Sura Ya Kumi Na Tatu

Waandishi wa historia wanasema kwamba Uthman alipochoshwa na kilio cha kutetea ukweli cha Abu Dharr alimfanyia kila aina ya ugandamizaji huko Madina. Amri yake ilikuwa hakuna ruhusa mtu yeyote kusema na kukaa naye. Alilazimishwa kunyamaza, lakini kilio chake cha kutetea ukweli kiliendelea.

Alipotoa hotuba kwenye msikiti wa Mtume, watu waliyasikia maneno yake. Alipozungumza kuhusu masuala yanayohusiana na makatazo ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hotuba yake ilisisimua nyoyo za watu wa kawaida. Watu walizidi kuudhika kwa sababu ya matendo maovu na shughuli za Uthman zilikuwa kinyume na Uislamu. Kwa hiyo, kisiasa aliona inafaa kumtoa nje ya mji. Katika kutekeleza lengo hili alimpeleka Syria. Labda alidhani kwamba kwa kuwa Muawiyah alikuwa Gavana wa Syria na pia mwerevu sana, Abu Dharr angepooza kabisa huko.

Kufuatana na uamuzi wake, Uthman alimlazimisha Abu Dharr kwenda Syria.

Abu Dharr aliondoka na kuacha maskani yake akiwa na familia yake na akafika Syria. Kufika kwake Syria ni tukio liliolothibitisha utabiri wa Mtume (s.a.w) ambao alitamka mbele ya Abu Dharr walipokuwa katika mazungumzo siku za nyuma. Kufuatana na ushawishi wa Mtume alioonesha uvumilivu na alikubali uhamisho wake bila ubishi (al-Ghadir Allamah Amyn, Juz. 8, uk. 302).

Abu Dharr alikwisha choshwa na kuchukizwa na mwenendo wa Uthman uliokiuka mafundisho ya Kiislamu, lakini alipofikia Syria na kuona tabia ya Muawiyah ambayo ilikuwa inaharibu Uislamu, alishangaa sana na akajisemea peke yake kwamba mfumo wote wa utawala ulikuwa mbovu. Alilazimika kufikiria kuhusu mtindo wa maisha ya Muawiyah kwamba Uislamu kama ulivyo dhihirishwa na Mtume si tu ulikuwa unadhoofu lakini ulikuwa unazimwa.

Kufuatana na hali hii, hisia zake za kawaida zilisisimuka.

Alilazimika kuanzisha tena kilio cha ukweli kufuatana na sifa zake za uaminifu na kusema kweli. Kwa kuwa alikuwa jasiri sana, hakusita kusema kweli; kwa hivyo, bila kufikiria kwamba Muawiyah alikuwa ndiye mtawala wakati huo, alianza kufanya kazi zake za Kiislamu na akaanza kusema kwa lengo la kumzuia Muawiyah. Alimwambia wazi kwamba alikuwa anaendesha utawala kinyume na Uislamu kama ule wa Uthman bin Affan. Alamah Subaiti ameandika kwamba Uthman alipochukua hatua ya kumhamisha Abu Dharr na kumpeleka Syria ni uthibitisho wa uhakika wa kweli kwamba alikuwa anakwepesha msimamo wa ukosoaji wa Abu Dharr kutoka kwake kwenda kwa Muawiyah (Abu Dharr al-Ghifari).

Mwandishi wa historia Balazari, Allamah Majlis, Allamah Subaiti na Allamah Amyni wameandika kwamba Abu Dharr alipofika Syria Muawiyah alikuwa anajenga Ikulu yake ‘al-Khizra.’ Maelfu ya vibarua walikuwa wanafanya kazi hapo.

Siku moja Muawiyah alikuwa anaiangalia Ikulu hiyo kwa majivuno. Abu Dharr akamuona, akamkaribia, na akasema, “Ewe Muawiyah! Endapo Ikulu hii inajengwa kwa kutumia hazina ya Taifa ni uvunjaji wa uaminifu na endapo inajengwa kwa fedha yako binafsi ni ubadhirifu.”

Aliposikia hivi Muawiyah alinyamaza kimya, aligeuza uso wake na kutazama upande mwingine na hakujibu. Abu Dharr aliondoka na akafika msikitini. Alitafuta nafasi akaketi. Baadhi ya watu walilalamika kwa Abu Dharr kuhusu Muawiyah kwa kusema kwamba hawajapata chochote katika zawadi ambazo hutolewa na sasa mwaka umepita.

Abu Dharr aliinamisha kichwa chake kuelekea mbele halafu akasimama. Watu walimwangalia.
Akasema; “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, bidaa za namna hii zinaenea siku hizi kwani hazipo kwenye Quran Tukufu au Hadith za Mtume. Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, nimeona kwamba ukweli unadumazwa na uwongo unazidi kuwa na nguvu. Watu wakweli wanasingiziwa kuwa waongo na waovu wanapewa upendeleo kuzidi waadilifu.

Enyi watu wakuu! Ewe Muawuyah na magavana wake! Wasikitikie masikini. Wale wanaokusanya dhahabu na fedha na hawatumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanajua kwamba nyuso zao, pande zote na migongo yao itapigwa chapa ya moto. Enyi mnaohodhi utajiri! Hamjui kwamba mtu anapokufa kila kitu hufarakana naye. Vitu vitatu tu hubaki naye; sadaka ya kudumu, elimu yenye manufaa, na mtoto mwema, ambaye humwombea yeye.”

Watu walisikia mhadhara wake wanaogandamizwa na masikini walikusanyika kumzunguka yeye na matajiri wakaanza kumuogopa. Habith bin Muslim Fahri alipoona kundi la watu karibu na Abu Dharr alisema, ‘Hali ni kero kubwa!” alikwenda kwa Muawiyah haraka na akamwambia; “Ewe Muawiyah! Abu Dharr atavuruga kabisa utawala wa Syria. Endapo unawahitaji watu wa Syria, lazima uzuie usumbufu huu kabla haujakomaa.Muawiyah alitafakari jambo hili peke yake.

“Nimshughulikie kwa ukali au kwa upole? Nikitumia ukali moto utawaka na kuenea. Je, Ni lazima nilalamike kwa Uthman? Lakini, Uthman atasema nini? “Atasema kwamba sikuweza kumfanya atengamae hata mtu mmoja miongoni mwa raia wangu. Kwa hiyo ni vizuri zaid kumwondoa Syria.”

Imekuwa ni mazoea ya kawaida kukandamiza kwa ukali maneno ya kweli ya watu wa kimungu kwa sababu ya uchungu wao. Ingewezekana wapenda dunia wanyamaze baada ya kusikia hotuba za Abu Dharr zenye hamasa ya kidini hilo ni la kawaida. Lakini inawezekanaje mtu ampende Muawiyah, baada ya ushauri wa Abu Dharr na angewezaje kuvumilia maneno yake makali?

Abu Dharr alitumia sauti ya kunasihi na alikuwa na desturi ya kukariri Aya ya Qurani:

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنْفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ{34}

“Na wanaokusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii kwa njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie habari ya adhabu iliyo chungu.” (Quran 9:34).

Na ilikuwa ni kawaida yake kwamba alikariri aya hii dhidi ya Muawiyah mwenye mitaa mingi zaidi na barabara za Syria. Kila alipokiariri Aya hii, masikini na wenywe kuhitaji wakimzunguka yeye na mara nyingi walimlalamikia kuhusu magavana wanaotafuta anasa za utajiri na umasikini wao.

Muawiyah alikuwa na kawaida ya kupata taarifa ya mahubiri yake mara kwa mara. Hatimaye alimwekea mipaka mikali na kumtesa kwa kila njia. Ilipoonekana kwamba hata hatua hii haikufaa, alimtishia Abu Dharr kwa kifo.

Abu Dharr aliposikia tishio hilo la kifo alisema, “Ufalme wa Muawiyah unanitishia mimi kwa umasikini na kifo. Ninapenda kuwaambia kwamba umasikini ni wa kutamanika zaidi kwangu kuliko utajiri, na ninapenda kuwa chini ya ardhi kuliko kuwa juu yake.

Wala siogopeshwi kwa tukio la kifo, ama kifo chenyewe.”

Allamah Majlisi ameandika kupitia kwa mamlaka ya Shaykh Mufid watu wa Syria walisema nini kuhusu hotuba nzito za Abu Dharr; “Uthman alipomhamisha Abu Dharr kutoka Madina kwenda Syiria, aliishi miongoni mwetu, na akaanza kuhutubia mlolongo wa hotuba ambazo zilitusisimua sana.

Alikuwa na mazoea ya kuanza hotuba yake kwa kumsifu Mwenyezi Mungu na Mtume na halafu alisema; “Kuwapenda uzao wa Mtume (s.a.w) ni wajibu wa kila mtu. Yule asiye wapenda hawa hatanusa hata ile harufu ya Pepo.”

Halafu aliongeza; “Enyi watu! Nisikilizeni. Nilikuwa na kawaida ya kuheshimu maagano yangu kabla sijakubali Uislamu, wakati wa ujahiliya kabla ya wahyi wa Quran na kabla ya kuteuliwa kwa Mtume. Alisema kweli, niliwafanyia wema majirani zangu, niliona kwamba ukarimu ni wajibu wangu, nilikuwa nawakirimu masikini, na niligawia utajiri wangu.

“Baadaye, Mwenyezi Mungu alipoleta ufunuo wa Kitabu chake na akamteua Mtume wake, niliulizia kuhusu mambo haya nikatambua kwamba ni namna na desturi zile zile tulizokuwa tunazitumia sisi, pia zilikuwepo kwenye nasaha za Mtume.

“Enyi watu! Inafaa zaidi Waislamu kuwa waadilifu. Ni kweli kwamba Waislamu walifuata mwenendo kufuatana na mafundisho ya Uislamu, lakini rafiki zangu! Tabia ya Waislamu ilikuwa njema kwa kipindi kifupi. Halafu ilitokea kwamba madhalimu walionesha matendo maovu ambayo tulikuwa hatujayaona kabla yake. Watu hawakuharibu Sunna za Mtume, walianzisha bidaa, walimpinga mtu aliyesema kweli, wakaungana na kundi la watu waovu na kuwaacha wale waliokuwa wacha Mungu na wanaofaa.

“Ewe Mwenyezi Mungu! Ichukue roho yangu endapo unayo mambo mazuri kwa ajili yangu kuliko haya yaliomo katika dunia hii, kabla sijapotosha imani Yako au kubadili Suna za Mtume Wako.”

‘Enyi watu! Shikamaneni na ibada ya Mwenyezi Mungu na mjiepushe na dhambi.” Halafu akaelezea sifa za Ahlul Bait ambazo alizisikia kutoka kwa Mtume na akawashauri watu waambatane na Ahlul Bait.

Watu wa Syria wanasema kwamba walisikiliza hotuba zake kwa umasikini sana na kundi kubwa la watu lilikusanyika kumzunguka yeye alipokuwa anahutubia, hadi Muawiyah akamtaarifu Uthman kuhusu matukio haya, kwa hiyo, alimwita Abu Dharr aende Madina.

Kwa kuwa Abu Dharr alimuudhi sana Muawiyah kwa mihadhara yake ya kidini, yeye, katika jitihada ya kumnyamazisha kwa vyovyote vile alifanya ujasiri wa kumpelekea mfuko wa fedha kwa sababu hakuweza kufikiria njia nyingine yoyote ya kufanya.

Wasomi na waandishi wa historia wanasema kwamba Muawiyah alimpelekea Abu Dharr mfuko wa dinari za dhahabu mia tatu zilizopelekwa na mjumbe ili kumnyamazisha. Alipoona hivi alisema, “Mwambie Muawiyah kwamba sihitaji fedha yoyote kutoka kwake,” na akarudisha mfuko huo. (al Ishtiraki az-Zahid, Tarikh Balazari, al-Ghandir, Juz. 8, uk. 293).

Abu Dharr aliona kwa macho yake baada ya kifo cha Mtume matukio yote hayo ya hatari ambayo Ale Muhammad (Uzao wa Mtume) walilazimishwa kupambana nayo.

Alisema wazi dhidi ya kuhodhi utajiri, kwani alikwisha elewa kwa ukamilifu, lengo la Hazina ya Taifa na madhumuni ya Qurani Tukufu, aliona namna ya utendaji wa Mtume na alikuwa anachunguza mwenendo wa maisha ya uzao wa Muhammad.

Alipoona tabia na namna ya maisha ya wale wenye madaraka ya Ukhalifa ni kinyume kabisa na Suna hizi, alihisi wasi wasi sana kwa sababu ya imani yake kuwa imara. Kamwe alikuwa hajafikiria yale aliyoyaona kwa macho yake. Mara tu baaada ya Uthman kushika hatamu ya serikali na Ukhalifa, alilazimisha hisia zake kutoka kwanye moyo wake na kuzipeleka mdomoni mwake na alilazimika kifichua kile alichokificha moyoni mwake kwa muda mrefu.

Aliona kwamba utajiri uliongezeka kuliko alivyofikiria, upendeleo na fadhila kwa ndugu ni mambo ambayo yalifika upeo wa juu sana, utajiri wa Hazina ya Taifa ulikuwa inagawiwa kwa ndugu, marafiki na wanaomunga mkono badala ya watu wanaostahili, bila hata kufikiria , na kwa sababu ya utajiri huu bida zilizokuwa zinatikisa misingi ya Uislamu, zilikuwa zinaongezeka bila ya kuzuizi.

Kwa hiyo, kufuatana na mkataba wa uaminifu aliofanya na Mtume, alianza kukataa na kuwakosoa wale wenye kuwajibika, ambayo matokeo yake alihamishwa Madina na kupelekwa Syria. Huko aliona bidaa nyingi za kutafuta starehe ambazo zilikuwa zinapingana na Uislamu na ambazo zilizidi hata njia za maisha ya anasa za Kaisari (wa Roma)na Khussoe (Shah wa Uajemi).

Kwa kuwa alilazimishwa na amri ya Mtume, na ahadi iliyofanywa kwake, na pia kwa uimara wake, wa kidini alianza pia kuhubiri huko. Alianza kuhadhiri huko Syria chini ya mwongozo wa Aya ile ile ya Quran ambayo ilikuwa kiini cha hotuba zake Madina. Katika uhusiano huu, alihutubia hotuba nyingi, baadhi ya hizo zimetajwa kwenye kurasa za nyuma.

Maelezo ya hotuba yake ya kushutumu kuhodhi utajiri ilikuwa Aya ifuatayo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۗ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنْفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ{34}

“Enyi mlioamini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki wanakula mali za watu kwa batili na wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie habari ya adhabu iliyochungu. Siku zitapotiwa moto katika Moto wa Jahanamu, na kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa; Haya ndio mliyojilimbikizia nafsi zenu, basi onjeni mliyokuwa mkilimbikiza.” (Qurani 9:34).

Wasomi na waandishi wa historia wanasimulia kwamba alipokuwa anahutubia kundi huko Syria, alisema; “Kwa jina la Mwenyezi Mungu! Ninaamini kwamba kweli utaangamia, udanganyifu unaendelezwa, watu wa kweli wanawekewa pingamizi na watu wanaendekeza uchoyo badala ya uchaji Mungu.” (al-Balazari, Juz. 5, uk. 56).

Aliendelea kusema; “Dhahabu na fedha zitageuka kuwa miale ya moto na zitawazunguka wale wanaoziweka kwa kuzifungia hadi wazitumie katika njia ya Mwenyezi Mungu.” Akisisitiza jambo hili alisema; “Vipande vilivyochomwa moto wa Jahanamu vitawekwa kwenye vifua vya wale wanaokusanya dhahabu na fedha, hadi vitoboe mbavu zao na mifupa ya mabega yao.” (Sahih Bukhari-Kitab az-Zakat).

Abdul Hamid, mwandishi wa Misri ameandika kwamba Abu Dharr alipowasili kwenye msikiti watu walikusanyika na kumzunguka na akawaambia; “Tumieni chochote ambacho Mwenyezi Mungu amewapeni. Tahadharini sana hivyo kwamba maisha ya dunia yasiwadanganye. Weka fungu la rasilimali yako liwe haki ya wasio nacho. Mtume amesema kwamba tama ya wingi wa rasilimali imefanya mzame kwenye kusahau.”

Mwanadamu anasema; “Mali yangu! Mali yanngu! Lakini mali yako ni ile ambayo umekula imeksisha au umetoa sadaka; kwa maana kwamba umeweka kwa lengo la kuhifadhi. Mwenyezi Mungu amezuia kuhodhi mali.

“Mtume amesema; “inasikitisha, inasikitisha dhahabu na fedha,” Ngawira ni haki ya Waislamu, lakini Muawiyah amehifadhi na kuitumia kwa watumishi na walinzi wake na kwa ufahari na maonesho yake. Muawiyah amesahau kwamba ni majoho mawili tu yanaruhusiwa kwake kutika kwenye hazina ya Taifa, moja kwa alili ya majira baridi na lingine kwa ajili ya majira ya joto. Zaidi ya hayo, anaweza kuchukua matumizi ya Hijja na familia yake tu kama ambavyo familia ya tabaka la kati ya Quraishii inaweza kuchukua.

“Ngawira lazima igawanywe kwa miongoni mwa Waislamu wote walio masikini. Lakini, sasa ardhi inatwaliwa, na nyumba zinajengwa, na maelfu ya dinari yanatumika katika kuziremba nyumba hizi na Waislamu walio masikini wanatelekezwa.”

Mtu alimnong’oneza sikioni mwake, “Tafadhali! Unasema nini kuhusu Muawiyah? Humuogopi?”

Abu Dharr alimjibu na kumwambia; “Rafiki yangu alinishauri niseme kweli, hata kama inaumiza, na bila kujali shutuma za anayeshutumu, ambapo nipo kwenye njia iliyonyoka. Ninamuomba Mwenyezi Mungu anilinde nisiwe na uoga, ubakhili na ujinga.” Halafu akaongeza, “Watu wameanza kupika vyakula vya aina tofauti, na wanatumia dawa ili visagwe.

Mtume wetu hakula chakula cha aina mbili kwa wakati mmoja hata siku moja hadi mwisho wa uhai wake. Kama alikula tende hakula mkate. Wazao wa Mtukufu Mtume kamwe hawakula mkate wa shayiri hadi kushiba kwa siku tatu mfululizo hadi mwisho wa uhai wao. Nyumbani kwa Mtume (s.a.w), mara nyingine ilitokea moto haukukokwa, ama mkate, ama chakula cha aina nyingine kilipikwa mfululizo kwa mwezi moja.”

Mtu mmoja aliuliza, “Aliwezaje kuwa hai Abu Dharr akajibu; “Mtukufu Mtume alikula tende na kunywa maji. Alisema kwamba hakuna mtu aliyeona chombo kibaya sana kuliko tumbo lake.

“Vipande vichache tu vinamtosha mtu kuwa hai. Endapo ni muhimu kula, theluthi moja ya tumbo liwe wazi kwa ajili ya chakula, theluthi moja kwa ajili ya maji na iliyobaki iwe kwa ajili ya hewa. Mtume ametushauri kwamba tusile chakula kupita kiasi kwa sababu hutengeneza ulegevu, huharibu mwili na kumhusisha mtu na magonjwa.

“Uwe na ulinganifu unaostahili katika mlo kwa sababu utaepukana na israfu, mwili utakuwa na nguvu na husaidia katika ibada. Mtume kamwe hakukusanya au kuhodhi kitu chochote. Kinyume chake, alikuwa akitoa sadaka chochote alichopata, hivyo kwamba hakuna kilichobaki kwa ajili ya mlo wake. Bila kuhusisha Hazina ya Taifa Mtume alikuwa anatoa hata mgao wake kama sadaka.”
Makabaila walimsihi Muawiyah na wakalalamika kuhusu propaganda ya Abu Dharr. Muawiyah alimwita na akamwambia kuhusu azimio imara la kuondosha tishio hili ambalo lilitikisa misingi ya serikali yake na kuvunja matumaini yake.

Abu Dharr aliingia kwenye baraza la Muawiyah akiwa na mwili mwembamba na mkondefu. Dalili za ushupavu na uimara zilionekana kwenye uso wake wa mviringo alisimama kumkaribisha na akamwonesha mahali pa kuketi karibu na yeye. Halafu akawaita watumishi na akawagiza walete chakula. Nguo ya chakula ilitandikwa na vyakula vya aina nyingi mbali mbali ambavyo vilizidisha ladha, vilitayarishwa.

Muawiyah akamwambia Abu Dharr, “Ndio, tafadhali.” Abu Dharr alikataa na akasema, “Mimi ninakula kilo mbili za ngano kwa juma moja. Haya yamekua mazoea yangu tangu uhai wa Mtume. Kwa jina la Mwenyezi Mungu sitafanya chochote kuzidi hapo hadi nitakapoungana naye.”

Halafu akamgeukia Muawiyah akamwambia, “Umebadili mwenendo wako chakula kinachotayarishwa kwa ajili yako sasa, sio kama kile cha zamani. Unakula mkate uliopikwa unga mzuri, unakula vyakula vya aina kadhaa kwenye mlo moja na unavaa nguo tofauti na ile ya jioni. Wewe hukuwa na tabia hii wakati wa uhai wa Mtume. Hali yako haikuwa tofauti na ile ya mtu masikini.” (Sahih Muslim, Sunan Nisai na Sunan Baihaqi).

Muawiyah; “Maafisa wangu wanalalamika kuhusu wewe. Wanasema kwamba unawachochea masikini wawachukie wao.”

Abu Dharr; “Ninawazuia wasihodhi.” Muawiyah; “Kwa nini unafanya hivyo?”

Abu Dharr: “Ninafanya hivi kwa sababu Mwenyezi Mungu amesema; “Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie bahari ya adhabu iliyochungu.” (Qurani 9:34).

Abu Dharr; “Ewe Muawiyah! Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sitaacha hadi hapo utajiri utakapowagawia masikini.”

Vyovyote vile, matatizo yalimzunguka Abu Dharr pande zote. Mateso makubwa yalimpata kutoka kwa Bani Umayyah. Aligandamizwa sana. Lakini hakuonesha udhaifu wowote na hakuacha kuhubiri. Sasa alianza mashambulizi makali zaidi.

Abdullah Subaiti, Abdul Hamid Misri na Manazir Ahsan Gilani wanasema kwamba Abu Dharr aliendelea kufanya kazi ya kuhubiri mara kwa mara na akiwaonya kuhusu adhabu kali kwa wanaohodhi. Hatimaye Muawiyah akaanza kufikiria mipango ya kujinasua kutoka kwenye michomo ya maneno yake na kuzuia utekelezaji wa malengo yake. Hata hivyo, aliamua kwamba pangeweza kuwepo fursa ya kuwa huru kutokana na mashambulizi endapo tabia ya kuhodhi mali inaweza kuthibitishwa na wale wanao ishambulia. Kwa hiyo, alipata mpango, na aliridhika kwamba mpango huo ungefanya kazi iliyokusudiwa.

Bin Athir baada ya kutaja Aya za Qurani, ameandika kwamba ilipoonekana si rahisi kumnyamazisha Abu Dharr kwa namna yoyote ile, Muawiyah alimtuma mtu na dinari elfu moja kwenda kwake wakati wa usiku. Abu Dharr alizichukua fedha hizo na akazigawa kwa masikini kabla ya alfajiri na hakubakisha hata sarafu moja kwa ajili ya matumizi yake.
Muawiyah, alimwita mtu aliyepeleka sarafu za dhahabu kwa Abu Dharr, baada ya Swala ya alfajiri, akamuamuru aende kwa Abu Dharr na amwambie kwa kujifanya anao wasi wasi, “Ewe Abu Dharr! Niokoe kutokana na mateso ya Muawiyah. Muawiyah aliniamuru nipeleke hizo sarafu za dhahabu kwa mtu mwingine lakini mimi nimekuletea wewe kwa makosa.”

Mjumbe wa Muawiyah alikwenda kwa Abu Dharr na kumwambia kama alivyoagizwa na Muawiyah. Abu Dharr akasema, “Ewe mwana! Mwambie Muawiyah kwamba fedha alizoniletea nilizigawa kwa watu wanaozihitaji kabla alfajiri leo. Sina hata sarafu moja sasa hivi na kama anataka fedha hizo zirudi kwake, atalazimika kunipa siku tatu, ambapo nitazipata fedha hizo kutoka mahali pengine ili nimrudishie.”

Mtu huyo alirudia taarifa hiyo kwa Muawiyah kama alivyoisikia kutoka kwa Abu Dharr, ambaye alisema, Bila shaka Abu Dharr hufanya yale ambayo huwaambia wengine wafanye.” (Tarikh kamil, Juz. 3, uk. 24, tafsir bin Kathir, sehemu ya 10, uk. 34).

Abdullah Subaiti, baada ya kunukuu tukio hili ameandika katika maelezo ya kifalsafa kwamba Abu Dharr alikuwa mtu mwenye tabia ya hali ya juu sana. Bani Umayyah walionesha kutokuwa na uwezo wa kuona mbali kiakili katika kumweleza yeye. Ndio sababu waliona umuhimu wa kufanya utapeli wa kisiasa.

Abdul Hamid Misri ameandika baada ya tukio hili. Muawiyah alielewa kwamba Abu Dharr alikuwa mkweli kwa maneno yake. Alitumia dinari zote kwa usiku moja. Muawiyah alishindwa kutimiza lengo lake. Alionesha huruma kwa Abu Dharr lakini haikufaa kitu. Halafu akatumia nguvu dhidi ya Abu Dharr lakini hakuathirika. Hatimaye akataka amnunue kwa dinari mia tatu, lakini hakufaulu. (Abu Dharr al-Ghifari, Uk. 133).

Kwa mujibu wa wasomi na waandishi wa historia, Abu Dharr alikuwa bado yupo Syria Muawiyah alipotuma jeshi kwa ruhusa ya Uthman kwa vita vya majini (Tarikh Abul Fida).

Abu Dharr alikuwa anashughulika na kazi yake. Baada ya vita hiyo kwisha, Muawiyah akamwagiza Abul Darda, Umar bin al-Aas, Ubadah bin Samit na Umme Hizam, ambao walikuwa masahaba wa Mtukufu Mtume waende kwake.

Walipofika, Muawiyah aliwaambia; “Nimechoka kumwonya Abu Dharr lakini hataki kunisikia. Inanisumbua. Nyinyi pia mmepewa heshima ya kuwa masahaba wa Mtume kama Abu Dharr alivyo. Nendeni kwake na mwambieni aache shughuli zake na aishi maisha ya kimya na utulivu. Nimechoshwa sana na mtu huyu na pia watu matajiri wa nchi hii.”

Watu hawa walikubali haraka sana kwamba wangekwenda kwa Abu Dharr na wangemwomba afanye kama ilivyoagizwa na Muawiyah. Kwa hiyo, walikubaliana kwa pamoja kuhusu mpango fulani na wakamtembelea. Wakamwambia Abu Dharr; “Tumekuja kwa niaba ya Muawiyah. Ametutuma tuje kwako na ombi kwamba uache mahubiri yako na uendeshe maisha yako kwa amani.”

Aliposikia hivi, Abu Dharr alikasirika. Alifikiria kwamba watu hao waliyaona mahubiri yake ni halali kabisa na walijua kwamba lolote alilokuwa anafanya liliendana na Radhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na bado walikwenda kwake kwa amri ya Muawiyah.

Kwanza kabisa alimwambia Ubadah bin Samit; “Ewe Abul Walid Ubadah! Hapana shaka kwamba unanitangulia mimi kwa kila namna na unanizidi kwa ubora katika kila njia. Wewe ni mkubwa kwa umri na umekuwa pamoja na Mtume kwa kipindi kirefu zaidi. Unazo busara, akili, unajua sana mambo ya dini na utu wako ni bora. Lakini ninasikitika kusema kwamba licha ya kujua kila kitu sawa, umekuja kunishauriu mimi ombi la Muawiyah.

“Ewe Ubadah! Kwani sielewi mambo? Hivi nimepoteza akili ya kuhoji. Hutambui hali ya mambo? Haya ninayo si sahihi? Nasaha zangu haziendani na nia ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake? Ewe Ubadah! Iliniuma sana kwamba wewe ni mtu mwenye akili, unajua kila kitu sana, unakuja kwangu kunishauri mimi. Sikiliza! Ninayo chuki kubwa kwa sababu mtu mwenye kuelewa mambo kama wewe umejumuika kwenye ujumbe huu.”

Halafu akamgeukia Abu Darda na akasema; “Ewe Abu Darda! Umepewa neema ya kumpenda Mtume angalau kidogo. Ilikuwa wazi kwako kwamba endapo hungekubali haraka, hungepewa heshima ya usahaba kwa sababu ya kifo cha Mtume. Lakini uliikubali imani, ukapewa heshima ya usahaba, na ukafikiriwa kuwa sahaba mzuri. Lakini sikiliza! Wewe hukufaidika na usahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w) kama nilivyofaidika mimi. Wewe huwezi kuelewa malengo yake kwa kiasi ninachoelewa mimi. Ninayaelewa malengo ya Mtume na ninafanya kufuatana na utashi wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Kwa hiyo, huna haki ya kunishauri mimi.”

Halafu akaanza kuzungumza na Umar bin Aas kwa kumwambia kwa sauti ya ukali; ‘Ewe Umara bin Aas! Ninakutambua wewe vizuri sana. Umefanya nini zaidi ya kushiriki kwenye vita? Kama hali ilivyo, ulipewa heshima ya usahaba wa Mtukufu Mtume lakini kwamwe hukupata nafasi ya kuishi na yeye. Kila mara ulikuwa mbali na Mtume (s.a.w) kwa sababu ya vita. Wala huwezi kuelewa nia yake ama kuwa na uwezo wa kutosha kuunda maoni sahihi kuhusu matendo na tabia yangu. Ninajua kwamba wewe upo kwenye mvuto wa Muawiyah wakati huu ndio maana umekuja kuniona mimi bila kufikiria kwanza.”

Halafu akamgeukia Ummu Hizam na kusema; “Nikwambie nini wewe? Wewe ni mwanamke, kwa kiwango chochote kile, na unazo akili za kike.” Halafu akasema; “Nendeni mwambieni Muawiyah aone akili zake, aendeshe mambo kufuatana na ushauri wangu na asipoteze imani kwa ajili ya dunia.”

Waliposikia mambo yote haya, wote walinyamaza kimya. Baada ya muda mfupi waliondoka kwa Abu Dharr na kurudi kwa Muawiyah. Walimwambia kwamba walifikisha ujumbe kwa Abu Dharr. Aliwauliza walichosema na majibu waliyopewa na Abu Dharr. Ubadah bin Samit alirudia tukio lote na mwishowe akasema, “Kamwe sijawahi kukaa mahali ambapo shutuma kali kama hizo zinatolewa kwa wazi sana.” (Musnad bin Hanbal, Masanid Abu Dharr).

Abu Dharr alikuwa anashughulika na mahubiri huko Syria wakati wa Hija ulipofika. Aliomba ruhusa kutoka kwa Uthman na kusema alitaka kutoka nje ya Syria aende kuhiji na akae kwenye kaburi la Mtukufu Mtume (s.a.w) kwa muda wa siku chache.

Uthman akampelekea barua ya ruhusa kutoka Madina na Abu Dharr akaenda Hija. Alifanya ibada ya Hija na akaenda Madina. Alikaa karibu na kaburi la Mtume kwa siku chache na halafu akarudi Syria. Balazari pia amesimulia tukio hili kwa sentenso chache.

Aliporudi kutoka Hija akaanza tena shughuli yake ya kuhubiri. Kwa upande moja alikuwa anatumia nguvu zake zote katika kutoa nasaha na kwa upande mwingine maombi mengi sana yalikuwa ya watu matajiri yalikuwa yanamfikia Muawiyah kwamba akomeshe kelele za Abu Dharr. Kiini cha maombi haya ni kwamba watu walikuwa wanakariri mitaani na barabarani Aya ya Qurani ambayo inawaonya watu wenye fedha ambao wanapigwa chapa kwa dhahabu na fedha iliyochomwa moto, kwa hiyo inakuwa vigumu wao kupita kwenda Syria. Na matokeo yake ni kwamba Muawiyah alitangaza kwamba hakuna mtu yeyote kuwasiliana kwa namna yoyote na Abu Dharr (Tabaqati ya bin Sad uk. 176).

Abu Dharr alipopata taarifa ya kususiwa kijamii, yeye mwenyewe alianza kuwaambia watu wasiende kwake au kuketi naye. Hii ni kwa sababu alidhani kwamba endapo mtu alikwenda kwake angeteswa na serikali. Lakini kwa kuwa yeye ilimwia vigumu kuacha kuhubiri, yeye mwenyewe alikwenda kwenye mikusanyiko ya watu na akaanza kufanya kazi yake.

Kwa mujibu wa bin Khaldun, kundi la watu lilipokwenda kumuona baada ya amri ya kumsusa, Abu Dharr aliwaambia watu hao waondoke na yeye abaki peke yake. (Tarikh bin Khaldun uk. 27).

Inaonyesha kutoka kwenye taarifa ya Balazari kwamba watu hao waliofanya mawasiliano na Abu Dharr na kusikiliza hotuba zake, walishughulikiwa kwa ukali zaidi kuliko hata Abu Dharr mwenyewe (Tarikh Balazari, Juz. 5, uk. 65). Abu Dharr alikuwa jasiri kiwango gani! Hakuvumilia ukatili wowote kwa wale waliokuwa wanamwendea, na hakutaka watu hao wapate usumbufu wowote. Lakini almuradi hisia zake za moyoni zilimpa msukumo, alisisitiza kuendelea kuzisoma kwa watu kwa imani na hamasa kamili.

Yeye hakujali kuhusu mafanikio au hasara yoyote katika njia ya Mwenyezi Mungu.