Table of Contents

Sehemu Ya Pili

Uchambuzi Kuhusu Historia Ya Kuingia Kipengele Cha Kuhimiza (Tathuwibi) Katika Adhana ya Alfajiri

At-Tathuwibi ni neno la Kiarabu litokanalo na kitenzi Thaba - Yathubu: Linaweza kuwa na maana ya kurejea, hivyo katika adhana litamaanisha kurejea kwenye amri kwa kuharakisha kuelekea kwenye Sala. Hivyo muadhini akisema: Njooni kwenye Sala atakuwa kawaita waelekee kwenye Sala, hivyo akisema tena: Sala ni bora kuliko usingizi atakuwa karejea katika maneno ambayo maana yake ni kuharakisha kwenda kwenye Sala. Mwandishi wa kamusi iitwayo: Al-Qamusi amefasiri kwa maana mbalimbali kati ya hizo maana ni: Kuomba waelekee kwenye Sala. Na ile hali ya kurudia mara mbili mbili ni ombi. Na pia kusema katika adhana ya alfajiri: Sala ni bora kuliko usingizi mara mbili - ni ombi.

Na amesema ndani ya kitabu Al-Magharibi kuwa: At-Tathuwibi ya zamani ilikuwa ni ile kauli aisemayo muadhini katika adhana ya asubuhi: Sala ni bora kuliko usingizi - mara mbili - Na hivi sasa At- Tathuwibi ni kusema: Sala Sala, imesimama 1

Dhahiri ni kuwa tathuwibi inatumika sana kwa maimam wa hadithi wakimaanisha ile kauli inayotajwa ndani ya adhana. Pia huenda ikatumika kumaanisha wito wowote unaokuja baada ya wito wa mwanzo hivyo hujumuisha wito wowote autoawo muadhini baada ya kumaliza adhana kwa kutamka tamko lolote alipendalo lenye maana ya wito wenye kuelekeza kwenye Sala.

As-Sanadiy amesema katika maelezo yake ya ziada ndani ya kitabu Sunanin-Nasai kuwa: Tathuwibi maana yake ni kurudia tangazo baada ya tangazo, Hivyo kauli ya muadhini: Sala ni bora kuliko usingizi ni sawa na hali hiyo hiyo, hivyo ikaitwa tathuwibi.2

Makusudio ya sehemu hii ni kutaka kudhihirisha hukumu ya kauli ya muadhini ndani ya adhana ya Sala ya alfajiri: Sala ni bora kuliko usingizi. Je ni kauli ya kisheria au ni bidaa iliyozushwa baada ya Mtume kutokana na pendekezo la baadhi ya watu walioona kuwa ni vizuri iwekwe kwenye adhana. Hiyo ni sawa iwe ndani ya adhana au hata baada ya adhana kwa wito wowote unaoelekeza kwenye Sala. Sawa iwe kwa tamko hili au lingine.

Hivyo tunasema kuwa tathuwibi kwa maana hii (Sala ni bora kuliko usingizi) imepatikana ndani ya hadithi za kisa cha ndoto ya adhana, na imepatikana tena katika hadithi nyingine. Ama katika fungu la kwanza imepatikana katika riwaya zifuatazo:

1. Riwaya aliyoipokea Ibnu Majah (Riwaya ya nne) na tayari umeshasikia maelezo ya As-Shaukaniy jinsi ilivyodhoofika3

2. Riwaya aliyoipokea Imam Ahmad nayo umeshajua udhaifu wa njia yake kwani yumo Muhammad bin Is’haqa na Abdallah bin Zaid bin Abdurabah4 . Riwaya aliyoipokea Saad katika kitabu chake At-Twabaqat. Katika njia yake yumo Muslim bin Khalid bin Qarqarat. Udhaifu wake tayari umeshaujua5.

Ama katika fungu la pili yaani tathuwibi katika hadithi zisizo za kisa cha ndoto ya adhana ni kwamba hadithi hizo zimenukuliwa na waandishi wa vitabu sita, na yafuatayo ni maelezo yao:

Aliyonukuu Ibnu Majah: ni kwa njia ifuatayo:

Alitusimulia Abu Bakr bin Shaybati kuwa: Alitusimulia Muhammad bin Abdallah Al-Asadiy toka kwa Abi Izraili toka kwa Al-Hakamu toka kwa Abdurahmani bin Layli toka kwa Bilal amesema kuwa: Mtume aliniamrisha nihimize (Sala ni bora kuliko usingizi ) katika Sala ya Asubuhi na akanikataza katika Sala ya Isha6.

Katika riwaya hii kuna dalili inayoonyesha kuwa katika kuhimiza unaweza kutumia wito wowote unaoelekeza kwenye Sala hata kama si tamko la: Sala ni bora kuliko usingizi. Dalili juu ya hilo ni kile kitendo cha kukataza kuhimiza katika Sala ya isha kwa sababu huwezi kuhimiza katika Sala hii isipokuwa kwa tamko lingine, mfano wa: Salat jamia, au imesimama Sala, au tamko lingine.

5-Ametusimulia Umar bin Rafi kuwa: Ametusimulia Abdallah bin Al- Mubarak toka kwa Maamari toka kwa Az-Zahariy toka kwa Saidi bin Al- Musayab toka kwa Bilal kuwa: Alikuja kumuadhinia Mtume kwa ajili ya sala ya asubuhi akaambiwa amelala, hapo akasema: Sala ni bora kuliko usingizi, Sala ni bora kuliko usingizi, basi ikaidhinishwa iwekwe kwenye adhana ya Sala ya alfajiri. Basi kwa namna hiyo jambo hilo likathibiti7. Njia zote mbili za upokezi ni pungufu.

Kwanza: Ibnu Abi Layli amezaliwa mwaka wa 17 na Bilal kafariki mwaka wa 20 au 21 huko Sham. Na Bilal alikuwa huko Sham tangu Shamu ilipofunguliwa hivyo Bilal ni mkazi wa Sham na Ibnu Abi Layli ni mkazi wa Kufa, hivyo itakuwaje asikie toka kwa Bilal ilhali kiumri yeye ni mdogo sana kwa Bilal na kimakazi yuko mbali na Bilal8.

Na Tirmidhi kapokea kama hivyo lakini kwa tofauti katika njia (sanad) asema: Hadithi ya Bilal hatuijui isipokuwa kupitia hadithi ya Abi Israii Al- Mlai, na huyu Abi Israili hajaisikia hadithi hii toka kwa Al-Hakamu (Ibnu Utayba).

Akasema: Hakika yeye aliipokea toka kwa Al-Hasani bin Amarat toka kwa Al-Hakam. Na Abu Israili jina lake ni Ismail bin Abi Is.haqa, na yeye kwa watu wa hadithi ni dhaifu9

Pili: ni kuwa Ibnu Majah amenukuu maneno toka kwa Az-zawaidi kwa kusema: Wapokezi wake ni wakweli isipokuwa njia yake ni pungufu kwa sababu Said bin Al-Musayabu hakuisikia toka kwa Bilal10 .

6. Aliyopokea an-Nasaiy

Alitupa habari Suwayd bin Nasri kuwa: Alitupa habari Abdallah toka kwa Sufiani toka kwa Jafari toka kwa Abi Salmani toka kwa Abi Mahdhurat amesema kuwa: Nilikuwa nikimuadhinia Mtume wa Mwenyezi Mungu na nilikuwa nikisema katika adhana ya Alfajiri ya mwanzo: (Njooni kwenye ushindi, Sala ni bora kuliko usingizi, Sala ni bora kuliko usingizi, Allah mkubwa Allah mkubwa, hapana mola wa haki isipokuwa Allah)11 .

Katika Sunan ya Al-Bayhaqiy12 na Subulu Salama13 sehemu ya jina Abi Salmani lipo jina Abi Sulaymani. Al-Bayhaqiy amesema: Na Abu Sulaymani jina lake ni Hamamul-muadhin, wala katika vitabu vyote tulivyonavyo vya wasifu wa wapokezi hakuna wasifu wa Hamamul- Muadhini hivyo Adh-Dhahabiy hakumtaja ndani ya kitabu chake (Mwenendo wa wasomi wema). Wala Al-Mazriy hakumtaja ndani ya Tahdhibil-Kimal na huyu Hamamu ni mtu asiyefahamika.

Ama Abu Mahdhurat yeye ni kati ya swahaba lakini mchache wa riwaya kwani riwaya alizopokea hazizidi kumi na alikuwa muadhini wa Mtume mwaka wa nane wakati wa vita vya Hunayni14 .

7. Aliyopokea Al-Bayhaqiy

Katika kitabu chake (Sunan) kuna njia inayokomea kwa Abi Qadamat toka kwa Muhammad bin Abdul-Malik bin Abi Mahdhurat toka kwa baba yake toka kwa babu yake kuwa amesema: Nilisema: Ewe Mtume wa Allah, nifundishe sunna ya adhana. Akasimulia hadithi husika, na katika maelezo yake Mtume akasema:

حي علي الصلاة حي علي الصلاة

(Njooni kwenye Sala njooni kwenye Sala), ikiwa ni sala ya Asubuhi sema:

الصلاة خيرمن النوم

(Sala ni bora kuliko usingizi, Sala ni bora kuliko usingizi).

8. Pia kapokea kwa njia inayokomea kwa Uthman bin Al-Saibu: Alinipa habari baba yangu na mama wa Abdul-Maliki bin Abi Mahdhurat toka kwa Abi Mahdhurat toka kwa Mtume. Mfano wa riwaya iliyopita15. Umeshajua hali ya Muhammad bin Abdul-Malik. Na Uthman bin Al-Saibu ni mtoto na mzazi wasiyojulikana hawana riwaya isipokuwa hiyo moja tu16

9-Aliyopokea Abu Daud

Amepokea kwa njia inayokomea kwa Al-Harith bin Ubaydi toka kwa Muhammad bin Abdul-Malik toka kwa baba yake toka kwa babu yake amesema kuwa: Nilisema: Ewe Mtume wa Allah nifundishe sunna ya adhana. Akaendelea mpaka akasema: Kama ni Sala ya asubuhi utasema: (Sala ni bora kuliko usingizi Sala ni bora kuliko usingizi)17.

Njia hii imemjumuisha Muhammad bin Abdul-Malik. Amesema Ibnu Hajari kuwa: Amesema Abdul-haqi kuwa: Njia hii si hoja. Na Ibnu Qaytani akasema: Huyu hajulikani, hatumjui aliyopokea toka kwake isipokuwa Al- Harith18. Na Amesema Al-Shaukani kuhusu Muhammad bin Abdul-Malik bin Abi Mahdhurat kuwa wasifu wake haujulikani. Na Al-Harith bin Ubaydi na yeye ana maelezo yake 19.

10-Pia amepokea kwa njia inayokomea kwa Uthman bin Saibu: Alinijulisha baba yangu na mama wa Muhammad binAbdul-Malik bin Abi Mahdhurat toka kwa baba Mahdhurat toka kwa Mtume Mfano wa habari hii20. Tayari umeshajua udhaifu wa njia hii.

11. Pia amepokea kwa njia inayokomea kwa Ibrahim bin Ismail bin Muhammad bin Abdul-Malik bin Abi Mahdhurat amesema kuwa: Nilimsikia babu yangu Abdul-Malik bin Abi Mahdhurat akisema kuwa alimsikia Abi Mahdhurat akisema kuwa: Mtume alinifundisha adhana herufi baada ya herufi - mpaka akasema: Alikuwa akisema katika Sala ya Alfajiri:

الصلاة خيرمن النوم

(Sala ni bora kuliko usingizi).21

Na Ibrahim bin Ismail ana riwaya moja tu na ukweli wake haujathibitishwa 22. Zaidi ya hapo huenda njia hii ni pungufu.

Aliyopokea Ad-Darqutniy

Nayo yamegawanyika:
12. Zipo riwaya zinazoonyesha kuwa ni sunna ndani ya adhana, amezipokea toka kwa Anas na Umar bila kuzinasibisha kwa Mtume nazo ni hadithi tatu:23

13. Zinazoonyesha kuwa Mtume alimuamrisha Bilal kufanya hivyo, lakini njia hiyo ni pungufu. Amepokea Abdul-Rahman bin Abi Layli toka kwa Bilal24 huku njia yake ni dhaifu kwa kuwemo Abdur-rahmani bin Al- Hasan ambaye huitwa Abu Mas.udi Az-Zajaju.Na Abu Hatim kamuelezea kwa kusema: Yeye si hoja hata kama wengine wakimlainisha 25.

14. Zipo zinazoonyesha tangazo kabla ya adhana kwa namna yoyote ile. Na hilo liko nje ya mada. Na baadhi ya waliyomo katika mtiririko wa njia hii wameidhoofisha26.

Aliyopokea Al-Daramiy

15. Ad-Daramiy kapokea kwa njia inayokomea kwa Az-Zahariy toka kwa Hafsa bin Umar bin Suad Muadhini.Hafsa amesema: .Walinisimulia ndugu zangu kuwa Bilal alikwenda kumuadhinia Mtume kwa ajili ya Sala ya Asubuhi, wakamwambia Mtume amelala, hapo Bilal akanadi kwa sauti ya juu:

الصلاة خيرمن النوم

(Sala ni bora kuliko usingizi:, ndipo ikapitishwa na kuwekwa ndani ya adhana ya Sala ya Alfajiri27. Riwaya hii si hoja: Kwanza kwa kuwemo Az-Zahriy na Hafsa ambaye hana riwaya isipokuwa moja tu nayo ni hii28.

Zaidi ya hapo ni kuwa hajulikani ni nani asili aliyenukuu riwaya hii.

16. Aliyopokea Imam Malik

Ni kuwa muadhini alikwenda kumuadhinia Umar bin Al-Khatab kwa ajili ya Sala ya Asubuhi hivyo akamkuta amelala, muadhini akasema:

الصلاة خيرمن النوم

(Sala ni bora kuliko usingizi), ndipo Umar akaamrisha kipengele hicho kiwekwe ndani ya wito wa Sala ya Asubuhi29.

Matokeo Ya Riwaya

Hakika riwaya zinazoelezea kipengele cha kuhimiza (Sala ni bora kuliko usingizi) zinapingana sana huwezi kuzioanisha katika maana moja. Na vifuatavyo ni vifungu vyake:

1. Zipo zinazoonyesha kuwa Abdallah bin Zaid aliota usingizini kipengele cha (Sala ni bora kuliko usingizi) katika ndoto yake na ilikuwa ni sehemu ya adhana tangu mwanzo wa adhana.

2. Zipo zinazoonyesha kuwa Bilal aliongeza kipengele hicho ndani ya adhana, na Mtume akakipitisha na kumtaka Bilal akiweke kiwe sehemu ya adhana, na hilo ni kama ilivyo kwenye riwaya ya Ad-Daramiy.

3. Zipo zinazoonyesha kuwa Umar bin Al-Khatabi alimuamrisha muadhini akiweke ndani ya wito wa asubuhi, hilo ni kama alivyopokea Imam Malik.

4. Zipo zinazoonyesha kuwa Mtume wa Allah alimfundisha Abi Mahdhurat, hilo ni kama ilivyo katika riwaya ya Al-Bayhaqiy katika kitabu chake.

5. Dhahiri ni kuwa Bilal alikuwa akinadi asubuhi akisema: حي علي خيرالعمل (Njooni kwenye amali bora), hivyo Mtume akamwamrisha atoe kipengele hicho na sehemu yake aweke kipengele:

الصلاة خيرمن النوم

(Sala ni bora kuliko usingizi), na aache حي علي خيرالعمل (njooni kwenye amali bora.
Haya ni kama alivyopokea Al-Muttaqiy Al-Hindiy ndani ya kitabu chake Kanzu 8 / 345 namba 23188 ).

Kutokana na mgongano huu wa wazi hatuwezi kutegemea riwaya hizo. Na kwa kuwa jambo lenyewe lipo kati ya hali mbili: ima liwe ni sunna au bidaa basi tunapasa kuliacha kwa kuwa hatutoadhibiwa iwapo tutaliacha kinyume na litakapokuwa ni bidaa.

Maneno Yawanavyuoni Kuhusiana Na: Kuhimiza Sala Ni Bora Kuliko Usingizi

Upande wa swahaba na tabiina wapo wanaoona kuwa jambo hilo ni bidaa wala Mtume hakuliamrisha, na kuwa lilizuka baada ya Mtume. Yafuatayo ni maelezo yao:

1. Ibnu Jariri anasema: .Amr bin Hafsa alinipa habari kuwa Saad muadhini ndiye mtu wa kwanza aliyesema:

الصلاة خيرمن النوم

(Sala ni bora kuliko usingizi), ilikuwa wakati wa utawala wa Umar hivyo Umar akasema: Ni bidaa, kisha akamuacha na wala Bilal hakumuadhinia Umar.

2. Pia amepokea toka kwake kuwa: Alinipa habari Hasan Muslim kuwa kuna mtu alimuuliza Twausi: Ni lini ilianza: Arabic text (Sala ni bora kuliko usingizi)? Akajibu: .Haikutamkwa hii wakati wa Mtume lakini Bilal aliisikia zama za Abu Bakr baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.) ilikuwa ikitamkwa na mtu asiye muadhini, hivyo akaichukua toka kwake, kisha akaadhini kwa kipengele hicho, lakini toka wakati huo Abu Bakr hakuishi sana zikawa zimeingia zama za Umar. Akasema Umar: Tungemkataza Bilal kuhusu hili alilolizusha, utadhani kalisahau ameendelea kuwaadhinia watu kwa hili mpaka leo30.

3. Amepokea Abdur-Razaqi toka kwa Uyynati toka kwa Laythu toka kwa Mujahidu kuwa amasema: .Nilikuwa na Ibnu Umar akasikia mtu akihimiza (tathuwibi). Akasema: .Hebu twende zetu tutoke kwa mtu huyu wa bidaa31.

Kwa riwaya ya Abu Daud ndani ya Sunan yake, dhahiri ni kuwa mtu huyo alihimiza katika Sala ya adhuhuri na Sala ya Alasiri na si Sala ya Asubuhi32

4. Yaliyopokewa toka kwa Abu Hanifa kama ilivyo ndani ya Jamiul- Masanidi toka kwa Hamadi toka kwa Ibrahimu amesema: Nilimuuliza kuhusu tamko la himizo (tathuwibi) akasema: Hilo ni katika mambo yaliyozushwa na watu, nalo ni jambo zuri kati ya mambo waliyoyazusha. Kisha akaongeza kuwa: wao tamko hilo lilikuwa baada ya muadhini kumaliza adhana yake husema: Arabic text (Sala ni bora kuliko usingizi) . mara mbili.

Amesema: Riwaya hii ameitoa Imam Muhammad bin Al-Hasan (As- Shaybani) ndani ya kitabu chake Al-athar. Wao wawili wamepokea toka kwa Abu Hanifa. Kisha Muhammad akasema: Nayo ni kauli ya Abu Hanifa na ndio tunayoifuata33.

Riwaya hii inaonyesha kuwa kipengele hiki kilikuwa kinawekwa baada ya kumaliza adhana hizo ni zama za mtukufu Mtume au makhalifa na wala hakikuwa ni sehemu ya adhana bali muadhini alikitamka yeye mwenyewe kwa ajili ya kuamsha watu toka usingizin, kisha baadaye kikaingizwa ndani ya adhana.

5. As-Shaukani kanukuu toka kwenye Al-Bahri Al-Zakhari kuwa: Alikizua Omar. Mwanae akasema: .Hii ni bidaa. Imepokewa toka kwa Ali (a.s.) kuwa baada ya kusikia tamko hilo (tathuwibi) alisema: .Msizidishe ndani ya adhana kitu ambacho hakimo.. Kisha baada ya kutaja hadithi ya Abu Mahdhurat na Bilal akasema: .Tunasema ikiwa ni kwa sababu ya kukanushwa na Ali (as) na mwana wa Omar na Twausi basi tumekubali. Hivyo timeamrishwa kwa ajili ya kuhisisha hali na wala si kama sheria, hiyo ni ili tuoanishe kati ya riwaya hizo34.

6. Al-Amiru Al-Yamaniy As-Swinaiy (Aliyefariki mwaka 182) amesema: .Nilisema: Kutokana na haya ni kuwa kipengele hiki

الصلاة خيرمن النوم

(Sala ni bora kuliko usingizi) si miongoni mwa matamshi ya adhana iliyowekwa na sheria kwa ajili ya kuwaita watu waelekee kwenye Sala huku ikionyesha kuwa wakati wa Sala umeingia. Bali kipengele hiki ni kati ya matamshi ambayo yalianzishwa ili kumuamsha yule aliyelala, hivyo matamshi hayo ni sawa na ile tasbihi ya mwisho ambayo hivi sasa watu wameizoea hasa badala ya adhana ya kwanza.
Kisha akasema: Basi ukishalijua hili utakuwa mwepesi kwako mjadala uliyozoeleka kati ya wanazuoni kuhusiana na matamshi hayo, Je yenyewe ni sehemu ya matamshi ya adhana au siyo. Na je ni bidaa au siyo35

7. Ibnu Qaddama amenukuu toka kwa Is.haqa kuwa baada ya kunukuu riwaya ya Abi Mahdhurat alisema: Hili ni jambo walilolizua watu.

Abu Isa amesema: .Hiki ndio kipengele cha kuhimiza (tathuwibi) kilichochukiwa na wanazuoni, na ndicho kilichomsababisha mwana wa Umar atoke msikitini alipokisikia36.

8. Kwa sababu riwaya nyingi zilizotoka kwa Maimam wa Ahlul-Bait zinathibitisha kuwa ni bidaa. Amepokea Sheikh Tusiy kwa njia sahihi toka kwa Muawiya bin Wahabi alisema kuwa: Nilimuuliza Aba Abdullah kuhusu tamko la kuhimiza ambalo huwa kati ya adhana na iqama akasema: Hatulijui37

9. Jambo lililodhihiri kwangu baada ya kudurusu riwaya zinazozungumzia adhana ni kuwa: Familia mbili zilifuatilia kwa undani yale yaliyopokewa toka kwa babu yao Abdallah bin Zaid na Abi Mahdhurat, hivyo zikafanya makusudi kueneza yale yaliyonasibishwa kwa babu yao kwa sababu yanaonyesha fadhila kwa familia, kwani laiti ingekuwa si hivyo basi jambo hili la sheria ya adhana kuletwa kwa ndoto, na kuongezwa kipengele cha kuhimiza katika adhana ya Sala ya Asubuhi lisingeenea kwa mapana ya namna hii. Kwa ajili hiyo huenda mtu angeweza kuyatilia shaka yale yaliyonukuliwa toka kwa babu yao.

Tayari umeshajua kuwepo kwa wapokezi ambao wanaonasibishwa na familia hizi mbili katika njia ya upokezi wa riwaya hizi.

10. Hakika kifungu cha kwanza na cha pili kinathibitisha kuwa yeye Allah ndiye Mungu wa ulimwengu wote na kisicho Yeye ni sawa na si rabi hakina utawala wowote mbele ya Allah. Kifungu cha tatu kinathibitisha kuwa Muhammad (s.a.w.w.) ni Mtume wa Allah ambaye alimtuma kufikisha ujumbe wake na kutekeleza wito wake. Hivyo mwisho wa kifungu hicho tangazo na wito wake unabadilika toka katika uthibitisho mpaka kwenye wito wa kuelekeza kwenye Sala ambayo ameifaradhisha Mwenyezi Mungu na ambayo mwanadamu huitumia kuwasiliana na Mwenyezi Mungu, na kupitia Sala hiyo unyenyekevu wa mwanadamu huchanganyikana na utukufu wa muumba. Kisha hutoa wito kuelekea kwenye ushindi na uokovu na amali bora ambayo ndio lengo la Sala. Na baada ya kumaliza wito wa ushindi na amali bora hurudia tena kutaja ukweli halisi wa milele ambao ulitamkwa wazi wazi mwanzo wa vifungu vya adhana, hivyo husema:

الله اكبر الله اكبر لااله الا الله لااله الا الله

Allah Mkubwa Allah Mkubwa. Hapana mola wa haki isipokuwa Allah. Hapana mola wa haki isipokuwa Allah.

Hii ndio hali halisi ya adhana na muundo wake huku yote mawili yakiwa katika mtiririko mmoja ambao umehitimishwa na sheria ya Mwenyezi Mungu kwa ufanisi. Huku ukielezea ukweli halisi wa milele na kumzuwia mwanadamu asijifunge katika minyororo ya dunia na udanganyifu wake. Hii ndio hali halisi anayoihisi kila anayesikia adhana na kila mwenye kufatilia vifungu vya adhana na maana yake. Lakini hapa kuna ukweli ambao mimi au mwingine hawezi kuuficha (Iwapo tu mtu huyo atajiepusha na mtazamo wake wa mwanzo au ubinafsi wa kimadhehebu) nao ni kuwa: Muadhini anapotoka katika kifungu cha wito wa kuelekea kwenye Sala na ushindi na amali bora (katika adhana ya asubuhi) kisha akaingia kwenye tangazo la kuwa:

الصلاة خيرمن النوم

Sala ni bora kuliko usingizi, hapo anakuwa katoka kwenye kilele cha fasaha na kwenda kwenye maneno yasiyo fasaha. Kwani anakuwa anatangaza jambo ambalo linafahamika hata kwa watoto wadogo, kwani anapigia kelele jambo ambalo linafa- hamika kwa wote isipokuwa yule asiyefahamu mambo ya kiakili. Kwa sababu kule kutangaza kuwa sala ni bora kuliko usingizi ni sawa na mtu anayesimama katika mkusanyiko wa watu na kutangaza eti mbili ni nusu ya nne.

Hili ndilo nililolihisi pindi nilipozuru Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu mwaka 1375 A.H. huku nikisikia adhana toka haramu mbili takatifu. Bado akili na ubongo wangu unaamini kuwa kifungu hiki si miongoni mwa maneno ya Allah, bali kilipandikizwa kati ya vifungu vya adhana kwa sababu maalumu. Na hilo ndilo lililonifanya nichambue maudhui hii na kuandika ujumbe huu.

 • 1. Al-Baharaniy: Al-Hadaiqu: 7/419 Angalia An-Nihayati mlango wa hadithi ya kustaabasha 1/226. (2)Lisanul-Arabi: kitenzi: Thawaba. Na Al-Qamusi kitenzi: Thawaba
 • 2. As-Sunan: 2/14 Upande wa nyongeza
 • 3. Angalia riwaya ya nne uk. 25 na maneno ya Ash-Shaukani katika kitabu hiki uk.39
 • 4. Angalia tuliyonukuu toka kwa Imam Ahmadi baada ya hadithi toka vitabu sita uk.41
 • 5. Angalia uk. 47 ndani ya kitabu hiki.
 • 6. Ibnu Majah: As-Sunan: 1/237 namba 715
 • 7. Ibnu Majah: As-Sunan: 1/237 namba 716
 • 8. Ash-Shaukaniy: Naylil-Awtari: 2/38
 • 9. At-Tirmidhiy : As-Sunan1/378 namba 198
 • 10. Ibnu Majah: As-Sunani:1/237 namba 716. Saidi Al-Musayabu amezaliwa mwaka 13 na kufariki mwaka 94
 • 11. An-Nasaiy: As-Sunan: 2/13 Mlango: kuhimiza katika adhana (Tathuwibi) 34
 • 12. Al-Bayhaqiy: As-Sunan: 1/422.
 • 13. Al-Swinaiy: Subulul-Salami: 1/221
 • 14. Ibnu Hazmi Muhispania: Majina ya maswahaba wapokezi:161 namba 188
 • 15. Al-Bayhaqiy: As-Sunan: 1/421- 422 Mlango: kuhimiza katika adhana ya Subhi
 • 16. .Al-Dhahabiy: Mizanul-Itidali: 2/114 namba 3075. (Al-Saibu), Ibnu Hajar: Tahdhibul-tahdhibi: 7/117 namba 252 (Uthman bin Al-Saibu)
 • 17. Abu-Daudi: As-Sunan: 1/136 namba 500
 • 18. Ibnu Hajar: Tahdhibul-Tahdhibi: 9/317
 • 19. Al-Shaukaniy: Naylul-Awtwari: 2/38
 • 20. Abu Daudi: As-Sunan: 1/136-137 Mlango: Muundo wa adhana namba 501
 • 21. Abu Daudi: As-Sunan:1/136-137 Mlango: Muundo wa adhana namba 504 36
 • 22. Jamalud-Dini Al-Maziy: Tahdhibul-Kamali: 2/44 namba 147
 • 23. Ad-Darqutniy: As-Sunan: 1/243 namba 38-39-40
 • 24. Ad-Darqutniy: As-Sunan:1/243 namba 41
 • 25. Angalia Mizanul-Itidali:2/556 namba 4851
 • 26. Ad-Darqutniy: As-Sunan:1/244-245 namba 48, 51, 52, 53
 • 27. Ad-Darqutniy: As-Sunan:1/270 Mlango: Kuhimiza katika adhana ya Al-fajiri 37
 • 28. Jamalul-Din Al-Maziy: Tahdhibul-Kamali: 7/30 namba 1399. Na Al-Dhahabiy amesema katika Mizanul-Itidali: 1/560 namba 2129 kuwa: Al-zaharii peke yake ndiye kapokea riwaya toka kwa Hafsu
 • 29. Al-Imam Maliki: Al-Muwatwau: 78 namba 8 38.
 • 30. . Al-Mutaqiy Al-Hindiy: Kanzul-Ummal: 8/357 namba 23252 na 23251. Na riwaya ya Abdul-Razaqi katika Al-Muswanaf: 1/474 namba1827 1828 na 1829.
 • 31. Abdul-razaqiy Al-Swinaiy: Al-Muswanafu:1475 namba 1832. Pia imepokewa na Al-Mutaqiy Al-Hindiy ndani ya Kanzul-Ummal: 8/357 namba 23250
 • 32. Abu Daudi: As-sunan:1/148 namba 538
 • 33. Al-Khawazimiy: Jamiul-Masanidi:1/296
 • 34. Al-Shaukaniy: Naylul-Awtwari: 2/38
 • 35. Al-Swinaiy:Siubulul-Salami fi Sharhi bulughul-Marami:1/120
 • 36. Ibnu qadamat Al-mughniy. 1/420
 • 37. Al-wasailu:4/650 mlango wa 22 mlango wa adhana na Iqama Hadithi ya 1