read

Aya 1 – 8: Mwezi Umepasuka

Maana

Saa imekaribia.

Maana yake ni sawa na Aya 57 ya sura iliyopita: “Tukio la karibu limekurubia.” Nayo ni kuwa siku ya Kiyama itafika tu, hilo halina shaka.

Na mwezi umepasuka!

Wafasiri wengi wamesema kuwa washirikina walimtaka Mtume wa Mwenyezi Mungu, (s.a.w.) aupasue mwezi mara mbili ikiwa yeye ni mkweli. Basi akamwomba Mola wake, na mwezi ukapasuka vipande viwili, kisha ukarudi kwenye hali yake ya kawaida.

Hakuna mwenye shaka kuwa hili linawezekana, lakini kuwezekana ni jambo jingine na kutokea ni jambo jingine.

Kwa sababu kutokea kunahitajia dalili ya kuthibitisha; wala hakuna dalili ya kuthibitisha; bali dalili ziko kinyume na hivyo; kama ifuatavyo:-

Kwanza: Haya hayaafikiani na Aya kadhaa zinazoelezea waziwazi kuwa Mtume (s.a.w.) hakuitikia maoni ya wa shirikina kutaka mambo yasiyokuwa ya kawaida, naye akawajibu kwa mujibu wa amri ya Mwenyezi Mungu:

قُلْ سُبْحَانَ رَبِّي هَلْ كُنْتُ إِلَّا بَشَرًا رَسُولًا {93}

“Sema: ametakasika Mola wangu! Kwani mimi ninani isipokuwa ni mwanadamu Mtume!”
Juz. 15 (17:93).

Pia Mwenyezi Mungu amebainisha kuwa wanotaka muujiza wataendela na ukafiri wao hata wakijibiwa maombi yao:

وَمَا مَنَعَنَا أَنْ نُرْسِلَ بِالْآيَاتِ إِلَّا أَنْ كَذَّبَ بِهَا الْأَوَّلُونَ ۚ {59}

“Na hapana kinachotuzuia kupeleka miujiza ila nikuwa watu wa zamani waliikanusha.”
Juz. 15 (17:59).

Akasema tena:

 وَإِنْ يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَا يُؤْمِنُوا بِهَا وَإِنْ يَرَوْا سَبِيلَ الرُّشْدِ لَا يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا وَإِنْ يَرَوْا سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ {146}

“Na wakiona kila Ishara hawaiamini na wakiona njia ya uongofu hawaishi- ki kuwa ndiyo njia, lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia,. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.” Juz. 9 (7:146).

Zaidi ya hayo ni kuwa mwenye kutaka visababu hana udhuru wowote baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwapa changa moto walimwengu wote na wakashindwa; pale aliposema: “Na mkiwa na shaka kwa (hayo) tuliyomteremshia mtumwa wetu, basi leteni sura moja iliyo mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.” Juz. 1 (2:23).

Pili: kupasuka mwezi ni tukio kubwa la kilimwengu, lau lingetokea wangeliona wa mashariki na wa magharibi, na wangeliliandika ulama na wanahistoria wengineo; kama walivyoandika matukio mengineyo.

Tatu: Kupasuka mwezi ni katika maudhui ambayo hayathibiti isipokuwa kwa khabar mutawatir na maudhui ya kupasuka mwezi yamekuja kwa Khabar Al-ahd. Tofauti ni kuwa katika Mutawatir wapokezi ni wengi na wanatofautiana hali zao na malengo yao, kwa namna ambayo, kwa kawaida, hawawezi kukongamana wakasema uwongo. Na Ahad ni kinyume na hivyo. Kwa hiyo unaweza kutofautisha kwamba mutawatir inategemewa zaidi kuliko Ahad.

Nne: Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Na umepasuka mwezi baada ya kauli yake: ‘Kimekurubia Kiyama.’ Inafahamisha kuwa mwezi utapasuka kitakapokuwa Kiyama na kwamba makusudio ya kupasuka mwezi hapa, ndio yale yaliyo katika kauli yake:

إِذَا السَّمَاءُ انْشَقَّتْ {1}

“Itakapopasuka mbingu.” (84:1).

Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: uchawi unaoendelea usiokuwa na mwisho.

Katika (74:24), Mwenyezi Mungu anamsimulia Walid bin Al-Mughira, kuwa alisema: “Haya si chochote ila ni uchawi ulionukuliwa.”

Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao.

Ujinga na hawaa umewapofusha na kila hoja na dalili. Kwa hiyo, pamoja na dalili za wazi, lakini wakakikadhibisha Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukutana naye.

Na kila jambo lina wakati maalum.

Hili ni kemeo kwa anayeiacha Qur’an. Maana ni kuwa kila kitu kimethibiti katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hakifichiki kwake jambo lolote likiwamo kuipinga Qur’an na kuachana nayo.

Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na watu wako wameikadhibisha nayo ni haki: Sema nami sikuwakilishwa juu yenu. Kila habari ina wakati maalum na punde mtajua.” Juz. 7 (6:66-67).

Na bila ya shaka zimewajia habari zenye makaripio.

Makusudio ya habari hapa ni kila Aya katika Qur’an yenye mawaidha na mazingatio, mapendekezo na makatazo, au zinazofahamisha njia ya imani, Siku ya Mwisho na wahyi ulioteremshwa kwa Mtume (s.a.w.).

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwabainishia washirikina, kupitia Nabii wake Muhammad (s.a.w.), dalili za kutosha juu ya haki, pia mawaidha ya kutosheleza ya kuikemea batili.

Hikima kamili.

Kila lilioko katika Qur’an ni hekima iliyofikia ukomo wa mawaidha na dalili juu ya haki, lakini maonyo hayafai kitu, kukiwa na inadi na kung’ang’ania ukafiri na upotevu. Basi jiepushe nao, ewe Muhammad, kwa sababu umewafikishia ujumbe wa Mola wako, lakini hawakukuitikia. Na ukafikisha nasaha, lakini hawakukubali.

Siku atakapoita mwitaji kuliendea jambo linalochusha. Macho yao yatainama; watatoka makaburini. Jambo linalochusha ni linalochukiwa na nafsi na kutochukulika. Makusudio yake hapa ni adhabu.

Hii ni kuwahofisha na kuwapa kiaga wale walioipinga haki, na kwamba wao wana siku ngumu isiyokuwa na kimbilio la adhabu yake, nayo ni siku watakayotoka makaburini kuelekea kwa Mola wao na hisabu, wakiwa madhalili wanyenyekevu, waamejawa na mshangao na kuchanganyikiwa.

Kama kwamba wao ni nzige waliotawanyika kutokana na wingi wao pale Mwenyezi Mungu atakapowafufua wafu na kuwausanya, watakapokutana wa mwanzo hadi wa mwisho.

Hapa kuna ishara ya kuwa ufufuo utakuwa kwa roho na mwili pamoja.

Wanamkimbilia mwitaji.

Yaani watakwenda haraka kwenye hisabu na malipo.

Makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu yenye vituko, hatari, maumivu na hofu.

Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtufu:

يَوْمَ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ سِرَاعًا كَأَنَّهُمْ إِلَىٰ نُصُبٍ يُوفِضُونَ {43}

خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۚ ذَٰلِكَ الْيَوْمُ الَّذِي كَانُوا يُوعَدُونَ {44}

“Siku watakapotoka makaburini kwa upesi; kama kwamba wao wanakimbilia kwenye mradi. Macho yao yatainama, fedhea itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyokuwa wakiahidiwa.” (70:43-44).

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ فَكَذَّبُوا عَبْدَنَا وَقَالُوا مَجْنُونٌ وَازْدُجِرَ {9}

Kabla yao kaumu ya Nuh walikadhibisha; wakamkadhibisha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa.

فَدَعَا رَبَّهُ أَنِّي مَغْلُوبٌ فَانْتَصِرْ {10}

Basi akamwomba Mola wake: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!

فَفَتَحْنَا أَبْوَابَ السَّمَاءِ بِمَاءٍ مُنْهَمِرٍ {11}

Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika.

وَفَجَّرْنَا الْأَرْضَ عُيُونًا فَالْتَقَى الْمَاءُ عَلَىٰ أَمْرٍ قَدْ قُدِرَ {12}

Na tukaipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo liliokadiriwa.

وَحَمَلْنَاهُ عَلَىٰ ذَاتِ أَلْوَاحٍ وَدُسُرٍ {13}

Na tukamchukua kwenye ile ya mbao na misumari.

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا جَزَاءً لِمَنْ كَانَ كُفِرَ {14}

Inakwenda kwa macho yetu. Ni malipo kwa alivyokuwa amekanushwa.

وَلَقَدْ تَرَكْنَاهَا آيَةً فَهَلْ مِنْ مُدَّكِرٍ {15}

Na hakika tuliiacha iwe ni Ishara. Basi je, yupo anayekumbuka?

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ {16}

Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo?

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِنْ مُدَّكِرٍ {17}

Na hakika tumeifanya Qur’an iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anayekumbuka?