Sura Ya Kwanza

Abu Dharr alikuwa mmojawapo wa hao masahaba wa Mtume wa Uislamu, Muhammad (s.aw.) ambao walikuwa wachaji Mungu na wapenda uhuru na walikuwa na tabia bora kwa mujibu wa maneno ya Mtukufu, Mtume: Pepo na wakazi wake wanawangojea kwa hamu. Alifaidika kuwa na Mtume katima uhalisi wake.

Abu Dharr mwenyewe anasema, “Jina langu halisi ni Jundab bin Junadah, lakini baada ya kuingia kwenye Uislamu, Mtume alinipatia jina la ‘Abdullah’ na hili ndilo jina ninalolipenda hasa.”

Abu Dharr ilikuwa Kuniyah yake (kutokana na mtoto wake wa kwanza aliyeitwa Dhar). Wanavyuoni wanakubaliana kwamba Abu Dharr alikuwa mtoto wa kiume wa Junadah bin Qays bin Saghir bin Hazam bin Ghafir na mama yake alikuwa Ramlah binti Wafiah Ghifariah. Alikuwa wa jamii ya Kiarabu na alikuwa wa kabila la Ghifar. Ndio sababu ya neno Ghifar; limeandikwa na jina lake.

Abdullah al-Subaiti ameandika, “Tunapoangalia wasifu wa Abu Dharr inaonekana kama vile ni nuru iliyopewa umbo la Binadamu. Alikuwa mfano halisi wa sifa za mtu mashuhuri. Alikuwa na sifa pekee ya akili, uelewa, busara na werevu.” Kwa maneno ya Imamu Jafar Sadiq: “Wakati wote alikuwa katika tafakuri na Swala zake ziliegemezwa kwenye mawazo kuhusu Mungu.” (Sahih Muslim).

Mwandishi maarufu wa Misri Abdul Hamid Jaudatus Sahar, kwenye kitabu ‘Al-Ishtiraki az-Zahid, ameandika: Wakati fulani ilitokea njaa kali. Watemi wa kabila la Ghifar walikusanyika kwa ajili ya kushauriana ili wapate ufumbuzi wa tatizo hilo kwa sababu ya ukame wa muda mrefu. Kwa hiyo hicho kilikuwa kipindi cha mateso makubwa. Wanyama walikonda na akiba kwenye maghala ilikwisha. Waliambizana wao kwa wao, ‘Hatujui kwa nini Mungu wetu (sanamu Manat) amekasirishwa na nini kutoka kwetu, ingawa tumeomba mvua, tumetoa sadaka ya ngamia na tumefanya kila linalowezekana ili atupendelee.

Msimu wa mvua sasa umekwisha. Hakuna hata dalili ya wingu angani. Hapajatokea mngurumo na rasha rasha ya mvua kipindi hiki, hakuna hata tone la mvua au manyunyu. Unafikiria nini? Tumekuwa wapotevu hivyo kwamba ghadhabu ya mungu wetu imetuangukia? Kwa nini ahisi amekosewa na sisi ambapo tumetoa sadaka nyingi kwa ajili ya kumfurahisha yeye?”

Watu walianza kutafakari juu ya jambo hili na kubadilishana mawazo. ‘Binadamu hawezi kuingilia mipango ya Mbinguni. Hakuna mtu yeyote anayeweza kuleta mawingu ya mvua kutoka angani. Anayeweza kufanya hivyo ni ‘Manat’ tu. Kwa hiyo hatuna njia nyingine isipokuwa sisi, wanaume na wanawake, twende Hija huku tunalia kwa huzuni na kusali na kumwombea kwa huzuni na kusali na kumwomba Manat atusamehe.

Labda inawezekana akatusamehe na mvua ikaanza kunyesha na kuifanya ardhi kuwa kijani kibichi baada ya ukame, ili umasikini wetu ubadilike kuwa mafanikio, uchungu kuwa furaha na matatizo kuwa raha na starehe.”

Kwa hiyo, kabila lote lilianza matayarisho ya safari ya kwenda kumuona Manat. Wale waliokuwa wamelala waliamka na kuweza kuweka mito ya kukalia juu ya migongo ya ngamia wao. Unais (ndugu yake Abu Dharr) naye pia alipanda ngamia wake na kumwendesha, ili aungane na msafara, karibu na Pwani ya bahari, Mushalsal na Qadid sehemu zilizomo kati ya Makkah na Madina, ambapo ndipo Manat alipo.

Unais alitazama huku na kule lakini hakumuona kaka yake. Alimbembeleza ngamia akakaa chini. alikimbia kuelekea nyumbani. Aliingia ndani huku akiita ‘Jundab! Jundab! alipoona kwamba Jundab alikuwa amelala kitandani pake kwa raha mstarehe, alisema: Unais: “Hukusikia ‘wito’ wa kwenda safarini”

Jundab: “Ndio, nilisikia. Lakini nifanye nini ambapo ninahisi kuchoka na pia sitaki kwenda kwenye Hija ya Manat.”

Unais: “Nyamaza! Mwombe mungu akuhurumie. Huogopi kwamba endapo mungu atakusikia anaweza kukutesa.”

Jundab: “Wewe unaridhika kwamba Manat hutusikia sauti zetu na hutuona?”

Unais: “Nini kimekutokea leo? Kuna jinni lolote limekuzidi nguvu, au umeugua ugonjwa? Njoo jisikitikie. Labda Manat anaweza akakubali toba yako.”

Abu Dharr alipoanza kujibiringisha kitandani mwake, kaka yake alisema, “Amka msafara umekwisha ondoka na kabila linakwenda huko.”

Hawa ndugu wawili walikuwa wanaendelea na mazungumzo ambapo mama yao aliwasili hapo na walinyamaza.

Mama: “Wanangu! Nini maoni yenu?”
Unais: Kuhusu nini mama?”
Mama: “Kuhusu mvua.”
Unais: “Tunakubaliana na pendekezo lako.”
Mama: “Ninapendekeza twende kwa mjomba wenu (kaka yake mama yao Abu Dharr na Unais) ambaye ni tajiri.”
Unais: “Sawa! Tutafanya upendavyo. Mungu na aifanye hali yetu kuwa nzuri zaidi.”

Abu Dharr, Unais na mama yao walikwenda nyumbani kwa mjomba wao. Mjomba wao aliwakaribisha kwa ukarimu mkubwa. Waliishi hapo kwa muda mrefu. Matatizo yao yaligeuka kuwa raha ma machungu yao yakawa starehe. Watu wa kabila lao walipoona kwamba mjomba wao alikuwa mtu mwema kwa Abu Dharr na Unais na aliwapenda kama watoto wake mwenyewe, waliwaonea wivu na walianza kufikiria mipango ya kumfanya awadharau. Waliendelea kufikiria na kushauriana wao kwa wao, hadi hatimaye waliamua kutumia hila na walimchagua mtu kutekeleza njama yao.

Mtu huyo alikwenda nyumbani kwa mjomba wake Abu Dharr na akaketi chini, akiwa kimya na ameinama. Mjomba wake Abu Dharr alimuuliza huyo, ‘Ndio, waonaje hali?”

Mtu huyo alionekana na huzuni sana na alisema, Nimekuja kwako kwa shughuli muhimu! kama ingelikuwa kwa sababu ya kukupenda na kukuheshimu wewe nisingekwambia, lolote.

Lakini uaminifu wangu umenilazimisha kufanya hivi. Nataka kufichua jambo usilolijua, ili uone nini kinachoendelea kwa sababu ninaona kwamba upendeleo wako unaelekezwa mahali pasipofaa!”

Mjomba wake Abu Dharr alihisi kuna jambo lenye maudhi limetokea. Alihuzunika, sana na akasema, “Sema usifiche.” Mtu huyo alisema: “Nitakwambiaje kwamba unapotoka nje ya makazi yako, mpwa wako Unais, hukaa na mkeo na kuzungumza naye kwa siri sijui huzungumza nini naye?”

Mjomba wake Unais alisema, “Haya ni mashtaka ya uongo dhidi yake, na siwezi kuamini kwa jinsi yoyote ile!” Alijibu: “Sisi pia tulidhani kwamba ni uongo. Lakini ninajuta kusema kwamba ni kweli.”

Alimwambia atoe ushahidi. Mtu huyo alimwambia, “Kabila lote linaweza kutoa ushahidi kuhusu jambo hili. Wote wamemuona na wanazo hisia kama zako. Kama unataka ninaweza kuleta mashahidi wasio hesabika kutoka kwenye kabila langu.”

Aliposikia hivyo mjomba wake Unais alianza kufikiria heshima na hadhi yake. Alihisi heshima yake binafsi ilichafuliwa. Mtu huyo alitoka nje ya nyumba alipoona ametimiza kazi yake.

Mjomba wake Unais aliridhika kwamba taarifa aliyopewa ilikuwa kweli. Alifanya kila jitihada kupata utulivu wa kiakili, lakini alishindwa. Alisikitika sana na alihisi uchungu mkali na mateso moyoni mwake na kila siku. Wakati wowote ambapo wapwa zake walipofika mbele yake aligeuzia uso wake upande mwingine. Ukimya ulienea ndani ya nyumba yote.

Abu Dharr alipoona dalili ya huzuni kwenye uso wa mjomba wake, aliamua kumuuliza, “Mpendwa mjomba! Nini Kimekusibu? Nimekuwa nikichunguza mabadiliko ya hali yako kwa muda wa siku kadhaa sasa. Unatusemesha mara chache sana na muda mwingi unakuwa na mawazo mengi na kufadhaika.”

Mjomba wake alimjibu, “Hakuna tatizo lolote.” Abu Dharr akasema, “Hapana, hakika ipo sababu ya hali hii. Tafadhali niambie. Labda ninaweza kukufariji kuhusu huo wasi wasi wako au ninaweza kuwa pamoja na wewe kuhusu baadhi ya matatizo yako.”

Akasema, “Siwezi kueleza jambo ambalo watu wa kabila langu wamenieleza.”

Abu Dharr akasema; “Tafadhali nijulishe. Watu wa kabila lako wamekwambia nini?” Mjomba wake alijibu, “Wamesema kwamba, Unais huzungumza na mke wangu kwa siri wakati mimi sipo.”

Aliposikia hivi Abu Dharr aligeuka rangi na kuwa nyekundu iliyoiva kwa hasira na akasema, “Umeharibu msaada wako wote uliotupatia. Sasa tunaondoka, na hatutakuona tena!”

Hatimaye waliondoka hapo na walikwenda sehemu iitwayo ‘Batu Mari’, karibu na Makkah. Hapa ndipo Abu Dharr alipopata kujua kwamba Mtume alitokea huko Makkah.

Alipata shauku ya kutaka kujua kuhusu taarifa hii. Haraka sana alimwita kaka yake Unais na akamuomba aende Makkah na afanye utafiti wa habari kamili kuhusu Mtume.

Unais alikuwa hajaondoka kwenda Makkah, ambapo mtu alionekana anawasili hapo kutoka huko, na alikwenda moja kwa moja kuungana na watu wa nyumba ya Abu Dharr. Abu Dharr alimuuliza, “Unatoka wapi?” Akajibu; “Nimekuja kutokea Makkah?”

Abu Dharr aliuliza, “Hali ya huko ikoje?”
Akajibu, “Yupo mtu anayesema kwamba yeye ni Mtume na hupata ufunuo kutoka mbinguni.” Abu Dharr akasema; “Watu wa Makkah walimfanya nini?”

Mtu huyo akasema; “Walimkadhibisha, walimtesa, na waliwazuia watu wasiende kwake. Humtishia na kumuogopesha yeyote anayekwenda kumuona.”

Abu Dharr akauliza; “Kwa nini watu hawamwamini?” Watamwaminije, alisema mtu huyo, ambaye huwatukana miungu wao, huwaambia wapumbavu na wahenga wao wapotevu.”
Abu Dharr alisema; “Ni kweli kwamba husema hivyo? Ndio, husema hivyo kwamba Mungu ni Mmoja. Ona sasa! Sio jambo la kushangaza hili?” alisema mtu huyo.

Abu Dharr alianza kufikiria mtu aliyesema Mungu ni Mmoja. Aliendelea kufikiria kimya kimya kwa kipindi kirefu. Mtu huyo mgeni alimtazama na akamuona anayo mawazo mengi akamuaga akaondoka.

Baada ya kuondoka mtu huyo Abu Dharr alimwambia ndugu yake Unais, “Nenda Makkah na ufanye utafiti wa habari kamili za mtu huyu. Anasema kwamba hupokea ufunuo kutoka mbinguni! Uongeaji wake ukoje? Angalia kama kuna ukweli katika mazungumzo yake au hapana.”

Unais aliondoka kwenda safari ya kuelekea Makkah. Baada ya kupita vituo mbali mbali alifika Makkah na akaenda Ka’abah na kuzunguka. Alipotoka hapo, aliona kundi la watu. Alimuuliza mtu aliyekuwa anakuja mbele yake, “Kuna nini kinachofanyika hapo?” Akajibu, “Mwasi anawaita watu waende kwenye imani mpya!”

Mara tu Unais aliposikia hivyo, alikimbia kwenda huko. Alipofika hapo, alimuona mtu anasema, “Sifa zote zinastahiki kwake Mwenyezi Mungu. Ninamsifu Yeye na ninahitaji msaada Wake. Ninamwamini Yeye, ninamtegemea Yeye na ninashahidilia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu na Hana mshirika.”

Katika nukuu ya Subaiti, Unais alimsikia mtu huyo akitangaza, “Enyi watu! Nimekuleteeni neema ya dunia hii na baada ya maisha haya. Semeni kwamba hapana mungu isipokuwa Allah ili muweze kupata ukombozi. Mimi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na nimekuja kwenu. Ninawaonya kuhusu adhabu ya siku ya Hukumu. Kumbukeni kwamba hakuna mtu atakayepata kuokolewa isipokuwa yule anayekuja mbele ya Mwenyezi Mungu kwa moyo wa unyenyekevu.

“Wala utajiri hautakuwa na manufaa kwake, wala watoto hawatawasaidieni. Mwogopeni Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atakuwa mwema kwenu. Enyi watu! Nisikilizeni!

Ninasema wazi kabisa kwamba mababu zetu walifanya upotovu kwa kuacha njia iliyonyooka na kuanza kuabudu masanamu haya na nyinyi mnafuata nyayo zao.

Kumbukeni kwamba masanamu wala hayawezi kuwaumizeni ama kuwanufaisheni. Wala hayawezi kuwazuieni ama kuwaongozeni.”

Unais aliposikia hotuba hii yenye ushawishi mkubwa alishangaa. Lakini katika kustajabu kwake aliona kwamba watu walikuwa wanasema mambo tofauti dhidi yake.

Aliposikia Mtume alisema, “Mitume hawasemi uongo. Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu mbali na Yeye, kwamba nimetumwa kwenu kama mjumbe. Kwa jina la Mwenyezi Mungu mtakufa kama mnavyolala na mtafufuka kama mnavyoamka. Mtaitwa kuhesabiwa matendo yenu. Halafu mtapewa Pepo au Jahanamu ya milele!”

Aliposema hivi watu walimuuliza Mtume, watafufukaje baada ya kuwa vumbi?

Wakati huu huu Mwenyezi Mungu aliteremsha Aya zifuatazo:

قُلْ كُونُوا حِجَارَةً أَوْ حَدِيدًا {50} أَوْ خَلْقًا مِمَّا يَكْبُرُ فِي صُدُورِكُمْ ۚ فَسَيَقُولُونَ مَنْ يُعِيدُنَا ۖ قُلِ الَّذِي فَطَرَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ ۚ فَسَيُنْغِضُونَ إِلَيْكَ رُءُوسَهُمْ وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هُوَ ۖ قُلْ عَسَىٰ أَنْ يَكُونَ قَرِيبًا {51}

“Sema: Kuweni hata mawe, na chuma. au umbo lolote mnaloliona kubwa katika vifua. Watasema: Nani atakayeturudisha tena? Sema: Yule aliye kuumbeni mara ya kwanza! Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: Lini hayo? Sema: Asaa akawa karibu!” (17:50-51).

Mara tu Mtume alipomaliza hotuba yake watu walinyanyuka. Wakati walipokuwa wanasambaa, mmoja wao alisema: “Huyu ni mtabiri?” Mwingine akasema, “Huyu ni mchawi.”

Unais alimsikiliza Mtume na watu. Aliinamisha kichwa chake kwa muda fulani na akanong’ona: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu maneno yake ni matamu. Hayo aliyoyasema ni kweli na watu wanaompinga ni wapumbavu.”

Halafu akapanda ngamia wake akaanza safari ya kuelekea kwao. Aliendelea kufikiria kuhusu Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu wakati wote wa safari yake, na alikuwa anashangaa kuhusu mazungumzo yake, hadi alipoonana na Abu Dharr.

Abu Dharr alipomuona Unais, alimuuliza kwa shauku kubwa, “Kuna taarifa gani? Uliona nini Makkah?”

Unais: “Wanasema kwamba mtu huyu ni mshairi, mchawi na mtabiri. Lakini nilipochunguza mazungumzo yake kulingana na wale wanaosema kuwa ni mshairi, niliona kwamba maneno yake si mashairi wala si utabiri kwani nimewahi kukutana na watabiri wengi, na mazungumzo yake si sawa na yale ya watabiri.

Abu Dharr: “Anafanya nini na anasema nini?”
Unais: “Ansema mambo ya ajabu.”
Abu Dharr: “Huwezi kukumbuka chochote katika yale aliyosema.”

Unais: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu! Hotuba yake ilikuwa tamu sana lakini sikumbuki chochote zaidi ya yale ambayo nimekwisha kwambia, lakini nimemuona anasali karibu na Al-Ka’abah, na pia nimemuona kijana moja mwenye sura ya kupendeza ambaye haja-balehe, akisali pamoja naye. Watu wanasema kwamba huyo ni binamu yake Ali. Pia niliona mwanamke anasali nyuma ya mtu huyu. Watu waliniambia huyo ni mke wake, Khadijah.