read

Aya 12 – 15: Ndani Yake Ni Rehma Na Nje Yake Ni Adhabu

Maana

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema kuwa mwenye kuamini na akatoa sabili kwa ajili ya radhi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, atakuwa na ujira mzuri. Sasa hapa anaubainisha ujira huo kwa kusema:

Siku utakapowaona waumini wanaume na waumini wanawake, nuru yao inakwenda mbele yao, na kuume kwao:

Wenye takuwa waliojitolea, dunini walikuwa wakienda kwa mwongozo wa Mola wao. Siku ya hisabu na malipo mwongozo huu wa Mwenyezi Mungu utawaangazia mwanga hasa wa kuhisiwa, kama inavyoashiria Aya kwa neno utawaona na neno kuume kwao; yaani utaona nuru yao kwa macho yako; kama unavyoona taa anavyoichukuwa mtu mkononi na kuifanya anavyotaka.

Kwa maneno mengine ni kuwa, waliifanyia kazi nuru hii duniani kwa bidii na ikhlasi, wakaikuta Akhera iko mbele yao ikiwangazia masafa.

Furaha yenu leo ni Bustani zipitiwazo na mito chini yake kukaa humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
Kesho waongofu watatoka makaburini mwao na kutembea kwenye mwangaza utakaowafichulia njia ya amani. Na kabla ya kufika mwisho utawajia mwito: Furahini kwa Pepo. Kuna furaha gani zaidi inayoweza kulingana na Pepo ya milele na neema yake? Na ni kufuzu gani kukubwa kuliko huku?

Siku wanafiki wanaume na wanafiki wanawake watapowaambia walioamini: Tuangalieni ili tupate mwangaza katika nuru yenu.

Neno kuangalia tulilolifasiri kutokana na neno la kiarabu nadhr lina maana ya kuona kwa macho, kutaamali au kuhurumia1. Sio mbali kuwa maana ya kuangalia hapa ni hii ya kuhurumia. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amelitumia neno hili kwa maana haya ya kuhurumia aliposema:

 وَلَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّهُ وَلَا يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ{77}

Wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawaangalia.” Juz. 3 (3:77).

Waongofu duniani walikuwa kwenye nuru ya Mola wao na Akhera watakuwa hivyo hivyo:

وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ {17}

“Na ambao wameongoka anawazidishia uongofu wao na anawapa takua yao” Juz.26 (47:17).

Na wanafiki duniani walikuwa katika viza vya hawaa na mtamanio, basi wao siku ya kiyama watakuwa kwenye giza juu ya giza:

وَمَنْ كَانَ فِي هَٰذِهِ أَعْمَىٰ فَهُوَ فِي الْآخِرَةِ أَعْمَىٰ وَأَضَلُّ سَبِيلًا {72}

“Na aliyekuwa kipofu katika hii, basi Akhera atakuwa kipofu zaidi na aliyepotea njia.”
Juz. 15 (17:72).

Hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu imetaka wanafiki waone nuru ya waongofu ikiwaangazia mbele yao, ili wazidi uchungu juu ya uchungu; kisha uchungu utazidi pale watakapotaka usaidizi kwa waumini kuwa waende kwenye njia yao waambiwe: Rejeeni nyuma yenu mkaitafute nuru!

Hili ndilo jawabu lao: rudini kwa rafiki yenu shetani na mtafute nuru kutoka kwake. Yuko nyuma yenu leo kama alivyokuwa nyuma yenu jana.

Nuru hii ni ya yule aliyeifanyia kazi duniani na katika Akhera yake. Mwenye kuyanunua maisha ya dunia kwa Akhera, basi hatatoka katika giza isipokuwa kwenye ubaya zaidi.

Utiwe baina yao ukuta wenye mlango - ndani yake mna rehema, na upande wake wa nje kuna adhabu.

Makusudio ya ukuta ni kizuizi na rehema ni Pepo. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaneemesha waumini kwa Pepo na akawaadhibu wanafiki kwa adhabu ya Moto. Baina ya Pepo na Moto kuna kizuizi kilicho na pande mbili.

Watawaita wawaambie: Kwani hatukuwa pamoja nanyi?

Wanafiki watazungumza kwa lugha ya maneno au lugha ya hali kuwa sisi duniani tulikuwa tukifunga na kuswali na kufanya mliyokuwa mkiyafanya nyinyi, kwanini nyinyi mmeingia Peponi na sisi tukaingia motoni?

Watawaambia: Ndiyo, lakini mlijifitini wenyewe.

Makusudio ya kujifitini ni kujiangamiza. Waumini watawajibu, ndio mlikuwa pamoja na sisi mkifunga na kuswali, lakini mliziangamiza nafsi zenu kwa uwongo na unafiki na mkangojea balaa iwafike waumini, na mkatia shaka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu na kauli zake, na matamanio yakawadanganya, pale mlipodhani kwamba hadaa yenu na unafi- ki wenu utawavusha salama bila ya hisabu na adhabu.

Mpaka ilipokuja amri ya Mwenyezi Mungu ya kukutana naye kwa hisabu na malipo, na mdanganyifu akawadanganya katika Mwenyezi Mungu na mkamsadiki shetani na ahadi yake kuwa mtasalimika na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Basi leo haitapokelewa kwenu fidia, wala kukubaliwa toba wala hamtaweza kuikimbia adhabu:

 فَلَنْ يُقْبَلَ مِنْ أَحَدِهِمْ مِلْءُ الْأَرْضِ ذَهَبًا وَلَوِ افْتَدَىٰ بِهِ ۗ أُولَٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ وَمَا لَهُمْ مِنْ نَاصِرِينَ {91}

“Basi haitakubaliwa kwa yeyote katika wao hata fidia ya dhahabu kwa kujaza ardhi lau angelitoa. Hao watapata adhabu iumizayo, wala hawatakua na wasaidizi.” Juz. 3 (3:91).

Wala kwa wale walio kufuru.

Vile vile haitakubaliwa fidia na toba kutoka kwa wale waliodhihirisha kufuru bila ya kufanya hadaa na unafiki kama nyinyi.

Makaazi yenu ni Motoni. Hakuna kukimbia wala usaidizi isipokuwa Jahannam ndio bora kwenu; na ni marejeo maovu yalioje!

أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَنْ تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِنْ قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ ۖ وَكَثِيرٌ مِنْهُمْ فَاسِقُونَ {16}

Je, bado haujafika wakati kwa walioamini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyoteremka? Wala wasiwe kama waliopewa Kitabu kabla yao, muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikasusuwaa, na wengi wao ni mafasiki.

اعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ يُحْيِي الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا ۚ قَدْ بَيَّنَّا لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ{17}

Jueni kwamba Mwenyezi Mungu huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Tumewabainishia Ishara ili mpate kutia akili.

إِنَّ الْمُصَّدِّقِينَ وَالْمُصَّدِّقَاتِ وَأَقْرَضُوا اللَّهَ قَرْضًا حَسَنًا يُضَاعَفُ لَهُمْ وَلَهُمْ أَجْرٌ كَرِيمٌ {18}

Kwa hakika wanaume wanaotoa sadaka, na wanawake wanaotoa sadaka, na wakamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, watazidishiwa maradufu na watapata ujira mzuri.

وَالَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّهِ وَرُسُلِهِ أُولَٰئِكَ هُمُ الصِّدِّيقُونَ ۖ وَالشُّهَدَاءُ عِنْدَ رَبِّهِمْ لَهُمْ أَجْرُهُمْ وَنُورُهُمْ ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ {19}

Na waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, hao ndio wakweli hasa; Na Mashahidi mbele ya Mola wao, watapata ujira wao na nuru yao. Na waliokufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.
  • 1. Hata kwenye lugha ya kiswahili pia kuangalia kuna maana hayo -Mtarjumu