Sura Ya Tatu

Baada ya kuingia kwenye Uislamu, Abu Dharr aliondoka Makkah kwenda nchini kwake. Abdullah Subaiti ameandika kwamba Abu Dharr alipoondoka, alikuwa anabubujika imani, kamili, na alikuwa na furaha sana. Alifurahia sana kwamba Mwenyezi Mungu, alimwongoza kwenye imani ambayo imekubaliwa na waliotakasika na dhamira imeridhika nayo na akili inakaribisha kwa ukamilifu.

Aliendelea na safari hadi nchini kwake. Mtu wa kwanza kumsalimia alikuwa kaka yake Unais na pia alikuwa mtu wa kwanza kupata mwamko wa imani yake.
Unais alikwenda kubusu miguu ya kaka yake na kusema, “Ewe ndugu yangu! Umepitisha siku nyingi sana Makkah sasa niambie ulichopata huko.”

Abu Dharr alisema, “Unais! Nimefanya uamuzi wenye busara. Niliamua baada ya kutafakari sana kwamba lazima nikubali imani ya Muhammad! Ewe Unais! siwezi kukuambia kwamba nilipokutana na Muhammad na kumtazama uso wake, nilihisi kama vile kifua changu kilikuwa kinaongezeka. Moyo wangu ulijaa furaha na akili yangu ililewa imani.

Mara nikakariri kalimah-shahada na kukubali Utume wake nilimwomba anifundishe vipengele vya imani. Kwa hiyo alinieleza kanuni za Uislamu. Ewe Unais ninakuomba kwa kweli na kwa moyo safi na nia njema uinamishe kichwa chako kwa unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu na uache kuabudu miungu hii iliyotengenezwa na mikono ya watu yenye asili ya mawe.”

Aliposikia hivi, Unais alikaa chini huku akiwa ameinamisha kichwa chake na kuanza kufikiri. Alipatwa na hali kama vile umelewa. Unais alikumbuka mambo hayo yote aliyo yaona huko Makkah. Baada ya muda fulani alisema, “Ewe Ndugu! Akili yangu imethibitisha ukweli wako na mantiki yangu inanieleza nikutii wewe. kwa hiyo sikiliza! Ninashahidilia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu na ninakiri kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.”

Abu Dharr alifurahi sana kuona Unais anaikubali imani. Alimwambia: “Sasa twende kwa mama yetu.” Wote wawili walikwenda kwa mama yao. Baada ya kumuamkia mama yao, Abu Dharr akasema, “Mama yangu mpendwa! Nakuomba unisamehe! Nimekuwa mbali na wewe kwa kipindi kirefu sana. Lakini, nimepata kitu cha nadra ambacho hakuna mtu aliye nacho hapa.”

Mama Akamuuliza, “Kitu hicho ni kipi?” Abu Dharr alisema, “Hii ni tunu ya imani mama. Nilikutana na mtu huko Makkah ambaye uso wake uling’aa nuru ya uadilifu, hana wa kumlinganisha kwa uzuri wa tabia yake na ukarimu wake. “Yeye husema kweli tupu. Yeye husema kilicho sahihi. Hutenda haki. Maneno yake yanayo busara. Mama! Maadui zake pia humwita mkweli na mwaminifu. Huwaita watu wamwelekee Mwenyezi Mungu ambaye ni muumba wa mbinguni na ardhi na mpangiliaji wa kuweza kudumu kwa ulimwengu huu.

“Nimekubali kumuamini mtu huyu kwa kuvutiwa na mwelekeo wake, maneno yake na semi zake, na Unais pia amekuwa Muislamu. Tumekubali Upweke wa Mwenyezi Mungu na Utume wa Muhammad.”

Mama yake Abu Dharr akasema: “Mwanangu, endapo ndio hivyo, mimi pia nina shahidilia kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na kukiri kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.”

Abu Dharr alitiwa moyo baada ya kaka yake na mama yake kuingia kwenye Uislamu na sasa alianza kutafakari jinsi ya kuwashawishi watu wa kabila lake na kuwavuta waelekee kwenye njia iliyonyooka.

Baada ya kufikiri sana Abu Dharr alitoka nje ya nyumba yake. Mama na kaka yake pia walikuwa naye. Baada ya kusafiri mwendo mfupi walipiga hema lao karibu na mahema ya watu wa kabila lao.

Usiku uliingia. Wasafiri hawa waliochoka walikuwa wamelala kwenye mahema yao walipohisi kwamba watu wengi wa kabila hilo waliokuwa pale walikuwa wanasimuliana hadithi wao kwa wao na kuelezea matukio mbali mbali. Walikuwa katika mazungumzo mfululizo.

Abu Dharr alipojaribu kusikiliza kwa siri walikuwa wanasema nini, alisikia kwamba walikuwa wanamsema yeye. Baada ya hapo watu waliondoka kutoka kwenye mahema yao na kwenda kwenye hema la Abu Dharr, akamwambia kaka yake, Unais, “Watu wa kabila letu wamekuja karibu na hema letu. Nenda nje ukawaone.”

Unais alitoka nje mara moja. Aliwaona vijana wa kabila hilo walikuwa karibu na hema. Walikwenda karibu na hema ili wajue endapo Unais na Abu Dharr walikuwa hapo. Walimsalimia. Baada ya Unais kujibu salamu yao, aliwauliza sababu ya wao kutembelea hapo. Wakasema, “Tumekuja tu kukuona wewe na Abu Dharr.”

Unais alirudi ndani na akamwambia Abu Dharr, “Vijana wa kabila letu wamekuja kutaka kujua hali ya safari.”

Abu Dharr alisema, “Waambie waingie ndani. Nitazungumza nao. Inawezekana labda nikawasilimisha waanze kumuabudu Mwenyezi Mungu, Aliye Pekee.”

Unais alitoka nje na akawaambia, “Ingieni ndani kwani kaka Abu Dharr anawaiteni.”
Wote walikwenda kwa Abu Dharr. Mmojawao akasema, “Ewe Abu Dharr! Hatujakuona kwa kipindi kirefu na matokeo yake ni kwamba tunasikitika sana.”

Abu Dharr akasema, “Wapendwa wangu vijana! Moyo wangu unayo mapenzi makubwa sana kwenu, na ninawahurumieni.”

Mtu mmoja: “Abu Dharr! Ulikuwa wapi kwa muda mrefu hivi? Tumeshindwa kukuona kwa kipindi kirefu.”

Abu Dharr: “Nilikwenda Makkah. Nilirudi siku chache zilizopita.” Mtu wa pili: “Tunafurahi kwamba ulikwenda Makkah.”

Abu Dharr: “Kama mambo yalivyo, nilikwenda Makkah, lakini sikutoa sadaka kwa Hubal wala sikuwasujudia Lat na Uzza. Vijana wangu! Kwa nini nifanye yote haya ambapo ninafahamu kwamba masanamu haya wala hayana uhai, ama kuweza kuumiza au kumnufaisha yeyote? Wala hayawezi kuona ama kusikia, ama kuzuia janga linaloweza kuwapata.

“Sikilizeni! Mimi nimekimbilia kwa Mwenyezi Mungu katika matendo yangu na mambo yangu yote. Hakika Yeye ni Peke yake, hana mfano wala mshirika, na ninakiri kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni Yeye peke yake anapaswa kuabudiwa, Yeye ni Muumbaji wa kila kitu na mwezeshaji wa kila kiumbe.

“Ninawaomba njooni kwangu tuwe pamoja katika mpango wetu wa utekelezaji na mshahidilie Upweke wa Mwenyezi Mungu kama sisi”

Waliposikia hivi, watu wote walianza kutetemeka. Mmoja wao alisema kwa mshangao, “Ewe Abu Dharr! Unasema nini?”

Abu Dharr: “Sikilizeni kwa yale ninayowaambieni ingawa siwezi kumuona Mwenyezi Mungu kwa macho yangu bado ninaweza kumuona Yeye kwa jicho langu la kiroho na sikilizeni! Inawezekanaje kitu chochote kinachotengenezwa na mikono ya mwanadamu kiwe na thamani ya kuabudiwa na binadamu? Si busara kuabudu masanamu yaliyotengenezwa kwa mawe na miti, na kuyaomba ili yatutimizie haja zetu.

“Watu wa kabila langu! mnajua kwamba masanamu haya hayana uwezo wowote. Wala hayawezi kuzuia uovu, ama kuwa na nguvu ya kupata manufaa?”

Baada ya kusikia ushawishi huu wa Abu Dharr, watu walianza kunong’onezana wao kwa wao.

Mmoja wao alisema; “Nimekwisha waambieni kwamba huko Makkah, mtu amejitokeza, anajiita yeye ni Mtume na anawaita watu kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja. Abu Dharr amekutana na mtu huyu, na mahubiri ya mtu huyu yamesisimua sana hivyo kwamba fikra zozote anazozitoa Abu Dharr ni za mtu huyo.”

Mtu mwingine akasema; “Hali ni mbaya sana. Sasa tupo hatarini ambayo inatujia kupitia kwa Abu Dharr na mahubiri yake. Tunadhani kwamba endapo ataendelea kuhubiri namna hii, tofauti zitajitokeza kwenye kabila letu na maisha yetu yataharibika. Ni vema twende kwa mtemi wetu Khafaf, tumwelekeze hatari zote zinazoweza kujitokeza, na tumsisitizie na alipatie jambo hili kipaumbele ili tuweze kukabiliana nalo.”

Vijana wa kabila la Ghifari waliondoka nyumbani kwa Abu Dharr na walikwenda kumwona Khafaf. Wakati wapo njiani walibadilishana mawazo wao kwa wao. Mmoja wao alisema, “Abu Dharr ameanzisha ghasia kubwa.”

Mwingine akasema, “Itakuwa aibu kubwa sana kwetu kama tutaifumbia macho dhambi hii kubwa ya Abu Dharr. Anaifanyia ufisadi dini yetu waziwazi na kukebehi miungu yetu.” Mtu wa tatu akasema, “Ni wajibu wetu kumfukuza kutoka kwenye kabila letu bila kuchelewa hata kidogo, kwa sababu kama tukichelewa kumtenga katika kipindi kifupi tu, atawaelemea vijana wetu, wanawake zetu, watumwa wetu na kuwatia mawazo yake maovu akilini mwao. Endapo inatokea hivyo, tutapata hasara kubwa sana.”

Mtu wa nne akasema, “Maoni yako ni sahihi. Lakini, nani atamfunga paka kengele? Huyu ni mtu mashuhuri wa kabila na ni mzee wa kaya. Ninaona kwamba hata Unais anayo mawazo haya haya, na yeye pia ni mtu mwenye kuheshimiwa.”

Mtu wa tano akasema, “Hakuna haja ya wasi wasi. Njooni tukamtaarifu Khafaf. Tunao uhakika kwamba Khafaf na watu wengine waungwana wa kabila ndio watakao mfukuza kutoka kwenye kabila.”

Mtu wa sita akasema, “Ninatafakari kuhusu mawazo yao. Sina uhakika kama wataweza kuwabadili. Inawezekana kwamba wao ndio watakao badilika na kwenda kwenye njia iliyo nyooka tusijisumbue, lakini na tutafakari kuhusu dini yao. Nisikilizeni! Ninaona kuna ukweli kwenye imani yao. Hata hivyo karibu tutafika kwa mtemi Khafaf. Baada ya mazungumzo yetu na yeye, tunategemea kufikia uamuzi wenye msimamo.”

Kwa ufupi, wakizungumza pamoja, watu hawa walifika nyumbani kwa mtemi wa kabila la Ghifar na wakamwambia, “Tumetoka kwa Abu Dharr kuja kwako.”

Khafaf: “Abu Dharr amerudi kutoka safari yake ya kutoka Makkah?” Mtu mmoja akasema, “Bwana, Abu Dharr ameasi. Aliwabeza miungu wetu. Anasema kwamba yupo mtu ameteuliwa kuwa Mtume. Kazi yake ni kuwaita watu waende kumuabudu Mungu Mmoja na pia kufundisha mambo mazuri. Abu Dharr haridhiki bila kukubali utume wa mtu huyu na kuendelea na msimamo huo, lakini wakati wote anahubiri kwa watu na kuwaita wote wengine waende kwa Mtume huyo na Mungu wake.

Khafaf aliposikia, alisema, “inasikitisha kuona kwamba Abu Dharr, anawaacha miungu wote, na kutangaza kumuabudu Mungu Mmoja. Ni uovu mkubwa sana na kutia kinyaa. Ninaona kwamba jambo hili litachochea vurugu kubwa katika kabila letu, na matokeo yake kabila litaangamia. Enyi vijana wangu! Msifanye haraka lakini nipeni, muda wa kutafakari kuhusu jambo hili la Abu Dharr.”

Baada ya vijana hao kuondoka na kurudi makwao, Khafaf mtemi wa kabila, alianza kufikiri kwa nini wote walikuwa wanasema kwa kumpinga Abu Dharr. Aliendelea kutafakari usiku wote akiwa kitandani kwake. Hali ilimkanganya sana na hakuweza kufanya msimamo hasa. Lakini akili yake ilikuwa na fikra nzito kuhusu maneno yaliyosemwa na Abu Dharr. Saa nyingi zilipita bila kupata usingizi, na alikuwa anafumba macho yake.

Mtemi Khafaf pia alikumbuka hotuba ya mwanafalsafa wa Kiarabu, Qays bin Saidah, pale sokoni. Alisema kwamba Muumbaji wa ulimwengu bila shaka ni Mmoja na ni Yeye tu ndiye anaye stahiki kuabudiwa.

Aliunga mkono kikamilifu maoni ya Abu Dharr kwenye hayo mahubri yake ya kusifika na pia alitamka kwamba fikra za Warqa bin Naufal, Zayd bin Amr, Uthman bin Hoverath na Abdallah bin Hajash kuelekea kwenye imani ya Abu Dharr.

Alikuwa katika hali hii ya kustaajabisha ambapo akili yake ilimuongoza na akajisemea mwenyewe, ‘Naam! Abu Dharr yu sahihi kwa sababu Qays bin Saida amemuunga mkono na ninao uhakika kwamba Qays hawezi akashindwa kuelewa wala kukubali itikadi yoyote ya uongo. Bila shaka, lazima atakuwepo muongozaji wa dunia hii, na lazima pawepo na nguvu yenye uwezo wa kuendesha mpangilio wote wa ulimwengu na ni dhahiri kwamba miungu wetu wa mawe na miti hawana kabisa uwezo kama huu. Ee Mungu wa Abu Dharr! Tuongoze na utukomboe kutoka kwenye uovu huu na utuweke kwenye njia ya haki.”

Wakati ambapo Khafaf alikuwa anafanya uamuzi wake muhimu, siku ilipambazuka hadi jua lilionekana angani pamoja na kuenea kwa mwanga wa jua, pia habari zilizidi kuenea kwamba Abu Dharr, kaka yake na mama yake wote wamerudi kutoka Makkah na wamemuabudu Mungu Mmoja tu.

Pamoja na kuenea habari hizi hasira ilichochewa. Watu walianza kumlaani Abu Dharr na kusema, ‘Amepata kichaa na hawezi kuelewa kwamba haya masanamu yetu hutuponya maradhi, yanatupatia riziki na kutulinda. Abu Dharr ni mtu wa ajabu ambaye anatuita twende kwa mungu asiyeonekana! Inaonyesha kama vile Abu Dharr anataka kuanzisha vurumai na matatizo miongoni mwa vijana wetu na kuwapotosha watoto wetu na wanawake wetu. Hakika mtu huyu ni muongo na madai yake si sahihi. Lazima afukuzwe kutoka kwenye kabila.”

Mmojawao akasema, “Kwa nini! Unawezaje kuelezea wazo la kumfukuza mtu huyu? Itafanyikaje? Hapana , kamwe! Haiwezekani kutokea. Huyu ni mtu jasiri katika kabila letu.”

Baada ya mazungumzo haya watu hao waliamua kutaka wasikilizwe na wazee kuhusu suala hili. Kufuatana na uamuzi wao, waliwaendea wazee wao kushughulikia jambo hili. Wazee wao waliamua kulipeleka jambo hili la Abu Dharr kwa mtemi. Kwa hiyo, wote walikwenda kwa Khafaf.

Mtemi wa kabila alimtuma mtumwa wake haraka aende kumwita Abu Dharr. Mtumwa huyo alipofika nyumbani kwa Abu Dharr alisema, “Abu Dharr! Wewe na Unais mnaitwa na Mtemi.”

Abu Dharr akajibu kwamba alikuwa tayari kwenda kwa mtemi. Mtumwa alipoondoka, Abu Dharr alichukua upanga wake na kuhifadhi kwenye mkanda na alimwambia kaka yake, Unais, “Njoo; twende kwa Khafaf!”

Unais: “Ewe kaka! Nimesikia mambo mabaya yanazungumzwa na watu kuhusu wewe. Nina hofu huu mkutano wetu unaweza usiwe na manufaa, jambo lisilotegemewa linaweza kutokea badala ya mategemeo yetu.”

Abu Dharr: “Hapana, siyo. Namjua Khafaf vizuri sana. Ni mtu mwenye hekima. Mwenyezi Mungu amempa hekima. Ni mtu mwenye akili sana miongoni mwa kabila letu.”

Ndugu hawa wawili waliendelea kuzungumza hadi wakafika kwa Khafaf. Hapo waliona kwamba watu maarufu wa kabila hilo walikuwa wamekaa kumzunguka Khafaf. Akawaamkia wote Abu Dharr akasema, “Salaamu Alaykum” (Amani iwe kwenu).

Waliposikia maamkizi ya Abu Dharr kwa jinsi ya Kiislamu, wazee wa kabila hilo walikasirika na walisema kwa hasira; “Salamu gani hii ambayo hatujawahi kuisikia kamwe.” Halafu mmojawao akasema “Inasikitisha. Hatujui Abu Dharr anakoelekea.”

Mtu mwingine akasema, “Hebu mtazame. Amekaa na upanga wake, na hana heshima kwa mtemi.” Mtu wa tatu akasema, maneno yako ni sahihi. Lakini, huyu ni mpanda farasi wa kabila letu na watu jasiri wakati wote huwa tayari kwa lolote.”

Abu Dharr akasema, “Silikizeni! Ninawaheshimu nyinyi kwa sababu ni watu maarufu wa kabila letu, ambao mnastahili kujivuniwa na kuwaenzi. Salaamu niliyo wapeni ni Salamu ya Kiislamu.”

Baada ya haya, Abu Dharr na Unais waliketi kwenye nafasi zao wakitazamana uso kwa uso na mtemi, Khafaf. Khafaf alisema kwa sauti ya upole lakini kali, “Ewe Abu Dharr! Ninayo Taarifa kwamba wewe umekuwa na msimamo wa kumuabudu Mwenyezi Mungu Ambaye haonekani. Watu mashuhuri wa kabila letu wamekasirika na msimamo wako huu. Wanasema kwamba Abu Dharr amewatukana miungu yao na anawaita hawana hekima yoyote.

“Ewe Abu Dharr! Tunakuheshimu lakini haimaanishi kwamba tupo tayari kustahamili miungu yetu kubezwa. Ninakuomba uache hoja ya mawazo yako ya sasa na urudi kwenye imani ya wahenga wako, au vinginevyo unatakiwa uieleze imani yako kwangu ili niweze kuelewa ukweli wa imani yako. Pia, ninakuhakikishia kwamba nitafikiria kuingia kwenye imani hiyo endapo utathibitisha kwamba imani yako haina shaka zaidi kuliko ya kwetu.

Abu Dharr naye alijibu, “Ewe mtemi wa kabila! Tunakuheshimu na kustahi chochote unacho sema. Lakini, wakati huo huo tunataka kueleza kwamba Mwenyezi Mungu, wa Pekee Ambaye tumeamua kumuabudu na Ambaye tunamwamini, ni huyu huyu ambaye ameumba dunia na mbingu, Ambaye huruzuku viumbe vyote, Ambaye kudhibiti maisha ya viumbe vyote vyenye uhai na Ambaye uwezo wake hauna mipaka.

“Masanamu ambayo tumekuwa tunayaabudu hadi sasa, yametengenezwa na mikono yetu kwa kutumia patasi na nyundo. Akili inaweza kuamrisha kwamba yule ambaye ametengenezwa na mikono yetu anaweza kuwa muumbaji wetu, anaweza kuruzuku na tusikiliza dua zetu?

“Mwanadamu ni kiumbe bora zaidi kuliko viumbe vya muumbo wote. Inawezekana yeye na heshima yake astahili kuinamisha kichwa chake mbele ya jiwe? Mtemi wangu! Tafadhali tafakari bila upendeleo kuhusu haya ninayosema. Masanamu hayana hata uwezo wa kufukuza adui yao.

“Nisikilize, ewe mtemi! Wakati fulani nilikwenda kwa Manat na nikampa sadaka ya kikombe cha maziwa. Nilikuwa bado nipo eneo hilo ambapo mbweha alifika hapo na akanywa maziwa hayo yote na akamkojolea Manat. Tukio hili liliniathiri sana na nilifikiri kwa nini mungu anashindwa kujilinda mwenyewe?

“Jambo hili lilinidhihirishia kwamba sanamu haiwezi kuwa mungu. Nina uhakika na kila mtu mwenye akili ataamini kwamba Muumbaji wa mbingu ni bora zaidi kuliko mbingu na muumbaji wa dunia ni bora zaidi kuliko ardhi.
Kwa mujibu wa kanuni hii yenye mantiki, masanamu hayawezi kuwa ni bora kuzidi sisi, haina maana sisi kuyaabudu.

“Ewe mtemi wangu! Nimekuja kwenye imani ya kweli kwamba Mwenyezi Mungu ni Peke Yake Ambaye ni Mumbaji na mwenye kuruzuku ulimwengu, na Muhammad Mustafa ambaye alipelekwa Makkah ni Mjumbe Wake.

“Anazo sifa nzuri kama hizo hivyo kwamba hakuna afananaye Naye hapa duniani. Quraishi ambao ni maadui zake wabaya wanakubali ukweli wake na uwezo wake. hata wanapojua kuwa Muhammad ni mpinzani mkubwa wa miungu yao na dini yao, wamempatia jina la Sadiq na Amin, kama ambavyo, nimetambua hivi karibuni tu. Sikiliza! Uso wake unang’aa nuru na hekima inatiririka kutoka kwenye maneno yake.”

Mara tu Abu Dharr alipomaliza hotuba yake, kelele kubwa ilitoka sehemu zote, “Jinsi gani maneno ya Abu Dharr yalivyo matamu! Kwa hiyo, miungu yetu haisikii na haisemi! Abu Dharr ameidhalilisha imani yetu na anaitukana miungu yetu!”

Kundi moja lilisema kwa pamoja, “Rafiki zangu! Msizungumze mambo yasiyo na mantiki. Kwa uaminifu tunasema kwamba lolote alilosema Abu Dharr linaonekana kuwa sahihi na akili inataka kwamba lazima tukubali ukweli. Tunao uhakika kwamba hatuwezi kupata mwongozo mzuri zaidi kuzidi yale ambayo Abu Dharr ametuletea.”

Sauti nyingine ilitokeza: “Nchi ya Arabuni inahitaji muongozaji na inaonyesha kama vile hakuna mwongoaji bora zaidi kuliko huyu ambaye amedhihirishwa na Abu Dharr.”

Halafu sauti nyingine ilitokeza, “Hotuba ya Abu Dharr ni ya maana sana.” na baada ya hii sauti ya juu sana ilitokeza; kama vile ingetoboa masikio, Ewe Abu Dharr! Ninashahidilia kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu na ninakiri kuamba Muhammad ni Mtume Wake!”

Alipoona hivi, Khafaf, mtemi wa kabila, baada ya kufikiri sana alinyanyua kichwa chake na akawaambia watu wake: “Wapendwa watu wa kabila langu! Nisikilizeni kwa makini. Mmesikia yote hayo aliyoyasema Abu Dharr. Ni wajibu wetu kutafakari kuhusu hotuba yake kwa uangalifu sana na kwa makini sana na tuweze kuona inayo kiasi gani cha ukweli.

“Uamuzi wa haraka haufai. Si busara kutupilia mbali ushauri wa mtu bila kuchunguza. Rafiki zangu! Mnatambua kiasi cha machafuko yaliopo miongoni mwetu na jinsi uhalifu ulivyo zidi ambao sisi tunahusika. Matajiri wanawanyonya masikini na hakuna mipaka katika kufanya dhambi na maovu.

“Mimi nimeamua kwamba lazima nikubali na kuunga mkono yale anayoyasema Abu Dharr. Sasa ni juu yenu nyinyi kujiamulia wenyewe. Sikilizeni nyinyi nyote. Ninashahidilia kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wake!”

Mara tu Khafaf alipotamka Kalimah (la ila ha illalah Muhammadan Rasulillah) palitokea kelele kubwa ndani ya kabila, Khafaf amekuwa Muislamu. Khafah ameingia Uislamu!”

Haikupita muda mrefu baada ya Khafaf kuingia kwenye Uislamu, hali ya kabila ilibadilika kabisa. Watu walio wengi walisilimu na kuwa Waislamu hapo hapo, ambapo wengine walingojea kukubali kuwa Waislamu mbele ya Mtukufu Mtume baada ya kuwasili huko Madina.
Kwa ufupi, kwa juhudi kubwa ya Abu Dharr watu wengi wa kabila la Ghifar walikubali kuwa Waislamu na palitokeza ukelele wa “Mungu Mkubwa! na “Mungu ndiye Mwenye Kusifiwa!” na jina la Mtukufu Mtume likaanza kutangazwa mchana na usiku.

Baada ya kujaza moyo wa Uislamu kwenye kabila la Ghifari na kuwasilimisha watu na kuingia kwenye Uislamu, Abu Dharr alielekeza umakini wake Asfan. Alipofika huko alianza kuhubiri Uislamu miongoni mwa watu.

Kwa kuwa sehemu hii ilikuwa kwenye njia kuu iliyotumiwa mara nyingi na Quraishi na alijenga hisia dhidi yao kwa sababu ya mateso aliyofanyiwa nao alifanya zoezi la nidhamu kali katika kuwafanya kuwa Waislamu. Kundi la Quraishi lilipopita hapo, aliwaeleza habari ya Uislamu na kwa hiyo idadi kubwa ya Quraishi walikubali kuwa Waislamu.