read

Hitimisho

Bidaa Baada Ya Bidaa

Hakika historia ya adhana na iqama imejaa bidaa huku mikono ya waanzilishi wa bidaa imetumika kwa malengo ya mapendekezo ambayo hayakubaliki ndani ya sharia. Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyozushwa (bidaa ) baada ya Mtume:

Adhana Ya Pili Siku Ya Ijumaa

Mwenendo wa Mtume zama zake na zama za mashekhe wawili (Abubakari na Umar) ni kuadhini pindi Imam anapopanda mimbari kwa ajili ya kutoa hotuba. Lakini baada ya watu kuongezeka zama za Khalifa wa tatu khalifa aliamrisha adhana ya pili, nayo ni adhana inayotolewa pindi unapoingia wakati wa adhana, nayo hufahamika kama adhana ya pili ya Khalifa.

Imepokewa toka kwa Shafii kuwa ni sunna siku ya ijumaa kuwa na adhana moja wakati wa kupanda mimbari1

Ikiwa adhana ni kati ya mambo yanayomuhusu Mwenyezi Mungu tu basi mwanadamu hana haki kisheria kuongeza au kupunguza chochote humo. Huku khalifa alikuwa na uwezo wa kutatua suala husika kwa njia nyingine, nayo ni njia ya kuwatangazia watu kwa njia ambazo kwa namna yoyote ile hazitoingiliana na sheria ya Kiislamu, wala haikupasa kumwamrisha muadhini atoe adhana nyingine ambayo haikuwepo kabla.

Na cha kushangaza zaidi ni kuwa hata wanazuoni wenyewe wametofautiana upande wa hukumu kuhusu adhana mbili za siku ya ijumaa, na ni ipi inayohusiana na uharamu wa kuuza uliyopo ndani ya Aya ya Mwenyezi Mungu:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِنْ يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ

Enyi mlioamini inaponadiwa kwa ajili ya Sala siku ya ijumaa, basi nendeni upesi kumtaja Mwenyezi Mungu na acheni biashara, hiyo ni bora kwenu ikiwa mnajua.. 62:9

2.Baada ya kipindi cha maswahaba kupita wanazuoni wa Kufa wa kihanafi walianzisha kipengele kipya cha kuhimizia (tathuwibi) nacho ni kuongeza:

حي علي الصلاة حي علي الفلاح

Njooni kwenye Sala, njooni kwenye ushindi mara mbili baada ya adhana na iqama katika adhana ya alfajiri. Na hiyo ilipendekezwa na wanazuoni wa zamani wa kihanafi iwe ni kwenye alfajiri tu, wakadai ni makuruhu nyakati nyingine, lakini wale wa sasa wakapendekeza iwe kwenye sala zote isipokuwa magharibi kwa ajili ya ufinyu wa wakati.

Na hilo ni baada ya watu kuanza kupuuzia mambo ya kidini wakasema: Kuhimiza kati ya adhana na iqama wakati wa sala kuwe kulingana na wanavyofahamu watu wenyewe wa mji husika, sawa iwe kwa kuunguruma au kusema: Sala sala au kwa namna nyingine

3.Abu Yusufu alizua jipya kwa kuruhusu tamko la kuhimiza kwa ajili ya kumtanabahisha kila anayesimamia mambo na masilahi ya Waislamu, kama vile Imam na kadhi na mfano wa hao, hivyo baada ya muadhini kumaliza adhana aseme: Amani iwe juu yako ewe kiongozi, njoo kwenye Sala njoo kwenye ushindi, kaswali Allah atakurehemu.

Katika hili wafuasi wa Shafi na baadhi ya wafuasi wa Maliki wameungana na Abu Yusufu. Pia wafuasi wa Hanbali wameungana naye kwa sharti tu iwapo Imam au mfano wake hakusikia adhana, lakini Muhammad bin Hasan amelikanusha kwa sababu watu wote ni sawa katika amri ya jamaa. Baadhi ya wafuasi wa Maliki wameungana naye katika hilo2.

Kuondolewakwa Kipengele: Njooni Kwenye Amali Bora

Tumesema mwanzo kuwa bidaa katika adhana si kuingiza kipengele cha kuhimiza tu bali kuna mfano mwingine kama huo nao ni kuondolewa katika vipengele vya adhana na iqama kipengele cha:

حي علي خيرالعمل

Njooni kwenye amali bora, eti kwa lengo la kuzuwia tangazo hili ndani ya adhana lisiwe ni sababu ya kuzuwia watu kwenda kwenye jihadi. Kwa sababu iwapo watu watajua kuwa Sala ni amali bora basi watajihusisha tu na Sala na wataacha jihadi.

Mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu hili ni kuichafua na kuigilia sheria ya Mwenyezi Mungu kwa falsafa ya kitoto. Kwani kwa hakika mwenye jukumu la kuweka sheria tangu mwanzo alifahamu tahadhari hiyo lakini pamoja na hayo yote aliingiza kipengele hicho katika adhana.

Al-Qushajiy (Mwana theiolojia wa kiashaira) amenukuu kauli ya Khalifa wa pili kwa kusema: .Khalifa wa pili alisema akiwa juu ya mimbari kuwa: Vitu vitatu vilikuwepo zama za Mtume na mimi navikataza na ninaviharamisha na nitatoa adhabu kwa atakayevitenda: Ndoa ya muda (muta.), Muta.atil-Hajji

حي علي خيرالعمل

na njooni kwenye amali bora.3

Mashia wote wamekubaliana kuwa hiki ni kifungu cha adhana na hivyo ndivyo walivyoanzia zama za Mtume mpaka leo, na hilo limekuwa ni alama yao. Wanahistoria wengi wamekuwa wakiwaita Mashia kwa jina la utani kuwa ni: Wasema حي علي خيرالعمل (njooni kwenye amali bora).

Abufarji amesema ndani ya kitabu Maqatilu Twalibina, mlango wa mauwaji ya Al-Husayni bin Ali bin Al-Hasan bin Al-Hasani bin Ali (a.s.) kuwa: Hakika yeye alitawala Madina ndipo Abdallah bin Al-Hasan Al- Aftusi akapanda kwenye mnara ambao upo kichwani kwa Mtume sehemu ya majeneza, akamwambia muadhini: Adhini kwa kutamka: حي علي خيرالعمل.Njooni kwenye amali bora. 4

Al-Halabiy amesema: Imenukuliwa toka kwa mwana wa Umar na toka kwa Zainul-Abidina Ali bin Husein (a.s.) kuwa wao wawili walikuwa ndani ya adhana zao wakisema baada ya .njooni kwenye ushindi.: .njooni kwenye amali bora.5

أُولَٰئِكَ الَّذِينَ هَدَى اللَّهُ ۖ فَبِهُدَاهُمُ اقْتَدِهْ

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza, basi fuata muongozo wao.. (6:90)

  • 1. .Al-Majimuu: 3/132
  • 2. Al-mausuat Al-fiqihiyat: 2/361 neno adhana
  • 3. Alaul-dini Al-Qushujiy (Alifariki mwaka 879 A.H. huko Qistwintwiniyya): Sharhul-Tajridi: Soma tafsiri yake katika kitabu chetu (Buhuthu fil-milali wal-Nihali Juzu ya 2. Chapa ya Beirut
  • 4. Abul - faju Al-isfihaniy (284 - 357): Maqtalul- twalibina:297
  • 5. Burhanil-Dini Al-Halabiy: As-Siyrat:2/305