Sura Ya Tisa

Wataalamu wa historia na wahadithi wa madhehebu yote mawili (Shia na Sunni) wanakubaliana kwamba pale ambapo Mtume (s.a.w) alitaka kuanza safari yake ya kwenda kwenye hija yake ya mwisho, alitangaza waziwazi kwamba masahaba wote lazima wafuatane naye kwenye safari hiyo.

Baada ya tangazo hili, masahaba wa Mtume walianza kufika Madina kutoka sehemu zote. Pia aliwataarifu watu kwamba wale ambao hawangeweza kufika Madina, waende Makkah moja kwa moja ili wahiji pamoja naye.

Mtume aliondoka Madina tarehe 25 ya mwezi wa Zilqadah, mwaka wa 10 Hijiriya (Tarikh bin Alward). Masahaba wengi sana walianza safari naye tangu madina, pamoja na Salman, Miqdad, Abu Dharr na Ammar.

Alipofika Makkah, Mtume alitekeleza ibada zote za Hijja. Ahlul-Bait wake wote, wake zake na masahaba wote walikuwa naye katika Hijja. Alitoa hotuba wakati wa Hijja na akaorodhesha mambo yenye kuendeleza matumaini kwa wafuasi wake na akaeleza njia ambazo umma ungepita ili upate kukombolewa.

Alipomaliza Hijja Mtume aliondoka Makkah kwenda Madina. Kufuatana na masimulizi ya Muhadithi Dehlavi walikuwepo masahaba 124,000 au kwa mujibu wa taarifa ya Khawand Shah 125,000. (Izalatul Khifa, Juz. 1, uk. 514 na Rauzatus Safa, Juz. 2, uk. 215).

Alipofika sehemu iitwayo Ghadir Khum akiwa na masahaba wake, malaika Jibril aliteremsha ujumbe wa Mungu usemao:

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنْزِلَ إِلَيْكَ مِنْ رَبِّكَ ۖ وَإِنْ لَمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ وَاللَّهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ{67}

“Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu.” (5:67).

Baada ya amri hii ya wazi hapakuwepo na chaguo lingine sipokuwa yeye (Mtume) alifikisha ujumbe kwa watu.

Aliagiza mimbari itengenezwe kufuatana na hali halisi kwa kutumia mito ya kukalia kwenye ngamia! Baada ya hapo alimwambia Bilal wa Afrika, “Ewe Bilal! Waite watu na waambie masahaba wangu kwamba wale walioko mbele warudi na wale ambao bado wapo nyuma, wafanye haraka kuja mbele.”

Bilal aliita, Hayya ala Khairil Amal (Kimbilieni kwenye kitendo kilicho bora). Kundi lilikusanyika kuzunguka mimbari ya Mtume. Alipanda kwenye mimbari na baada ya hotuba ndefu sana alimwita Ali aende aliposimama. Halafu, akiwa ameshika mikono miwili ya Ali kwa mikono yake mwenyewe, alinyanyua mikono hiyo juu sana hivyo kwamba weupe wa kwapa za Ali ulionekana wazi. Halafu akasema; “Yeyote anayeafiki mimi kuwa mtawala na mlezi wake lazima pia amuafiki Ali kuwa mtawala na mlezi wake. Ee Mwenyezi Mungu! Uwe rafiki ya mtu ambaye ni rafiki yake Ali na uwe adui ya mtu ambaye ni adui yake Ali.”

Mara watu waliposikia taarifa hii walitamka kwa sauti kubwa kuonesha kumuuunga mkono. Mtukufu Mtume aliondoka kwenye mimbari na akamwamuru Ali kupokea hongera kutoka kwa masahaba kwenye hema la kijani.

Ali alipokea pongezi za kumrithi Mtume na aliwashukuru watu kwa kumpongeza. Imeandikwa kwenye Maarijun Nubuwwah kwamba, licha ya masahaba, wake zake Mtume pia walimpongeza Ali kwa kuwa mtawala na kiongozi wa umma wa Waislamu.

Kwa mujibu wa Tarikh bin Khalqami Mtume katika hotuba yake ya Ghadir iliweka wazi kuhuzu kuwa na sifa, fahari na kukubalika kwa Ali akasema kwamba Ali alikuwa na uhusiano sawa na yeye kama Harun alivyokuwa na Musa.

Ukifuatana na Mustadrak al-Hakim alisema, “Ninawaachieni vitu viwili vya thamani sana miongoni mwenu, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul Bait wangu. Hamtapotoka mkivishikilia vitu hivyo.” Maneno kama hayo yameandikwa kwenye Khasais an-Nasai. Kwa mujibu wa Rauzatul Ahbab, Mtukufu Mtume pia alisema, “Ee Mwenyezi Mungu!

Mfanye rafiki yako yule anayempenda Ali na uwe adui wa yule ambaye ni adui wa Ali na pia ielekeze kweli upande huo ambako Ali huelekeza uso wake.”

Imeandikwa kwenye Asbab al-Nuzul Tafsir Durrul Manthur, kwenye Tafsir Fatahul Bayan kilichoandikwa na Siddiq Hasan, kwamba Aya hii ‘Balligh’ imeteremshwa kuhusu Ali tu. Imeandikwa kwenye Sharh Bukhari Aini, Tafsir Gharaibul Qurani of Naishapuni, Tarikh bin Wazih, Kanzul Ummal na kadhalika, kwamba Aya ya ‘Balligh’ imeteremshwa kuhusu hadhi na ubora wa Ali.

Imeandikwa kwenye Tarikh Abul Fida kwamba baada ya kurudi kutoka Ghadir al-Khum, Mtukufu Mtume aliugua mwishoni mwa siku za Safar (Machi), 11, Hijiriya. Kwa mujibu wa Mishkat Sharif, sababu ya ugonjwa ilikuwa sumu ile ile iliyopelekwa huko Khaybar na ambayo ilionesha athari yake nyakati fulani. Imetaarifiwa kwenye Tarikh bin Alward kwamba aliwaomba masahaba wake wote kwenda na jeshi la Usmah bin Zayd na akasema kwamba alimteua Usamah kuwa ndiye kamanda wa jeshi.

Muhadithi Dehavi ameandika kwenye Madarij kwamba siku iliyofuata Mtukufu Mtume akiwa mahututi, alimkabidhi Usamah bendera ya vita na akamwomba aondoke aende kupigana na makafiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Usamah alimpa bendera hiyo Buradah bin Khazib nje ya jiji na akamteua kuwa mbeba bendera ya jeshi. Akaanza safari yake kutoka Madina na akasimama ‘Jaraf’ sehemu ambayo ipo karibu na Madina hadi jeshi lilipokusanyika.

Pia Mtume aliagiza kwamba Muhajirina na Ansar isipokuwa Ali lazima wajiunge na jeshi la Usamah na kwenda naye. Baadhi ya masahaba walianza kulaumu kwamba Mtukufu Mtume alimteua mtumwa na kumweka juu ya Muhajirina na Ansari wenye vyeo vya juu.

Kwa hiyo walijiingiza katika ukosoaji wa wazi kuhusu suala hili. Taarifa hii ilipomfikia Mtukufu Mtume alihuzunika sana, na licha ya homa, alitoka nje ya nyumba yake akiwa amekasirika sana na alipanda kwenye mimbari. Hapo, aliwahutubia watu, “Enyi watu! Haya ni mazungumzo gani ambayo mmejiingiza kuhusu kuteuliwa kwa Usamah kama kamanda wa jeshi, kama mlivyofanya wakati wa Vita ya Motah ambapo baba yake Usamah aliteuliwa kuwa kamanda wa jeshi. Kwa jina la Mwenyezi Mungu Usamah anastahili kuwa kamanda kama alivyokuwa baba yake.”

Ni kwenye al-Milal wan Nahl kilichoandikwa na Shahristan na Hujajul Karamah kilichoandikwa na Sidiq kwamba Mtukufu Mtume aliwaambia masahaba kufanya matayarisho ya haraka kwa ajili ya jeshi la Usamah. “Alaaniwe mtu anaye pinga jeshi la Usamah!”

Kwa mujibu wa Madarijun Nubuwwah, Abu Bakr na Umar walibaki Madina na Usamah akaondoka na jeshi. Alipokaribia kuondoka mama yake alimwambia kwamba hali ya Mtume haikuwa nzuri. Alimshauri asiendelee na safari na hakwenda. Kwa mujibu wa Tarikhut Tabari, katika hali hiyo, Mtume aliagiza Ali aende kwake.

Aishah alimshauri amwite baba yake (Abu Bakr) badala ya Ali, na Hafsa alishauri jina la baba yake (Umar) badala ya jina la Ali. Wakati huo watu hawa walikusanyika hapo. Lakini Mtume alisema, “Rudini makwenu. Nitawaiteni mimi endapo nitawahitaji.” Waliposikia hivyo watu hao waliondoka.

Kwenye Sahih Muslim imetaarifiwa kutoka kwa Bin Abbas kwamba Mtukufu Mtume alikaribia kutawafu akiwa kitandani kwake, Umar bin Khatab na masahaba wengine walikuwepo hapo nyumbani kwake Mtume. Mtukufu Mtume akasema, “Niletee kipande cha karatasi na kalamu ili kwamba niweze kuandika kitu (kama wosia wangu) kwa ajili yenu msije mkapotoka baada yangu.” Umar akasema, “Mtume haya kwa sababu ya weweseko. Tunayo Quran Tukufu na hiyo inatosha.” Hapo hapo palitokea mzozo miongoni mwa watu waliokuwepo hapo.

Baadhi yao walisema, “Ni wajibu wetu kutii maagizo yake ili kwamba aweze kuandika chochote apendacho kutuandikia.” Baadhi yao walimuunga mkono Umar. Ilipotokea kelele kubwa kuhusu suala hili, Mtume alisema, “ondokeni hapa kwangu.” Ilikuwa kwa sababu hii kwamba Bin Abbas alikuwa akisema, “Ulikuwa msiba mkubwa na maafa kwamba Mtume hankuweza kuandika chochote kwa sababu ya kelele na mfarakano miongoni mwa watu.”

Abdullah bin Abbas amenukuliwa na anasema kupitia kwa simulizi ya Said bin Jubayr alieleza kwenye Sahih Bukhari. “Ni siku ya janga iliyoje siku hii ya Alhamisi!” Baada ya kusema hivi, alilia na halafu akasema, “Siku hiyo ya Alhamisi, ugonjwa wa Mtume ulizidi sana, akasema nileteeni kitu cha kuandikia ili niweze kuandika kitu kwa namna ya wosia wangu ambao mkiufuata hamtakengeuka baada yangu.”

Baada ya kusikia haya watu walianza kubishana na kupingana Mtume akasema: “Haifai kugombana mbele ya Mtume.” Watu wakasema, Mtume anasema katika hali ya kuweweseka. Mtume akasema, “Ondokeni hapa kwangu. Hali yangu ni njema hata iwe vyovyote vile. Si sahihi vyovyote vile mtakavyo sema. Niacheni peke yangu. Ondokeni hapa.”

Baada ya hapo Mtukufu Mtume alitamka wosia zake tatu kwanza kuwa fukuza kwa nguvu washirikina wote waliopo kwenye Rasi ya Uarabuni na pili, kuridhia ujumbe uliotoka sehemu za mbali. Msimulizi hakusimulia wosia wa tatu au alisahau.”

Imesimuliwa kutoka kwa Said bin Jubayr kwenye Musnad Ahmad Bin Hanbal na Sahih Muslim kwamba Abdullah bin Abbas alisema, “Ni siku iliyoje siku hii ya Alhamisi, akalia sana hivyo kwamba machozi yalitiririka kwenye mashavu yake kama nyuzi za lulu.

Baada ya hapo alielezea kwamba Alhamisi ni siku ambapo Mtukufu Mtume alisema, “Nipeni vitu vya kuandikia ili kwamba niweze kuandika kitu kwa ajili yenu ambacho kwa njia ya wosia wangu msije mkapotoka kwamwe baada yangu.” Lakini, pamoja na yote hayo, watu walisema, “Anasema akiwa katika kuweweseka.”

Shahabuddin Khafaji ameandika kwenye Nasimur Riyaz Sharah Shafa Qadhi Ayaz kwamba kufuatana na maelezo ya hadith zingine kuhusu tukio hili, Umar alisema, “Mtume anasema akiwa katika kuweweseka.” Shahristani ameandika katika kitabu chake al-Milal wan Nihal kwamba mabishano na tofauti ya kwanza wakati Mtume anaugua ni pale ambapo Muhammad Ismail bukhari amesimulia kutoka kwa Abdallah bin Abbas kwa mamlaka ya kwake kwenye kitabu chake- Sahih Bukhari kwamba wakati maradhi yaliyosababisha kifo cha Mtume yalipozidi, alisema, “Nipeni kidau cha wino na karatasi ili niweze kuandika kwa ajili yenu hati kwa njia ya uthibitisho msije mkapotoka baada yangu.”

Aliposikia hivi, Umar alisema, “Mtume anasema hivyo kwa sababu ya ukali wa maumivu ya ugonjwa. Kitabu cha Mungu kitafanya kazi hiyo.” Hivyo, palitokea mzozo, Mtume alisema, “Ondokeni niacheni mimi na msibishane na kuhojiana mbele yangu.”

Hii ndio sababu iliyomfanya Abdullah bin Abbas aseme baadae, “Ni balaa iliyoje iliyo sababishwa na mabishano hayo! Ilikuwa baina yetu na kuandika kwa Mtume na ilisababisha asiandike.”

Allamah, Shibli Nomani ameandika, “Lipo neno la Hayr kwenye hadith lenye maana ya kuweweseka. Umar aliifasiri hotuba ya Mtukufu Mtume kama kuweweseka.” (Al-Faruq, ul. 61) kwenye kamusi maana ya neno ‘Hizyan’ imeoneshwa kama mazungumzo ya upuuzi (Sirat Juzuu ya 2, uk. 522).

Nazir Ahmad Dehlavi ameandika, “Wale waliokuwa na njozi za Ukhalifa katika akili zao walitangua mpango huo kwa kutumia ugomvi wa kuhalalisha upinzani wao kwa kusema kwamba Qurani ilitosha kufanya yote na kwa kuwa Mtume alikwishapoteza fahamu hapakuwepo na haja ya kumpa karatasi na kidau cha wino au vinginevyo angetoa imla ya mambo yasio na umuhimu.” (Ummahatul Ummah, uk. 92).

Imamu Ghazali ameandika kwamba kabla ya kifo chake Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwaambia masahaba wake wampe kalamu, karatasi na wino ili aandike ni nani aliyestahili kuwa Imamu na Khalifa wao. Lakini wakati huo Umar, aliwaambia watu kumwacha mtu huyo kwani alikuwa anasema upuuzi. (Sirral Alamin, Sharah Muslim Navi, Juzuu ya 2).

Kwa ufupi, Mtume aliponyimwa kalamu na wino palitokea mzozo miongoni mwa wale waliokuwepo hapo. Ufahamu wangu wa kihistoria umesema kwamba wakati huo Abu Dharr, Salman, Miqdadi na bin Abbas na kadhalika walipinga kitendo cha kukataa na wanawake wakawaasa kutoka nyuma, “Nini kimewatokea! Kwa nini hamsikilizi kile anachosema Mtukufu Mtume? Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, mpeni anachotaka.” Waliposikia hivyo Umar akasema, “Nyamazeni! Nyini ni sawa na wanawake wa Yusuf. Mnalia wakati Mtume mgonjwa na mnamghasi wakati anayo afya njema.” Mtume aliposikia sauti yake akasema, “Usiwakaripie kwani wao ni bora zaidi kuliko nyinyi.” (Tabrani).

Kwa mujibu wa Rauzatul Ahbab, wakati wa kifo chake, Mtume alimwambia mwanawe Fatimah Zahra awaite wanawe wa kiume. Aliwapeleka mbele yake. Wajukuuu hao wawili, waliketi karibu na babu yao baada ya kumpa heshima yake na walipomwona yupo katika maumivu makubwa ya ugonjwa, walilia sana hivyo kwamba watu waliowaona nao pia wakaanza kulia. Hasan aliweka uso wake kwenye uso wa Mtume na Husein aliweka kichwa chake kwenye kifua chake. Mtume alifungua macho na akawatazama kwa huba, akawapapasa kwa mahaba, na akaonesha utashi wake kwa watu kwamba wanastahili kuheshimiwa na kunyenyekewa.

Pia ipo Hadith kwamba baada ya kumsikia Husain analia, wote wale waliokuwa hapo walianza kulia na alipowasikia Mtume pia alianza kulia. Halafu akaagiza ndugu yake mpendwa, Ali aende kwake, Ali alikwenda na akaketi kuelekea kichwa cha Mtume. Aliponyanyua kichwa chake, Ali alikuwa anasogea karibu naye, alikiweka kichwa cha Mtume kwenye mkono wake.

Mtume akasema, “Ali! Nimekopa kiasi hiki cha deni kutoka kwa Myahudi fulani kwa ajili ya vifaa vya jeshi la Usamah. Mlipe kiasi hicho cha fedha. Ewe Ali! Utakuwa mtu wa kwanza kuja kwangu kwenye Haudhi ya Neema na utapata matatizo makubwa baada yangu. Yakabili matatizo hayo kwa uvumilivu na utakapoona kwamba watu wamechagua dunia, wewe shughulikia mambo ya akhera.” (Madarijun Nubuwwah, Juzuu ya 2, na Tarikhul Baghaad, Juzuu ya 11).
Pia imeandikwa kwenye Madarijun Nubuwah kwamba Fatimah Zahra alipata mshituko mkubwa kwa sababu ya kifo cha Mtume na alilia sana kwa uchungu. Muhadithi Dehlavi ameandika kwenye kitabu ‘Ma thabatabis Sunnah” kwamba matukio mengi ya hatari yalitokea baada ya kifo cha Mtume. Ameyataja kwenye shairi akisema kwamba endapo matatizo ambayo yalimpata, yangeipata mchana ungegeuka kuwa usiku wa giza. Mwandishi wa Rauzatul Ahbah anasema kwamba baada ya kifo cha Mtume hakuna mtu aliyemwona akicheka.

Tabaqat cha bin Sad ameandika kwamba kichwa cha Mtume kilikuwa kwenye paja la Ali wakati wa mwisho wa uhai wake. Hakim anasema kwenye Mustadirak kwamba Mtume kabla hajakata roho alipitisha siri kwa Ali na alitatua matatizo yake ya kimuujiza.

Abdul Barr kwenye kitabu chake, Istiab amemnukuu Abdullah bin Abbas akisema, “Ali anazo sifa nne za aina hiyo na hakuna miongoni mwenu aliye nazo. Kwanza, Alikuwa mtu wa kwanza kupata heshima ya kuswali na Mtukufu Mtume. Pili, alikuwa ndiye mshika bendera pekee wa Mtume katika kila vita. Tatu, ambapo wakati wa vita vitakatifu wakati mwingine watu walikuwa wanakimbia kutoka kwenye uwanja wa vita na kumwacha Mtume nyuma, Ali alikuwa imara kuwa pamoja na Mtume. Nne, Ali ni mtu aliyeiosha maiti ya Mtume na kuizika kaburini.”

Kwa mujibu wa imani ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, Mtukufu Mtume alifariki siku ya Jumatatu terehe 28 ya mwenzi wa Safar (machi), 11A.H. (Muwaddatul Qurba), uk. 49 kimechapishwa Bombay, 1310 A.H). Baada ya kifo chake palikuwepo na masikitiko na kilio miongoni mwa watu wa nyumba yake na masahaba walioheshimiwa.

Abu Dharr, Salman, Miqdad, Ammar na masahaba wengine waaminifu walikuwa wanalia sana. Kwa ufupi alikuwa kama rafiki mpenzi aliyekuwa na masikitiko kando yake. Historia inaonyesha kwamba Abu Dharr Ghifari alikuwa na maono ya kudumu kuhusu msiba huu.

Manazir Aksan Gilan ameandika, “Kwenye maelezo mengi ya maisha ya Abu Dharr japokuwa dalili za wazi zinaonekana za maumivu hayo ambayo bila ya kuwepo muumini anakuwa si muumini, hata hivyo yapo matukio kadhaa ya kutia moyo ambayo yanadhihirisha taswira nzuri ya uhusiano wa wote wawili yaani anayependa na anayependwa katika macho ya akili zetu.” (al-Ishteraki az-Zahid, uk. 90).

Wakati Mtukufu Mtume anakata roho, Abu Bakr alikuwa nyumbani kwake, Sakh, umbali wa maili moja kutoka Madina. Umar alizuia taarifa ya kifo isienee na Abu Bakr alipofika wote wawili walikwenda Saqifah Banni Saidah iliyopo maili tatu kutoka Madina, na pamoja nao pia alikuwa Abu Ubaydah bin Jarrah ambaye kazi yake ilikuwa mwosha. Vyovyote vile, masahaba wakuu wa Mtume walikwenda kuungana na kugombea Ukhalifa na kuacha maiti yake, na Ali alifanya mpango na akamudu mambo ya kuosha maiti ya Mtume na maziko.

Ali aliosha maiti, Fazal bin Abas alinyanyua kaptura yake, Abbas na Qathm walimgeuza na Usamah na Shaqran walimwagia maiti maji. Baada ya maiti ya Mtume kuoshwa, ilivishwa sanda. Abu Talhah alichimba kaburi. Ali, aliongoza Swala ya kumsalia maiti na yeye ndiye aliyeingia kaburini na kuilaza maiti inavyo stahili mahali pake.

Baadda ya hayo, alifukia kaburi kwa masikitiko makubwa. Abu Bakr na Umar na wengineo hawakushiriki matayarisho ya maziko yaani kuosha maiti, kuvisha sanda kusalia hadi kushusha maiti ndani ya kaburi, na kufukia kaburi la Mtukufu Mtume.
Kwa sababu waliporudi kutoka Saqifah, Mtume alikwishazikwa. (Kanzul Ummal, Juzuu ya 3, uk. 140 Arjahul Matalib, uk. 670, Fatahul Bari, Juz ya 6, uk. 4).
Mtukufu Mtume alikuwa na umri wa miaka 63 alipotawafu. (Abul Fida, Juz. ya 1, uk. 152).