read

Aya 1 – 6: Ndiye Wa Mwanzo Na Ndiye Wa Mwisho

Maana

Katika Juz. 14 (16:49), Mwenyezi Mungu anasema: “Vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.”

Kumsabihi Mwenyzi Mungu na kumsujudia ni kukiri uweza wa Mwenyezi Mungu mtukufu na hikima yake. Kukiri huku kunakua katika hali mbili: Moja ni kwa lugha ya kusema na nyingine ni kwa lugha ya hali. Mtu huwa anatumia hali zote mbili, lakini viumbe vingine visivyoweza kutamka huwa vinasujudi na kusabihi kwa lugha ya hali. Kwa sababu hakuna kiumbe chochote isipokuwa kinafahamisha kuweko mwenye kukifanya na kukipa sura. Tazama Juz. 15 (15:44) kifungu cha ‘Kila kitu kinamsabihi.’

Katika vitabu vya sera, Hadith na Tafsiri imeelezwa kuwa Fatima binti wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikuwa akifanya kazi zote za nyumbani yeye mwenyewe, akimuhudumia mumewe na watoto wake. Siku moja akamweleza baba yake hali yake, naye akaona athari ya juhudi yake kwenye mikono yake. Basi akamtaka ampatie mjakazi katika mateka wa vita ili amsaidie kazi za nyumbani.

Mtume akasema: sitakupa mjakazi na hali kuna mwingine anafunga tumbo lake kwa njaa. Kisha akaendelea kusema: Unaonaje nikikufahamisha jambo lilio na heri zaidi kuliko mjakazi – kusabihi Mwenyezi Mungu mara 33, kumhimidi mara 33 na kumfanyia takbira mara 34. Fatima akasema: Nimeridhia ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Tasbihi hii inajulikana kwa jina la Tasbih Zahra.

Yeye ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Anahuisha na anafisha.

Kama kwamaba muulizaji ameuliza kwanini vikamsabihi Mwenyezi Mungu vilivyo katika ardhi na mbingu? Na Yeye ni Mwenye uweza wa kila kitu. Analolitaka hua na asilolitaka haliwi.

Yeye ndiye wa Mwanzo bila ya kuanza kulikokuwa kabla yake na kutoka kwake ndio chanzo cha kila kitu. Na ndiye wa Mwisho, bila ya kuweko na ukomo baada yake na kwake Yeye ndio mwisho wa kila kitu.

Naye ndiye wa Dhahiri kwa athari na vitendo sio kwa kuhisiwa. Na wa Batini, akili na dhana haziwezi kufikiria hakika yake; isipokuwa anadhihiri kwa athari zake.

Kwenye Nahjul-balagha imesemwa: “Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye ameonyesha athari za mamlaka yake na ukuu wa ukubwa wake, zilizozubaisha mboni za macho kwa maajabu yake na kuzuia dhana za nafsi kujua hakika ya sifa zake... amekuwa karibu akawa mbali na amekua juu akawa chini. Kuwa kwake kumetangulia nyakati, na kupatikana kwake kumetangulia kukosekana, na ukale wake umetangulia kuanza.”

Naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.

Ni mjuzi wa kila kitu kwa vile ameumba kila kitu.

Yeye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha akastawi juu ya Arshi.

Makusudio ya siku ni mikupuo, kustawi ni kutawala na arshi ni ufalme. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:54), 11 (10:3), 12 (11:7), 19 (25:59) na 21 (32:4).

Anayajua yanayoingia katika ardhi miongoni mwa hazina, mbegu na maji; hata milipuko ya mabomu ardhini wanayoilipua maadui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu, Mwenyezi Mungu anaijua hakika yake na atahri yake. Pia anajua lengo lake kuwa ni kutawala waja wa Mwenyezi Mungu na kuwawafanya wawanyenyekee na wakuze viwanda vya silaha

Vile vile Mwenyezi Mungu anayajua na yanayotoka humo, ikiwemo mimea wadudu na maji. Hata mafuta pia Mwenyezi Mungu anajua yanatoka kwenye ardhi gani, mikono inayoyatoa, mashirika yanayoyapora na vita vinavyosababishwa nayo. Na yanayoteremka kutoka mbinguni, yakiwemo maji theluji, nuru na heri nyinginezo.

Pia amewajua wale waliokwenda kwenye mwezi ili waweze kupata nyenzo watakayoitumia kuhodhi baraka za mbinguni na kuwanyima waja wa Mwenyezi Mungu; sawa na walivyoifanyia ardhi na heri zake. Lakini Mwenyezi Mungu ambaye imetukuka hikima yake, aliwarudisha nyuma kwa visigino vyao kwenye jaribio la tatu na wakarudi utupu.

Na yanayopanda humo.

Vile vile Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anajua yanayoendelea kwenye anga za juu, hata ndege za ujajusi na zile zinazobeba makombora na setilaiti zinazozunguka juu ya ardhi kwa malengo ya kishetani; kama vile ujasusi, na ugaidi kwa walala hoi na kuwapora riziki zao.

Naye yuko pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayoyatenda. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake. Na mambo yote yanarejeshwa kwa Mwenyezi Mungu.

Huu ni ukemeo na utisho kwa kila taghuti na dhalimu, kuwa matendo yake yamehifadhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba amewekwa rahani na atahisabiwa hisabu ya ndani na nzito na kuadhibiwa adhabu chungu.

Huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku. Na Yeye ni Mwenye kuyajua yaliomo vifuani.

Sayari zinataharaki na misimu inageuka, kuna msimu sehemu ya usiku inachukuliwa na mchana na mwingine mchana unachukuliwa na usiku na pia kuna siku unakuwa sawa usiku na mchana. Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (3:27), 17 (22:61), 21: (31:29) na 22 (34:13).

وَمَا لَكُمْ لَا تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ ۙ وَالرَّسُولُ يَدْعُوكُمْ لِتُؤْمِنُوا بِرَبِّكُمْ وَقَدْ أَخَذَ مِيثَاقَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ {8}

Na mna nini hata hamumwamini Mwenyezi Mungu na hali Mtume anawaita mumwamini Mola wenu? Naye amekwishachukua ahadi yenu, ikiwa nyinyi ni waumini.

هُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ عَلَىٰ عَبْدِهِ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ لِيُخْرِجَكُمْ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَإِنَّ اللَّهَ بِكُمْ لَرَءُوفٌ رَحِيمٌ {9}

Yeye ndiye anayemteremshia mja wake Aya zinazobainisha wazi ili awatoe gizani muingie kwenye nuru. Na hakika Mwenyezi Mungu kwenu ni Mpole, Mwenye kurehemu.

وَمَا لَكُمْ أَلَّا تُنْفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَلِلَّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا يَسْتَوِي مِنْكُمْ مَنْ أَنْفَقَ مِنْ قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ ۚ أُولَٰئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِنَ الَّذِينَ أَنْفَقُوا مِنْ بَعْدُ وَقَاتَلُوا ۚ وَكُلًّا وَعَدَ اللَّهُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ {10}

Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale waliotoa baadae na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi Mungu amewaahidi wema. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.

مَنْ ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ وَلَهُ أَجْرٌ كَرِيمٌ {11}

Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amrudishie maradufu, na apate ujira mzuri.