read

Aya 16 – 19: Je, Bado Haujafika Wakati Kwa Walioamini

Maana

Je, bado haujafika wakati kwa walioamini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyoteremka?

Kuunganisha haki iliyoteremka juu ya kumbuka Mwenyezi Mungu ni kwa kitafsiri; kwamba hakuna tofauti baina ya kinachounganishwa na kinachounganisha isipokuwa matamshi tu. Makusudio ya walioamini ni kundi katika wao.

Kabla ya kuleta ubainifu wa Aya, tunatanguliza maelezo kuwa imani inatofautiana kwa nguvu na udhaifu. Kuanzia imani inayomwajibisha aliye nayo kuwa maasumu; kama manabii; hadi imani ya uaminifu; kama vile baadhi ya maswahaba, hadi walio na daraja ya chini na kuendela chini zaidi.

Makusudio ya walioamini hapa ni wale waliotosheka na imani ya juu juu sio ya ndani na kwa dhahiri sio kwa hali halisi, wala haliwashughulishi jambo lolote la watu na masilahi ya umma.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amelizindua kundi hili la waumini kwenye Aya za jihadi alizoziteremsha katika Kitabu chake na kuhimiza kufanya uadilifu, kuinusuru haki na watu wake na kuwasuluhishia watu. Amewazindua kwenye hakika ya dini kwa mfumo huu wa upole ‘Je, bado haujafika wakati,’ ili waweze kusikia na kuwa na akili?

Wala wasiwe kama waliopewa Kitabu kabla yao, muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikasusuwaa.

Watu wa Kitabu ni wayahudi na wanaswara. Kususuwaa nyoyo zao ni kinaya cha kugeuka kwao baada ya Musa. Vile vile wanaswara baada ya Isa, basi nanyi waislamu msigeuke baada ya Muhammad (s.a.w.); kama walivyogeuka watu wa Kitab hapo mwanzo. Mfano wa Aya ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِنْ مَاتَ أَوْ قُتِلَ انْقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ {144}

“Hakuwa Muhammad ila ni Mtume; wamekwishapita Mitume kabla yake. Je, akifa au akiuliwa mtarudi nyuma? Juz. 4 (3:144)

Na wengi wao ni mafasiki.

Makusudio ya ya wengi ni viongozi wa kiyahudi na kinaswara (kikiristo) walioipotoa Tawrat na Injil kwa kupupia vyeo na chumo.

Jueni kwamba Mwenyezi Mungu huifufua ardhi baada ya kufa kwake.

Wafasiri wengi wamesema kuwa huku ni kufananisha nyoyo zilizosusuwaa na ardhi iliyokufa na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu anaipa uhai ardhi kwa mvua vile vile ataziongoza nyoyo zilizosusuwaa kwa mawaidha.

Tuonavyo sisi ni kuwa huu ni utisho na onyo kwa wale watakaogeuka baada ya Muhammad (s.a.w.) – kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafufua; sawa na anavyoifufua ardhi, na atawalipa kuritadi kwao baada ya nabii wao.

Maana haya yanatiwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyokuja moja kwa moja inayosema: Tumewabainishia Ishara ili mpate kutia akili. Hakika nyinyi mtaulizwa siku ya Kiyama yale mliyoyazusha baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.).

Kwa hakika wanaume wanaotoa sadaka, na wanawake wanaotoa sadaka, na wakamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, watazidishiwa maradufu na watapata ujira mzuri.

Husomwa bila ya shadda katika herufi swad kwa maana ya waumini na husomwa kwa shadda kwa maana ya wanaotoa sadaka.
Makusudio ya mkopo mwema ni kutoa sadaka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa hiyo hakuna kukaririka. Makusudio ya ujira mzuri ni kuwa nuru yao iko mbele yao siku ya Kiyama kuongezea mahurilaini makasri n.k.

Umetangulia mfano wake katika Aya 11 ya sura hii na Juz. 2 (2:245)

Na waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wakatenda kwa mujibu wa imani yao, hao ndio wakweli hasa; yaani waliodumu na ukweli katika imani yao kwa kauli na vitendo, na ukweli ni njia ya uokovu kwa kila maangamizi.

Na Mashahidi mbele ya Mola wao, watapata ujira wao na nuru yao.

Mashahidi ni wale waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Ama ujira wao mbele ya Mola wao, ameibainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kauli yake: “Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba wao wapate Pepo, wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wanaua na kuuawa. Ni ahadi aliyojilazimisha kwa haki katika Tawrat na Injil na Qur’an.”Juz. 11 (9:111).

Ama nuru yao ameiashiria katika Aya ya 12 ya sura hii. Mtume (s.a.w.) anasema: “Hakuna yeyote atayeingia Peponi kisha akapenda kutoka kwenda duniani, hata kama atakuwa na ardhi na vilivyomo ndani yake, isipokuwa shahidi. Atatamani arudi duniani auawe mara kumi, kutokana na karama aliyoiona kwa Mwenyezi Mungu.

Na waliokufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.

Hii ni desturi ya Qur’an kulinganisha wenye takuwa na wakosefu na thawabu zao na adhabu zao kwa kusudia kupendekeza na kuhadharisha.

Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; ikiwemo ile iliyo katika Juz.7 (6:32). Dunia inayoshutumiwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kupitia kwa mitume wake, ni ile dunia inayotafutiwa matamanio, starehe, mchezo, upuzi, kiburi na kujifaharisha. Ama dunia ambayo haja za wahitaji zinatekelezwa, udhalimu unapingwa na kunufaika ndani ya dunia hiyo na Akhera, basi hiyo haishutumiwi.

اعْلَمُوا أَنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَزِينَةٌ وَتَفَاخُرٌ بَيْنَكُمْ وَتَكَاثُرٌ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ ۖ كَمَثَلِ غَيْثٍ أَعْجَبَ الْكُفَّارَ نَبَاتُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَكُونُ حُطَامًا ۖ وَفِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَغْفِرَةٌ مِنَ اللَّهِ وَرِضْوَانٌ ۚ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ {20}

Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na upuzi, na pambo, na kujifaharisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Ni kama mfano wa mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yana rangi ya njano kisha yakawa makapi. Na akhera kuna adhabu kali na maghufira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.

سَابِقُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِنْ رَبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا كَعَرْضِ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أُعِدَّتْ لِلَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّهِ وَرُسُلِهِ ۚ ذَٰلِكَ فَضْلُ اللَّهِ يُؤْتِيهِ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَاللَّهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ{21}

Kimbilieni maghufira ya Mola wenu, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyowekewa waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.

مَا أَصَابَ مِنْ مُصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنْفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِنْ قَبْلِ أَنْ نَبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرٌ {22}

Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujaziumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

لِكَيْلَا تَأْسَوْا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ ۗ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ {23}

Ili msihuzunike kwa kilicho wapotea, wala msifurahi kwa alichowapa. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna, anayejifaharisha.

الَّذِينَ يَبْخَلُونَ وَيَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبُخْلِ ۗ وَمَنْ يَتَوَلَّ فَإِنَّ اللَّهَ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ{24}

Ambao wanafanya ubakhili, na wanaamrisha watu wafanye ubakhili. Na anayegeuka, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.