read

Aya 1 – 26: Litakapotukia Tukio

Maana

Litakapotukia hilo Tukio. Hapana cha kukanusha kutukia kwake.

Makusudio ya tukio hapa ni Kiyama. Katika maisha ya duniani kuna wanaoisadiki Akhera na wanaoikanusha. Lakini ikashafikia wakati wake na kutekelezewa kila nafsi iliyoyachuma, hapo ndio wataikubali na kukiri.

Kwanini? Kwa vile tukio lake ndilo Literemshalo linyanyualo. Linawainamisha wakosefu na kuwainua wenye takua.

Itakapotikiswa ardhi kwa mtikiso, Na milima itaposagwasagwa, Iwe mavumbi yanayopeperushwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaashiria kuharibika ulimwengu. Ardhi itavunjwavunjwa na tetemeko na majabali yatageuka vumbi.

Na nyinyi mtakuwa namna tatu:

Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atawakusanya watu na kuwafanya makundi matatu:

Basi watakuwepo wa kuume; je, ni yapi ya wa kuume?

Ni ambao kesho watapewa vitabu vyao kwa mikono yao ya kuume. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

“Na ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kuume, atasema: Haya someni kitabu changu! Hakika nilijua kuwa nitapokea hisabu yangu.

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَيَقُولُ هَاؤُمُ اقْرَءُوا كِتَابِيَهْ {19}

إِنِّي ظَنَنْتُ أَنِّي مُلَاقٍ حِسَابِيَهْ {20}

فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَاضِيَةٍ {21}

Basi yeye atakuwa katika maisha ya kuridhiwa.” (69:19-21).

Kundi, hata kama ni katika watakaookoka, lakini sio kama kundi la tatu.

Na wa kushoto; je, ni yapi ya wa kushoto?

Hawa ni wale watakopewa vitabu vyao kwa mikono yao ya kushoto. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِشِمَالِهِ فَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُوتَ كِتَابِيَهْ {25}

وَلَمْ أَدْرِ مَا حِسَابِيَهْ {26}

يَا لَيْتَهَا كَانَتِ الْقَاضِيَةَ {27}

“Na ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto, atasema: laiti nisingelipewa kitabu changu wala nisijue nini hisabu yangu. Laiti mauti yangelikuwa ni ya kumaliza.”
(69:25-27).

Na waliotangulia ndio waliotangulia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema waliotangulia, lakini hakubainisha wametangulia kwenye jambo gani; hata hivyo amebainisha mahali pengine: “Hakika wale ambao humwogopa Mola wao wanamnyenyekea. Na wale ambao wanaamini ishara za Mola wao. Na wale ambao hawamshirikishi Mola wao.

Na wale ambao wanatoa walichopewa na hali nyoyo zao zinaogopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao. Hao ndio wanokimbilia kwenye kheri na ndio watakaotangulia kuzifikia.” Juz. 18 (23: 57-61).

Kwa hiyo basi waliotangulia ni wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu peke yake bila ya kuwa na mshirika, na wakaamini siku ya mwisho, wala wasipuuze kumtii kwa kuhofia ghadhabu na adhabu yake, na wakawa wanajitolea mhanga ulio ghali kwa kutaka radhi na thawabu zake.

Hao ndio watakaokaribishwa katika Bustani zenye neema.

Wana hadhi kubwa ya kukaribishwa kwenye utukufu wake mtukuka na wana fungu kubwa la neema yake.

Fungu kubwa katika wa mwanzo, Na wachache katika wa mwisho.

Wametofautiana wafasiri kuwa ni nani hao wa mwanzo, wa mwisho na wachache? Kuna waliosema kuwa makusudio ya wa kwanza ni walioami- ni na wakatangulia kwenye heri kabla ya Muhammad (s.a.w.). Wengine wakasema wote wa kwanza na wa mwisho ni katika umma wa Muhammad (s.a.w.).

Tuonavyo sisi ni kwamba wa kwanza ni ishara ya zama za uislamu wa dhahabu, pale ulipokuwa na nguvu na madaraka na waislamu wakawa wanauamini kwa kauli na vitendo wakiupigania kwa roho na mali. Na wengine ni ishara ya waumini wachache katika zama za baadae. Kauli hii inasadikishwa na kauli ya Imam Ali (a.s.):

“Zitakuja zama kwa watu haitabakia Qur’an isipokuwa maandishi tu, na Uislamu isipokuwa jina lake. Misikiti yao itajengwa vizuri, lakini itakuwa mibovu ya uongofu. Wakazi wake na waamirishaji wake ndio watakuwa washari zaidi katika watu wa ardhi.
Kutoka kwao itatokea fitna na kwao itaishia hatia. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Ninaapa nitawapelekea hawa fitna nimwache mpole hana la kufanya.”

Watakuwa juu ya viti vya fahari vilivyodariziwa.

Vitakuwa vimefuwa kulingana na mili ya watu wa Peponi iliyo myororo na nyuso zenye kunyinyirika.

Wakiviegemea wakielekeana.

Hawana shughuli wala fikra ya familia.

Watawazunguukia vijana wa milele Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi.

Vikombe vyenye asali safi, pombe ya ladha kwa wanywaji, mvinyo wenye kusiliwa. Katika kuyapata basi nawashindane wenye kushindana.

Hawataumwa kichwa kwa hivyo wala hawataleweshwa.

Vinywaji hivyo havimwondolei mnywaji akili yake wala hataumwa na kichwa.

Na matunda wayapendayo, na nyama ya ndege kama wanavyotamani. Na Mahurulaini, walio kama mfano wa lulu zilizohifadhiwa.

Kinywaji safi, nyama freshi, matunda aina kwa aina, wanawake wazuri, matandiko na viti. Ni raha na utulivu. Yote hayo ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda ya heri na masilahi ya umma bila ya riya wala kupigiwa ngoma au nzumari.

Humo hawatasikia upuzi wala maneno ya dhambi. Isipokuwa maneno ya Salama, Salama.

Watasikia wapi upuzi na porojo na peponi hakuna matamshi isipokuwa heri tu. Yote haya ni ya wale waliotangulia. Ama watu wa kuume Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebainisha fungu lao, katika Aya zifuatazo.

وَأَصْحَابُ الْيَمِينِ مَا أَصْحَابُ الْيَمِينِ {27}

Na wa kuume; je, ni yapi ya wa kuume?

فِي سِدْرٍ مَخْضُودٍ {28}

Katika mikunazi isiyo na miba,

وَطَلْحٍ مَنْضُودٍ {29}

Na migomba iliyopangiliwa,

وَظِلٍّ مَمْدُودٍ {30}

Na kivuli kilichotanda,

وَمَاءٍ مَسْكُوبٍ {31}

Na maji yanayomiminika,

وَفَاكِهَةٍ كَثِيرَةٍ {32}

Na matunda mengi;

لَا مَقْطُوعَةٍ وَلَا مَمْنُوعَةٍ {33}

Hayakatiki wala hayakatazwi,

وَفُرُشٍ مَرْفُوعَةٍ {34}

Na matandiko yaliyonyanyuliwa.

إِنَّا أَنْشَأْنَاهُنَّ إِنْشَاءً {35}

Hakika Sisi tumewaumba upya.

فَجَعَلْنَاهُنَّ أَبْكَارًا {36}

Na tutawafanya bikira,

عُرُبًا أَتْرَابًا {37}

Wanaopenda, walio marika.

لِأَصْحَابِ الْيَمِينِ {38}

Kwa ajili ya watu wa kuume.

ثُلَّةٌ مِنَ الْأَوَّلِينَ {39}

Fungu kubwa katika wa mwanzo.

وَثُلَّةٌ مِنَ الْآخِرِينَ {40}

Na fungu kubwa katika wa mwisho.