Sura Ya Sita

Shahidi Thalit Allamah Nurullah Shustari ameandika:
Abu Dharr alikuwa mmoja wa masahaba mashuhuri sana na anahesabiwa miongoni mwa masahaba wa mwanzo kabisa walioingia kwenye Uislamu. Katika kuukubali Uislamu alikuwa mtu wa tatu, hivyo kwamba, aliingia kwenye Uislamu baada ya mama wa Waumini Khadijahtul Kubra na Amiri wa Waumini Ali. Kwa mujibu wa mwandishi wa kitabu cha ‘Isti’ab’ alikuwa na sifa ya juu katika ujuzi, kushikilia maadili, uchaji Mungu na kuwa mkweli, miongoni mwa masahaba wote.

Ali amesema kwamba, Abu Dharr alifanikiwa nafasi hiyo katika kupata na kuelewa mafundisho ya kidini ambayo hakuna mwingine ambaye angeyafikia. Mtukufu Mtume alikuwa anasema, “Abu Dharr yu kama Mtume Isa katika umma wangu. Abu Dharr anashikilia maadili kama alivyofanya Mtume Isa.”

Kwa mujibu wa hadithi, mtu anayetaka kuona mfano wa Mtume Isa amuone Abu Dharr. Shaykh Saduq katika kitabu chake Uyumul Akhbar al-Ridha ameandika kwamba Imamu Ali al-Ridha amesema kutoka kwa mamlaka ya wahenga wake kwamba kwa mujibu wa Hadith ya Mtume, “Abu Dharr ni mtu mkweli wa umma huu.”

Ali anasema kwamba Abu Dharr ndiye mtu peke yake asiye jali kamwe kushutumiwa kwa sababu ya Mwenyezi Mungu maamrisho na maagizo yake, ni kwamba, yeye alisema lolote ambalo ni haki na atatekeleza kwa vitendo, na wala hatajali vitisho vyovyote kuhusu jambo hili, ama kuogopeshwa na uwezo wa serikali.

Wanavyuoni wameandika kwamba Abu Dharr alitoa kiapo cha uaminifu kwa Mtume kwa ahadi kwamba katika imani ya Mwenyezi Mungu hangejali mtu yeyote anayemshutumu na kwamba angesema ukweli hata ungelikuwa na athari ya aina yoyote ile.

Ukweli na ujasiri ni sifa ambazo hata watu mashuhuri sana hushindwa kushikilia. Mtukufu Mtume ameitabiri sifa hii ya Abu Dharr na akasema kwamba Abu Dharr angetoa mchango mkubwa katika jambo hili na ataendelea kushikilia hata katika mateso makali ambayo angeyavumulia.

Mtume alisema: “Hapana mtu mkweli zaidi ya Abu Dharr kati ya utando wa mbingu na ardhi.” (Mustadrak Hakim uk. 342 Isabah bin Hajar Asqalani, Juz. 2, uk. 622, Feheist Tusi, uk. 70).

Katika ufafanuzi wa hadithi hii Allamah Subaiti ameandika: “Mtukufu Mtume aliwahutubia masahaba wake alisema: “Enyi masahaba wangu! Ni nani miongoni mwenu ambaye atakutana na mimi mnamo siku ya Hesabu katika hali hiyo hiyo ambayo nitamwacha nayo hapa duniani?”

Waliposikia hivi, kila mmoja wao alinyamanza kimya isipokuwa Abu Dharr aliyesema kuwa mtu huyo ni yeye. Mtukufu Mtume akasema, “Bila shaka! umesema kweli.”

Baada ya hapo, aliongeza, “Enyi masahaba wangu! kumbukeni ninayowaambieni. Hakuna mtu kati ya mbingu na dunia ambaye ni mkweli zaidi kuliko Abu Dharr.” (Tazama Tarikhi Himmah uk. 251).

Allamah Majlis ameandika maelezo baada ya kunukuu hadithi hiyo hapo juu kwenye kitabu chake (Hayatul Qulub).

Bin Babwayh ameeleza kupitia mamlaka ya kuaminika kwamba mtu fulani alimuuliza Imamu al-Sadiq endapo Abu Dharr alikuwa bora zaidi ya Ahlul –Bait wa Mtukufu Mtume au vinginevyo. Imamu Alisema, “Mwaka mmoja una miezi mingapi?” Alijibu, “Kumi na miwili.” Imamu akasema, “Miongoni mwa miezi hiyo mingapi inaheshimika na kutakaswa?” Akasema, “Miezi minne,” Imamu aliuliza, “Mwezi wa Ramadhani umejumuishwa katika miezi hii minne?” Akasema, “Hapana.” Imamu aliuliza, “Mwezi wa Ramadhani ni bora zaidi au miezi hiyo ni bora zaidi.”

Akajibu, Mwezi wa Ramadhani ni bora zaidi.” Imamu Akasema, “Ndivyo ilivyo na sisi, Ahlul-Bait. Huwezi kumlinganisha yeyote na sisi.”

Siku moja Abu Dharr alikuwa ameketi katika kundi la watu ambao walikuwa wanaeleza maadili ya taifa hili. Abu Dharr alisema, “Ali ni bora kuliko wote katika taifa hili, na yeye ni mpaka wa Pepo na Jahanamu, ni Siddiq na Farooq wa Umma na utibitisho wa ujuzi wa mambo ya dini ya taifa hili.” Waliposikia maelezo haya kutoka kwake wanafiki hao waligeuza nyuso zao na kutazama upande mwingine na kukanusha tamko lake na kumwita muongo. Haraka Abu Amamah alinyanyuka na akaenda kwa Mtukufu Mtume na kumwambia alichosema Abu Dharr, na jinsi kundi hilo lilivyokataa kukubali. Mtukufu Mtume akasema, “Hapana mtu kati ya ardhi na mbingu ambaye ni mkweli kuliko Abu Dharr.”

Kitabu hiki hiki kimeeleza kupitia mamlaka nyingine kwamba mtu mmoja alimuuliza Imamu Jafar al-Saqiq endapo hadhithi hiyo ilikuwa sahihi ambamo Mtukufu Mtume ametangaza hivyo. Imamu alisema, “Ndio.” Akasema, “Kama ndio hivyo, Mtukufu Mtume, Ali, Imamu Hasan, na Imamu Husein na nafasi yao ni ipi?”

Imamu akajibu, “Sisi ni kama mwezi wa Ramadhani ambao ndani mwake upo usiku huo ambao ibada yake ni sawa na ile ya miezi elfu moja ambapo masahaba ni sawa na mwezi unao heshimika ikilinganishwa na miezi mingine, na hapana mtu anayeweza kulinganishwa na sisi, Ahlul-Bait.”

Ni dhahiri kama mwanga wa mchana kutoka kwenye hadithi hiyo hapo juu ya Mtukufu Mtume kwamba Abu Dharr alikuwa hana wa kumlinganisha naye katika ukweli.

Maelezo na ufafanuzi wa hadithi hii hii kama yalivyotolewa na Subaiti inaeleza kwamba Abu Dharr ataondoka hapa duniani akiwa katika hali ile ile ambayo Mtume alimwacha nayo, na atamuona akiwa katika hali hiyo hiyo huko Peponi.

Kama hadithi hii ikitazamwa kwa umakini zaidi, msimamo imara wa Abu Dharr kwenye njia ambayo iliimarishwa na Mtukufu Mtume unadhihirisha uadilifu wake.

Wanavyuo wanakubaliana kwenye mtazamo huu kwamba Abu Dharr hakutetereka hata nchi moja kutoka katika njia ya Mtukufu Mtume. Baada ya Mtume, hata sabaha kama Salman alilazimishwa kutoa kiapo cha utii na siku moja alipigwa sana ndani ya msikiti hadi shingo yake ikavimba. Lakini Abu Dharr kamwe hakunyamaza.

Allamah Subaiti ameandika: “Abu Dharr alikuwa mmojawapo wa wafuasi wa Mtukufu Mtume ambao walishika njia yao na walisimama imara kuhusu agano lao walilofanya na Mwenyezi Mungu, Ali, na Mtukufu Mtume kwa uaminifu, alifuata nyayo zake na kuiga mwenendo wake. Hakuachana na Imamu Ali hata kidogo, alimfuata hadi mwisho na akapata faida ya nuru ya ujuzi wake.”

Allamah Majlis ameandika: “Bin Babwayh anaeleza kupitia kwa mamlaka ya kuaminika kutoka kwa Imamu Ja’far al-Sadiq kwamba siku moja Abu Dharr alikuwa anapita karibu na Mtume wakati Jibril alikuwa anazungumza naye katika faragha katika umbile la ‘Dahyah Kalbi.’

Abu Dharr alirudi nyuma kwa kudhani kwamba Dahyah Kalbi alikuwa anazungumza na Mtume kwenye faragha. Aliporudi Jibril alimwambia Mtume, “Ewe Muhammad! Abu Dharr alikuja muda mfupi uliopita na akarudi bila kunisalimia.

Amini kwamba endapo angenisalimia, hakika ningejibu salamu yake. Ewe Muhammad! Abu Dharr anayo dua yake ambayo inajulikana kwa watu wa Peponi. Tazama! Nitakapoandoka kwenda mbinguzi muulize kuhusu taarifa hii. Akasema, “Vema.”

Jibril alipoondoka na Abu Dharr akarudi kwa Mtume, Mtume akasema; “Ewe Abu Dharr! Kwa nini hukutusalimia ulipokuja hapa muda mfupi uliopita? Abu Dharr alijibu, Nilipokuja, Dahyah Kalbi alikuwa ameketi na wewe na mlikuwa na mazungumzo. Nilidhani mnazungumza kuhusu mambo fulani ya siri na mimi sikuona vema kuingilia kati.

Kwa hiyo nikarudi. Mtukufu Mtume akasema, “Huyo hakuwa Dahyah Kalbi lakini huyo alikuwa Jibrili aliyenijia katika umbile la Dahyah Kalbi. Ewe Abu Dharr! Alikuwa ananiambia kwamba endapo ungemsalimia naye angejibu salamu yako.

Pia aliniambia kwamba unayo dua ambayo inajulikana sana miongoni mwa watu wa Peponi.” Abu Dharr aliondoka akiwa na haya sana na akaonyesha kujutia kitendo chake.

Halafu Mtukufu Mtume akasema, “Ewe Abu Dharr! Niambie dua unayosoma na ambalo linazungumziwa sana mbinguni” Abu Dharr akamwambia Mtume “Dua hiyo ni hii ifuatayo:

Allahumma inni Asalukal Amna wal Imana bika wat tasdiqa bi nabiyyika wal ‘Aafiyata min jami’il blaa’i’ washukra ‘alal ‘afiyat wal ghina’an shirarin naasi.” (Hayatul Qulub, Juz.1, uk. 166, Rabiyl Abrar, sura 23 iliyoandikwa kwa mkono, Mamba’us Sadiqin).

Zipo hadithi nyingi sana upande wa madhehebu ya Shia na Suni ambamo maagizo maalum yametolewa kuwapenda masahaba wanne. Wanavyuo wanasema kwamba masahaba hao wane ni Ali, Abu Dharr, Miqdad na Salman.

Umar Kashi ameandika kwenye Rijal yake, Abu Jafar Qummi kwenye Khasail, Abdullah Humayri kwenye Qurbul Asnad, Shaykh Mufid kwenye Iktisas, Ayashi kwenye maelezo yake, Saduq kwenye Uyun Akhbar al-Riza, Abdul Barr kwenye Istiab, Bin Sad kwenye Tabaqat na mwandishi wa Usudul Ghabah kwenye kitabu chake:

Mtukufu Mtume (s.a.w) amesema kwamba Mwenyezi Mungu amemuagiza kuwaweka masahaba wangu wanne kuwa marafiki zangu na niwapende, na pia nimeambiwa kwamba Yeye pia amewafanya marafiki masahaba hawa: Ali bin Abi Talib, Abu Dharr Al-Ghifari, Miqdad bin Al-Aswad na Salman Farsi (Mishkat Sharif uk. 572).

Hadithi inasema kwamba hao masahaba wanne ni Salman, Abu Dharr, Miqdad na Ammar. Wanachuo wanafikiria kwamba hawa masahaba wanne ambao Pepo na wakazi wa Pepo wanawapenda sana. Inasimuliwa kwenye hadithi kwamba mtangazaji atatangaza mnamo siku ya Hukumu, “Wako wapi hao masahaba wa Muhammad bin Abdullah ambao hawakuvunja ahadi yao ya kuwapenda Ahlul Bait al-Risalah, lakini walikuwa imara kuendelea nayo?” Salman, Miqdadi, na Abu Dharr watasimama.

Allamah Nuri ameandika kwa kumnukuu Raudhatul Waidhin cha Shaykh Shahia Muhammad bin Ahmad bin Ali bin Fital Naishapuri kwamba Imamu Muhammad al-Baqir amesema, zimo daraja kumi za imani. Miqdad amepata daraja nane, Abu Dharr amepata daraja tisa na Salman amepata zote kumi.

Dhamana ya udugu inakumbusha hilo tukio la kihistoria ambalo Mtukufu Mtume aliasisi udugu katika jozi moja ya masahaba wake kabla na baada ya kuhamia Madina.

Kabla ya Hijiriya aliasisi dhamana ya udugu baina ya kila masahaba wawili ili kwamba waweze kuhurumiana kwenye udugu huu alifikiria mfanano wa tabia wa masahaba wawili. Aliwafanya hao masahaba wawili kuwa ndugu wa kila mmoja kwa kuwa tabia zao zilikuwa zinafanana na kulingana kwa mwenendo. Kwa njia hii alitangaza udugu kati ya Abu Bakr na Umar, Talhah na Zubayr, Uthman na Abdur Rahman bin Auf, Hamza na Zayd bin Harith, Salman na Abu Dharr na Ali na yeye Mtume.

Halafu baada ya miezi mitano au minane, baada ya Hijiriya, Mtume (s.a.w) kwa mara nyingine aliasisi dhamana ya udugu kwa njia ile ile. Ilikuwa muhimu kuanzisha udugu baina ya wahamiaji na wenyeji wa Madina kwa lengo la kujenga misingi ya kuhurumiana baina yao. Mtume alianzisha udugu miongoni mwa masahaba hamsini.

Allamah Sahibli Nomani ameandika: “Kwenye himaya ya Uislamu yapo maadili na tabia safi sana. Ilikuwa ikizingatiwa kwamba masahaba ambao walipewa dhamana ya udugu baina yao walikuwa na mfanano wa upendo. Muungano huu wa upendo baina ya mwalimu na mwanafunzi ni muhimu kwa lengo la usilimishaji wa ujuzi. Baada ya kupima ilionekana kwamba muungano huu wa upendo wa watu hao wawili waliofanywa ndugu ulizingatiwa, tunaona kuwa ni vigumu kujua upendo wa mamia ya watu kwa muda mfupi, hivyo lazima tukubali kwamba uamuzi wa Mtukufu Mtume ulifanyika kwa sifa maalumu ya Utume. (Siratu Nabi, Juz. 1, uk. 112)

Juu ya hayo, hili pia linafaa kukumbukwa kwamba Mtume hakupata mtu mwenye upendeleo unaofanana na ule wa Ali ama miongoni mwa Muhajirina (wahamiaji) au Ansari. Ali akasema, “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu umeniunganisha na nani?” Akasema, “Wewe ni ndugu yangu hapa duniani na baada ya hapa duniani (Peponi)”

Ndio maana ya Ali alitangaza mara kwa mara kwenye mimbari ya Msikiti wa Kufa, “Mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu na ndugu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu.” (Tarikh Abul Fida, Juz. 1, uk. 127) Mtukufu Mtume pia alisema kuhusu Salman, “Salman ni mmoja wetu sisi Ahlul Bait.”

Kwa maoni yangu hii pia ni mojawapo ya sifa bora za Abu Dharr kwamba mtu mwenye uamuzi uliokomaa kama Mtukufu Mtume alimtangaza kuwa ndugu yake Salman. Allamah Subaiti amenukuu usemi wa Saleh al-Ahwal ambaye alimsikia Imamu Jafar al-Sadiq akisema kwamba Mtukufu Mtume alianzisha dhamana ya udugu baina ya Salman na Abu Dharr na alimwambia Abu Dharr asije akampinga Salman. (Abu Dharr al-Ghifar uk. 86, Kama ilivyonukuliwa na Usulul Kafi).

Hadith ya Abu Dharr ni ya juu sana hivyo kwamba aya za Quran Tukufu zimeteremshwa kwa ajili ya kumsifu yeye. Moja ya Aya hizo ni kama ilivyonukuliwa hapa chini:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَانَتْ لَهُمْ جَنَّاتُ الْفِرْدَوْسِ نُزُلًا{071}

“Hakika wale walioamini na wakatenda mema mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo ya Firdausi.” (Surah 18:107).

Imamu Jafar al-Sadiq anasema kwamba Aya hii imeteremshwa kuhusu Abu Dharr, Miqdadi, Ammar na Salman.

Kwa mujibu wa hadithi, Mtume alisema kwamba Mwenyezi Mungu alimuamuru ampende Salman, Abu Dharr, Miqdadi na Ammar na akaongeza zaidi kwamba yeye mwenyewe aliwafanya marafiki zake.
Kwa mujibu wa hadithi nyingine Mtume alisema, “Pepo inayo shauku na watu hawa.” (Hayatul Qulubi, Juz.2)

Allamah Gilani ameandika kwamba heshima ya Abu Dharr na hadhi yake ni hali zilizoongezeka sana siku hadi siku katika mazingira ya Mtume, hivyo kwamba, Mtukufu Mtume alipokwenda kwenye Vita ya Zaat al-Ruqa1 alimfanya yeye kuwa mtemi wa Madina, na si yeye tu kuwa mtemi lakini kwa ajili yake wakati fulani Ghifari wengine pia walipata cheo hiki. Mathalani, Mtukufu Mtume alimteua Saya’ bin Urfah al-Ghifari kama Mtemi wa Madina wakati wa Vita ya Daumatul Jandal, (Zaadul Ma’ad).

Ilikuwa kawaida ya huko Arabuni kwamba wakati wowote ilipotokea mtu anapanda ngamia alimfanya mtu wake maalumu kuwa ‘sanjari’ wake. Sanjari alipoketi nyuma, alikuwa akishika hatamu kwa kuzungusha kiunoni. Kwa mujibu wa hadith hii ya kawaida Mtukufu Mtume pia alimfanya mtu kuwa Sanjari wake.

Wakati wa hija ya mwisho, Sanjari wake alikuwa Fazal bin Abbas bin Abdul Muttalib.

Masahaba waliona kuwa ni heshima kuwa Sanjari. Sanjari wa Mtume aliitwa ‘Radifun Nabi.’ Wasomi wanasema kwamba Mtume zaidi alimpa heshima hii Abu Dharr. Mtume alikuwa na desturi ya kupanda wanyama wengine wadogo.

Punda pia mara nyingi walitumika kumbeba Mtume. Alikuwa na tabia ya kumruhusu Abu Dharr kukaa nyuma yake na waliendelea na safari huku wanazungumza. (Tabaqat Ibn Sa’d).
Shah Walyullah Dehlavi, anapoelezea ghasia kwenye Uislamu, ameandika kuhusu tukio la Harrah. Abu Dawudi amemnukuu Abu Dharr ambaye alisema, “Siku moja niliketi nyuma ya Mtukufu Mtume tukiwa tumepanda punda.

Tulipokuwa nje ya Madina- sehemu isiyokaliwa na watu, aliniuliza hali yangu ingekuwaje wakati njaa itakapoikumba Madina, na ningeshindwa kuvumilia kabla ya kufika msikitini baada ya kutoka kitandani mwangu.” Nikasema, “Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanajua zaidi.”

Akasema, “Ewe Abu Dharr! Usije ukaenda kuomba wakati huo.” Halafu akasema, “Hali yako itakuwaje ambapo bei ya kaburi italingana na ile ya mtumwa kwa sababu ya kiasi kikubwa cha vifo?” Nikasema. “Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanajua zaidi.” Akasema, “Ewe Abu Dharr! Jizoeze uvumilivu.”

Halafu aliuliza tena, “Ewe Abu Dharr! Hali yako itakuwaje ambapo patatokea mauaji ya halaiki hapa Madina hivyo kwamba mawe na mchanga vitaloa damu?” Nikajibu, “Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanajua zaidi.” Alisema, “Wakati huo utatakiwa ukae nyumbani kwako.”

Nilimuuliza, “Itabidi nishike upanga wakati huo?” Alijibu, “Kama ukifanya hivyo utafikiriwa kuwa ni mshirika wao.” Halafu nilimuuliza, “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Nifanye nini wakati huo?” Alisema, “Hata kama unaogopa kwamba mng’ao wa upanga utafanya macho yako yasione vizuri, funika uso wako tu kwa kipande cha nguo yako na usipigane, lakini nyamaza kimya.”

Maelezo haya yapo ukurasa wa 176 kwenye Juzuu ya 5 ya Musnad Ahmad bin Hanbal iliyochapishwa Misri. Kwamba Mtukufu Mtume alikuwa na kawaida ya kumdokeza Abu Dharr siri zake na akasema kwamba alikuwa anamwamini sana. Abu Dharr naye pia, alikuwa mwangalifu sana kuficha siri hizo. Wakati wowote alipoulizwa kuhusu Hadith, alisema, “Isipokuwa mambo yale ambayo Mtukufu Mtume ameniambia kuwa ni siri, nipo tayari kukueleza kila kitu. Unaweza kuniuliza chochote unachotaka.”