Table of Contents

Adhana Kilugha Na Kisheria

Na nafasi ya muadhuni mbele ya Allah

Adhana kilugha: Ni tangazo. Mwenyezi Mungu amesema:

وَأَذَانٌ مِنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ إِلَى النَّاسِ يَوْمَ الْحَجِّ الْأَكْبَرِ

“Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa watu siku ya Hijja kubwa.”(9:3).

Maana yake ni tangazo kwa watu kutoka kwa wao wawili.

Kisheria: Ni tangazo la kuingia wakati wa Sala ya faradhi kwa kutumia maneno maalumu yaliyopokewa kwa sifa mahususi. Nayo ni kati ya amali bora ambazo humkurubisha mtu kwa Mwenyezi Mungu, na ni yenye fadhila nyingi na ujira mkubwa.

Amepokea Sheikh Tusi katika (Tahdhib) kutoka kwa Muawiya bin Wahabi, toka kwa Abu Abdillah (a.s.) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: “Atakayeadhini muda wa mwaka mmoja ndani ya mji kati ya miji ya Waisilamu basi atawajibika kupata pepo.”1

Pia amepokea toka kwa Saadil-askafu kuwa: “Nimemsikia Aba Abdillah akisema: Atakayeadhini muda wa miaka saba kwa ajili ya kupata radhi za Allah basi atakuja siku ya Kiyama akiwa hana dhambi yoyote.”2

Amepokea Swaduq toka kwa Al-Urzumiy toka kwa Aba Abdillah kuwa: “Watakaokuwa na shingo ndefu sana siku ya Kiyama zaidi ya watu wote niwaadhini.”3

Ameandika Ahmadi Muhammad Al-Barqiy katika kitabu Al-Mahasini toka kwa Jafar Al-Jaafy toka kwa Muhammad bin Ali Al-Baaqir kuwa: “Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Muadhini mwenye kutaka radhi za Allah ni sawa na mpiganaji katika njia ya Allah, mwenye kupigana kati ya makundi mawili.”4

Na nyingine nyingi riwaya kama hizi zenye kuhimiza kutoa adhana huku zikiwataka watu wa tabaka zote kuitangaza, na kukerwa na kitendo cha madhaifu kuificha adhana kwa udhaifu wao.

Tumeleta uchambuzi huu kwa ajili ya kubainisha mambo mawili:

Kwanza: Hakika sheria ya adhana ni sheria ya Mwenyezi Mungu haina uingiliano wowote na mwanadamu.

Pili: Kusoma historia ya tamko la الصلاةخيرمن النوم Sala ni bora kuliko usingizi (Tathwib) katika Sala ya asubuhi. Huku tukithibitisha kuwa tamko hili si sehemu ya adhana bali liliongezwa kwa kuungwa mkono na baadhi ya watu.

Hivyo mazungumzo yatahusu sehemu mbili.

  • 1. At-Tahdhibu: 2 /283 ?1126
  • 2. At-Tahdhibu: 2 /283 ?1128
  • 3. Thawabul-Amali: 52
  • 4. Al-Mahasin: 48 Namba: 68