Sura Ya Kumi Na Tisa

Waandishi wa historia wanasema kwamba Abu Dharr alitoa hotuba zake kuhusu mada maalum. Msikitini, nje ya msikiti, kwenye baraza, kwenye viwanja vya maonyesho ya michezo, mitaani na mahali popote alipopata fursa ya kufanya hivyo. Hakuogopa kuuawa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu alikwisha mwambia kwamba hakuna mtu ambaye angeweza kumua au kumfanya aache imani yake wala hakuogopa shutuma kwa sababu aliapa mbele ya Mtukufu Mtume kuhusu suala hili. Alikuwa na uhakika kabisa kwamba lolote alilofanya ilikuwa linakubaliana na utashi wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Ndio sababu alikuwa anashughulika wakati wote katika kutekeleza kazi yake kwa ujasiri na hamasa kubwa.

Kwa upande moja mahubiri ya Abu Dharr yalizidi kupamba moto na kwa upande mwingine Uthman alikuwa anaendelea na zoezi la kuipima dhamiri yake kwenye kioo cha tabia yake mwenyewe. Alitaka ushauri kutoka kwa Marwan ili aweze kujua Abu Dharr angenyamazishwa kwa njia gani na shutuma zake kuhusu tabia ya Uthman na upinzani wake kuhusu kuhodhi utajiri ungesitishwa.

Marwan akasema, “Ipo njia moja tu ya kuweza kufanikiwa ni kwamba, kiasi fulani cha fedha kipelekwe kwa Abu Dharr. Labda anaweza akakubali na kunyamaza.” Uthman alisikia jibu hili la Marwan na akanyhamaza. Sababu ya kimya chake ni kwamba alikuwa anatambua tabia ya Abu Dharr. Alijua kwamba Abu Dharr alikuwa hana tama ya fedha. Marwan aliwaita watu wawili, akawapa mfuko wenye dinari mia mbili na akasema, “Mpelekeeni Abu Dharr na mwambieni kwamba Uthman anamtakia kila la kheri na amemwomba akubali kuchukua mfuko huo wa fedha na atumie apendavyo.”

Watu hao walikwenda kwa Abu Dharr usiku wakiwa na huo mfuko wa fedha. Wakati huo alikuwa anasali msikitini. Labda alikuwa anakaa kwenye msikiti wa Mtume wakati huo kwa sababu Uthman alimuita kwa lazima kutoka Syria ambapo familia yake ilikuwa bado huko.

Akiwatazama wageni, Abu Dharr aliwauliza wao walikuwa nani na walikuwa na madhumuni gani? Wakampa mfuko wa fedha na wakasema, “Khalifa Uthman amekupa salamu zake na anakuomba ukubali kuchukua hizi dinari mia mbili kwa ajili ya matumizi yako.” (Kashkol Bahai).
Abu Dharr akasema, “Je! Amegawa kiasi kama hiki kwa Muislamu mwingine pia?” Wakajibu, “Hapana, hajampa yeyote. Huu ni ukarimu wa Khalifa kwako peke yako.

“Tafadhali rudusha.”Abu Dharr akasema, “Mimi pia ni mmojawapo wa Waislamu ambapo Khalifa hajampa Muislamu yeyote, mimi peke yangu siwezi kukubali kuchukua. Mimi sihitaji fedha ambapo Waislamu wengine masikini hawakupata. Nendeni, mrudishieni na mwambieni kwamba mimi ninatosheka na ngano kidogo tu, mimi hupata ujira wa riziki yangu. Nifanye nini na dinari hizi?” (Abu Dharr Ghifari, uk. 126, na Hayatul Qulub Juz. 2, uk 1039).
Marwan alikosea kufanya uamuzi huo kuhusu Abu Dharr. Yeye alidhani kwamba kama vile watafutaji wengine wa dunia hawakujali imani na itikadi kwa ajili ya utajiri, Abu Dharr naye angefanya hivyo. Hakujua kwamba Abu Dharr alikuwa kwenye daraja la juu zaidi kulinganishwa na watafutaji wa dunia.

Tukiliangalia tukio hili kwa uangalifu, Abu Dharr alifuata kwa karibu sana nyayo za Mtukufu Mtume na Ali kwa kurudisha fedha na kwa kusema, “Maana yake nini kunipelekea fedha peke yangu na kutowajali Waislamu wengine?” Hawa (Mtume na Ali) ni watu ambao walijali kuwatumikia Waislamu zaidi kuliko kutumikia nafsi zao. Wao hawakutaka wawe wanabilingika kwenye utajiri ambapo masikini waendelee kuwa masikini. Wao hawakupenda kuwepo na hata ile tofauti ndogo baina yao na watu masikini. Kwa uthibitisho tunaweza kutoa mfano wa tukio la kufuturu kwa Ali kama ilivyosimuliwa na Ahnaf bin Qays mbele ya Muawiyah barazani kwake.

Kwa mujibu wa Mansur bin Husein Abi alikufa 422 A.H) kwenye kitabu chake Nass ud-Duras, kama ilivyo nukuliwa na Shaykh Muhammad husayn Ale Kashiful Ghita; Ahnaf bin Qays alisema, “Wakati fulani nilikwenda kwa Muawiyah. Aliweka mbele yangu vyakula vya aina nyingi mno. Nilikuwa bado ninashangaa ambapo aliweka mbele yangu chakula maalum ambacho sikuweza kukitambua. Nikamuuliza hicho kilikuwa chakula gani.

“Akajibu kwamba huo ulikuwa utumbo wa bata uliojazwa ubongo na kukaangwa kwenye mafuta na kunyunyiuzia viungo. Niliposikia hivi nilianza kulia. Muawiyah akaniuliza sababu ya kulia, nikamwambia kwamba nilimkumbuka Ali wakati huo.

“Siku moja nilikuwa na Ali ambapo muda wa kufturu ulifika. Aliniomba nisiondoke. Wakati huo huo mfuko ulio zibwa vizuri uliletwa. Nikamuuliza mfuko ulikuwa na nini. Akajibu kwamba huo ulikuwa unga wa shayiri iliyokaushwa . Nikamuuliza kwa nini mfuko huo ulizibwa kwa uangalifu kiasi hicho, ilikuwa ni sababu ya kuzuia usiibwe au matatizo ya kiuchumi. Akajibu kwamba haikuwa sababu yoyote kati ya hizo mbili zilizotajwa. tahadhari hiyo ilikuwa kuwazuia wanawe wasije wakachanganya unga huo na mafuta ya samli au michikichi.

“Niliendelea kuuliza endapo mafuta ya samli au mchikichi yaliharamishwa. Akajibu kwamba hayakuharamishwa. Bado, ilikuwa muhimu kwa viongozi wa umma kujiweka katika hali iliyo sawa na ile ya watu masikini, ili kwamba ukosefu wa njia za kujikimu isije ikawa sababu ya tabaka la watu masikini kugeuka kuwa waasi. Muawiyah akaniambia kwamba nilimkumbuka mtu ambaye uadilifu wake si rahisi kukanusha.”

Hata hivyo, wale waliopeleka mfuko wa dhahabu kwa Abu Dharr walirudi kwa Uthmani na wakamwambia alivyowaambia Abu Dharr. Uthman akamwambia Marwan, “Nilijua kabla kwamba Abu Dharr hangekubali kuchukua fedha hiyo.”

Abu Dharr aliendelea na shughuli yake ya kuhubiri kama kawaida. Kila alichosema haikuwa upinzani ulioelekezwa kwa mtu fulani pekee. Hakika, alitaka watu wasimsahau Mwenyezi Mungu kwa sababu ya kuhodhi fedha lakini kuimarisha kanuni za Uislamu kwa kuwahurumia masikini. Abu Dharr hakuweza kuvumilia kuona utajiri wa Hazina ya Taifa unatumika kwa kupewa watu wasiostahili bila sababu yoyote ambapo watu wanaohitaji wanateseka njaa.

Hakuvumilia hata kupasuliwa na kuchomwa Quran. Hakuchoka kuwashutumu wale ambao walikuwa na hatia kwa kufanya uhalifu kama hao.
Alikuwa nazo amri za Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Alikuwa anazingatia kanuni za Uislamu. Alitaka watawala Waislamu kufuata njia ya Uislamu.

Kwa ufupi, kwa upande moja Abu Dharr alikuwa anashughulika na kazi yake ya kuhubiri na kwa upande mwingine, Uthman alikuwa na shauku ya kupata njia ya kumnyamazisha.Katika kutimiza lengo hili alijaribu kushauri kila aina ya mpango lakini hakuweza kufaulu. Hatimaye alitoa amri katika tangazo la jumla, “Hakuna ruhusa mtu yeyote kukaa na Abu Dharr, wala kusema naye.” (al-Masud).

Agizo la mtawala lilitakiwa kutekelezwa bila masharti. Mara tu tangazo hili lilipofanywa watu waliacha kuwasiliana naye na wakaacha kusema naye. Watu waliondoka popote pale Abu Dharr alipopita kuepuka wasije wakashtakiwa kwa khalifa. Hakuna mtu aliyemsikiliza Abu Dharr wala kufika mahali alipokuwa. Lakini Abudhar alikuwa mtu jasiri aliyoje. Hakujali mambo haya. Alikuwa anasadiki kwamba lolote alilofanya lilikuwa linalingana na Radhi ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, alikuwa anaridhika kabisa na yale aliyokuwa anayafanya na hakuna sharti lolote ambalo lingefaulu.

Subaiti anasema kwamba licha ya tangazo, Abu Dharr aliendelea kuwapa nasaha watu kama kawaida. Kwa bidii sana hivyo kwamba humo Madina watu wa ukoo wa Umayyah ambao walikuwa waunga mkono wa Uthman, walichoshwa naye na wakalalamika kwa Uthman, kwamba Abu Dharr alikuwa hajaacha kuhubiri. “Sasa ametuchosha sana, kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na ufanywe mpango mwingine.”

Aliposikia hivi, Uthman aliamuru Abu Dharr apelekwe kwenye baraza lake.

Kwa amri ya Uthman watu wakamkamata Abu Dharr na kumpeleka kwa Uthman ambaye alisema, “Ewe Abu Dharr! Nimekuonya kwa kila njia lakini hutaki kuzingatia ushauri wangu. Nini kimekutokea?” Abu Dharr akajibu, “Laana iwe juu yako, ewe Uthman! Je, Mwenendo wako ni sawa na ule wa Mtukufu Mtume, au sawa na ule wa Abu Bakr bin Quhafa na Umar bin Khatab? Wewe unafanya mambo miongoni mwetu yale ambayo madhalimu hufanya.” Uthman akasema, “Sijui lolote. Toka nje ya jiji langu!”

Abu Dharr, “Mimi pia sitaki kukaa karibu na wewe. Sawa, niambie niondoke nielekee wapi?”

Uthman, “Nenda popote unapotaka lakini ondoka hapa!”
Abu Dharr, “Naweza kwenda Syria?”

Uthman, “Hapana, nimekuita na ukaburuzwa kutoka huko. Umewafanya watu wa Syria wanione mimi ni mkosaji kwao. Ninaweza kukupeleka huko tena?”
Abu Dharr, “Labda niende Iraq?”

Uthman; “Hapana, unataka kwenda ambako watu hawashutumu watawala wao?”
Abu Dharr, “Kama hivyo, niende Misri?” Uthman, “Hapana!”
Abu Dharr; “Niende Kufah?” Uthman, “Hapana.”
Abu Dharr, “Sasa niende wapi? Niende Makkah?” Uthman, “Hapana!”
Abu Dharr; “Ewe uthman! Hutaki mimi niende kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu! Kuna tatizo gani kwako endapo mimi ninakwenda huko na kumuabudu Mwenyezi Mungu hadi kifo changu?”

Uthman, “Hapana, kwa jina la Mwenyezi Mungu, kamwe!”
Abu Dharr, “Basi niambie niondoke niende wapi. Niende porini.”

Uthman, “Hapana”
Abu Dharr; “Basi nirudi kwenye siku zangu kabla ya Uislamu na niende kuishi Najd. Kwa vyovyote vile niambie mahali pa kwenda.”
Uthman, “Ewe Abu Dharr! Niambie ni sehemu gani unapenda zaidi zaidi.”
Abu Dharr, “Madina au Makkah au Jerusalem.”
Uthman, “Huwezi kuishi huko kwa vyovyote vile. Sasa niambie sehemu unayo ichukia kuliko zote.”

Abu Dharr, “Rabzah”
Uthman, “Vema, ninakuamuru uondoke uende Rabzah!”
Aliposikia hivi, Abu Dharr akasema; “Mwenyezi Mungu Mkubwa! Mtukufu Mtume alisema kweli kwamba yote haya yatatokea.” Uthman, “Mtume alisema nini?”

Abu Dharr, “Alisema Mtume kwamba, ningehamishwa kutoka Madina, ningezuiwa kwenda Makkah ningelazimishwa kuishi sehemu mbaya sana Rabzah ambapo ningeuawa na ningezikwa na kundi la watu wa Iraq ambao wangekuwa wanakwenda Hijaz.”

Aliposikia hivi Khalifa Uthman kwa mujibu wa Athan Kufi, alisema, “Nyanyuka ondoka kwenda Rabzah. Kaa huko na usiende popote.” Kwa mujibu wa Damah Sakibah Juz. 1, uk 194, aliteswa na kujeruhiwa sana. Halafu Khalifa akamuagiza Marwan ampeleke Rabzah akiwa amepanda ngamia asiye na tandiko la kukalia, na atangaze kwamba hakuna mtu atakaye ruhusiwa kumuona wakati anaondoka! (Murujudh Dhahab- Masud Juz. 1, uk. 438; Tarikh Yaqubi, Juz. 2, uk. 148; Tabaqati bin Sad, Juz. 4, uk 169. Hayat Qulubi, Juz. 2, uk. 1033; Majalisul Mumin, uk. 94, Tarikh Atham Kufi, uk. 131; Kitab al-Sufiyania, Abu Uthman Jahiz.

Haiwezekani kukanushwa kwamba kuhamishwa kwa lazima ni sawa na kuuawa. Wale wanaofukuzwa kutoka nchini kwao hupendelea zaidi kuuawa kuliko kuhamishwa. Matukio yanajieleza yenyewe kwamba watu waliofukuzwa kutoka kwenye nchi ya uzalendo wao kila mara walilia sana. Uzalendo ni zawadi ya viumbe vyote. Hadith zimeiita hali hiyo ni sehemu ya imani. Mtume Yusufu alikuwa na kawaida ya kulilia kwao alikozaliwa wakati ameketi kwenye kiti cha ufalme wa Misri.

Bila kutaja Mitume wengine, na tutafakari matukio ya Mtume Muhammad (s.aw). Alilazimika kuhama Makkah na kwenda Madina. Lakini kila alipokumbuka Makkah au alipowaona wakazi wa jiji hilo, macho yake yalijaa machozi. Loo! Abu Dharr alikuwa anafukuzwa kutoka kwenye mji wa nyumbani. Fikiria jinsi ambavyo alijihisi hususan alipokuwa anaondoka na kuacha kaburi la Mtume. Lakini hapakuwepo na uchaguzi wowote kwa sababu aliondolewa na kuhamishwa kwa mujibu wa mwandishi wa historia Tabari, ilikuwa ni utendaji wa Uthman kwamba alimfarikisha mtu kutoka watu, aliye kuwa kero kwake na alikuwa na kawaida ya kusema kwamba hakuna adhabu iliyokuwa kali kama hiyo. (Tarikh Tabari, Juz. 4, uk. 527).

Amri zilitolewa kwa ajili ya kuhamishwa kwa Abu Dharr na pia kwamba hakuna mtu aliyeruhusiwa kumuaga au hata kusema naye au kumtembelea.

Abdullah bin Abbas anasema kwamba Abu Dharr alipohamishwa Madina kwenda Rabzah tangazo lilitoka kwamba hakuna mtu aliyeruhusiwa kusema na Abu Dharr au kumuona anaondoka. (Saqifah Ahmad bin Abdul Aziz Janhari, Murujuz Zahab, Juz. 1, uk. 438; Sharh bin Hadid). Hili ni agizo ambalo lilifadhaisha watu na kuwazuia makwao. Hakuna mtu aliyeweza kuwa jasiri kutoka nje ya nyumba yake kwa madhumuni ya kumuona sahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w) mwenye kuheshimiwa kama Abu Dharr isipokuwa Imamu Ali, Hasan, Husein, Aqil, Abdullah bin Jafar, Abdulah bin Abbas na Miqdadi bin al-Aswad.

Ingawa masahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w) hawakuweza kutoa maoni yao dhidi ya agizo la Uthman kuhusu uhamisho wa Abu Dharr, bado walipata wasi wasi sana. Si tu masahaba waliokuwa pale ambao walisumbuliwa na tukio hili lakini pia wale ambao walikuwa nje ya Madina lakini walisikia habari ya kufukuzwa kwa Abu Dharr Madina.
Mathalan Abdullah bin Masud1 ambaye alikuwa Kufah na pia watu wa kabila lake walipatwa na fadhaa.

Abdullah bin Masud aliposikia habari hizi akiwa Kufah, alipata wasi wasi na akahutubia kundi la watu ndani ya msikiti wa Kufah, “Enyi watu! Mmewahi kuisikia Ayah hii? “Bado, ni nyinyi ndio mnao waua watu wenu, na mnawafukuza baadhi yao nje ya makazi yao.” Alipinga khalifa kwa kukariri ayah hii.

Walid, gavana wa Kufah alimtaarifu Khalifa Uthman kuhusu tukio hili. Khalifa alimjibu barua yake kwa kumuagiza ampeleke bin Masud kwake. Abdullah bin Masud alipofika Madina, Uthman alikuwa na hutubia. Alipomuona, Uthman alimuamuru mtumishi wake Aswad ampige bin Masud. Alimvuta na kumtoa nje ya msikiti na kumtupa chini na akamcharaza sana, akamzuia nyumbani mwake na akasitisha ruzuku yake kwa maisha yake yote. (Abu Dharr Ghifari, uk. 146, Musnad Ahmad bin Hanbal, Juz. 5, uk 197).

Lazima ieleweke kwamba Ali pia ameonesha masikitiko yake kuhusu kufukuzwa kwa Abu Dharr kwa maoni ya ‘Zammul Quraysh.” (Sahifah Alawiyah).

Kwa ufupi, kufuatana na agizo la Uthman, Marwan alimpeleka ngamia ambaye hakuwekewa tandiko la kukalia kwa lengo la kumsafirisha Abu Dharr kusiko julikana ambapo ghafla Ali, Hasan, Husein, Aqil, Ammar, Abdullah bin Jafar, Miqdadi bin al-Aswad na Abdullah bin Abbbad walifika hapo na kusema; “Wewe Marwan uliye laaniwa! Acha!
Usimkalishe kwenye ngamia. Lazima tumpe kwa heri.”

Halafu Imamu Ali akawaambia wanawe waagane na mjomba wao. Baada ya kusikia hivyo, Imamu Hassan akasema, “Ewe mpendwa wangu mjomba Abu Dharr! Mwenyezi Mungu na akuhurumie. Nyoyo zetu zinateseka. Usiwe na wasi wasi. Mwenyezi Mungu ndiye kiongozi wako na ni Yeye unatakiwa umweke mbele yako. Ewe Mjomba! Hakuna kitu kizuri kama uvumilivu. Mwamini Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mpangaji wa mambo yako.”

Ammar alisema kwa hasira, “Mwenyezi Mungu na asimhurumie mtu ambaye amekupa taabu kubwa sana na ampe wasi wasi mtu ambaye anakusumbua. Ewe Abu Dharr, kwa jina la Mwenyezi Mungu, endapo ungeikumbatia dunia ya watafutaji wa dunia, hawangekufukuza na endapo angekuwa umekubali tabia yao, wangekufanya wewe rafiki yao. Uliposimama kidete kwenye imani yako, wapenda mambo ya dunia wamechoshwa na wewe. Usiwe na wasi wasi kwa sababu Mwenyezi Mungu yupo pamoja na wewe.

Watu hawa ni wale wenye bahati mbaya ambao mawazo yao yanatamani dunia na wamo kwenye hasara kubwa sana. Vivyo hivyo, watu wengine pia walisema na kumliwaza Abu Dharr kwa maneno tofauti.

Baada ya kusikia hotuba hizi Abu Dharr akalia sana na akasema, “Enyi Watu wa familia ya Mtukufu Mtume mlio neemeshwa! Nilipowaoneni, nilimkumbuka Mtukufu Mtume (s.a.w) na neema zikanizunguka. Enyi watu ninaowaenzi! Ni nyinyi peke yenu mlikuwa njia ya kupita faraja hapa Madina! Wakati wowote nilipowaoneni nilipata hali ya kuridhisha moyo wangu na utulivu wa akili yangu.

“Enyi wazee wangu! Kama ambavyo nilikuwa mzigo kwa Uthman hapa Hijaz, nilikuwa mzigo kwa Muawiyah huko Syria, kwa sababu anaye kaka yake wa kuchangia ziwa Abdallah bin Sarah kama gavana wa Misri, na mtoto wa kiume wa mama yake mdogo, Abdullah bin Amir kama Gavana wa Basra. Sasa ananipeleka mahali ambapo ni jangwa ambapo sina anayeniunga mkono mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, natambua kwamba ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye msaidizi wangu na kwa ajili Yake peke Yake sitajali upweke wa nyika.”

Kwa mujibu wa Allamah Subaiti, baada ya haya, Abu Dharr ambaye alikwisha kuwa mzee na dhaifu, alinyanyua mikono yake kuelekea mbinguni na akasema, “Ee Mwenyezi Mungu! uwe shahidi kwamba mimi ni rafiki yao Ahlul Bait na kila mara nitakuwa rafiki yao kwa ajili yako na kwa ajili ya Akhera, hata kama nitakatwa vipande kwa ajili ya mapenzi yangu kwa vitu hivi viwili.”

Baada ya haya Ali (a.s) akasema, “Ewe Abu Dharr! Mwenyezi Mungu na akuhurumie. Tunatambua sana kwamba sababu pekee ya wewe kufukuzwa kutoka sehemu moja na kupelekwa nyingine ni mapenzi yako kwetu, wazao wa Mtukufu Mtume (s.a.w).2

Hata hivyo, watu hawa mashuhuri waliporudi Madina baada ya kuagana na Abu Dharr kwa huzuni, Uthman alikasirika sana.
Atham Kufi ameandika, Abu Dharr alianza safari ya kwenda Rabzah na masahaba wengine na Ali wakarudi. Khalifa akaagiza Ali aende kwake na akamuuliza sababu ya kutoka nje ya Madina na kumuaga Abu Dharr na kwa nini alichukua kundi la masahaba kwenda naye, bila kujali amri yake. Ali alimuuliza Khalifa endapo ilikuwa wajibu kwake kufuata amri za Uthman hata pale ambapo zilipingana na utii kwa Mwenyezi Mungu na ukweli. Halafu akaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba kamwe hangefanya hivyo.” (Tarikh Atham Kufi, uk. 131, chapa Delhi).

  • 1. Allamah Subaiti anasema kwamba masahaba wa Mtume walionesha kukasirika kwao kwa sababu ya kufukuzwa Abu Dharr kutoka Madina na kupelekwa Rabzah. Kwa mujibu wa Mustadirak wa Hakim, Abu Darda aliposikia habari za kufukuzwa kwake alisema kwa mshangao, “Inna Lillahi wa inna illahe rajiun!” (Sisi tumetoka kwa Mwenyezi Mungu na tutarudi Kwake) Alirudia maneno haya mara kumi Ali akasema; “Ewe Abu Dharr! Usiwe na wasi wasi. Watu walikuogopa kwa sababu ya tamaa ya mambo ya dunia, na wewe hukuwaogopa kwa sababu ya imani yako hadi wakati walipofukuza. Abu Dharr! Mchamungu hupatwa na kila aina ya matatizo, lakini kumbuka kwamba Mwenyezi Mungu ni stadi wa kutengeneza njia za ajabu za ukombozi kwa wacha mungu. Hakuna kitu kinachoweza kukupatia maliwazo isipokuwa ‘ukweli’. Ukweli’ ndio utakao kuwa sahaba wako huko kwenye upweke. Najua kwamba wewe unaweza kupata mshtuko wa hofu kutokana na uwongo na hali hiyo haiwezi kuja karibu na wewe.
  • 2. Abu Dharr alitambua kwamba kuwapenda Ahlul Bait ndio msingi wa Uislamu. Kwa mujibu wa Jazairi, Imamu Jafar al-Sadiq amemnukuu Mtukufu Mtume akisema, "Kama ambavyo kila kinacho msingi, msingi wa Uislamu ni kutupenda sisi, Ahlul -Bait (Anwar Nomaniah