Sura Ya Pili

Baada ya kumsikiliza kaka yake, Abu Dharr alisema, “Sijaridhishwa na ripoti yako. Nitakwenda huko mimi mwenyewe, nimuone na nimsikilize mimi binafsi.”

Abu Dharr alifika Makkah, aliingia kwenye eneo la Ka’abah na akaanza kumtafuta Mtume, lakini wala hakumuona pale, ama kusikia akitajwa. Alikaa hapo hadi machweo ya jua. Ali aliwasili hapo na akapita karibu na pale alipoketi Abu Dharr. Alimuuliza, “Unaonekana kuwa msafiri. Ni kweli?”

Abu Dharr: “Ndio.”
Ali: “Njoo nifuate.”

Ali alimchukua nyumbani kwake. Wote wawili walikuwa kimya wakati wanakwenda nyumbani kwa Ali. Abu Dharr hakumuuliza Ali kitu chochote hadi walipofika nyumbani. Ali alitayarisha mahali pa kulala na Abu Dharr akalala. Kesho yake asubuhi alikwenda tena Ka’abah kumtafuta Mtume. Wala hakumuuliza mtu yeyote ama mtu yeyote kumwambia chochote. Abu Dharr aliendelea kungoja kwa hamu kubwa hadi mwisho wa siku. Ali alikwenda tena kwenye Al-Ka’abah kama kawaida yake na alipita mbele ya Abu Dharr: mara alipomuona Abu Dharr, alimuuliza: “Kwa nini? hujaenda nyumbani hadi sasa?”

Abu Dharr: “Hapana.”
Ali: “Vema! Sasa twende nifuate Mimi.”
Wote walili walikuwa wanakwenda kimya Ali alipouliza, “kwa nini! Umekuja hapa kwa sababu gani?”
Abu Dharr: “Ninaweza kukuambia sababu endapo hutamwambia mtu mwingine.”
Ali: “Sema wazi chochote unachotaka kusema. Sitamwambia mtu yeyote.”

Abu Dharr: “Nimekuja kumuona mtu baada ya kupata taarifa kwamba mtu huyu anajiita yeye Mtume. Nilimtuma kaka yangu azungumze naye. Aliporudi hakunipa taarifa ya kuridhisha. Sasa, nimeamua kumuona mtu huyu mimi mwenyewe.”

Ali: “Umefika. Sasa ninakwenda pale alipo. Nifuate. Ingia popote nitakapoingia. Endapo nitaona hatari yoyote nitaanza kukiweka sawa kiatu changu, nikiwa nimesimama karibu na ukuta, na nikianza kufanya hivyo, wewe rudi.”

Abu Dharr anasema, “Ali alinipeleka hadi ndani ya nyumba. Niliona nuru katika umbo la mtu inaonekana hapo. Mara tu nilipo muona, nilivutiwa kwake na nikahisi ninataka kubusu miguu yake. Kwa hiyo, nilimsalimia Assalamu Alaykum.” (Alikuwa mtu wa kwanza kumsalimia Mtume wa Uislamu kwa desturi ya Kiislamu, kabla ya kusilimu).

Alijibu salamu, akasema, “Waa Alaykum as Salam, wa Rahmatullah wa Barakatuh. Ndio Unataka nini?”
Nilijibu; “Nimekuja kuwako kwa moyo na imani.”
Alinielekeza mambo fulani muhimu na akanitaka nikariri Kalimah (Shahada) yaani (La ilaha illalah Muhammadun Rasulul lah) nilisoma hivyo, na kwa hiyo nikaingia kwenye Uislamu.

Baada ya hapo, aliondoka kwenda Ka’abah. Alipofika hapo alipoona kundi kubwa la makafiri wa kabila la Quraishi, alisema kwa sauti kubwa, “Sikilizeni enyi Maquraishi nina shuhudia kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja na Muhammad ni Mtume Wake.”

Sauti hii iliwaogopesha Maquraishi. Hisia za Quraishi kwamba heshima ya masanamu yao imeshushwa iliwatia wasiwasi sana.

Hatimaye watu walimzunguka Abu Dharr wakaanza kumpiga sana hadi akazirai. Ilibakia kidogo afe lakini Abbas bin Abd al-Mutalib alifika hapo ghafla. Alipoona kwamba mfuasi wa Muhammad alikaribia kufa, alilazimika kumlalia Abu Dharr.

Akasema: “Enyi watu! Nini kimewatokea ninyi? Munataka kumuua mtu mkubwa wa kabila la Bani Ghifar. Mmesahau kwamba nyinyi hufanya biashara na Bani Ghifar na huwa mnatembelea huko mara kwa mara. Hamliogopi kabila lake kabisa!”

Baada ya kusikia hayo, watu hao waliondoka hapo na Abu Dharr ambaye alikuwa anatoka damu, alinyanyuka na kwenda kwenye kisima cha zam zam.

Alihisi kiu sana kwa sababu ya majeraha makubwa na kutoka damu nyingi. kwa hiyo, kwanza alikunywa maji halafu akasafisha mwili wake. Baada ya hapo alikwenda kwa Mtukufu Mtume huku akigumia. Mara tu Mtume alipomuona katika hali ile, alisikitika sana na akasema, “Abu Dharr! Umekula au kunywa chochote?”

Abu Dharr: “Bwana wangu! Nimeona nafuu kidogo baada ya kunywa maji ya Zam zam.”
Mtume: “Bila shaka maji hayo hutoa nafuu.”

Baada ya hapo alimliwaza Abu Dharr na akampa chakula. Ingawa Abu Dharr aliumia sana kwa sababu ya hotuba yake, bado hamasa ya dini haikumruhusu aondoke kwenda kwao kimya kimya. Imani yake ilimtaka awafanye Maquraishii waamini kwamba akili ya mwanadamu hudharau ushirikina wa uchaji masanamu.

Aliondoka hapo akaenda kwenye eneo la Al-Ka’abah tena. Alisimama sehemu iliyoinuka na akaita kwa sauti ya ushupavu imara. “Enyi watu wa Quraishii! Nisikilizeni! Ninashudia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu na ninashuhudia kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu.”

Waliposikia hivyo wale wapotovu ambao waliona misingi ya miungu yao inatikiswa na ambao walikasirishwa sana na hotuba yake ya mwanzo, kwa mara nyingine waligutushwa na wakawa katika hali ya wasiwasi na wakageuka kuelekea upande inakotoka sauti na haraka sana walikusanyika na kumzunguka yeye. Walikuwa wanapiga kelele “Muueni huyu Ghifari haraka iwezekanavyo kwani yeye nia yake ni kuwatukana miungu wetu.”

Mkusanyiko wote ulisema kwa sauti moja, Mueni Abu Dharr.” Kwa hiyo walimpiga Abu Dharr hadi akazirai.

Abbas bin Abdul Muttalib alipoona hivi alijitokeza mbele na kumlalia Abu Dharr kama ilivyofanya jana yake, na akasema; “Enyi Quraishi! Nini kimewatokeeni kwamba mnamuua mtu wa kabila la Ghifari ingawa mnao uhusiano mzuri na kabila lake na biashara yenu inaendelea vizuri kwa msaada wa kabila lake. Msiendelee kumpiga.”

Baada ya kusikia haya, watu wote waliondoka na kumwacha Abu Dharr akiwa amepoteza fahamu. Alipopata fahamu, alikwenda kwenye kisima cha Zam zam! na baada ya kunywa maji alisafisha mwili wake uliokuwa umetapakaa damu.

Abdullah Subaiti ameandika kwamba ingawa Abu Dharr aliteseka sana kwa majeraha lakini hata hivyo aliwalazimisha Quraishi kuwa na maoni kwa mujibu wa hotuba zake kwamba Uislamu ulikwisha enea kwa watu na uliwavutia sana.

Kwa ufupi Abu Dharr alinyanyuka kutoka kwenye kisima cha Zamzam na kwenda kwa Mtukufu Mtume. Mtume alipomuona Abu Dharr katika hali hiyo alisema, “Ewe Abu Dharr! Ulikwenda wapi na kwa nini umekuwa katika hali hii?” Abu Dharr alijibu, “Nilekwenda kwenye Ka’abah tena. Nilitoa hotuba tena na nikatapakaa damu kwa kipigo. Sasa nimekuja kwako baada ya kuoga maji ya Zam zam.”

Mtume akasema; “Ewe Abu Dharr! Sasa ninakuamuru urudi nchini kwako mara moja. Nisikilize! Utakapofika nyumbani kwako, mjomba wako tayari atakuwa amekufa. Kwani hana mrithi mwingine isipokuwa wewe, wewe utakuwa mrithi wake na kuwa mmiliki wa rasilimali yake. Nenda ukatumie mali hiyo kwa kutangaza Uislamu. Baada ya muda mfupi nitakwenda na kuhamia Madina mji wa mitende. Wewe endelea kufanya kazi huko hadi nitakapohamia huko.” Abu Dharr alisema, “Ndio! Bwana wangu vyema sana. Nitaondoka hivi karibuni na kuendelea kutangaza Uislamu.” Sahih Bukhari, Sura ya Uislamu na Abu Dharr, chapa ya Misri, 1312 Hijiriya.