Sura Ya Nne

Abdul Hamid Jaudatus Sahar wa Misri ameandika, Uislamu ulienea Madina kama moto wa mbuga ya majani makavu.” Kabila la Ghifar lilifurahishwa sana na hali hiyo. Waislamu walipongezana wao kwa wao kwamba makabila mawili ya Aus na Khazraj, ambao walikuwa wasemaji sana, wapiganaji wazuri sana na waunga mkono wazuri sana walikubali kuingia kwenye Uislamu, na pia kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikwisha ridhika kuinyanyua dini Yake na alinuia kumsaidia Mtukufu Mtume na kutimiza ahadi yake.

Unais alikwenda kwa kaka yake Abu Dharr akiwa na habari za kufurahisha na akasema “Uislamu umeenea Madina na Aus na Khazraj wamekubali Uislamu!”

Abu Dharr akasema, “Mtume wa Mwenyezi Mungu atakwenda na kuhamia huko baada ya kipindi kifupi.”

Unais alimwangalia kaka yake kwa mshangao na alisema,
“Umepokea habari zozote za aina hiyo?”

Abu Dharr, “Hapana, wala sina taarifa yoyote kuhusu habari hizi, ama kujua kwamba watu wa Yathrib wamekuwa waumini.”

Unais, “Vipi sasa ulijua kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu atahamia Yathrib?”

Abu Dharr, “Aliniambia siku hiyo hiyo nilipokutana naye, kwamba alitarajia kwenda kwenye mji wa mitende na nadhani sehemu hiyo ya Yathrib, Mtume alisema kweli.”

Unais, “Inawezekana kwamba kabila lake litamruhusu aondoke hapo akiwa na Waislamu, ili kwamba baada ya matayarisho kamili awashambulie?”

Abu Dharr, “Wanaweza wakamruhusu au wasimruhusu, lakini baada ya kipindi kifupi atahamia huko. Kama mambo yalivyo, ni Mwenyezi Mungu tu ndiye anaye jua ni vipi na lini itatokea.”

Abu Dharr alisilimisha kabila lake na kuingia kwenye Uislamu baada ya yeye kuwa muumini. Halafu akaelekeza shughuli hiyo Madina.

Tangu aliporudi kutoka Makkah hadi kuhama kwa Mtukufu Mtume, Abu Dharr alikuwa anashughulika na kuhubiri Uislamu na aliendelea kufanya juhudi kuipeleka dini ya Mungu kwa umma Mtukufu Mtume aliendelea kufanya kazi yake ya kuhubiri Uislamu na Quraishi waliendelea kufanya kazi yao ya kumtesa Mtume. Walimpa mateso makubwa sana hivyo kwamba hakuwa na uchaguzi mwingine isipokuwa kuondoka nyumbani kwake.

Kwa ufupi, kwa amri ya Mwenyezi Mungu Jibril alimwambia aondoke Makkah baada
ya kumwambia Ali alale kwenye kitanda cha Mtume. Alifanya alivyoagizwa.

Alimwambia alale kitandani pake na akaondoka, hivyo kwamba Quraishi hawangejua
kama hayupo kitandani pake. Baada ya kukaa siku tatu kwenye pango la Hira
aliondoka kwenda Madina.

Abu Dharr alikuwa anangojea uhamiaji Madina. Watu wa kabila lake pia walikuwa wanangojea na walikuwa wanauliza mara kwa mara habari za Mtukufu Mtume kwa mtu yeyote aliyetokea sehemu hiyo.

Kuanzia Makkah na baada ya kukaa kwa muda wa siku chache pangoni, Mtume aliondoka kwenda Madina. Kabila la Ghifar lilipopata taarifa kwamba alikuwa kati ya Makkah na Madina walifurahi sana. Abu Dharr alihisi wimbi la neema lilikuwa linakuja. Aliungana na kabila kungoja.

Watu walikusanyika na kumzunguka na walimuuliza kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu, mwenendo wake na umbile lake alijibu, “Mtamuona baada ya muda si mrefu. Yeye ni bora kuliko wote na anamzidi kila mtu kwa sifa.”

Watu walipongojea kwa kipindi kirefu, Abu Dharr alikuwa anaangalia njia, ili awe mtu wa kwanza kuwataarifu watu atakapo wasili Mtume na kutuliza nyoyo za watu na kuondoa hofu iliyokuwa inawaelemea kwa kungojea kwa kipindi kirefu hivyo.

Muda uliendelea kupita. Watu wa kabila la Ghifar walikuwa na shauku kubwa ya kumpokea Mtume. Abu Dharr alipotupa jicho aliona ngamia anakwenda hapo. Watu wote walikuwa wanaangalia macho ya Abu Dharr. Baada ya muda mfupi, Abu Dharr akasema kwa sauti ya kushangaa, “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mtume anawasili!”

Allamah Subaiti ameandika, “Uso wa Mtukufu Mtume ulikuwa unatoa nuru. Kwa ufupi watu wote walimfuata Abu Dharr, huku wakisema kwa sauti moja, “Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuja! Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuja!” Abu Dharr alikwenda mbele haraka na akashika hatamu ya ngamia wake.

Watu walianza kusema, “Allahu Akbar.” (Mwenyezi Mungu Mkubwa) huku wakimzunguka Mtume kwa hamu kubwa. Wanawake wote, vijana na vikongwe, wavulana na wasichana walikuwa wanashangilia kwa furaha kubwa. Mtume wa Mwenyezi Mungu amewasili! Mtume wa Mwenyezi Mungu amewasili!”

Baada ya hapo watu wa kabila la Aslam walisema, “Pia na sisi tumekuwa Waislamu kama walivyo fanya ndugu zetu wa kabila la Ghifar.” Mtume wa Mwenyezi Mungu alifurahi sana na alinyanyua mikono yake kuelekea mbinguni aliomba, “Ee Mola wa ulimwengu! Wasamehe kabila la Ghifari na uwaweke kabila la Aslam salama.”

Baada ya hapo Mtukufu Mtume aliteremka kwenye ngamia na akaanza kukariri Quran. Sauti yake iliingia kwenye nyoyo za watu. Halafu akaanza kuhubiri. Watu walikwenda mbele kwa makundi na kutoa kiapo cha utii kwake. Abu Dharr alisimama kwa maringo karibu na Mtume akiwa amefurahi kupita kiasi.

Watu wa kabila la Ghifari walijitokeza mbele na wakasema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Abu Dharr alitufundisha yote yale uliyomwambia. Tukasilimu na kuwa Waislamu na tukakiri kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.”

Baada ya hapo watu walifurahi sana na walikuwa wanaangalia uso wa Mtume mara kwa mara. Abdul Hamid Jaudatus Sahar ameandika, “Watu walianza kuangalia uso wa Mtume kwa makini, waliona kwamba alikuwa mtu mwenye uso unao ng’aa midomo inayo tabasamu na tabia njema kuhusu umbo lake, hakuwa mwembamba au aliye konda ama mnene. Alikuwa na sura nzuri ya kupendeza.

“Macho yalikuwa makubwa na meusi, kope za macho zilikuwa ndefu, nyusi zake nyeusi zilizojikunja mfano wa tao, nywele nyeusi, shingo ndefu na ndevu nyingi. Alikuwa Mtukufu wakati ametulia na alikuwa anatia moyo kwa heshima wakati anasema.

Mazungumzo yake yalikuwa matamu. Wala hakuwa mkimya au msemaji. Alikuwa na sura ya kupendeza sana akiwa mbali na mzuri sana akiwa karibu.

“Saizi ya umbile lake ilikuwa ya kati, wala hakuwa mrefu sana kiasi cha kutokupendeza kumwangalia, ama mfupi sana kiasi cha kufikiriwa kuwa mtu duni.

“Baada ya hapo Mtukufu Mtume aliondoka kwenda Madina na Abu Dharr aliendela kuishi na kabila lake.”

Kutoka hapo, Mtukufu Mtume aliondoka kuelekea Madina. Alipofika Madina, watu walimkaribisha kwa moyo mkunjufu. Mara tu baada ya kufika, alianza kuhubiri ujumbe wa Uislamu. Abu Dharr ambaye hakuweza kumsindikiza Mtukufu Mtume huko Madina aliishi mjini kwake kwa kipindi kirefu sana hivyo hakuwepo katika vita kuu tatu za Kiislamu (Ghazawat) vita vya Badr, mwaka wa 2, Hijiriya, Uhud mwaka wa 3 Hijiriya, na Ahzab mwaka wa 5/

Baada ya vita ya Ahzab, aya ya Quran Tukufu ilimlazimisha Abu Dharr kuondoka kwenda Madina. Siku moja alikuwa anashughulika na dua baada ya Swala ya jioni kwenye msikiti wa mjini kwake, ambapo alisikia mtu anasoma kwa sauti Aya (61:10)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ تِجَارَةٍ تُنْجِيكُمْ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ{01}

Enyi mlio amini! Nikuonyesheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iliyo chungu.”(61:10)

Baada ya kutafakari maana ya Aya hii alipata shauku ya Jihadi na akamwambia Unais, “Nitaondoka kwenda Yathrib kesho.”

Unais: “Sawa! Nenda. Mwenyezi Mungu na akufikishe huko Salama!”

Abu Dharr, “Sitarudi. Nitatumia maisha yangu yote katika kumtumikia Mtukufu Mtume.”

Unais, “Ewe ndugu yangu! Umekuwa muumini wa kweli na imani imepenya kwenye moyo na roho yako. Kabila lako na watu wako hapa wanakutaka sana. Patakuwepo pengo kubwa sana ukiondoka hapa. Nadhani ungeacha mpango wa kwenda Madina na uishi hapa hadi mwisho wa uhai wako.”

Abu Dharr; “Mtukufu Mtume ni bora zaidi kuliko watu hawa. Chochote ambacho kimetekelezwa kinatosha. Mtukufu Mtume alipigana Badr, Mimi sikuwa naye. Akapigana huko Uhud Mimi si kuwepo. Hadi lini nitaendelea kulitumikia kabila langu na nikose baraka za kufa shahidi. Yote hayo ambayo yamefanyika mpaka sasa yanatosha. Sasa sitakata tama hata kwa dakika moja kuhusu uamuzi wangu wa kwenda Yathrib.”

Unais, “Pendekezo langu ni kwamba wewe uendelee kuishi hapa nyumbani kama kawaida. Mtukufu Mtume atakuita yeye mwenyewe atakapokuhitaji. Wewe angalia walikuwepo watu wengi waliokuwa katika miji ya kwao na waliondoka kwenda Madina baada ya kuitwa na Mtukufu Mtume.”

Abu Dharr akasema: “muda wa kungojea umepita. Endapo Mtume hajaniita mimi pia nina wajibu. Sitaendelea kungoja, nitakwenda huko bila kuitwa.”

Unais: “Vema! Lakini usifanye haraka. Chukua mahitaji ya muhimu kwa safari.”

Abu Dharr; “Sihitaji chochote. Vipande vya mikate mikavu vinanitosha.”

Abu Dharr aliondoka nyumbani kwake na kuelekea Madina. Alipofika huko alipata heshima ya kukutana na Mtume na akawa naye.

Alikuwa na desturi ya kulala kwenye msikiti wa Mtume usiku na wakati wa mchana alikutana na watu. Alikula chakula pamoja na Mtume na akaiga maisha yake ya kidunia kwa uchaji Mungu na uadilifu. Alifanya bidii sana kujifunza hadithi za Mtume na kuzihifadhi katika kumbu kumbu.

Baada ya kufika Madina Abu Dharr aliugua kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa. Mtume alipata taarifa ya ugonjwa wake. Akaenda kumuona Abu Dharr na akamwambia; “Abu Dharr! Unatakiwa uishi nje ya Madina kwa muda fulani sehemu ambayo ngamia, kondoo na mbuzi huchungwa na uzingatie kwamba usile chochote isipokuwa maziwa wakati wote utakapo kuwa kule.”

Mara tu baada ya kupokea amri ya Mtume, Abu Dharr aliondoka kwenda mahali hapo alipoambiwa akiwa na mkewe.

Ugonjwa ulikuwa mkali sana kwa kipindi cha siku kadhaa lakini, ulipungua pole pole akapata afya nzuri hadi akaweza kutimiza tendo la ndoa na mke wake. Sasa, palijitokeza tatizo la upatikanaji wa maji kwa ajili ya josho kubwa la kuondoa janaba kabla ya Swala. Hadi hapo alikuwa hajajua Tayamamu. Kwa hiyo alikuwa hajui la kufanya kwa muda fulani.

Hatimaye akili yake ilimwongoza na akaenda kumuona Mtume kwa mwendo wa haraka sana wa ngamia. Mara tu Mtume alipomuona Abu Dharr alitabasamu na alisema kabla Abu Dharr hajasema, “Abu Dharr! Usiwe na wasiwasi. Maji yametayarishwa kwa ajili yako hapa na sasa hivi. kwa hiyo, msichana aliyekuwa mtumishi wa Mtume alitayarisha maji na Abu Dharr akaoga.

Baadaye alikwenda kwa Mtukufu Mtume na akafundishwa jinsi ya kutumia udongo kwa ajili ya kuchukua Wudhu (Tayamamu)- (Musnad Ahmad bin Hanbal).

Abu Dharr alikuwa anaendesha maisha yake ambapo Vita ya Tabuk ilitokea mnamo mwaka wa 9 Hijiriya. Waandishi wa historia wanasema kwamba Mtume alijua kwamba Wakristo wa Syria walifanya uamuzi thabiti wa kushambulia Madina na wapiganaji elfu arobaini kutoka kwa Harcules, Mfalme wa Roma. Kwa hiyo, Mtume aliamua kuondoka kwenda Syria kama hatua ya tahadhari akiwa na wapiganaji kati ya elfu thelathini hadi arobaini. Alimteua Ali kuwa mbadala wake Madina. Baada ya kutayarisha jeshi lake aliondoka Madina.

Baada ya kuondoka Mtume wanafiki walianza kumdhihaki Ali kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alimwacha ili kupunguza mzigo wake mwenyewe. Katika kuwathibitishia kwamba wanafiki ni waongo aliamua kwenda kwa Mtume.

Kwa kufuatana na Mtume mahali paitwapo Jaraf na akamtaarifu kuhusu dhihaka ya wanafiki.

Mtume akasema, “Wanafiki ni waongo. Nimekuja hapa baada ya kukufanya wewe kuwa kaimu wangu. Ewe Ali hufurahikii cheo chako cha juu zaidi. Uhusiano wako na mimi ni sawa na uhusiano aliokuwa nao Harun na Musa ila tofauti moja tu ni kwamba hapatakuwepo na Mtume baada yangu.

Maana yake ni kwamba Musa alipokwenda kwenye Mlima wa Tur alimteua Harun kuwa kaimu (wakili) wake na yeye (Mtukufu Mtume) alifanya namna hiyo hiyo.”

Aliposikia hivi Ali alirudi Madina na Mtume aliendelea na safari ya kwenda Tabuk sehemu iliyokuwa kwenye mpaka wa iliyokuwa Falme ya Roma katika urefu wa vituo kumi kutoka Madina na Dameski. Alipofika Tabuk, alikaa hapo kwa muda wa siku kumi. Wakati wa kuwepo yeye hapo, alimtuma Sariys (jeshi la Uislamu linaloongozwa na mtu mwingine na si Mtume) sehemu zote, na alisisitiza kuwaita watu waingie kwenye Uislamu. Hakuna jeshi lililofika hapo kutoka Roma kwa madhumuni ya vita. Kwa hiyo, alilazimika kurudi Madina.

Wakati wa safari hiyo, siku moja usiku wanafiki walitaka kumuua wakati anapita kwenye bonde la Aqaba Zi Fata, kwa kumuogofya ngamia wake, ambaye angeweza kumwangusha chini, lakini Hudhayfah bin Yaman na Ammar bin Yasir walimwokoa.

Baada ya Mtukufu Mtume kuvuka bonde, alimwambia Huzayfah bin Yaman majina ya wanafiki waliotaka kumuua kwenye giza, na akamuamuru kuwa majina hayo iwe siri yake. Masahaba maarufu walikuwemo kwenye orodha hiyo. (Madarijum Nuduwah uk. 302).

Kwa mujibu wa Tahzibut Tahzib, watu hao walijaribu kupata majina hayo kutoka kwa Hudhayfah lakini hakufichua.

Hatimaye mmoja wapo wa masahaba hao alikiri mwenyewe, “Uniambie ama usiniambie, kwa jina la Mwenyezi Mungu, mimi nilikuwa miongoni mwa wanafiki hao!” Kwa ufupi, Mtume alirudi Madina wakati wa mwezi wa Ramadhani.

Wakati wa kuondoka kutoka Madina kwa madhumuni ya Vita ya Tabuk, Abu Dharr alikuwa naye. Lakini kwa kuwa ngamia wake alikuwa dhaifu na kukonda, hakuweza kuwa katika msafara. Abu Dharr, hata hivyo, alibaki nyuma ya msafara kwa umbali wa muda wa safari ya siku tatu.

Alijitahidi sana kuwa karibu na Mtume lakini alishindwa. Alihuzunika sana alipotambua kwamba haingewezekana yeye kuwa ndani ya msafara.

Kwa mujibu wa maelezo mengine, alipobaki nyuma, watu fulani walimwambia Mtume kwamba ilikuwa vigumu sana Abu Dharr kuwa naye. Aliposikia hivi, Mtume akasema, “Mwacheni huyo hivyo alivyo. Atafika Inshallah. Kwa hiyo msafara uliendelea na Abu Dharr alizidi kubaki nyuma akiwa amefadhaika na wasi wasi. Wakati mwingine alifikiria kurudi Madina na halafu tena alishawishika kuendelea na safari hadi Tabuk kwa jinsi yoyote ile kwa sababu kuwa nyuma ya Mtume ni hali ambayo ilimtesa sana.

Aliendesha ngamia wake kwa msisimko mkubwa lakini hakuweza kwenda haraka kwa sababu ya udhaifu wake.

Alipogundua hivi, aliteremka kutoka kwenye ngamia na akachukua mzigo wake wote na kubeba mgongoni mwake na akaendelea na safari kwa mguu. Ulikua msimu wa joto kali. Kwa hiyo, ni jambo linalojulikana kwa wasafiri kiasi cha ukali wa kiu ambayo ingempata.

Alikuwa anatembea na mzigo mgongoni mwake wakati ambapo kiu ilikaribia kumwelemea. Tayari alikwisha choka na wakati huo kiu ilifanya hali yake kua mbaya zaidi. Abu Dharr akiwa na kiu kali, alitafuta maji huku na kule akaona maji ya mvua yaliyokuwa kwenye dimbwi.

Akafika kwenye dimbwi la maji ambapo alikuwa na kiu sana, na alitaka kunywa maji yaliyojaa kwenye kiganja chake, ambapo ghafla, aliwaza kwamba maji hayo yalikuwa baridi sana na haikuwa vema yeye kunywa maji hayo kabla ya Mtukufu Mtume. Kwa hiyo, baada ya fikra hii kuingia akilini mwake akayamwaga maji hayo na akajaza maji hayo kwenye gudulia.

Abu Dharr alikuwa peke yake huku akiwa na kiu kali sana na gudulia lililojaa maji hadi akafika Tabuk.

Mara tu alipofika Tabuk, Waislamu walimuona na wakamtaarifu Mtume kuhusu kuwasili kwa msafiri aliyedhikika. Mara moja alisema, huyu ni sahaba wangu, Abu Dharr. Kimbieni, enyi masahaba wangu, na mleteni kwangu. Waliposikia hivyo, masahaba walikwenda haraka kwa Abu Dharr na wakamfikisha kwa Mtume.

Baada ya Mtume kuuliza kuhusu afya yake, akasema, “Ewe Abu Dharr, unayo maji. Kwa nini basi unakiu kali namna hii?”

Abu Dharr; “Bwana wangu, kama unavyoona, maji yapo, lakini siwezi kunywa.”
Mtume; “Kwa sababu gani?”

Abu Dharr; “Bwana wangu! Nilipokuwa njiani. Kuja hapa niliona maji karibu na kilima, lakini dhamiri yangu haikuniruhusu kunywa maji haya kwa ajili yako. Mimi nitayaonja baada ya wewe kunywa.”
Aliposikia hivi Mtume alisema; “Ewe Abu Dharr! Mwenyezi Mungu Atakuhurumia. Utaishi peke yako na utaondoka hapa duniani peke yako. Utafufuka peke yako mnamo Siku ya Hukumu. Utaingia Peponi peke yako na kundi la watu wa Iraq watapata furaha kamili kwa sababu yako, ni kwamba watakuosha watakuvika sanda na kusalia maiti yako.”

Tukio hili si tu linaonyesha mapenzi makubwa ya Abu Dharr kwa Mtume lakini kupitia kwenye tukio hili Mtukufu Mtume kwa wazi kabisa alitabiri matatizo na majanga ambayo yangemfika Abu Dharr katika maisha yake. Amenukuu tukio kutoka kwa Bin Babway kutoka kwa Abbas kwamba siku moja Mtume (s.a.w) alikuwa ameketi ndani ya msikiti wa Quba na masahaba wake wengi walikuwa wamemzunguka.

Alisema, “Mtu ambaye atakuwa wa kwanza kuingia kwenye lango la Msikiti huu, atakuwa ametoka kwenye kundi la watu wa Peponi.” Baada ya muda mfupi Abu Dharr aliingia kupitia kwenye lango hilo. Alikuwa wa kwanza ambaye alitoka nje akiwa peke yake. Mtukufu Mtume akasema hapo hapo, “Ewe Abu Dharr! Wewe unatoka kwenye watu wa Peponi.” Aliendelea kusema, wewe utafukuzwa Makkah kwa sababu ya kuwapenda watu wa Nyumba yangu. Utaishi ugenini na utakufa katika hali ya upweke. Kundi la watu wa Iraq wataneemeka kwa kushughulikia maziko yako na utakuwa pamoja na mimi Peponi.”