikh Yaqubi, Juz. 2, uk. 148).

Allamah Majlis ameandika kwamba baada ya kurudi kutoka Syria, Abu Dharr aliugua. Siku moja aliingia barazani akiwa na mkongojo. Alikuwa ndio amefika hapo ambapo maofisa wa serikali waliingia hapo wakiwa na dinari 100,000, ambazo walikusanya kutoka sehemu mbali mbali za nchi. Mara tu Abu Dharr alipoziona akasema, “Ewe Uthman! Rasilimali hiyo ni ya nani?” Akajibu, “Rasilimali ya Waislamu.”

Akauliza, “Itakuwa kwenye hazina hadi lini kabla haijawafikia Waislamu?” Khalifa akasema, “Fedha hii nitakuwa nayo hadi zitakapopatikana dinari zingine 100,000, kwa sababu wameniletea mimi utajiri huu. Kwa hiyo, ninangojea zingine zaidi, ili niweze kumgawia yeyote ninayemtaka, na kuzitumia ninapoona pana stahili.” Abu Dharr akasema, “Zipi nyingi, dinari nne au 100,000?” Uthman akasema; “100,000 ndizo nyingi.”

Aliposikia hivi Abu Dharr akasema: “Ewe Uthman! Hukumbuki ya kwamba siku moja wewe na mimi tulikwenda kwa Mtume usiku sana na tulipomuona amehuzunika tukamuuliza sababu ya huzuni yake, hata hakusema na sisi kwa sababu ya uzito wa majonzi yake. Halafu tuliokwenda kumuona tena asubuhi tulimkuta anafurahi na anacheka, tukamuuliza kwa nini usiku wa jana yake alisema na huzuni sana na kwa nini alifurahi sana asubuhi hiyo, Mtume akajibu “Usiku wa jana, baada ya kugawa rasilimali ya Waislamu zilibaki dinari nne tu, kwa hiyo nilifadhaika sana. Lakini nimempa mtu aliye na haki ya kuzipata. Kwa hiyo, sasa ninafurahi.”