Sura Ya Tano

Historia inashuhudia kwamba Abu Dharr alielimika sana baada ya kuwa Muislam hivyo kwamba hapakuwepo wa kumlinganisha naye miongoni mwa masahaba. Alipata utakaso ulio bora wa imani na unyofu wa moyo hivyo kwamba alihakikisha kwamba yeye ni nguzo ya nuru kwa watu wenye utambuzi. Alizirutubisha akili za watu kwa ushauri, baada ya kuja kwa Uislamu, aliwafundisha watu masomo ya usawa na upendo na aliwafundisha jinsi ya kumtii Mwenyezi Mungu na Mtukufu Mtume.

Maisha yake ya Kiislamu yaliheshimika sana hivyo kwamba hapakuwepo na mtu wa kulingana naye miongoni mwa waumini. Abdulah Subaiti ameandika kwamba Abu Dharr alijipatia sifa sana miongoni mwa masahaba hao ambao walifanya vizuri kuzidi wengine katika uchaji Mungu, kujihini, kumuabudu Mwenyezi Mungu, ukweli, uimara wa imani na hakuna wa kumfananisha katika kujisalimisha kwa Radhi ya Mwenyezi Mungu.

Wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w) chakula chake cha kila siku kilikuwa kilo tatu za tende na aliendelea hivyo hadi mwisho wa maisha yake.

Anaendelea kuandika Abdullah Subaiti kwamba Abu Dharr alinyanyuliwa juu sana katika maadili na tabia yake hiyo kwamba Mtukufu Mtume alimjumuisha kwenye kundi la Ahlul-bait (watu wa Nyumba ya Mtume) kama alivyo mjumuisha Salman Farsi. Hafiz Abu Naim anasema kwamba Abu Dharr alikuwa msalihina, mtu mchaji Mungu, na alikuwa na moyo ulioridhika. Alikuwa mtu wa nne katika msululu wa kukubali Uislamu. Aliacha maovu yote hata kabla ya kuanza kutekeleza sharia ya Kiislamu.

Hili lilikuwa lengo lake alilolihifadhi, kukataa kuwatii watawala dhalimu. Alikuwa imara katika kuvumilia maumivu na huzuni. Alijipatia sifa ya juu katika kuhifadhi hadithi na nasaha za Mtukufu Mtume.

Abu Naim ameandika kwamba Abu Dharr alitoa huduma kubwa kwa Mtukufu Mtume na alipata ujuzi wa vipengele vya imani na utekelezaji akiwa naye, na alijiepusha na maovu. Sifa yake maalum ilikuwa kuuliza maswali kwa Mtukufu Mtume.
Alijifunza kuhifadhi maana na fahamu zilizotolewa na yeye (Mtume) na alikuwa na shauku sana kuhusu jambo hili.

Kwa ufupi, kwa kadiri alivyoweza, hakuridhika na kuuliza maswali tu lakini pia alikusanya hazina kubwa ya ujuzi wa Kiislamu kwa ajili ya wafuasi wa Uislamu.

Kitendo kingine maarufu cha maisha yake ni kwamba alifuata nyayo za Mtukufu Mtume alizozitilia maanani na kuzithibitisha, na ambazo aliziamuru zifuatwe.

Akaambatana na Imamu Ali baada ya Mtukufu Mtume na hakumkana hata kidogo. Alimfuata na alipata manufaa kutokana na ujuzi mkubwa wa Imamu Ali. Abu Dharr alihifadhi akilini ukarimu, maadili mema na tabia njema za Imamu Ali. Ndio sababu Mtume (s.a.w) alisema, “Abu Dharr ni Mtu mkweli zaidi katika taifa hili.”

Mahali pengine alisema, “Abu Dharr yu kama Mtume Isa katika ibada ya kujinyima anasa za mwili.” Kwa mujibu wa hadithi alisema, “Mtu anayetaka kuona mfano wa maisha na staha ya Isa amwangalie Abu Dharr.”

Ni dhahiri kwamba ibada ya dini kama alivyofanya Abu Dharr, haikuwekewa mpaka kwenye Swala peke yake. Alikuwa hodari kiutendaji katika aina zote za ibada. Ni jambo lisilo na upinzani kwamba, kutafakari kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na muumbo wake, pia ni ibada kubwa. Abu Dharr alifanikiwa katika ibada hii pia.

Waandishi wa historia na hadithi wanakubaliana kwa pamoja kwamba Abu Dharr alipata kiwango kikubwa cha ujuzi na hii ilikuwa kwa sababu alipata ujuzi kwa moyo ulionyooka wakati anafuatana na Mtukufu Mtume. Alimuuliza maswali Mtume kila wakati na alijifunza na kuhifadhi majibu yake. Alikuwa na uzoefu mkubwa wa ujuzi wakati anafuatana na Mtume.

Mwandishi wa Kitabu Darayatus Rafiah anasema kwamba Abu Dharr alihesabiwa katika safu ya wanachuo wakubwa na washikilia maadili na alikuwa na daraja la pekee la kitaalam. Alikuwa sahaba mwandamizi wa Mtume alikuwa miongoni mwa watu hao waliotimiza agano lao na Mwenyezi Mungu yaani, watu hao walitimiza ahadi ambayo waliahidiana Naye kuhusu wao kuwa wafuasi wa imani iliyokamilika, na alikuwa mmojawapo wa wale watu wanne ambao waumini wote wanawajibika kuwapenda.

Allamah Manazir Ahsan Gilani ametoa maelezo mafupi kuhusu utaalamu wa juu wa Abu Dharr, ameandika, Soma tamko la Ali, mbora wa majaji miongoni mwa masahaba, na lango la Ujuzi na uhitimishe mwenyewe kwamba anaposema, “Abu Dharr alikuwa na shauku na hamu kubwa ya kupata ujuzi;” anasema jambo lililo sahihi.

Je! Hivi ushahidi huu wa Imam Ali, hauhalalishi madai ya Abu Dharr? Wakati mwingine Abu Dharr mwenyewe alikuwa akisema kwa shauku kubwa, “Tumetenganishwa na Mtukufu Mtume wakati ambapo hakuna hata mmoja wetu ambaye anaweza kujitegemea mwenyewe, kwa sababu bado hatujajua mambo fulani maalum.” (Tabaqat bin Sad Juzuu ya 4, uk. 10).

Allamah Gilani ameandika kuhusu ujuzi wa Abu Dharr, “Mtu mmoja alimuuliza Imamu Ali, alimfikiriaje Abu Dharr.
Akamjibu kwamba ‘Yeye, Abu Dharr alihifadhi ujuzi ambao ulimuemea.’

Umesoma na kuona jinsi alivyo kuwa mwepesi kukubali fikira, na wewe mwenyewe unaweza kukisia kutokana na matukio. Ndio maana kila mara alikuwa tayari kutekeleza kwa mujibu wa vile alivyosikia kutoka kwa Mtukufu Mtume. Kama vile alivyo jaribu kusikia kutoka kwa Mtukufu Mtume, alitaka kutekeleza kwa vitendo bila kusita hata kidogo. Ilikuwa utashi wa dhati kuona kwamba tendo lake liliendana kwa ukamilifu na ujuzi.

Abu Dharr alinuia sana na alikuwa imara kuhusu kipengele hiki hivyo kwamba hakujali kamwe mamlaka yenye uwezo mkubwa kuliko zote hapa duniani kama ingekuwa kipingamizi chake. Hotuba na ushawishi hazikuweza kumtikisa kutokana na msimamo wake aliokuwa nao.

Akajivunia sifa hii wakati mwingine alisema, “Enyi watu! Mnaona siku ya Hukumu, mimi nitakuwa karibu sana na Mtume (s.a.w) na kundi lake, kwa sababu nimemsikia akisema kwamba atakayekuwa karibu sana naye mnamo siku ya Hukumu atakuwa mtu ambaye ataondoka katika dunia hii katika hali ile ile ambayo alimwacha. Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba sasa hapana yeyote aliyeachwa miongoni mwenu ambaye yumo katika hali ile ya wakati wa uhai wa Mtukufu Mtume isipokuwa mimi na sijanajisiwa na kitu chochote kipya. (Tabaqat bin Sad na Musnad ya Ahmad bin Hanbal).

Hili halikuwa dai la haki peke yake tu, lakini pia kiongozi wa dunia na Mtume wa mwisho alishuhudia hivyo.

Allamah Subaiti amesema kwamba mifano ya uadilifu iliyowekwa na Abu Dharr inastahili pongezi. Msimulizi anasema, “Nilipomuona Abu Dharr amejifunika blanketi na amekaa kwenye kona ya msikiti, nilimuuliza kwa nini alikuwa amekaa peke yake hapo? Alisema kwamba alimsikia Mtukufu Mtume anasema, “Ni vizuri kukaa kwenye kona peke yako kuliko kuketi katikati ya kundi la watu wabaya na ni vema kuketi na watu wenye maadili mema kuliko kuketi peke yako. Kimya ni kizuri kuliko kusema jambo baya na kusema jambo zuri ni vema kuliko kunyamaza kimya.”

Abu Dharr alisema kwamba Mtukufu Mtume amemwambia mengi kuhusu maelekezo ya maadili mema. Yapo Saba:

1. Fanya urafiki na watu masikini na jaribu kuwa nao karibu.

2. Ili uweze kuboresha hali yako waangalie watu wenye hali ya chini kuzidi wewe na usijilinganishe na watu wenye hali nzuri kuzidi yako.

3. Usimwombe mtu yeyote msaada wa mambo ya kidunia na ujenge tabia ya kuridhika.

4. Wahurumie ndugu zako na wasaidie wanapohitaji msaada.

5. Usisite kusema kweli hata kama dunia itakugeukia wewe.

6. Usijali shutuma za Kafiri kuhusu Mwenyezi Mungu.

7. Kila mara sema. “La hawla wa la quwwata illa billah.” (Hapana mweza isipokuwa Mwenyezi Mungu). Kwa maneno mengine, ‘Mwenyezi Mungu ni Uwezo Usiowezwa.

Abu Dharr anasema, baada ya kusema mambo haya, Mtume alisema huku anashika kifua changu, “Ewe Abu Dharr hakuna busara nzuri zaidi kama kupanga mambo vizuri, hakuna uchaji Mungu ulio bora zaidi kama kujizuia na hapana kitu kizuri zaidi kama maadili mema.”

Allamah Gihani alikinukuu Musnad ya Ahmad bin Hanbal anataja madili mawili tu miongoni mwa maadili haya yaliyotajwa hapo juu, ambayo yanaendana na kufanya urafiki na watu maskini na kuwatazama watu wenye hali ya chini kuzidi ya kwako, na halafu ameandika:

“Kwa kweli, haya ndio marekebisho mazuri kuliko yote dhidi ya maradhi ya kupenda utajiri na kupenda anasa za dunia. idhaniwe kwamba yupo mtu ambaye analo shati la Muislamu na suruali ndefu kuvaa, mkate wa ngano na nyama ya kondoo kwa ajili ya chakula, na nyumba ya udongo wa mfinyazi iliyo pangwa vizuri na safi kuishi humo.

Sasa, endapo mtu huyu anajilinganisha na mtu ambaye hana kitu isipokuwa nguo iliyo duni. Mkate wa shayiri nyumba iliyoezekwa kwa mabua, atamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hali yake nzuri zaidi na hatateseka kisaikolojia, mateso ambayo angeyapata endapo angejilinganisha na mtu tajiri mwenye nguo za gharama zadi na chakula kizuri. Njia hii ndio bora zaidi kupata kujitosheleza kidunia na manufaa mengineyo ya kidunia.

Lakini wangapi miongoni mwetu wanatekeleza hivi leo? Kwa hakika mtu hatapata matatizo yoyote endapo anafuata kanuni hii. Hii peke yake ndio kanuni ya muhimu kwa ajili ya dunia hii na kwa ajili ya Peponi, ambayo imeelezewa katika sentenso ifuatayo` ya Sheikh Sa’d, bingwa wa mashairi wa Iran.

“Nilikuwa nalilia jozi ya viatu hadi nilipo muona mtu asiyekuwa na miguu.” Baada ya kupenda utajiri sehemu nyingine ya kupenda dunia ni kupenda daraja na uwezo. Hii inayo hatari zaidi na ni sababu ya uovu wa mpangilio wa dunia. Uharibifu unaendelezwa duniani na watumwa wa utajiri ni pungufu zaid kuliko ule unaosababishwa na watu wenye uroho wa cheo na uwezo.

Sababu halisi ya maradhi haya ni kwamba mtu anapohisi ubora wake katika fani fulani, husahau uwezo wa yule ambaye amemboresha, na hujifikiria yeye ni matokeo ya hivi hivi tu. Halafu hajaribu kuwafanya watu wengine, wako karibu naye, watambue umuhimu wake ambao amejipachika mwenyewe. Akiwa na hitimisho la fikra hii, hutayarisha mipango kwa mujibu wa uwezo wa akili yake.

Ni mara chache sana kuonekana kwamba mtumwa wa ulafi na uchoyo ashindwe kufanya kila awezalo kwa lengo la kutimiza kusudio lake. Hujaza akili yake unafiki na wakati wote hubakia kuwepo kwake kupitia njia za halali na mbaya sana. Ubora ambao Abu Dharr alipata au alikaribia kuupata, ulikuwa ule wa uchaji Mungu.

Palikuwepo hofu kwamba hali ile ingemfanya kuwa na majivuno na kupenda makuu, ambayo baadaye tamaa ya hadhi na heshima huvuruga amani ya hapa duniani na Peponi. Kwa hiyo Mtume alizuia hiyo mapema na akamwambia Abu Dharr, siku moja kwa maneno ya wazi.

Mwenyezi Mungu alisema: “Enyi waja wangu! Wote nyinyi mnazo dhambi isipokuwa hao ambao nimewapa kinga. Kwa hiyo wote lazima msali mkiomba msamaha kwa utaratibu unaokubalika. Nitawasameheni.

“Nitasamehe dhambi za mtu anayeniona Mimi kuwa ninao uwezo wa kutosha kumkomboa kutoka kwenye dhambi zake na kwamba ninawaokoa, na kwa mtu aliyeomba msamaha wa dhambi zake kupitia kwenye uwezo Wangu.

“Enyi waja wangu! Nyote nyinyi ni wapotovu isipokuwa hao Ninawaonyesha njia iliyonyooka. kwa hiyo lazima mniombe Mimi ili niwaongoze. Wote nyinyi ni masikini na wahitaji isipokuwa wale Ninao wafanya matajiri.

“Niombeni Mimi kwa ajili ya riziki yenu na kumbukeni kwamba endapo nyinyi nyote mlio hai na wafu, wazee na vijana, waovu na waadilifu, muungwana na kujizuia msiombe chochote kutoka kwangu hapataongezeka chochote kwenye milki Yangu.

Na endapo nyote nyinyi wafu na walio hai, wazee na vijana, waovu na waadilifu mnakusanyika pamoja na kuniomba Mimi niwatimizie mahitaji yenu na kuwatosheleza mahitaji yenu, hapatatokea upungufu wowote kwenye himaya yangu hata wa kulingana na tone la maji yaliyochukuliwa na ncha ya sindano mtu anapoitumbukiza baharini. Hii ni kwa sababu Mimi ni Mkarimu, Msamehevu, Mkuu, Anayetukuzwa na Aliyeko kila mahali.

Mtu yeyote anaweza kujivunia kuwepo kwake au mafanikio yake na utulivu wake baada ya kuamini ukweli wa Utulivu wa Mungu na Ufahari ambao unauona katika hali hii? Hivi mtu yeyote anaweza kuwa na kiburi hata kwa sekunde moja baada ya hapa? Mtu yeyote anayemwamini Mwenyezi Mungu anaweza kuchochea uhaini hapa duniani kwa ajili ya kituo chake cha maisha, heshima, kujionyesha na hudumu baada ya hao? Nani mwenye wazimu anayeweza kujivunia uchaji Mungu wake ambapo kila mmoja wetu ana dhambi?

Pale ambapo utajiri wa watu matajiri upo kwenye udhibiti na mamlaka ya Mwenyezi Mungu; yeyoye huyo anayeonyesha pesa si mpumbavu? Endapo ni sahihi kwamba makubwa na madogo yetu hayawezi hata kwa kuungana kuongeza hata nukta moja upana wa himaya ya Mungu, mtu ambaye ni vumbi la kujaa kiganja tu atajivunia nini? Inapokuwa hii ni hali ya uhuru wake kutokana na utashi hata katika mambo ya mwongozo na ukomavu wa akili anafikiria upendeleo na uwezo a Mwenyezi Mungu kuwa ndio wakala halisi, ni katika misingi gani mhudumu wa dini au mrekebishaji atafikia juhudi zake zikastahili kuthaminiwa?

Endapo kila kitu ni mali yake na sisi ni masikini na wahitaji, kwa nini basi kiburi hiki na kwa nini ufidhuli huu na majigambo haya?

Hizi zilikuwa amri na hotuba ambazo ziliiingiza maadili ya Mtume Isa kwenye moyo wa Abu Dharr. Hata hivyo, hali ilikuwa hiyo na hata zaidi ya Mtume alivyokuwa na desturi ya kuchokonoa tabia ya kujinyima ya Abu Dharr.

Lakini tunatakiwa kutazama kwa makini zaidi wa upande huo wa mafundisho yake na nasaha ambamo humo ndimo Uislamu umesimama na kutofautiana na dini zingine zote.

Lazima utajihisi unataka kujaribu kufikiria kwamba kama haya yalikuwa mafundisho ya Mtukufu Mtume, kwa nini Uislamu ulipinga maisha ya utawa na kuyafikiria kuwa ni bidaa zilizoendakezwa na watawa na wahudumu wa kanisa? Nitajaribu kuelekeza usikivu wako kwenye jibu la swali hili. kwa ujumla kujizuia na uchaji mungu maana yake ni kuondoka mijini na kwenda milimani na misituni kuabudu Mwenyezi Mungu katika hali ya upweke. Abu Dharr anaeleza ifuatavyo:

“Mtukufu Mtume alimwabia kwamba pia ni jambo zuri kuondoa mawe njiani, kuwasaidia wasiojiweza pia ni hisani na hata tendo la ndoa na mkeo ni kitendo cha fadhila.
(Musnad Ahmad bin Hanbal)

“Nilimuuliza Mtukufu Mtume kwa mshangao, pia ni sadaka kufanya tendo la ndoa na mke wake, ingawa anatosheleza tamaa yake kwa tendo hili? Endapo mwanamume anatosheleza tamaa yake, pia atapata fidia kwa tendo hilo? Mtume alisema, “Vema, niambie, haitakuwa dhambi endapo ungetosheleza tamaa kwa kufanya kitendo kisicho halali na kilicho harimishwa?” Nilijibu, “Bila shaka.”

Akasema, “Nyinyi watu mnafikiria kuhusu dhambi lakini si matendo mema. Kwa kawaida watu wanaoishi maisha ya kushikilia maadili kuacha kufanya kazi ili wajipatie riziki na baadaye pale ambapo mahitaji ya kidunia yanapowabana sana wanaanza kuomba.”

“Siku moja Mtume (s.a.w) aliniita na akasema, “Unaweza kutoa kiapo cha uaminifu kwamba baada ya hapo patakuwepo Pepo tu inakungojea wewe.” Nikajibu, “Ndio” Halafu nikanyosha mkono wangu. Mtukufu Mtume akasema, “Ninataka useme kwamba hutaomba kitu chochote kutoka kwa mtu yeyote?” Nikajibu “Sawa” akasema, “hata ule mjeledi unaoanguka kutoka kwenye farasi wako unatakiwa uteremke chini na kuchukua wewe mwenyewe.”

Abu Dharr anasema kwamba Mtukufu Mtume alimwambia, “Usifikirie wema wowote na upendeleo kuwa ni kitu kisichokuwa na thamani na kidogo. Endapo hunacho kitu cha kumpa ndugu yako Muisilamu, angalau ni muhimu ukutane naye huku unatabasamau.”

Abu Dharr anasema, “Mpendwa wangu (yaani Mtume) ameniusia kwamba niendelee kuonyesha wema kwa ndugu zangu, hata kama siwezi kutimiza kikamilifu, (Musnad Ahmad bin Hanbal) kwa sababu ni vigumu sana. Hata hivyo mtu anatakiwa kuwafanyia wema watu wote kadiri iwezekanavyo.”

Tabia ya Abu Dharr inadhihiri ambapo tunaona kwamba kila mara yupo na watu fukara na wenye kuhitaji. Alikuwa makini sana kuhusu mafundisho ya Mtume na hakuna miongoni mwa masahaba wenye mioyo migumu ambao hawakuathiriwa na maadili ya Mtume. Alikuwa muungaji mkono madhubuti wa Imamu Ali hivyo kwamba alichota tabia ya kiwango cha juu cha desturi njema za Mtume.

Agizo la Mtume lilikuwa: “Wape watumwa wako na watumishi wako chakula unachokula wewe, na wape nguo unazovaa wewe.” (Musnad ya Ahmad bin Hanbal) Na Abu Dharr alifuata utaratibu huo huo. Kila siku aliwapa watumwa wake na watumwa wasichana chakula alichokula yeye na aliwapa nguo alizovaa yeye.

Kwa mujibu wa hadithi ya Mtukufu Mtume, Abu Dharr aliona ndoa ni jambo la muhimu. Alioa lakini kwake ndoa kamwe haikuwa na maana ya starehe na furaha. Alidhani kwamba ndoa ilikuwa ni jina la kufuata Hadith ya Mtukufu Mtume. Inaeleweka kwamba alifuatana na mke wake popote alipokwenda.

Kwa kuwa mke wake alitoka Afrika, wakati fulani watu walisema, “wewe unaye mke mweusi?” Alijibu, “Nafikiri ni bora zaidi kuwa na mke mweusi na mwenye sura mbaya kuliko mke wenye sura inayopendeza na watu wanitembelee kwa sababu tu ya uzuri wa sura ya mke wangu.” Abu Dharr alikuwa anamjali sana mkewe.

Ukarimu si tu ndio mojawapo ya sifa bora sana, lakini ni kiini cha ubinadamu. Jinsi mtu anavyozidi kutambua kanuni za Uislamu ndivyo anayozidi kujaa moyo wa huruma.

Naim Bin Qanat Riyath anasema, “Siku moja nilikwenda kumtembelea Abu Dharr na nikamwambia kwamba ninampenda na ninamdharau wakati huo huo.” Abu Dharr akasema, “Inawezekanaje hali hizi mbili zije pamoja?”

Nilisema, “Nimekuwa nikiwaua watoto wangu. Sasa nimetambua kwamba hicho ni kitendo kiovu. Kwa hiyo, kila mara ninapofikiria kuja kwako kukuuliza kuhusu vipi nitaokolewa na kusamehewa, hisia hizi kubwa zinapanda pamoja. Nilipofikiria kwamba ingekuwa bora kama ungeniambia kuhusu ufumbuzi wake hisia za mapenzi zilipanda juu sana, lakini nilipofikiria kwamba ningeumia daima milele endapo ungetangaza kwamba dhambi hiyo haisameheki, chuki dhidi yako ilizidi kuongezeka. Sasa nimekuja kutaka kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili.”

Abu Dharr alisema, “Sawa! Niambie endapo umefanya yote haya mnamo siku za ujahilia au baada ya kuingia kwenye Uislamu?

Nilisema, “Wakati wa ujahilia.” Abu Dharr akasema, “Dhambi yako imesamehewa. Uislamu ni ukombozi wa uchafu wa aina hiyo yote na dhambi zote.”

“Niliposikia hivi niliridhika. Baadae nilitaka kuondoka akasema, “Ngoja!” Na nilifuata maelekezo yake.

“Baadaye alimwambia mkewe kwa alama alete chakula ambaye alikwenda ndani na akarudi akiwa na chakula. Abu Dharr alisema, “Naim, Bismillah (maana yake kula katika jina la Mwenyezi Mungu).

Kabla sijaanza kula nilimwambia tule wote. Akasema, “Mimi nimo kwenye Swaumu.” Aliposema hivi akaanza kuswali. Mimi nikaanza kula na nilipokaribia kumaliza, naye akamaliza Swala na akaanza kula.

Nilisema, “kusema uongo ni dhambi kubwa katika Uislamu na hata kama nikimdhania mtu fulani kuwa ni mwongo inawezekana kwamba anaweza kuwa mwongo, lakini nikufikirie vipi wewe?”

Abu Dharr alisema, “Umekaa muda mrefu na mimi. Jambo gani limekufanya unifikirie mimi kuwa ni mwongo?”
Nikasema, “Muda mfupi uiliopita uliniambia kwamba unafunga Swaumu na sasa unakula na mimi.”

Aliniambia, “Sijakuambia uongo. Nimefunga Swaumu na wakati huo huo ninakula na wewe.”

Akasema, Mtukufu Mtume amesema kwamba yeyote anayefunga Swaumu terehe 13, 14, na 15 ya mwezi huu wa Shabani, kwa namna nyingine ni sawa kama amefunga Swaumu ya mwezi mzima. Kwa maneno mengine, atapata thawabu ya kufunga Swaumu ya siku thelathini yaani kila Saumu ya siku moja inabeba uzito wa Swaumu ya siku kumi.

Kwa kuwa nimefunga Swaumu katika siku hizi ninayo haki ya kusema kwamba ninafunga Swaumu ya mwezi mzima.” (Musnad Ahmad bin Hanbal na Hayatul Qulubi-Allamah Majlis).

Alamah Bayhaqi pia amesimulia tukio la aina hiyo hiyo. Muhtasari wake ni kama ifuatavyo:
Siku moja Abu Dharr na Abdullah bin Shafiq Uqaili walikwenda nyumbani kwa mtu kama wageni. Abu Dharr alikwisha sema kwamba yeye anafunga Saumu na chakula kilipoletwa alianza kula. Abdullah alidokeza, “Wewe unafunga Saumu.” Abu Dharr alisema, “Ninaikumbuka Swaumu yangu. Sijaisahau Saumu yangu. Kila mara nipo makini kufunga Swaumu katika hizo siku tatu za kila mwezi ambazo huitwa “Ayyam al-Beydh.” na kwa mujibu wa hadithi ya Mtukufu Mtume (s.a.w), uelewe kwamba mimi ninafunga Saumu (Sunan Bayhaqi).